126-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Muumin Si Anayekashifu Watu, Au Kulaani, Kunena Machafu Au Mwenye Ufidhuli

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 126

 

Muumin Si Anayekashifu Watu, Au Kulaani, Kunena Machafu Au Mwenye Ufidhuli

 

 

 

 

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ ابْن مَسْعُودٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ:  ((لَيْسَ الْمُؤْمِنُ بِالطَّعَّانِ ولاَ اللَّعَّانِ وَلاَ الْفَاحِشِ وَلاَ الْبَذِيءِ)) رواه الترمذي وَقَالَ حَدِيثٌ حَسَنٌ   

 

Imepokelewa kutoka kwa ‘Abdullaahi bin Mas’uwd (رضي الله عنه) amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Muumin si yule anayekashifu watu, wala anayelaani sana, wala anayenena machafu, wala mfedhuli na mtovu wa adabu)). [At-Tirmidhiy na amesema: Hadiyth Hasan]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Ukamilisho na uthibitisho wa iymaan ya Muumin ni kutokuwa na sifa mbovu kama hizo za kukashifu, kulaani, kunena machafu na utovu wa adabu.

 

 

2. Uislamu unasisitiza tabia njema, kwani ni sababu kuu ya kuweko amani baina ya watu na inazuia ufisadi na mtafaruku.

 

 

 

3. Muumin anapaswa kuwa na tabia njema na kujiepusha na tabia ovu kama alivyotufunza Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) katika Hadiyth nyingi.

 

Rejea Hadiyth namba (21), (22), (23), (65), (67), (94), (95).

Naye ni kigezo bora kabisa kwetu kwa tabia na khulka zake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى) kumwambia Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم):

 

وَإِنَّكَ لَعَلَىٰ خُلُقٍ عَظِيمٍ﴿٤﴾

Na hakika wewe bila shaka una tabia adhimu. [Al-Qalam (68: 4)]

 

 

Rejea pia: Aal-‘Imraan (3: 159), At-Tawbah (9: 128).

 

Na inapaswa kumfuata. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 

 لَّقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّـهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِّمَن كَانَ يَرْجُو اللَّـهَ وَالْيَوْمَ الْآخِرَ وَذَكَرَ اللَّـهَ كَثِيرًا ﴿٢١﴾

Kwa yakini mna kigezo kizuri kwa Rasuli wa Allaah kwa mwenye kumtaraji Allaah na Siku ya Mwisho na akamdhukuru Allaah kwa wingi. [Al-Ahzaab (33: 21)]

 

 

 

4. Ulimi wa Muumin unapasa kutoa maneno mazuri daima na si maovu yanayompatia dhambi. Hadiyth kadhaa zimeonya kuhusu maovu ya ulimi.

 

Rejea Hadiyth namba (87), (88), (89), (93), (98).

 

 

 

5. Maneno maovu, kulaani, kukashifu n.k. ni miongoni mwa dhambi zinazohusiana na haki za watu, nazo Allaah (سبحانه وتعالى) Hazisamehi hadi aliyetendewa asamehe, au malipo ni Siku ya Hesabu kwa kuchukuliwa mema yake mtu na kutupiwa madhambi.

 

Rejea Hadiyth namba (19).

 

 

6. Maneno maovu na machafu ni ukosefu wa kuwa na haya jambo ambalo Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amelilinganisha na iymaan.

 

Rejea Hadiyth namba (69).

 

 

 

Share