096-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Haifai Kubughudhiana, Kuhusudiana, Kuendeana Kinyume, Kukatana Na Kukhasimiana Kwa Zaidi Ya Siku Tatu

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 96

 

Haifai Kubughudhiana, Kuhusudiana, Kuendeana Kinyume,

Kukatana Na Kukhasimiana Kwa Zaidi Ya Siku Tatu

 

 

عَنْ أَنَسُ (رضي الله عنه) أنّ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((لاَ تَبَاغَضُوا، وَلاَ تَحَاسَدُوا، وَلاَ تَدَابَرُوا، وَلاَ تَقَاطَعوا، وَكُونُوا عِبَادَ اللَّهِ إِخْوَانًا، وَلاَ يَحِلُّ لِمُسْلِمٍ أَنْ يَهْجُرَ أَخَاهُ فَوْقَ ثَلاَثَةِ أَيَّامٍ)) متفق عليه

Imepokelewa kutoka kwa Anas (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Msibughudhiane [msichukiane], wala msihusudiane, wala msipeane mgongo, wala msikatane, kuweni waja wa Allaah ni ndugu, wala haifai kwa Muislamu kumhama nduguye kwa zaidi ya siku tatu [asiseme naye])). [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Kubughudhiana, kuhusudiana, kuendeana kinyume, kukatana, kukhasimiana, yote ni maovu yanayohusu haki baina ya watu na ambayo yanaleta mtafaruku baina ya watu.

 

Rejea Hadiyth namba (22), (42), (72), (93), (94).

 

 

 

2.  Maovu hayo ni aina ya maradhi ya moyo. Ikiwa Muislamu anayo maradhi kama hayo basi ajitahidi kusoma du’aa ifuatayo iliyomo katika Aayah ya Qur-aan:

 

 رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ﴿١٠﴾

“Rabb wetu! Tughufurie na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa iymaan na wala Usijaalie katika nyoyo zetu mafundo ya chuki kwa wale walioamini; Rabb wetu! Hakika Wewe ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu. [Al-Hashr (59: 10)]

 

 

 

3. Bin Aadam ni dhaifu, ana hisia za moyo anapoudhiwa, lakini ni Rahmah ya Allaah (سبحانه وتعالى) kumpa mja Wake muda wa siku tatu kuungulika na  kuvumilia. Kisha inampasa arudishe moyo wake katika kusamehe, kupuuzilia mbali na kujaribu kusahau.

 

Katika kisa cha Ifk, Abu Bakr (رضي الله عنه) aligoma kwanza kuendelea kumpa sadaka jamaa yake aliyehusika katika kumzulia Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها), lakini Allaah (سبحانه وتعالى) Alipoteremsha kauli Yake ifuatayo, Abu Bakr alikiri kuwa anataka kughufuriwa madhambi yake, na akaendelea kuitoa sadaka yake kwa jamaa huyo jamaa yake:

 

وَلَا يَأْتَلِ أُولُو الْفَضْلِ مِنكُمْ وَالسَّعَةِ أَن يُؤْتُوا أُولِي الْقُرْبَىٰ وَالْمَسَاكِينَ وَالْمُهَاجِرِينَ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ ۖ وَلْيَعْفُوا وَلْيَصْفَحُوا ۗ أَلَا تُحِبُّونَ أَن يَغْفِرَ اللَّـهُ لَكُمْ ۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٢٢﴾

Na wala wasiape wale wenye fadhila miongoni mwenu na wenye wasaa wa mali kuwa hawatowapa (swadaqah) jamaa wa karibu, na masikini, na Muhaajiriyn katika njia ya Allaah. Na wasamehe na waachilie mbali. Je, hampendi Allaah Akughufurieni? Na Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu.  [An-Nuwr (24: 22)]

 

 

Na kusamehe watu pamoja na kuzuia ghadhabu kutokutamka maneno maovu ni katika sifa za ihsaan na Allaah (سبحانه وتعالى) Anampenda mtu huyo mwenye kusamehe watu kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

الَّذِينَ يُنفِقُونَ فِي السَّرَّاءِ وَالضَّرَّاءِ وَالْكَاظِمِينَ الْغَيْظَ وَالْعَافِينَ عَنِ النَّاسِ ۗ وَاللَّـهُ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ ﴿١٣٤﴾ 

Ambao wanatoa (kwa ajili ya Allaah) katika hali ya wasaa na katika hali ya shida, na wanazuia ghadhabu, na wenye kusamehe watu. Na Allaah Anapenda wafanyao ihsaan. [Aal-‘Imraan (3: 134)]

 

Na atakayeanza kumsemesha mwenziwe ni mbora zaidi ya mwengine. Hadiyth ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): 

 

 عن أبي أيوب الأنصاري رضي الله عنه قال : قال النبي صلى الله عليه وسلم: ((لا يَحِلُّ لِمُسْلِمٍ أَنْ يَهْجُرَ أَخَاهُ فَوْقَ ثَلَاثِ لَيَالٍ، يَلْتَقِيَانِ فَيُعْرِضُ هَذَا وَيُعْرِضُ هَذَا، وَخَيْرُهُمَا الَّذِي يَبْدَأُ بِالسَّلام))  

((Haimpasi Muislamu amhame ndugu yake kwa zaidi ya siku tatu hata wanapokutana huyu anamgeuzia [uso] huyu na huyu anamgeuzia [uso] huyu. Na aliye mbora wao kati ya hao wawili ni yule anayeanza kutoa salaam)). [Al-Bukhaariy na Muslim] Pia:

 

Na katika Riwaayah nyengine:

 

((فَمَنْ هَجَرَ فَوْقَ ثَلاَثٍ فَمَاتَ دَخَلَ النَارَ ))  

((Atakayemhama [mwenzake] kwa zaidi ya siku tatu akafariki, basi ataingia motoni)). [Abuu Daawuwd]

 

Rejea pia Hadiyth namba (97).

 

 

 

4. Waislamu wote ni ndugu. Kwa hiyo, wanapasa kupendana, kuoneana huruma, kuheshimiana, kutokuudhiana na kuoneana choyo n.k.

 

Rejea Al-Hujuraat (49: 10), Al-Fat-h (48: 29).

 

 

 

5. Ni wajibu wa Waislamu kuwasuluhisha waliokhasimikiana, kwani fadhila zake ni kuu na zimetajwa katika Qur-aan na Sunnah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

لَّا خَيْرَ فِي كَثِيرٍ مِّن نَّجْوَاهُمْ إِلَّا مَنْ أَمَرَ بِصَدَقَةٍ أَوْ مَعْرُوفٍ أَوْ إِصْلَاحٍ بَيْنَ النَّاسِ ۚ وَمَن يَفْعَلْ ذَٰلِكَ ابْتِغَاءَ مَرْضَاتِ اللَّـهِ فَسَوْفَ نُؤْتِيهِ أَجْرًا عَظِيمًا ﴿١١٤﴾

Hakuna khayr katika minong’ono yao mingi isipokuwa anayeamrisha swadaqah, au mema, au kusuluhisha baina ya watu. Na atakayefanya hivyo kutaka radhi za Allaah, basi Tutampa ujira adhimu. [An-Nisaa (4: 114)]

 

Rejea pia Al-Hujuraat (49: 10).

 

Na ni wajibu kwa waliokhasimikiana kusameheana, kwani kuna malipo mema.  

 

 

Share