093-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Kumtukana Muislamu Ni Ufasiki Na Kupigana Naye Ni Ukafiri

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 93

 

Kumtukana Muislamu Ni Ufasiki Na Kupigana Naye Ni Ukafiri

 

 

 

 

عَنْ ابْن مَسْعُودٍ (رضي الله عنه) قَال: قَالَ رَسُولُ الله صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((سِبَابُ الْمُسْلِمِ فُسُوقٌ وَقِتَالُهُ كُفْرٌ)) متفق عليه

Imepokelewa kutoka kwa bin Mas’uwd (رضي الله عنه)  ambaye amesema: “Nabiy (صلى الله عليه  وآله وسلم ) amesema: ((Kumtukana Muislamu ni ufasiki, na kupigana naye ni ukafiri)). [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Makatazo ya kutukana, kwani ni kudharauliana, kuvunjiana heshima, hadhi na kusababisha ukhasama baina ya Waislamu. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ameonya:  ((…Kila Muislamu juu ya Muislamu mwenziwe ni haramu damu yake, mali yake na heshima yake)).  [Muslim]

 

 

Rejea pia Hadiyth namba (22), (87), (88), (89), (94), (126).

 

 

2. Uislamu unasisitiza masikilizano na amani baina ya watu, kwani kutukanana na kupigana ni kunyimana haki na kunasababisha ukosefu wa usalama na amani baina ya watu katika jamii.

 

 

3. Makatazo ya kupigana na Muislamu, kwani wote ni ndugu, na pindi wanapopigana huwa ni waajib kwa wengine kuwapatanisha kama Anavyoamrisha Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 

 وَإِن طَائِفَتَانِ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ اقْتَتَلُوا فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا ۖ فَإِن بَغَتْ إِحْدَاهُمَا عَلَى الْأُخْرَىٰ فَقَاتِلُوا الَّتِي تَبْغِي حَتَّىٰ تَفِيءَ إِلَىٰ أَمْرِ اللَّـهِ ۚ فَإِن فَاءَتْ فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا بِالْعَدْلِ وَأَقْسِطُوا ۖ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ﴿٩﴾

Na ikiwa makundi mawili ya Waumini yakipigana, basi suluhisheni baina yao. Lakini mojawapo likikandamiza jengine, basi piganeni na ambalo linakandamiza mpaka lielemee kwenye amri ya Allaah. Likishaelemea, basi suluhisheni baina yao kwa uadilifu, na timizeni haki haki. Hakika Allaah Anapenda wanaotimiza haki.

 

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ فَأَصْلِحُوا بَيْنَ أَخَوَيْكُمْ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ﴿١٠﴾

Hakika Waumini ni ndugu, basi suluhisheni baina ya ndugu zenu. Na mcheni Allaah ili mpate kurehemewa. [Al-Hujuraat (49: 9-10)]

 

 

4. Kupigana na ndugu Muislamu kumefananishwa na ukafiri, hivyo ni onyo linalohusiana na iymaan ya mtu.

 

 

  

Share