18-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Isti’aanah (Kuomba Msaada) Kwa Asiyekuwa Allaah

 

إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم

 

Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!

 

18- Isti’aanah (Kuomba Msaada) Kwa Asiyekuwa Allaah

Alhidaaya.com

 

 

 

 

Maana Ya Isti’aanah (kuomba msaada) na dalili zake:

 

Isti’aanah ni kuomba msaada. Na Isti’aanah kwa Allaah ni kuomba katika mambo ya Dini na ya dunia na inajumuisha mja kujidhalilisha kwa Mola wake na kuwa na yakini na kumtegemea Yeye (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Pekee kama Anavyosema:

فَاعْبُدْهُ وَتَوَكَّلْ عَلَيْهِ

basi mwabudu Yeye na tawakali Kwake. [Huwd: 123]

 

 

Na katika Suwratul-Faatihah ambayo inajumuisha aina zote za Tawhiyd, Muislamu anakariri katika Swalaah zake zote:

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ ﴿٥﴾

Wewe Pekee tunakuabudu na Wewe Pekee tunakuomba msaada. [Al-Faatihah: 5]

 

 

Kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

إِيَّاكَ نَعْبُدُ

Inathibitisha Tawhiyd ya Uluwhiyyah (kumpwekesha Allaah katika kumwabudu); yaani aina zote za ‘ibaadah zinahitaji kuelekezwa Kwake Pekee Subhaanahu wa Ta’aala.

 

Na

وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ 

Inathibitisha Tawhiyd ya Ar-Rubuwbiyyah (kumpwekesha Allaah katika Uola) kwa sababu ni kuomba msaada kwa Ar-Rabb (Mola) Ambaye ni Al-Khaaliq (Muumbaji), Ar-Raaziq (Mtoaji rizki), Al-Mudabbir (Mwendeshaji mambo), Al-Maalik (Mwenye kumiliki) Ambaye mambo yote yamo Mikononi Mwake. Kwa hiyo anapaswa Yeye kuombwa mahitaji yetu kama vile Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alivyomuusia Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) ambaye amehadithia:

 

كُنْتُ خَلْفَ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم يًوْماً، فقال: ((يا غُلامُ، إنِّي أُعَلِّمُكَ كلِماتٍ: احْفَظِ اللهَ يَحْفَظْكَ، احْفَظِ اللهَ تَجِدْهُ تُجاهَك، إذا سأَلْتَ فاسْأَلِ اللهَ، وإذا اسْتَعنْتَ فاسْتَعِنْ باللهِ، واعْلَمْ أنَّ الأُمَّة  لَوِ اجْتَمَعَتْ على أَنْ يَنْفَعُـوكَ بِشَيءٍ لَمْ يَنْفَعُوكَ إلا بِشَيْءٍ قدْ كَتَبَهُ اللهُ لَكَ، وإن اجْتَمَعُوا على أن يَضُرَّوكَ بِشيءٍ لَمْ يَضُروكَ إلا بِشَيءٍ قَدْ كَتَبهُ اللهُ عَلَيْكَ، رُفِعَتِ الأقْلامُ وَجَفَّتِ الصُّحُفُ))

Siku moja nilikuwa nyuma ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaniambia: “Ee kijana! nitakufundisha maneno (ya kufaa); Mhifadhi Allaah (fuata maamrisho Yake na chunga mipaka Yake) Atakuhifadhi.  Muhifadhi Allaah utamkuta mbele yako. Ukiomba, muombe Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), ukitafuta msaada tafuta kwa Allaah. Tambua kwamba ikiwa ummah mzima utaungana kukunufaisha wewe kwa kitu, basi hutonufaika ila tu kwa kile Alichokwishakuandikia Allaah. Na wakikusanyika kukudhuru kwa chochote, hutodhurika ila tu kwa kile Allaah Alichokwishakukuandikia (kuwa kitakudhuru), kwani kalamu zimeshanyanyuliwa (kila kitu kishaandikwa) na swahifa zimeshakauka.” [At-Tirmidhiy, na amesema Hadiyth Hasan Swahiyh]

 

Kumuomba bin-Aadam msaada wa jambo ambalo limo katika uwezo wake inafaa kwa dalili zifuatazo katika Qur-aan na Sunnah:

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَىٰ ۖ وَلَا تَعَاوَنُوا عَلَى الْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ

Na shirikianeni katika wema na taqwa, na wala msishirikiane katika dhambi na uadui. [Al-Maaidah: 2]

 

Na Hadiyth ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

عن أبي هُرَيْرَة رضي اللهُ عنه، عن النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم قال:  "مَنْ نَفَّسَ عَنْ مُؤمِنٍ كُرْبَةً مِنْ كُرَبِ الدُّنْيا نَفَّسَ اللهُ عَنْهُ كُرْبَةً من كُرَبِ يوْمِ القيامَةِ، ومَنْ يَسَّرَ على مُعْسِرٍ يَسَّرَ اللهُ عليه في الدنْيا والآخِرَةِ، وَمَنْ سَتَرَ مُسْلِماً سَتَرَهُ الله في الدُّنْيا والآخِرَةِ  واللهُ في عَوْنِ الْعَبْدِ ما كانَ الْعَبْدُ في عَونِ أخيهِ"  

Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Yeyote atakayemuondoshea shida ya kidunia Muislamu mwenzake, Allaah Atamuondoshea moja katika shida za Siku ya Qiyaamah. Na yeyote yule atakayemsaidia muhitaji (maskini) Allaah Atamsaidia haja zake hapa duniani na Aakhirah. Na yeyote yule atakayemsitiri Muislamu, Allaah Atamsitiri hapa duniani na Aakhirah. Allaah Humsaidia mja wake wakati wote madamu mja (huyo) yungali anamsaidia nduguye (Muislamu).” [Muslim]

 

Pia,   

 

عَنْ عَبْدِ الله بنِ عُمَرَ رَضِيَ الله عَنْهُما، أَنَّ النَّبِيَ صَلَّى الله عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: "أَحَبُّ النَّاسِ إِلَى الله أَنْفَعُهُمْ لِلّنَاسِ، وَأَحَبُّ الأَعْمَالِ إِلَى الله سُرُورٌ تُدْخِلُهُ عَلَى مُسْلِمٍ  أَوْ تَكْشِفُ عَنْهُ كُرْبَةً  أَوْ تَقْضِيَ عَنْهُ دَيْناً أَوْ تَطْرُدُ عَنْهُ جُوعاً، وَلأَنْ أَمْشِيَ مَعَ أَخِي المُسْلِمِ فِي حَاجَةٍ أَحَبُّ إِلَيَّ مِنْ أَنْ أَعْتَكِفَ فِى هَذَا المَسْجِدِ يعني مسجدَ المدينةِ شهرًا، وَمَنْ كَفَّ غَضَبَهُ سَتَرَ اللهُ عَوْرَتَه وَمَنْ كَظَمَ غَيْظَهُ وَلَوْ شَاءَ أَنْ يُمْضِيَه أَمْضَاهُ مَلأَ اللهُ قَلْبَهُ رَجاءً يَوْمَ القِيَامَةِ وَمَنْ مَشَى مَعَ أَخِيهِ المُسْلِمِ فِى حَاجَةٍ حَتَّى تَتَهَيَّأَ لَهُ أَثْبَتَ اللهُ قَدَمَهُ يَوْمَ تَزِلُّ الأَقْدَامُ وَإِنَّ سُوءَ الخُلُقِ لَيُفْسِدُ العَمَلَ كَمَا يُفْسِدُ الخلُّ العَسَلَ"

‘Abdullaah bin ‘Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Mtu ambaye ni kipenzi kabisa kwa Allaah ni yule ambaye ni mbora kabisa katika kunufaisha wenziwe. Na ‘amali zilizokuwa kipenzi kabisa kwa Allaah ('Azza wa Jalla) ni furaha aingizayo kwa Muislamu, au kumuondoshea shida, au kumtimizia deni lake, au kumuondoshea njaa. Na hakika mimi kwenda kumtimizia ndugu yangu haja yake, ni kipenzi kwangu kuliko nikae I’tikaaf (kijifunga katika ‘ibaadah Msikitini) mwezi mzima katika Masjid hii (Masjid Nabawiy). Na atakayeacha ghadhabu zake, basi Allaah Atamsitiri aibu zake. Na atakayezuia ghaydhi (ghadhabu na huzuni moyoni) zake japokuwa haogopi kuzionyesha, lakini anazuia, Allaah Atamjaza moyo wake kwa matumaini Siku ya Qiyaamah. Na atakayetembea na nduguye katika kumtimizia haja mpaka akamsaidia kikamlifu basi Allaah Atamthibitisha miguuu yake Siku ambayo miguu haitothibitika. Hakika khulqu (tabia) mbaya inaharibu ‘amali kama vile siki inavyoharibu asali.” [As-Silsilah Asw-Swahiyhah (906)]

 

Mifano ya mtu kumuomba bin-Aadam mwenziwe;

 

“Ee fulani! Nakuomba unisaidie kunilipia deni langu!”

 

“Ee fulani! Nakuomba unisaidie kunilipia gharama za matibabu ili nitibiwe!”

 

Au kuomba msaada wa mtu kumsimamia kazi yake, kumpatia anachohitaji katika matumizi, au kuomba kushirikiana katika ‘amali za khayr, au kuomba kusaidia jambo lolote la khayr ambalo litampatia thawabu kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa kumfanyia wema mwenziwe kama ilivyothibiti katika Hadiyth zilizotangulia.

 

Ama kuomba jambo ambalo halimo katika uwezo wa ki-bin-Aadam hapo huwa ni shirki. Mfano mtu kumuomba mtu amsaidie kupata kizazi, au kumwendea mtabiri amsaidie kumtazamia mambo ya ghayb, au mchawi kumuomba amfanye awe tajiri, au kuwaomba msaada wa riziki walio kaburini au kuwaomba wawaondoshee maradhi n.k.

 

Hizo ni aina za ‘ibaadah zipasazo kuelekezwa kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Pekee, kwa hiyo, 'Ibaadah kuielekeza kwa mwengine ni shirki kubwa kabisa kwa sababu ni kumshirikisha Allaah na viumbe Vyake katika mambo ambayo ni Allaah ('Azza wa Jalla) Pekee Mwenye uwezo nayo. Na shirki hii inamtoa mtu nje ya Uislamu kwa dalili kauli ya Allaah (Subahaanahu wa Ta’aalaa):

 

وَمَن يَدْعُ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ لَا بُرْهَانَ لَهُ بِهِ فَإِنَّمَا حِسَابُهُ عِندَ رَبِّهِ ۚ إِنَّهُ لَا يُفْلِحُ الْكَافِرُونَ ﴿١١٧﴾

 

Na yeyote yule anayeomba du’aa (au kuabudu) pamoja na Allaah muabudiwa mwengine hana ushahidi wa wazi wa hilo; basi hakika hesabu yake iko kwa Rabb wake. Hakika hawafaulu makafiri. [Al-Muuminuwn: 117]

 

 

Ilhali Allaah ('Azza wa Jalla) Ametuamrisha tumuombe Yeye Pekee kama Anavyosema:

 

وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ ۖ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ ۖ فَلْيَسْتَجِيبُوا لِي وَلْيُؤْمِنُوا بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ﴿١٨٦﴾

Na watakapokuuliza waja Wangu kuhusu Mimi, basi Mimi ni Niko karibu (kwa ujuzi); Naitikia du’aa ya muombaji anaponiomba. Basi waniitikie Mimi na waniamini Mimi, wapate kuongoka. [Al-Baqarah: 186]

 

 

Na Yeye Allaah ('Azza wa Jalla) Ndiye Mwenye kumuondoshea mtu dhiki zake Anapoombwa Yeye Pekee bila ya kumshirikisha, Anasema Allaah (Subahaanahu wa Ta’aalaa):

 

أَمَّن يُجِيبُ الْمُضْطَرَّ إِذَا دَعَاهُ وَيَكْشِفُ السُّوءَ وَيَجْعَلُكُمْ خُلَفَاءَ الْأَرْضِ ۗ أَإِلَـٰهٌ مَّعَ اللَّـهِ ۚ قَلِيلًا مَّا تَذَكَّرُونَ ﴿٦٢﴾

Au nani Anayemuitika mwenye dhiki mno anapomwomba, na Akamuondoshea ouvu na Akakufanyeni makhalifa wa ardhi? Je, yuko mwabudiwa pamoja na Allaah? Ni machache mno mnayokumbuka. [An-Naml: 62]

 

Na pia Akamuamrisha Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kumpwekesha na kutokumshirikisha na kwamba hata yeye Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hana uwezo wa kumnufaisha mtu wala kumdhuru wala kumjaalia hidaaya:

 

قُلْ إِنَّمَا أَدْعُو رَبِّي وَلَا أُشْرِكُ بِهِ أَحَدًا﴿٢٠﴾

Sema: (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Hakika mimi namuomba Rabb wangu na wala simshirikishi na yeyote.”

 

 

قُلْ إِنِّي لَا أَمْلِكُ لَكُمْ ضَرًّا وَلَا رَشَدًا﴿٢١﴾

Sema: “Hakika mimi sikumilikieni dhara na wala uongofu.” [Al-Jinn: 20-21]

 

Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 وَلَا تَدْعُ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَنفَعُكَ وَلَا يَضُرُّكَ ۖ فَإِن فَعَلْتَ فَإِنَّكَ إِذًا مِّنَ الظَّالِمِينَ﴿١٠٦﴾

Na wala usiombe badala ya Allaah visivyokufaa wala visivyokudhuru. Na ukifanya, basi hakika utakuwa miongoni mwa madhalimu.

 

 

وَإِن يَمْسَسْكَ اللَّـهُ بِضُرٍّ فَلَا كَاشِفَ لَهُ إِلَّا هُوَ ۖ وَإِن يُرِدْكَ بِخَيْرٍ فَلَا رَادَّ لِفَضْلِهِ ۚ يُصِيبُ بِهِ مَن يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ ۚوَهُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ﴿١٠٧﴾

Na Allaah Akikugusisha dhara, basi hakuna wa kuiondosha isipokuwa Yeye. Na Akikutakia kheri, basi hakuna wa kurudisha fadhila Zake, Anasababisha kumfikia kwayo (fadhila Yake) Amtakaye katika waja Wake. Naye ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [Yuwnus: 106-107]

 

 

Na maharamsho mengineyo mengi yanapatikana katika Qur-aan:

 

إِنَّ الَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ عِبَادٌ أَمْثَالُكُمْ ۖ فَادْعُوهُمْ فَلْيَسْتَجِيبُوا لَكُمْ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ﴿١٩٤﴾

Hakika wale mnaowaomba badala ya Allaah ni waja kama nyinyi. Hebu waiteni wakuitikieni ikiwa nyinyi ni wakweli. [Al-A’raaf: 194]

 

 

Wale ambao wanaombwa, hawawezi kujiondoshea wenyewe madhara wala kujinufaisha Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

قُلِ ادْعُوا الَّذِينَ زَعَمْتُم مِّن دُونِهِ فَلَا يَمْلِكُونَ كَشْفَ الضُّرِّ عَنكُمْ وَلَا تَحْوِيلًا ﴿٥٦﴾

Sema: “Iteni wale ambao mnadai (ni waabudiwa) pasi Naye, basi hawamiliki kukuondesheeni dhara na wala kuihamisha (kwa mwengine).” [Al-Israa: 56]

 

 

Na Anasema (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

قُلِ ادْعُوا الَّذِينَ زَعَمْتُم مِّن دُونِ اللَّـهِ ۖ لَا يَمْلِكُونَ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ فِي السَّمَاوَاتِ وَلَا فِي الْأَرْضِ وَمَا لَهُمْ فِيهِمَا مِن شِرْكٍ وَمَا لَهُ مِنْهُم مِّن ظَهِيرٍ ﴿٢٢﴾

Sema: “Ombeni wale mnaodai kwa dhana (ni waabudiwa) badala ya Allaah, hawamiliki hata uzito wa sisimizi mbinguni wala ardhini, na wala hawana humo ushirika Naye, na wala Yeye (Allaah) Hana msaidizi miongoni mwao.” [Sabaa: 22]

 

 

Hakuna anachokipata yule ambaye anamshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) isipokuwa ni khasara duniani na Aakhirah na kujiweka katika upotofu:

 

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَعْبُدُ اللَّـهَ عَلَىٰ حَرْفٍ ۖ فَإِنْ أَصَابَهُ خَيْرٌ اطْمَأَنَّ بِهِ ۖ وَإِنْ أَصَابَتْهُ فِتْنَةٌ انقَلَبَ عَلَىٰ وَجْهِهِ خَسِرَ الدُّنْيَا وَالْآخِرَةَ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الْخُسْرَانُ الْمُبِينُ ﴿١١﴾

Na miongoni mwa watu yuko anayemwabudu Allaah ukingoni. Inapompata kheri, hutumainika kwayo; Na inapompata mtihani hugeuka nyuma juu ya uso wake (kurudia kufru). Amekhasirika duniani na Aakhirah. Hiyo ndiyo khasara bayana.

 

 

يَدْعُو مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَضُرُّهُ وَمَا لَا يَنفَعُهُ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الضَّلَالُ الْبَعِيدُ ﴿١٢﴾

Humwomba badala ya Allaah ambavyo visivyomdhuru na wala visivyomnufaisha. Huo ndio upotofu wa mbali.

 

يَدْعُو لَمَن ضَرُّهُ أَقْرَبُ مِن نَّفْعِهِ ۚ لَبِئْسَ الْمَوْلَىٰ وَلَبِئْسَ الْعَشِيرُ ﴿١٣﴾

Humwomba yule ambaye dhara yake iko karibu kuliko manufaa yake. Bila shaka ni mlinzi muovu kabisa, na bila shaka ni rafiki muovu kabisa. [Al-Hajj: 11-13]

 

 

Na Anasema pia (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَمَنْ أَضَلُّ مِمَّن يَدْعُو مِن دُونِ اللَّـهِ مَن لَّا يَسْتَجِيبُ لَهُ إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ وَهُمْ عَن دُعَائِهِمْ غَافِلُونَ﴿٥﴾

 “Na nani aliyepotoka zaidi kuliko ambaye anayeomba asiyekuwa Allaah ambaye hamuitikii mpaka Siku ya Qiyaamah; nao wala hawatambui  maombi yao.” [Al-Ahqaaf: 5]

 

 

 

Pia, maharamisho kadhaa katika Sunnah za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) yameshatangulizwa katika silsilah za maudhui hii ya “Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!”

 

 

 

Share