099-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Kumhukumia Mtu Kuwa Hatoghufuriwa Dhambi Zake Ni Kuporomoka 'Amali Zake

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 99

 

Kumhukumia Mtu Kuwa Hatoghufuriwa Dhambi Zake Ni Kuporomoka ‘Amali

 

 

 

 

عَنْ جُنْدَبٍ بن عَبْدِ الله (رضي الله عنه) قَال: قَال رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((قَالَ رَجُلٌ:  وَاللَّهِ لاَ يَغْفِرُ اللَّهُ لِفُلاَنٍ. فَقَالَ اللهُ عَزَّ وّجّلَّ:  مَنْ ذَا الَّذِي يَتَأَلَّى عَلَيَّ أَنْ لاَ أَغْفِرَ لِفلاَنٍ؟  فَإِنِّي قَدْ غَفَرْتُ لِفلاَنٍ وَأَحْبَطْتُ عَمَلَكَ)) مسلم

Imepokelewa kutoka kwa Jundab bin ‘Abdillaah  (رضي الله عنه) ambaye amesema: “Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم ) amesema:  ((Mtu mmoja alisema: Wa-Allaahi! Allaah Hatomghufuria fulani! Allaah Aliyetukuka na Jalali Akasema: Ni nani huyo anayeniapia kuwa Sitomghufuria fulani? Mimi Nimeshamghufuria fulani na Nimeziporomosha ‘amali zako)). [Muslim]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Tahadharisho la kuapa viapo visivyokuwa vya kheri. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

  وَاحْفَظُوا أَيْمَانَكُمْ ۚ  

Na hifadhini yamini zenu.  [Al-Maaidah (5: 890]

 

 

 

2. Tisho la kuchukia Waislamu wengineo.

 

 

3. Bainisho la wasaa na Rahmah ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwamba Anamghufuria Amtakaye hata kama ana madhambi makubwa vipi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا ۚ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ﴿٥٣﴾

 Sema: Enyi waja Wangu ambao wamepindukia mipaka juu ya nafsi zao: “Msikate tamaa na rahmah ya Allaah; hakika Allaah Anaghufuria dhambi zote; hakika Yeye Ndiye Mwenye kughufuria, Mwenye kurehemu.” [Az-Zumar: 53]

        

Rejea pia:  Al-Araaf (7: 56),   Al-An’aam (6: 147).

 

 

4. Hakuna ajuaye hatima yake wala ya mwenziwe, hivyo haipasi kumhukumia mtu kuwa ana madhambi na kwamba hatoghufuriwa au kumtakasa mtu na kumtukuzia malipo yake.

 

 

5. Katazo la kuingilia hukmu ya Allaah (سبحانه وتعالى) inayomhusu Yeye Pekee, nayo ni ukosefu wa adabu kwa Allaah (سبحانه وتعالى).

 

 

6. Tahadharisho la kuporomoshwa ‘amali za mtu kwa kumhukumia mtu hatima yake.

 

 

7. Hakuna bin Aadam asiyekuwa na makosa kama alivyosema Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):

 

 ((كلُّ بني آدمَ خطَّاءٌ وخيرُ الخطَّائينَ التوَّابونَ))

((Kila bina Aadam ni mkosa,  lakini mbora kwa wale wenye kukosea ni wale wenye kutubia)) [Hadiyth ya Anas bin Maalik (رضي الله عنه) ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh Ibn Maajah (3447), Swahiyh Al-Jaami’ (4515)].

 

Na kumhukumia mtu maovu yake ni kujisahau mtu nafsi yake ni dalili ya mtu kujiona kuwa yeye ni mbora kuliko wenziwe.

 

 

 

Share