05-Sifa Kumi Na Fadhila Zake: Wanaosubiri Wanaume Na Wanawake

 

Sifa Kumi Na Fadhila Zake

 

05 - Wanaosubiri Wanaume Na Wanawake  

 

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

إِنَّ الْمُسْلِمِينَ وَالْمُسْلِمَاتِ وَالْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ وَالْقَانِتِينَ وَالْقَانِتَاتِ وَالصَّادِقِينَ وَالصَّادِقَاتِ وَالصَّابِرِينَ وَالصَّابِرَاتِ 

 

Hakika Waislamu wanaume na wanawake, na Waumini wanaume na wanawake, na watiifu wanaume na wanawake, na wasemao kweli wanaume na wanawake, na wanaosubiri wanaume na wanawake, [Ahzaab: 35]

 

 

Sifa ya tano ni wanaosubiri wanaume na wanawake.   Fadhila za subira zimetajwa tele katika Qur-aan na Sunnah.  

 

Aina za subira:

 

 

1. Subira katika utiifu.

 

‘Ibaadah zinahitaji subira; kama Swalaah inahitajia unyenyekevu ambao haupatikani bila ya kuwa na subira kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

وَاسْتَعِينُوا بِالصَّبْرِ وَالصَّلَاةِ ۚ وَإِنَّهَا لَكَبِيرَةٌ إِلَّا عَلَى الْخَاشِعِينَ ﴿٤٥﴾

Na tafuteni msaada kupitia subira na Swalaah; na hakika hilo ni kubwa isipokuwa kwa wanyenyekevu. [Al-Baqarah: 45]

 

Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَعِينُوا بِالصَّبْرِ وَالصَّلَاةِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ مَعَ الصَّابِرِينَ ﴿١٥٣﴾

Enyi walioamini! Tafuteni msaada kwa subira na Swalaah; hakika Allaah Yu pamoja na wanaosubiri. [Al-Baqarah: 153]   

 

 

Swawm pia inahitajia subira kukaa na njaa na kiu na kujizuia na matamanio ya nafsi.

 

Zakaah hali kadhalika inahitajia subira kwa sababu inahitaji azimio la nguvu mtu kuitoa mali yake.

 

Hajj nayo inahitajia subira kutokana na mashaka yanayotokana na safari hii na kutekeleza taratibu za Hajj.

 

 

 

2.Subira katika kujiepusha na maasi:

 

Nayo ni kufanya jihaad ya nafsi kuzuia matamanio maovu. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

 

..أيُّ الْهِجْرَةِ أَفْضَلُ، قَالَ: ((أَنْ تَهْجُرَ مَا كَرِهَ رَبُّكَ))

Hijrah gani iliyokuwa bora zaidi? Akasema: ((Ni kuhama yale Anayochukia Rabb wako)) [Swahiyh An-Nasaaiy 4176]

 

Mfano mwenye kupenda sana muziki, ambapo mara nyingi shaytwaan katika jambo hili humfanyia binaadamu liwe gumu kabisa kwake kuliepuka, kwani anaweza Muislamu kuacha maasi mengine makubwa lakini inapofika kutaka kuacha nyimbo (muziki) huwa ni jambo zito, kwa vile wengi wanafikiri kuwa nyimbo si maasi makubwa na hali Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amekataza katika Qur-aan Anaposema:

 

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَشْتَرِي لَهْوَ الْحَدِيثِ لِيُضِلَّ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ بِغَيْرِ عِلْمٍ وَيَتَّخِذَهَا هُزُوًا ۚ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ مُّهِينٌ﴿٦﴾

Na miongoni mwa watu yuko ambaye hununua maneno ya upuuzi ili apoteze (watu) njia ya Allaah bila elimu, na huichukulia mzaha. Hao watapata adhabu ya kudhalilisha. [Luqmaan: 6]

 

 

Ibn Mas'uwd (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema kuhusu   Aayah hii: "Naapa kwa Allaah hii ina maana ni nyimbo" [At-Twabariy 20:127]

 

 

3. Subira katika da’wah (kulingania).

 

 

Hii ni kazi ngumu kabisa ambayo mitihani yake imewasibu Rusuli wa Allaah.

 

Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), naye pia alipata maudhi makubwa ya kutukanwa, kupigwa na kutengwa, na ndipo kila mara Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alikuwa akimkumbusha kuwa si pekee mwenye kupata misukosuko ya watu, bali Rusuli wenzake pia wamepitia maudhi na Akimsimulia visa vya Manabii na Rusuli katika Qur-aan.

 

Kazi ya da’wah (kulingania) inapasa pia itekelezwe na watu wa Ummah huu. Na pindi mtu akianza da’wah basi akaye tayari kupata maudhi na avute subra.  Luqmaan alimnasihi mwanawe:

 

يَا بُنَيَّ أَقِمِ الصَّلَاةَ وَأْمُرْ بِالْمَعْرُوفِ وَانْهَ عَنِ الْمُنكَرِ وَاصْبِرْ عَلَىٰ مَا أَصَابَكَ ۖ إِنَّ ذَٰلِكَ مِنْ عَزْمِ الْأُمُورِ ﴿١٧﴾

 “Ee mwanangu! Simamisha Swalaah, na amrisha mema na kataza ya munkari, na subiri juu ya yale yatakayokusibu. Hakika hayo ni katika mambo ya kuazimiwa. [Luqmaan: 17]

 

 

 Na Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَالْعَصْرِ ﴿١﴾

Naapa kwa Al-‘Aswr (zama).

 

إِنَّ الْإِنسَانَ لَفِي خُسْرٍ ﴿٢﴾

Hakika mwana wa Aadam bila shaka yumo katika khasara.

 

إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَتَوَاصَوْا بِالْحَقِّ وَتَوَاصَوْا بِالصَّبْرِ ﴿٣﴾

Isipokuwa wale walioamini na wakatenda mema na wakausiana haki na wakausiana subira. [Al-'Aswr: 1-3]

 

 

 

4-Subira katika maafa, misiba na kadhalika:

 

Maafa, madhara, misiba mbali mbali inahitaji subira na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amewabashiria wenye kusubiri kupata fadhila zake Anaposema: 

 

 

وَلَنَبْلُوَنَّكُم بِشَيْءٍ مِّنَ الْخَوْفِ وَالْجُوعِ وَنَقْصٍ مِّنَ الْأَمْوَالِ وَالْأَنفُسِ وَالثَّمَرَاتِ ۗ وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ ﴿١٥٥﴾

Na bila shaka Tutakujaribuni kwa kitu katika khofu na njaa na upungufu wa mali na nafsi na mazao. Na wabashirie wenye kusubiri.

 

الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ﴿١٥٦﴾

Wale ambao unapowafika msiba husema: “Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea.”

 

أُولَـٰئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ ﴿١٥٧﴾

Hao zitakuwa juu yao Barakah kutoka kwa Rabb wao na rahmah, na hao ndio wenye kuongoka. [Al-Baqarah: 155-157]

  

 

Vile vile Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Huwapa waja Wake wema wenye kuvuta subira ujira mwingi usiohesabika kama Anavyosema: 

 

إِنَّمَا يُوَفَّى الصَّابِرُونَ أَجْرَهُم بِغَيْرِ حِسَابٍ ﴿١٠﴾

Hakika wanaosubiri watalipwa kikamilifu ujira wao bila ya hesabu. [Az-Zumar: 10]

 

 

Na Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametuelezea fadhila za subira vile vile katika Hadiyth nyingi, chache ni kama zifuatazo:

 

 

عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ قال : قال رسول اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ : ((مَنْ يَتَصَبَّرْ يُصَبِّرْهُ اللَّهُ، وَمَا أُعْطِيَ أَحَدٌ عَطَاءً خَيْرًا وَأَوْسَعَ مِنْ الصَّبْر))  البخاري ومسلم

    

Kutoka kwa Abuu Sa'iyd Al-Khudriyyih (Radhwiya Allaah 'anhu) kwamba, amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam: ((Atakayetaka kusubiri (kufanya subira) basi Allaah Atampa subira. Na hakupewa mtu jambo la kheri na pana kama subira)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 Pia:

 

عَنْ أُمِّ سَلَمَةَ رضي الله عنها أَنَّهَا قَالَتْ : سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُول((مَا مِنْ مُسْلِمٍ تُصِيبُهُ مُصِيبَةٌ فَيَقُولُ مَا أَمَرَهُ اللَّهُ " إِنَّا لِلَّهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ ، اللَّهُمَّ أْجُرْنِي فِي مُصِيبَتِي وَأَخْلِفْ لِي خَيْرًا مِنْهَا " إِلا أَخْلَفَ اللَّهُ لَهُ خَيْرًا مِنْهَا)) روى مسلم

  

Imetoka kwa Ummu Salamah (Radhwiya Allahu 'anhaa) ambaye amesema: Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Muislamu yeyote atakayepatwa na msiba akasema yale aliyoamrisha na Allaah:

إِنَّا لِلَّهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ ، اللَّهُمَّ أْجُرْنِي فِي مُصِيبَتِي وَأَخْلِفْ لِي خَيْرًا مِنْهَا

 

 Sisi ni wa Allah nasi Kwake tutarejea. Ee Allaah Nipe ujira katika msiba wangu na nibadilishie ulio bora kuliko huo."

Basi Allaah Atampa ulio na kheri kuliko huo [msiba])) [Muslim]

 

 

Katika waja wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) waliokuwa na subira ya ajabu ni Nabiy Ayyuwb ('Alayhis-salaam) pindi aliposibiwa na kupoteza mali, na kupatwa na maradhi na kufariki watoto wake wote akavuta subra miaka mingi mpaka Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akamfariji.

 

 

Kisa Cha Subira Ya Swahaabiyyah Al-Khansaa:  

 

Jina lake hasa ni Tamaadhwur Bint 'Amru bin Ash-Shariyd bin Rabaah As-Sulaymiyyah. Alijulikana kwa jina la Al-Khansaa  na vile vile  Umm Ash-Shuhadaa (mama wa Shuhadaa) kutokana na watoto wake waliofariki katika jihaad. Pia alijulikana kuwa ni mwanamke mwenye haiba nzuri iliyojaa fadhila, tabia njema njema, ushujaa na subira kubwa.

 

Alipokuwa katika ujaahiliyyah (kabla ya Uislaam), alikuwa akitunga mashairi ya beti mbili tatu hadi walipofariki kaka zake Mu'aawiyah na Swakhar bin 'Amru, alifikwa na huzuni kubwa sana hata akawatungia mashairi. Mashairi hayo yakawa maarufu, naye akawa mashuhuri. Inavyosemekana hakuweko mwanamke aliyekuwa hodari wa mashairi kama yeye.

 

Baada ya vifo vya kaka zake, alikuja kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na watu wake wa Bani Sulaym akasilimu.

 

Ilipofika wakati wa vita vya Qaadisiyyah alidhihirisha subira yake kubwa alipokwenda vitani pamoja na watoto wake wanne wa kiume na akawausia kwa kuwaambia maneno yafuatayo:

 

"Enyi watoto wangu, naapa kwa Yule Ambaye hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye, nyinyi ni watoto wa baba mmoja, sikumkhini baba yenu, mmesilimu kwa kutii, mmehajiri kwa khiari yenu…" hadi akasema "Mtakapoamka kesho In Sha-Allaah kwa salama, nendeni vitani kupigana na adui zenu, kwani mnajua Aliyowaandalia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ya thawabu nyingi kwa kupigana na makafiri. Tambueni kuwa nyumba ya milele (Jannah) ni bora kuliko nyumba ya kutoweka (Dunia), Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اصْبِرُوا وَصَابِرُوا وَرَابِطُوا وَاتَّقُوا اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٢٠٠﴾

Enyi walioamini! Subirini na zidini kuvuta subira na bakieni imara na mcheni Allaah ili mpate kufaulu. [Al-'Imraan: 200].

 

 

Wakaenda vitani na alipopata habari ya vifo vyao wote alisema: "AlhamduLLaah kwa Yule Aliyenipa heshima ya kuuliwa kwao (wanangu) na namuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Aniunganishe nao kwa Rahma Zake".

 

Al-Khansaa (Radhwiya Allaahu 'anhaa) alifariki katika Ukhalifa wa 'Uthmaan bin 'Affaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu).

 

Share