083-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Makatazo Ya Kujumuika Kaburini, Kumswalia Nabiy Kunamfikia

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 83

 

Makatazo Ya Kujumuika Kaburini, Kumswalia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Popote Ulipo Kunamfikia

 

 

 

 

 عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((لاَ تَجْعَلُوا قَبْرِي عِيدًا، وَصَلُّوا عَلَيَّ فَإِنَّ صلاَتَكُمْ تَبْلُغُنِي حَيْثُ كُنْتُمْ)) رواه أبو داود بإسنادٍ صحيح

 

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Msifanye [msijikusanye] kaburini mwangu kama mnavyojikusanya (wakati wa) sikukuu, niswalieni, hakika Swalaah yenu inanifikia popote mnapokuwa)). [Abuu Daawuwd kwa isnaad Swahiyh]

 

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

 

1. Makatazo ya vitendo visivyoruhusiwa wakati wa kuzuru kaburi la Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kama kupandisha sauti, kugusa kuta na kujipangusa mwilini na usoni kutafuta baraka na mambo mengineyo ya uzushi ambayo mengineyo yanapelekea katika shirki. Baadhi ya Waislamu wanatenda haya katika kuzuru kaburi la Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) huko Madiynah.  Hali kadhaalika katika kuzuru makaburi ya waja wema kuwaomba na hata kuwaabudu. Hivyo ni kupindukia mipaka ambayo imekatazwa katika Shariy’ah ya Dini yetu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى)

 

 يَا أَهْلَ الْكِتَابِ لَا تَغْلُوا فِي دِينِكُمْ

Enyi Ahlal-Kitaabi! Msipindukie mipaka katika dini yenu [An-Nisaa (4: 171)]

 

 

 

2. Pendekezo la kuzuru kaburi la Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa kufuata adabu zake katika Shariy’ah na si kinyume chake.

 

 

 

3. Amri ya kumswalia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

إِنَّ اللَّـهَ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ ۚ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيمًا ﴿٥٦﴾

Hakika Allaah na Malaika Wake wanamswalia Nabiy. Enyi walioamini mswalieni na msalimieni kwa mamkizi ya amani na kwa tasliymaa. [Al-Ahzaab (33: 56)]

 

 

Rejea Hadiyth namba (82).

 

 

4. Fadhila kwa Waislamu katika kumswalia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

Rejea Hadiyth namba (82)

 

 

 

Share