088-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Miongoni Mwa Adhabu Za Kaburi: An-Namiymah, Asiyejisafisha Akimaliza Kukojoa

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya  85

 

Miongoni Mwa Adhabu Za Kaburi: An-Namiymah (Kufitinisha), Na Asiyejisafisha Akimaliza Kukojoa

 

 

 

عَنْ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما) أنَّ َ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ  مَرَّ بِقَبْرَيْنِ فَقَالَ: ((إِنَّهُمَا يُعَذَّبَانِ، وَمَا يُعَذَّبَانِ فِي كَبِير! بَلى إنَّه لكَبِيرٌ. أَمَّا أَحَدُهُمَا فَكَانَ يَمْشِي بِالنَّمِيمَةِ، وَأَمَّا الأَخَرُ فَكَانَ لاَ يَسْتَتِرُ مِنْ بَوْلِهِ)) متفق عليه وهذا لفظ إحدى روايات البخاري

Imepokelewa kutoka kwa bin ‘Abbaas (رضي الله عنهما)  kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم ) aliyapitia makaburi mawili akasema: ((Hakika hawa wanaadhibiwa. Wala hawaadhibiwi kwa sababu ya jambo kubwa. Bali la! Hakika ni jambo kubwa. Mmoja wao alikuwa akifitinisha, na mwengine alikuwa hajikingi na mkojo [anapokojoa])). [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Uharamisho wa kufitinisha baina ya watu jambo ambalo ni miongoni mwa madhambi makubwa yanayompatia mtu adhabu ya kaburi. Kwa sababu kufitinisha watu kunasababisha uadui baina ya ndugu wa Kiislamu. Allaah (سبحانه وتعالى) Anakataza hayo katika kauli Yake:

 

  وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَىٰ ۖ وَلَا تَعَاوَنُوا عَلَى الْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۖ إِنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ ﴿٢﴾

 Na shirikianeni katika wema na taqwa, na wala msishirikiane katika dhambi na uadui. Na Mcheni Allaah; hakika Allaah ni Mkali wa kuakibu.  [Al-Maaidah (5: 2)].

 

 

 Na pia Allaah (سبحانه وتعالى) Anatahadharisha ufitinashaji kama Anavyosema:

 

وَلَا تُطِعْ كُلَّ حَلَّافٍ مَّهِينٍ﴿١٠﴾

Na wala usimtii kila mwingi wa kuapa, dhalili.

هَمَّازٍ مَّشَّاءٍ بِنَمِيمٍ﴿١١﴾

Mwingi wa kukashifu, mpitaji huku na kule kwa kufitinisha. [Al-Qalam: 10-11]

 

 

 

2. Mfitinishaji haingii Jannah kwa dalili Hadiyth ifuatayo:

 

 عن حذيفة رضي الله عنه قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: ((لا يَدْخُلُ الجَنَّةَ نَمَّامٌ))  رواه البخاري ومسلم

Kutoka kwa Hudhayfah (رضي الله عنه)  ambaye amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)  amesema: ((Mchongezi (Mfitinishaji) hataingia Jannah)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

 

3 Wajibu wa mtu kujitwaharisha vizuri anapomaliza kukojoa asiache athari yoyote ya mkojo, kwani Allaah (سبحانه وتعالى) Anapenda wanaojitwaharisha kama Anavyosema:

 

 فِيهِ رِجَالٌ يُحِبُّونَ أَن يَتَطَهَّرُوا ۚ وَاللَّـهُ يُحِبُّ الْمُطَّهِّرِينَ﴿١٠٨﴾

Humo mna watu wanaopenda kujitwaharisha. Na Allaah Anapenda wanaojitwaharisha. [At-Tawbah (9: 108)]

 

Na Anasema pia:

 

 

وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الْمَحِيضِ ۖ قُلْ هُوَ أَذًى فَاعْتَزِلُوا النِّسَاءَ فِي الْمَحِيضِ ۖ وَلَا تَقْرَبُوهُنَّ حَتَّىٰ يَطْهُرْنَ ۖ فَإِذَا تَطَهَّرْنَ فَأْتُوهُنَّ مِنْ حَيْثُ أَمَرَكُمُ اللَّـهُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ التَّوَّابِينَ وَيُحِبُّ الْمُتَطَهِّرِينَ ﴿٢٢٢﴾ 

Na wanakuuliza kuhusu hedhi. Sema: “Hiyo ni dhara; basi waepukeni wanawake katika hedhi. Wala msiwakaribie kujimai nao mpaka watwaharike. Watakapotwaharika basi waendeeni kupitia pale Alipokuamrisheni Allaah.”  Hakika Allaah Anapenda wenye kutubia na Anapenda wenye kujitwaharisha.   [Al-Baqarah: 222].

 

 

4. Uislamu unafunza usafi wa kila aina khasa katika mwili  mwa bin Aadam.

 

 

5. Thibitisho la kuweko adhabu za kaburi na himizo la kujikinga nazo.

 

 

6. An-Namiymah ni miongoni mwa maradhi ya moyo yanayotokana na uhasidi, choyo, na kupendelea shari baina ya ndugu wanaopatana na kupendana. Hakuna kitakachomfaa mtu Siku ya Qiyaamah isipokuwa atakayefika akiwa na moyo uliosalimika na maovu mfano wa hayo ya uhasidi, chuki na kadhaalika. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

يَوْمَ لَا يَنفَعُ مَالٌ وَلَا بَنُونَ ﴿٨٨﴾

 “Siku hayatofaa mali wa watoto.

 

إِلَّا مَنْ أَتَى اللَّـهَ بِقَلْبٍ سَلِيمٍ ﴿٨٩﴾

 “Isipokuwa yule atakayemfikia Allaah na moyo uliosalimika. [Ash-Shu’araa (26: 88-89)].

 

 

 

7. An-Namiymah ni aina ya ufisadi katika jamii jambo ambalo   Allaah (سبحانه وتعالى) Analiharamisha na Halipendi kabisa kama Anavyosema:

 

  وَلَا تَبْغِ الْفَسَادَ فِي الْأَرْضِ ۖ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ الْمُفْسِدِينَ ﴿٧٧﴾

Na wala usitake ufisadi ardhini. Hakika Allaah Hapendi mafisadi.” [Al-Qaswasw (28: 77)].

 

 

 

8. Rejea pia Hadiyth namba (21), (22), (89), (94)

 

 

 

Share