06-Tawbah Hukmu Na Fadhila Zake: Allaah Anampenda Mja Anayeomba Tawbah

Tawbah Hukmu Na Fadhila Zake

 

06-Allaah Anampenda Mja Anayeomba Tawbah

 

 

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ التَّوَّابِينَ وَيُحِبُّ الْمُتَطَهِّرِينَ ﴿٢٢٢﴾

Hakika Allaah Anapenda wenye kutubia na Anapenda wenye kujitwaharisha. [Al-Baqarah: 222]

 

 

Tusome Kisa hiki kidogo kilichoelezewa katika Hadiyth Swahiyh:

 

 عن أَنَسُ بْنُ مَالِكٍ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم: ((الَلَّهُ أَشَدُّ فَرَحًا بِتَوْبَةِ عَبْدِهِ حِينَ يَتُوبُ إِلَيْهِ مِنْ أَحَدِكُمْ كَانَ عَلَى رَاحِلَتِهِ بِأَرْضِ فَلاَةٍ فَانْفَلَتَتْ مِنْهُ وَعَلَيْهَا طَعَامُهُ وَشَرَابُهُ فَأَيِسَ مِنْهَا فَأَتَى شَجَرَةً فَاضْطَجَعَ فِي ظِلِّهَا قَدْ أَيِسَ مِنْ رَاحِلَتِهِ فَبَيْنَا هُوَ كَذَلِكَ إِذَا هُوَ بِهَا قَائِمَةً عِنْدَهُ فَأَخَذَ بِخِطَامِهَا ثُمَّ قَالَ مِنْ شِدَّةِ الْفَرَحِ: "اللَّهُمَّ أَنْتَ عَبْدِي وَأَنَا رَبُّكَ" ‏ أَخْطَأَ مِنْ شِدَّةِ الْفَرَحِ)) مسلم

Amesimulia Anas (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: Allaah Hufurahikiwa mno na tawbah ya mja Wake wakati anapotubia Kwake kuliko furaha ya mmoja wenu aliyekuwa amempanda mnyama wake kwenye jangwa (la joto kali hakuna mtu), kisha mnyama huyo aliyebeba chakula chake na maji yake akampotea, na akakata tamaa kabisa ya kumpata tena. Akaenda kwenye mti, akalala chali ya kivuli chake huku akiwa amekata tamaa kabisa ya kumpata tena mnyama wake. Akiwa katika hali hiyo (ya kutojua nini la kufanya), mara anashtuka kumwona huyo amesimama mbele yake, akaikamata hatamu yake, na kwa ile furaha akasema:  "Ee Allaah, Wewe ni mja wangu na mimi ni Rabb wako.” Alikosea (kumshukuru Rabb wake) kwa wingi wa furaha aliyokuwa nayo.” [Muslim]

 

 

Vile vile Hadiyth Al-Qudsiy ifuatayo inatuonyesha vipi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alivyo Mpole na Mwenye Rahmah nyingi kiasi cha kwamba yuko tayari kupokea tawbah zetu hata dhambi zikiwa na ukubwa gani.  

 

 عن أَنَسُ بْنُ مَالِكٍ قَالَ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ: ((قَالَ اللَّهُ تَبَارَكَ وَتَعَالَى يَا ابْنَ آدَمَ،  إِنَّكَ مَا دَعَوْتَنِي وَرَجَوْتَنِي غَفَرْتُ لَكَ عَلَى مَا كَانَ فِيكَ وَلَا أُبَالِي، يَا ابْنَ آدَمَ لَوْ بَلَغَتْ ذُنُوبُكَ عَنَانَ السَّمَاءِ ثُمَّ اسْتَغْفَرْتَنِي غَفَرْتُ لَكَ وَلَا أُبَالِي، يَا ابْنَ آدَمَ إِنَّكَ لَوْ أَتَيْتَنِي بِقُرَابِ الْأَرْضِ خَطَايَا ثُمَّ لَقِيتَنِي لَا تُشْرِكُ بِي شَيْئًا لَأَتَيْتُكَ بِقُرَابِهَا مَغْفِرَةً))  أخرجه الترمذي وحسنه الألباني في الصحيحة  

Anas (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia kwamba: Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “Allaah Tabaaraka wa Ta’aalaa  Amesema: Ee bin-Aadam! Hakika ukiniomba na ukanitaraji (kwa malipo) Nitakughufuria yale yote uliyonayo na wala Sijali, Ee bin-Aadam! Lau zingefikia dhambi zako ukubwa wa mbingu, kisha ukaniomba maghfirah, Ningekughufuria bila ya kujali (kiasi cha madhambi uliyoyafanya). Ee bin-Aadam! Hakika ungenijia na madhambi yakaribiayo ukubwa wa ardhi, kisha ukakutana nami na hali hukunishirikisha chochote, basi Nami Nitakujia na maghfirah yanayolinga nayo.” [At-Tirmidhiy na Shaykh Al-Albaaniy kaipa daraja ya Hasan]

 

Na Hadiyth ifuatayo pia inazidi kutuonyesha uvumilvu na upole wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwamba hata kama mja anarudia kufanya dhambi, madamu tu anarudi kwa Rabb wake kila mara kutubia, basi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Humghufuria:

 

 عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فِيمَا يَحْكِي عَنْ رَبِّهِ عَزَّ وَجَلَّ قَالَ: ((أَذْنَبَ عَبْدٌ ذَنْبًا فَقَالَ: اللَّهُمَّ اغْفِرْ لِي ذَنْبِي،  فَقَالَ تَبَارَكَ وَتَعَالَى:  أَذْنَبَ عَبْدِي ذَنْبًا فَعَلِمَ أَنَّ لَهُ رَبًّا يَغْفِرُ الذَّنْبَ وَيَأْخُذُ بِالذَّنْبِ ثُمَّ عَادَ فَأَذْنَبَ فَقَالَ:  أَيْ رَبِّ اغْفِرْ لِي ذَنْبِي،  فَقَالَ تَبَارَكَ وَتَعَالَى: عَبْدِي أَذْنَبَ ذَنْبًا فَعَلِمَ أَنَّ لَهُ رَبًّا يَغْفِرُ الذَّنْبَ وَيَأْخُذُ بِالذَّنْبِ ثُمَّ عَادَ فَأَذْنَبَ فَقَالَ: أَيْ رَبِّ اغْفِرْ لِي ذَنْبِي،  فَقَالَ تَبَارَكَ وَتَعَالَى: أَذْنَبَ عَبْدِي ذَنْبًا فَعَلِمَ أَنَّ لَهُ رَبًّا يَغْفِرُ الذَّنْبَ وَيَأْخُذُ بِالذَّنْبِ. اعْمَلْ مَا شِئْتَ فَقَدْ غَفَرْتُ لَكَ)) البخاري و مسلم

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuhusu mambo aliyohadithia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kutoka kwa Rabb Wake (‘Azza wa Jalla) kwamba ((Mja wa Allaah alifanya dhambi na akasema: Ee Rabb nighufurie dhambi zangu. Na yeye Allaah (Tabaaraka wa Ta’aalaa) Akasema: Mja wangu kafanya dhambi kisha kajua kwamba anaye Rabb Ambaye Anaghufuria dhambi na Anayeadhibu kwa kufanya dhambi. Kisha akarudi tena kufanya dhambi akasema: Ee Rabb nighufurie dhambi zangu. Na yeye Allaah (Tabaaraka wa Ta’aalaa) Akasema: Mja wangu kafanya dhambi kisha kajua kwamba anaye Rabb Ambaye Anaghufuria dhambi na Anayeadhibu kwa kufanya dhambi. Kisha akarudia tena dhambi na akasema: Ee Rabb nighufurie dhambi zangu. Na yeye Allaah (Tabaaraka wa Ta’aalaa) Akasema: Mja wangu kafanya dhambi kisha kajua kwamba anaye Rabb Ambaye Anaghufuria dhambi na Anayeadhibu kwa kufanya dhambi. (Allaah Akasema): Fanya utakavyo, kwani Nimekughufuria)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

 

 

Share