109-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Amelaaniwa Mla Ribaa, Mwakilishi Shahidi, Na Mwandishi Wake

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 109  

 

Amelaaniwa Mla Ribaa, Mwakilishi Shahidi, Na Mwandishi Wake

 

 

 

 

عَنْ إبنِ مَسْعُودٍ (رضي الله عنه) قَالَ: لَعَنَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ آكِلَ الرِّبَا وَمُؤْكِلَهُ مسلم. زاد الترمذي وغيره:  وَشَاهِدَيْه وَكَاتِبَهُ  

Imepokelewa kutoka kwa bin Mas’uwd (رضي الله عنه) amesema: “Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amemlaani mla ribaa na mwakilishi wake”. [Muslim, At-Tirmidhiy] Na At-Tirmidhiy na wengineo wameongeza: “… na mashahidi wake na mwandishi wake.”

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Haramisho la kula ribaa na tisho lake kuwa ni kupata laana ya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

 

2. Haramisho la ribaa limekemewa kwa hali ya juu kabisa hadi kwamba imetangazwa vita pamoja na Allaah na Rasuli Wake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

فَإِن لَّمْ تَفْعَلُوا فَأْذَنُوا بِحَرْبٍ مِّنَ اللَّـهِ وَرَسُولِهِ ۖ وَإِن تُبْتُمْ فَلَكُمْ رُءُوسُ أَمْوَالِكُمْ لَا تَظْلِمُونَ وَلَا تُظْلَمُونَ ﴿٢٧٩﴾

Na msipofanya basi tangazeni vita kutoka kwa Allaah na Rasuli Wake. Na mkitubu basi mtapata rasilimali zenu msidhulumu na wala msidhulumiwe. [Al-Baqarah (2: 279)]

 

Na hadi imekuwa Aayah hizo zinafuatia Aayah ya mwisho kuteremshwa kama walivyonukuu Ma’ulamaa wa Tafsiyr: 

 

 وَاتَّقُوا يَوْمًا تُرْجَعُونَ فِيهِ إِلَى اللَّـهِ ۖ ثُمَّ تُوَفَّىٰ كُلُّ نَفْسٍ مَّا كَسَبَتْ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ ﴿٢٨١﴾

Na iogopeni Siku mtakayorejeshwa ndani yake kwa Allaah, kisha kila nafsi italipwa kamilifu iliyoyachuma nao hawatodhulumiwa. [Al-Baqarah (2: 281)]

 

 

 

3. Kula ribaa ni miongoni mwa mambo saba yanayoangamiza.

 

Rejea Hadiyth namba (108).

 

 

4. Dhambi za ribaa zinamfikia sawasawa anayewakilisha, shahidi na mwandishi wake. Hii ni sawa na mwenye kutenda uzushi katika Dini kwamba akishirikiana na jambo la bid’ah, atapata dhambi sawa na aliyeanzisha. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

إِنَّا نَحْنُ نُحْيِي الْمَوْتَىٰ وَنَكْتُبُ مَا قَدَّمُوا وَآثَارَهُمْ ۚ وَكُلَّ شَيْءٍ أَحْصَيْنَاهُ فِي إِمَامٍ مُّبِينٍ ﴿١٢﴾

 Hakika Sisi Tunahuisha wafu, na Tunaandika yale waliyoyakadimisha na athari zao na kila kitu Tumekirekodi barabara katika daftari bayana. [Yaasiyn (36: 12)]

 

 

Rejea pia An-Nahl (16: 25).  

 

Rejea pia Hadiyth namba (16).

 

 

5. Muumin ajiepushe na shubuhaat (mambo yenye shaka, utata, tuhuma) ili aepukane na maasi kama haya, kwani kuna hatari ya kufuata matamanio na baadhi ya watu wanaotoa Fatwa zisizokubalika ki-Shari’ah.

 

Rejea Aal-Imraan (3: 7).

 

Rejea pia Hadiyth namba (64). 

 

 

6. Uislamu unazuia hatua zote za kufikisha maovu kwa kumzuia kila anayeshiriki katika ovu hilo.

 

 

Share