Mapenzi Ya Kujionyesha

SWALI:

Assalaam alaykum

Swali: naomba munisaidie katika swali langu hili,nilipokuwa na mumewangu, kila nnapotaka kuwa karibu nae hunikwepa, kwa kujidai anaudhu. Lakini nilikuwa nikihisi akiona wasichana wetu wa kazi wanakuja yeye hutaka kunikaribia, kitu ambacho mie sikupenda kitendeke mbele ya mtu yeyote .aliwahi kuniambia kuwa wakija watu tuwaoneshe kuwa tunapendana, nikamwambia mimi siwezi kuonesha watu, kama kupendana tupendane bila ya kuonesha. Na mimi siwezi kufanya hivyo, kwani binaadam tumeumbwa na haya. Naomba mnifafanulie kama nimekosea katika kuwajibisha haki yake. Jazaakumu llaah kheir wanafaana waiyyakum

Wassalaam alaykum wa rahmatullah            

 


 

JIBU:

AlhamduliLlaah - Himdi Na Sifa Zote Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani dada yetu kwa swali lako zuri. Ni muhimu kuwa tuelewe kuwa maumbile ya mwanadamu ni kuona haya na kutoweza kufanya lolote ambalo linakwenda kinyume na ada za maumbile yake. Baina ya mume na mke, mwanamke ndiye mwenye hayaa zaidi katika suala la kufanya chochote mbele ya watu. Qur-aan inatueleza habari za yule binti wa yule mzee mkongwe mcha Mngu pindi alipokwenda kumchukua Nabii Muusa (‘Alayhis Salaam) alipotumwa na babake. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Basi akamjia mmoja wao katika wale wawili, anakwenda na huku anaona haya” (28: 25).

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) naye anatuambia: “Ikiwa huoni hayaa basi fanya unalotaka”. Amesema tena: “Hayaa ni sehemu ya Imani” (al-Bukhaariy). Na pia, “Hayaa haiji ila kwa kheri”.

Mapenzi baina ya mume na mke yanafanywa wakiwa peke yao chumbani sio mbele ya watu kabisa. Ndio kwa minajili hiyo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akakataza wanandoa kufichua wanayofanya wakiwa wawili. Ikiwa mapenzi hayapo huwezi kuyaleta kwa kuonyesha watu, kwani mapenzi baina ya wanandoa yanakuwa ndani ya vifua vyao kwa kusikitikiana, kupendana, kuoneana huruma, kuridhishana na kufanya tendo la ndoa bila kuonekana na watu.

Ni wazi kuwa mwanzo Allaah Aliyetukuka na Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wamekataza kabisa watu kufanya amali kwa kujionyesha (Riyaa). Kufanya Riyaa kunamfanya Muislamu awe atakuwa ni mwenye kupata adhabu Siku ya Qiyaamah, kwani huwa hafanyi kwa ajili ya Allaah Aliyetukuka.

Nasaha yetu kwako awali ya yote ni wewe kuweza kumuweka mumeo chini na kumueleza hayo kinaganaga bila kuficha kwa sababu hiyo si tabia ya Muislamu mwema wa kuanza kumshika mke wake wakiwa wapo watu mbele na ikiwa hapana mtu basi kumkimbia na kutotaka kabisa kuwa karibu naye. Hilo ulilofanya dada yetu ni sawa sawa kwani munkari (uovu) unafaa uondoshwe kwa mkono, ikiwa mtu hawezi kwa mkono, basi kwa mdomo na ukishindwa kabisa, basi ni kuchukia moyoni na huo ni udhaifu wa Imani.

Kufanya hivyo hujamkosea kabisa katika haki bali ni kumfundisha haki zake ambazo anafaa azifahamu na asiwe ni mwenye kuvuka mipaka iliyowekwa na Sharia. Tunaona kwa tatizo hilo itabidi ukae na mumeo na umueleze uhakika wa mambo namna Uislamu unavyomtaka yeye awe akiwa nawe kama mke wake.

Tunakutakia kila la kheri na tawfiki katika kumrekebisha mumeo. Tunamuomba Allaah Amuondolee mumeo riyaa na mushikamane katika ya kheri na kuachana na yaliyo maovu.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share