091-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Aliyehifadhi Qur-aan Anatukuzwa Duniani Na Aakhirah

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 91

 

Aliyehifadhi Qur-aan Anatukuzwa Duniani Na Aakhirah

 

 

 

 

عن جابر (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ كَانَ  يَجْمَعُ بَيْنَ الرَّجُلَيْنِ مِنْ قَتْلَى أُحُدٍ  يَعْنِي  فِي الْقَبْرِ ثُمَّ َيَقُولُ: ((أَيُّهُمَا أَكْثَرُ أَخْذًا لِلْقُرْآنِ ))  فَإِذَا أُشِيرَ لَهُ إِلَى أَحَدِهِمَا قَدَّمَهُ فِى اللَّحْدِ – رواه البخاري

Imepokelewa kutoka kwa Jaabir (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akiwajumuisha kaburini watu wawiliwawili katika Mashahidi wa vita vya Uhud, kisha akiuliza: ((Ni yupi kati yao aliyebeba [aliyehifadhi] Qur-aan zaidi?)) Anapoashiriwa mmojawapo humtanguliza katika mwanandani.   [Al-Bukhaariy]

 

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Utukufu wa hali ya juu wa Qur-aan kwani ni maneno ya Rabb Mumba wa kila kitu.

 

 

 

2. Qur-aan humtoa mtu katika kiza cha upotofu na kumuingiza katika Nuru. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

الر ۚ كِتَابٌ أَنزَلْنَاهُ إِلَيْكَ لِتُخْرِجَ النَّاسَ مِنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ بِإِذْنِ رَبِّهِمْ إِلَىٰ صِرَاطِ الْعَزِيزِ الْحَمِيدِ ﴿١﴾

Alif Laam Raa. Kitabu Tumekiteremsha kwako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) ili uwatoe watu kutoka kwenye viza kuwaingiza katika nuru kwa idhini ya Rabb wao, waelekee katika njia ya Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye kustahiki kuhimidiwa kwa yote. [Ibraahiym (14: 1)]

 

 

Rejea pia: Al-Maaidah (5: 160),  Al-Hadiyd (57: 9), Atw-Twalaaq (65: 11).

 

 

 

3. Fadhila tele kwa aliyehifadhi Qur-aan; huzipata duniani kabla ya Aakhirah. Miongoni mwa fadhila za duniani ni:

 

 

-Mwenye elimu ya Qur-aan hupewa uimamu katika Swalaah:

 

Kutoka kwa Abuu Mas’uwd Al-Answaariyy kwamba Nabiy (صلى الله عليه  وآله وسلم) amesema: ((Awaswalishe watu yule mwenye kujua kusoma zaidi Kitabu cha Allaah na wakiwa katika kusoma wako sawa, basi mwenye ujuzi zaidi wa Sunnah, na wakiwa kwenye Sunnah wako sawa, basi aliyetangulia hijrah, na wakiwa katika hijrah wako sawa, basi mkubwa wao kwa umri, wala asiswalishe mtu katika nyumba yake wala katika mamlaka yake wala asikae kwa heshima yake  isipokuwa kwa ruhusa yake)).  [Al-Bukhaariy]  

 

 

-Mwenye elimu ya Qur-aan huwa ni mbora kabisa kati ya watu kama alivyosema Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) katika Hadiyth:

 

 

عن عثمانَ بن عفانَ رضي الله عنه أنَّ النبيَّ صلى الله عليه وسلّم قالَ    ((خَيرُكُم مَنْ تعَلَّمَ القُرآنَ وعَلَّمَه))   صحيح البخاريِّ

Kutoka kwa 'Uthmaan bin 'Affaan (رضي الله عنه)  kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Mbora wenu anayejifunza Qur-aan akaifunza)). [Al-Bukhaariy, Muslim, At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Abu Daawuwd, Ahmad] 

 

Rejea pia Hadiyth namba (80).

 

 

-Mwenye elimu ya Qur-aan hupewa uongozi katika vituo vya Dini, hufadhilishwa katika kuoa, hupendwa na watu:

 

قال عمر رضي الله عنه : أما إن نبيكم صلى الله عليه وسلم قد قال : (( إن الله يرفع بهذا الكتاب أقواماً ويضع  به آخرين ))  صحيح مسلم  

Kutoka kwa 'Umar (رضي الله عنه)  ambaye amesema, Nabiy wenu (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:    ((Allaah Atawanyanyua baadhi ya watu kwa kitabu hiki (Qur-aan) na Atawadhalilisha wengine kwa kitabu hiki))  [Muslim, Ibn Maajah, Ahmad] 

 

 

-Mwenye elimu ya Qur-aan ni miongoni mwa watu makhsusi wanaopendwa na Allaah (سبحانه وتعالى):

 

عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ قَالَ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: (( إِنَّ لِلَّهِ أَهْلِينَ مِنْ النَّاسِ)) قَالُوا يَا رَسُولَ اللَّهِ مَنْ هُمْ قَالَ:  ((هُمْ أَهْلُ الْقُرْآنِ أَهْلُ اللَّهِ وَخَاصَّتُهُ)) أحمد و إبن ماجه

 

Imepokelewa kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah Anao watu wake kati ya wanaadam)). Wakamuuliza: Ee Rasuli wa Allaah ni nani hao? Akasema: ((Hao ni watu wa Qur-aan na ni watu wa Allaah na wateule Wake))  [Ahmad, Ibn Maajah]

   

 

-Mwenye elimu ya Qur-aan atahifadhiwa na fitna za Masiyhud-Dajjaal kwa kuhifadhi Aayah za mwanzo za Suratul-Kahf.  [Muslim] 

 

 

 

4. Fadhila za Aakhirah ni nyingi zaidi ya kwanza iliyotajwa katika Hadiyth kwamba anaanza maisha yake ya Aakhirah kwa kufadhilishwa anapoingizwa kaburini. Fadhila nyinginezo ni kama zifuatazo:

 

-Qur-aan itamuombea shafaa’ah, atavalishwa taji na Malaika, na kuu zaidi atapata Radhi za Allaah (سبحانه وتعالى)

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((يَجِيءُ الْقُرْآنُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ فَيَقُولُ يَا رَبِّ حَلِّهِ ، فَيُلْبَسُ تَاجَ الْكَرَامَةِ ثُمَّ يَقُولُ: يَا رَبِّ زِدْهُ, فَيُلْبَسُ حُلَّةَ الْكَرَامَةِ ثُمَّ يَقُولُ: يَا رَبِّ ارْضَ عَنْهُ فَيَرْضَى عَنْهُ فَيُقَالُ لَهُ: اقْرَأْ وَارْقَ.  وَتُزَادُ بِكُلِّ آيَةٍ حَسَنَةً))  

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Qur-aan itakuja siku ya Qiyaamah na itasema: “Ee Rabb, Mpambe” [Mwenye kuhifadhi Qur-aan]. Kisha atavalishwa taji. Kisha [Qur-aan] itasema: “Ee Rabb, muongezee”. Kisha huyo mtu atavishwa nguo ya heshima. Kisha itasema: “Ee Rabb Ridhika naye”. Allaah, Ataridhika naye. Kisha ataambiwa: “Soma na panda”. Atapokea thawabu zaidi ya mema kwa kila Aayah [atakayosoma])   [At-Tirmidhy na Al-Haakim]

 

 

-Hupandishwa Daraja Jannah:

 

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عَمْرٍو عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ:  ((يُقَالُ لِصَاحِبِ الْقُرْآنِ اقْرَأْ وَارْتَقِ وَرَتِّلْ كَمَا كُنْتَ تُرَتِّلُ فِي الدُّنْيَا فَإِنَّ مَنْزِلَتَكَ عِنْدَ آخِرِ آيَةٍ تَقْرَأُ بِهَا))

Kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amr kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Huambiwa Aliyeiandama na Qur-aan: Soma na panda [juu katika daraja za Jannah] na uisome kwa 'Tartiyl' [kufuata hukmu zake] kama ulivyokuwa ukiisoma ulipokuwa duniani, kwani makazi yako ni pale utakapofika katika Aayah ya mwisho utakayoisoma)).  [At-Tirmidhiy, Abu Daawuwd, Ibn Maajah, Ahmad] 

 

 

-Pia kwa kuhifadhi Suratul-Baqarah na Suratul-‘Imraan zitakuwa ni kivuli chake Siku ya Qiyaamah. [Muslim]

 

 

 

5. Kila mwana Aadam Muislamu au kafiri anaihitaji Qur-aan kwani ni poza ya vifua dhidi ya shirki, kufru, unafiki, uasi, uhasidi na kila aina ya maradhi ya moyo yaliyotajwa katika Qur-aan na Sunnah. Bali ni hazina bora ya kila kitu kuliko hazina zinazotafutwa na kupendwa na watu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 

 يَا أَيُّهَا النَّاسُ قَدْ جَاءَتْكُم مَّوْعِظَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَشِفَاءٌ لِّمَا فِي الصُّدُورِ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ﴿٥٧﴾

Enyi watu! Kwa yakini yamekujieni mawaidha kutoka kwa Rabb wenu, na shifaa ya yale yaliyomo vifuani, na mwongozo na rahmah kwa Waumini.

 

قُلْ بِفَضْلِ اللَّـهِ وَبِرَحْمَتِهِ فَبِذَٰلِكَ فَلْيَفْرَحُوا هُوَ خَيْرٌ مِّمَّا يَجْمَعُونَ﴿٥٨﴾

Sema: “Kwa fadhila za Allaah na kwa rahmah Yake basi kwa hayo wafurahi.” Hayo ni kheri kuliko wanayoyakusanya. [Yuwnus (10: 57-58)]

 

 

 

6. Wahyi wa Qur-aan umeitwa Ruwh (roho) kama ilivyotajwa katika Qur-aan, ni kama kumpa mtu uhai wa moyo. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَكَذَٰلِكَ أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ رُوحًا مِّنْ أَمْرِنَا ۚ مَا كُنتَ تَدْرِي مَا الْكِتَابُ وَلَا الْإِيمَانُ وَلَـٰكِن جَعَلْنَاهُ نُورًا نَّهْدِي بِهِ مَن نَّشَاءُ مِنْ عِبَادِنَا ۚ وَإِنَّكَ لَتَهْدِي إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ﴿٥٢﴾

 Na hivyo ndivyo Tulivyokuletea Ruwh (Qur-aan) kutoka amri Yetu. Hukuwa unajua nini Kitabu wala iymaan, lakini Tumeifanya ni Nuru, Tunaongoa kwayo Tumtakaye miongoni mwa waja Wetu. Na hakika wewe (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) bila shaka unaongoza kuelekea njia iliyonyooka. [Ash-Shuwraa (42: 52)].

  

 

Vile vile Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 أَوَمَن كَانَ مَيْتًا فَأَحْيَيْنَاهُ وَجَعَلْنَا لَهُ نُورًا يَمْشِي بِهِ فِي النَّاسِ كَمَن مَّثَلُهُ فِي الظُّلُمَاتِ لَيْسَ بِخَارِجٍ مِّنْهَا ۚ كَذَٰلِكَ زُيِّنَ لِلْكَافِرِينَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١٢٢﴾

Je, aliyekuwa maiti kisha Tukamhuisha na Tukamjaalia nuru anatembea kwayo kati ya watu, ni sawa na yule ambaye yumo katika viza si mwenye kutoka humo? Hivyo ndivyo walivyopambiwa makafiri yale waliyokuwa wakiyatenda. [Al-An’aam: 122]

 

 

7. Qur-aan imejumuisha kila jambo, na ufumbuzi wa kila tatizo kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى):

  وَنَزَّلْنَا عَلَيْكَ الْكِتَابَ تِبْيَانًا لِّكُلِّ شَيْءٍ وَهُدًى وَرَحْمَةً وَبُشْرَىٰ لِلْمُسْلِمِينَ﴿٨٩﴾

 Na Tumekuteremshia Kitabu kikiwa ni kielezo bayana cha kila kitu na ni mwongozo na rahmah na bishara kwa Waislamu. [An-Nahl (16: 89)]

 

 

 

8. Jamii isisitize mafunzo ya Qur-aan kwa watoto na watu wazima, yakiwemo kuifundisha usomaji wake kwa Tajwiyd (hukmu zake), kuiihifadhi, kufundisha lugha ya Kiarabu ili kuifahamu tafsiyr yake. Mafunzo haya yapewe umuhimu sawa kuliko yanavyopewa umuhimu wa masomo ya kisekula, kwani haya ndiyo yatakayomfaa mtu duniani na Aakhirah.

 

 

 

Share