Inafaa Kununua Kitu Kilichoibiwa?


SWALI:

Je yafaa kununua kitu ambayo imeibiwa? na ni kama waihitaji hiyo kitu sana na huna uwezo wa kununua pia haifai?? 


 


 

JIBU:

 Sifa zote njema anastahiki Allah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum)  na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho


Haifai kununua kitu ambacho unajua kuwa kimeibiwa kwa sababu zifuatazo:

1)      Kwanza utakuwa unampa nguvu mwenye kuiba aendelee kuiba na kuuza vitu vya wizi na kupata chumo lisilo halali, hivyo kuacha kununua kwake itakuwa ni fundisho kwake. Na pia inakupasa kumnasihi aache kufanya hivyo maadam umejua kuwa amefanya makosa hayo.

2)      Kitu cha haramu huwa hakifai kutumika kwa vyovyote, ikiwa ni chakula au nguo au kitu chochote cha matumizi ya kila siku kwani Allaah سبحانه وتعالى Hapokei kitu chochote kibaya. Na pia huwa hapokelewi mtu du'aa zake kama anachuma chumo la haram au kula, kutumia na kufanyia kwa kile cha haram alivyosema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم :

  ( يا أيها الناس إن الله طيب لا يقبل إلا طيبا ، و إن الله أمر المتقين بما أمر به المرسلين فقال : ((يَا أَيُّهَا الرُّسُلُ كُلُوا مِنَ الطَّيِّبَاتِ وَاعْمَلُوا صَالِحًا إِنِّي بِمَا تَعْمَلُونَ عَلِيمٌ)) (المؤمنون 51)  و قال : ((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ كُلُواْ مِن طَيِّبَاتِ مَا رَزَقْنَاكُمْ ))  (البقرة 172)   ثم ذكر الرجل يطيل السفر أشعث أغبر يمد يديه إلى السماء يا رب يا رب و مطعمه حرام و مشربه حرام و غذي بالحرام فأنى يستجاب لذلك))    رواه مسلم    

Allah ni Mzuri na Hapokei ila kilicho kizuri. Na Allah Amewaamrisha wenye kumcha Mungu kama Alivyowaamrisha Mitume Aliposema: ((Enyi Mitume! Kuleni vyakula vizuri na tendeni mema. Hakika Mimi ni Mjuzi wa mnayoyatenda)) [Al-Muuminuun 51] Na Akasema: ((Enyi mlioamini! Kuleni vizuri Tulivyokuruzukuni )) [Al-Baqarah: 172] Kisha (Mtume صلى الله عليه وآله وسلم) akataja kisa cha mtu aliyekuwa safarini akiwa katika hali ya uchafu na mavumbi akiinua mikono yake mbinguni akiomba ((Ee Allaah, Ee Allaah, na hali chakula chake ni haram, kinywaji chake ni haram na kurutubika kwake Ni haram vipi atakubaliwa du'aa yake?)) [Muslim] 

Na tuchukue mifano mema ya kutoka kwa waja wema wa zamani ambayo ina mafundisho makubwa yenye kuzidisha iymaan na taqwa.

Inasemekana kuwa Imaam Abu Haniyfah alijizuia kula mbuzi kwa muda wa miaka ya kukisia umri anaoishi mbuzi tokea kuzaliwa hadi kufa, kwa sababu tu wakati huo aliibiwa mbuzi mjini na hakujulikana nani aliyemuiba au kujulikana huyo mbuzi ni yupi.

Wa Allaahu A'alam

 

Share