Kumsamehe Mume Aliyekudhulumu

 

SWALI:

Assalamu alykum warahmatu allahi wabarakatu.

Nataka kuanza kuwashukuru mwanzo ndugu zetu kwa kutupa website ambao inatufungua akili zetu nakutuburudisha nyoyo zetu.Allah awajaze kila la kheir inshallah.

Nataka kuwauliza swali kuhusu mswamaha.

Mimi nimeachika,katika ndoa yangu mimi nilijitahidi sana kimaisha kumuenua mume wangu lakini pindi alipojiona anaweza kusimama bila ya usaidizi wangu aliniwacha na kutafuta mke mwengine.Huyu mtalaka wangu mbele ya uso wangu naona kuwa amenidhulumu.Naamini ju ya qadar ya ALLAH (SWT),lakini sanyengine kama binadamu hunijia hasira sana,nikiona mambo yake yamemnyokea na yuko furahani,sio ati namuonea uhasidi bali najiuliza nafsi yangu lipi alolifanya yule bwana kupata furaha yote ambapo mimi amenidhulumu?Moyo wangu huwa mzito sana,kutaka kumsamehe wakati kama huwo.Ambapo tumeambiwa na mola wetu tuwasamehe wenzetu,lakini kama nilivyosema huja siku nyengine nikawa na hasira sana kwasababu yule mume hujigamba nakupita kunisema.Mimi sitaki kukosa subra yangu lakini wakati mwengine hushindwa nikaingiwa na chuki rohoni mwangu na nikataka maovu yamfikie yeye pamoja na watu wake,kwani wote wamenigeuka bila kisa wala sababu kazi kusikiliza maneno anayosema huyo mwanamume na kumuamini.Naomba munisaidie na dua yoyote ambayo itanisaidia nisimuweke shaitwani mbele nakuhamaki ili na mimi nikawa kama yeye kupita nikitoa aibu zake.Pia nataka dua nipate kuzidisha subra yangu na nisivuke mipaka ya mola wetu ili nipate ridhaa yake ALLAH.Shukran.

 


JIBU:

 


Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Tumepitia barua za waulizaji wengi na ingawa ziko waliouliza kabla yako, tumeona kwanza tukujibu wewe dada yetu uliyekuwa katika dhiki hii ili upate nasaha zetu, tukitumaini kuwa zitakuwa na nafuu kwako Insha Allah.

 

Kama unavyoamini mwenyewe 'Al-Qadhwaa wa Al-Qadar' ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala), (majaaliwa na mipango ya Allah), basi endelea kuweka imani zaidi katika moyo wako kuwa hayo ndio majaaliwa uliyoandikiwa na huna la kufanya ila ni kusubiri tu.

 

Kumbuka kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Huwapa mitihani waja wake Anaowapenda. Na kila daraja ya mja inapokuwa juu zaidi ndipo anapozidi kupata mitihani ili Amjaribu imani yake. Hivyo wewe unatakiwa uendelee na subira yako hadi Atakapokupa faraja Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) ama kwa kukuwezesha usahau kabisa hayo aliyokutendea mumeo au Akuruzuku mume mwengine ambaye atakuwa na kheri na wewe zaidi. Soma kauli za Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) ambazo inampasa mtalaka wako  azijue na azifuate:

 

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ لاَ يَحِلُّ لَكُمْ أَن تَرِثُواْ النِّسَاء كَرْهًا وَلاَ تَعْضُلُوهُنَّ لِتَذْهَبُواْ بِبَعْضِ مَا آتَيْتُمُوهُنَّ إِلاَّ أَن يَأْتِينَ بِفَاحِشَةٍ مُّبَيِّنَةٍ وَعَاشِرُوهُنَّ بِالْمَعْرُوفِ فَإِن كَرِهْتُمُوهُنَّ فَعَسَى أَن تَكْرَهُواْ شَيْئًا وَيَجْعَلَ اللّهُ فِيهِ خَيْرًا كَثِيرًا))

((Enyi mlioamini! Si halali kwenu kuwarithi wanawake kwa nguvu. Wala msiwadhikishe ili muwapokonye baadhi ya mlivyo wapa - isipokuwa wakifanya uchafu ulio wazi. Na kaeni nao kwa wema, na ikiwa mmewachukia, basi huenda mkakichukia kitu, na Mwenyezi Mungu Ametia kheri nyingi ndani yake)) [An-Nisaa: 19]

Nawe huwezi kujua, pengine ni kheri yako kuachika na mume huyo!

 

((وَعَسَى أَن تَكْرَهُواْ شَيْئًا وَهُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ وَعَسَى أَن تُحِبُّواْ شَيْئًا وَهُوَ شَرٌّ لَّكُمْ وَاللّهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لاَ تَعْلَمُونَ))

((Na huenda mkachukia kitu nacho ni kheri kwenu. Na huenda mkapenda kitu nacho ni shari kwenu. Na Allah Anajua na nyinyi hamjui)) [Al-Baqarah:216]

 

Kumbuka dada yetu kwamba, kuwa na subira katika mitihani kuna thawabu kubwa ambazo zimetajwa sana na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) katika Qur-aan. Lakini sio kila mtu ni mwenye kuweza kusubiri, ila wale wenye iymaan kubwa na kuwa na tawakkul na Mola wao. Tunakuwekea kauli chache hapa upate kurudisha subira yako Insha Allah:

 

 ((إِنَّمَا يُوَفَّى الصَّابِرُونَ أَجْرَهُم بِغَيْرِ حِسَابٍ))

((Hakika wenye subira watapewa ujira wao bila ya hisabu)) [Az-Zumar: 10]

 

Kusubiri kwako kwa maudhi yake na bila kumlipa maovu basi jazaa yako ni Pepo:

 

 ((وَالَّذِينَ صَبَرُواْ ابْتِغَاء وَجْهِ رَبِّهِمْ وَأَقَامُواْ الصَّلاَةَ وَأَنفَقُواْ مِمَّا رَزَقْنَاهُمْ سِرًّا وَعَلاَنِيَةً وَيَدْرَؤُونَ بِالْحَسَنَةِ السَّيِّئَةَ أُوْلَئِكَ لَهُمْ عُقْبَى الدَّارِ))

 

 (( جَنَّاتُ عَدْنٍ يَدْخُلُونَهَا وَمَنْ صَلَحَ مِنْ آبَائِهِمْ وَأَزْوَاجِهِمْ وَذُرِّيَّاتِهِمْ وَالمَلاَئِكَةُ يَدْخُلُونَ عَلَيْهِم مِّن كُلِّ بَابٍ))   ((سَلاَمٌ عَلَيْكُم بِمَا صَبَرْتُمْ فَنِعْمَ عُقْبَى الدَّارِ)) 

 

 

((Na ambao husubiri kwa kutaka radhi ya Mola wao Mlezi, na wakashika Swalah, na wakatoa, kwa siri na kwa uwazi, katika tulivyowapa; na wakayaondoa maovu kwa wema. Hao ndio watakaopata malipo ya Nyumba ya Akhera)). 

((Nayo ni Bustani za milele, wataziingia wao na walio wema miongoni mwa baba zao, na wake zao, na vizazi vyao. Na Malaika wanawaingilia katika kila mlango))  

(Wakiwaambia) ((Assalamu ‘Alaykum! Amani iwe juu yenu, kwa sababu ya mlivyosubiri! Basi ni mema mno malipo ya Nyumba ya Akhera)) [Ar-Ra'ad: 22-24]

 

Tambua vile vile kuwa mtu mwenye kukufanyia uovu, kukusengenya nyuma yako anakufutia dhambi zako. Ingawa unaposikia mtu amekuteta huumia moyoni, lakini fikiria kwamba anakupatia thawabu za bure ambazo unazipata bila ya wewe kuzifanyia kazi.

Inasemekana moja wa Salaf Swaalih (Wema waliopita) alisikia kuwa kuna mtu amemsengenya. Alinunua zawadi na kumpelekea kwa kuwa amempatia thawabu za bure.

 

Kwa hiyo usimlipe maovu kwa lolote alilokudhulumu. Bali jitahidi umsamehe kwani kama ulivyotambua katika barua yako kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anapenda wanaosamehe. Na kufanya hivyo ni kukupandisha daraja yako kuwa katika wafanyao wema 'muhsiniyn'  

 

((الَّذِينَ يُنفِقُونَ فِي السَّرَّاء وَالضَّرَّاء وَالْكَاظِمِينَ الْغَيْظَ وَالْعَافِينَ عَنِ النَّاسِ وَاللّهُ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ))  

((Ambao hutoa wanapokuwa na wasaa na wanapokuwa na dhiki, na wanajizuia ghadhabu, na wasamehevu kwa watu; na Allah  Huwapenda wafanyao wema)) [Al-'Imraan:133]

 

Soma du'aa ifuatayo sana ambayo imo katika Qur-aan Insha Allah ikusaidie kuondosha kila ovu katika moyo wako na upate ridhaa ya Mola wako.

 

((رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالإِيمَانِ وَلاَ تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَؤُوفٌ رَّحِيمٌ))  


 

Rabbanaghfir Lanaa Wa Liikhwaaninal-Ladhiyna Sabaquunaa Bil Iymaani Wa Laa Taj'al Fiy Quluubinaa Ghillal-Lilladhiyna Aamanuu  Rabbannaa Innaka Rauufur-Rahiym.

Mola wetu, Tughufirie sisi na ndugu zetu waliotutangulia kwa Imani, wala usijaalie ndani ya nyoyo zetu undani kwa walioamini. Mola wetu, hakika Wewe ni Mpole na Mwenye kurehemu. [Al-Hashr: 10]

Pia soma du'aa za kuondosha dhiki na huzuni katika kungo kfuatacho:

Duaa ukiwa na hamu na huzuni

Tunakuombea Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Akuondoshee kila dhiki na Akupe faraja ya karibu Insha Allah.

Na Allah Anajua zaidi

 

Share