31-Wewe Pekee Tunakuabudu: Tawassul Za Shirki Kufru Na Bid’ah: Kutawassal Kwa Kuchinja Kukusudiwa Asiyekuwa Allaah

 

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

Wewe Pekee Tunakuabudu Na Wewe Pekee Tunakuomba Msaada

 

Tawassul Za Shirki Kufru Na Bid’ah

 

31- Kutawassal Kwa Kuchinja Kukusudiwa Asiyekuwa Allaah

 

 

 

 

Kuchinja ni miongoni mwa ‘ibaadah tukufu ambayo inapaswa kumkusudia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Pekee. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ ﴿٢﴾

Basi swali kwa ajili ya Rabb wako na chinja kwa ajili Yake. [Al-Kawthar: 2]

 

Na pia Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika kauli Yake ambayo pia ni miongoni mwa du’aa ya kufungulia Swalaah: 

إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٦٢﴾

“Hakika Swalaah yangu, na kuchinja kafaara na ‘ibaadah zangu na uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allaah Pekee Rabb wa walimwengu.” [Al-An’aam: 162]

 

Mifano ya vichinjo vya shirki na bid’ah ni kuchinja kwa ajili ya majini au waliokufa makaburini.

 

Kadhalika, baadhi ya mila huchinja kwa ajili ya wanandoa na kuikanyaga damu wakiitakidi kuwa ni kinga ya husda au jicho baya. 

 

Wengine huchinja kwa ajili kumwaga damu katika nyumba mpya wanayohamia na hali kuna du’aa kutoka katika Sunnah iliyothibiti pindi mtu anapoteremka katika sehemu (makazi) mpya kama ifuatavyo:  

 

عن خَوْلَةَ بِنْتَ حَكِيمٍ السُّلَمِيَّةَ (رضي الله عنها) تَقُولُ سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) يَقُولُ: ((مَنْ نَزَلَ مَنْزلاَ ثُمَّ قَالَ: "أَعُوذُ بِكَلِمَاتِ اللَّهِ التَّامَّاتِ مِنْ شَرِّ مَا خَلَقَ" لَمْ يَضُرَّهُ شَيْءٌ حَتَّى يَرْتَحِلَ مِنْ مَنْزِلِهِ ذَلِكَ))

Kutoka kwa Khawlat bint Hakiym As-Sulamiyyah kwamba: Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Atakayeteremka katika kituo [makazi] kisha akasema:  A’uwdhu bikalimaati-LLaahit-ttaammati  min sharri maa Khalaq (Najikinga kwa maneno ya Allaah yaliyotimia na shari Alichokiumba), basi hakuna kitakachomdhuru hadi atakapoondoka katika kituo hicho)) [Muslim]

 

Tahadhari pia kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Humlaani mtu mwenye  kuchinja kwa kukusudia asiyekuwa Yeye.

 

عَنْ أَبِي الطُّفَيْلِ (رضي الله عنه) قَالَ: قُلْنَا لِعَلِيٍّ أَخْبِرْنَا بِشَيْءٍ أَسَرَّهُ إِلَيْكَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ): فَقَالَ: مَا أَسَرَّ إِلَيَّ شَيْئًا كَتَمَهُ النَّاسَ وَلَكِنْ سَمِعْتُهُ يَقُولُ: ((لَعَنَ اللَّهُ مَنْ ذَبَحَ لِغَيْرِ اللَّهِ، وَلَعَنَ اللَّهُ، وَلَعَنَ اللَّهُ مَنْ لَعَنَ وَالِدَيْهِ وَلَعَنَ اللَّهُ مَنْ غَيَّرَ تُخُومَ الأَرْض))

Kutoka kwa Abuu Twufayl (Radhwiya Allaahu 'anhu)  kwamba tulimuuliza ‘Aliy: Tujulishe jambo alokutajia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa ni siri. Akasema: Hakunipa siri yoyote ambayo ameificha kwa watu, lakini nimemsikia akisema: ((Allaah Amelaani anayechinja pasi na Allaah, na Allaah Amelaani anayempa makazi (himaya) mzushi na Allaah Amelaani anayemlaani mzazi wake, na Allaah Amelaani anayebadilisha mistari ya mipaka ya ardhi [anayomiliki])) [Muslim, An-Nasaaiy, Ahmad]

 

Na maana ya laana ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni kuepushwa na rahmah Zake.   

 

Kwa vile kuchinja ni ‘ibaadah ya kumkurubisha mja kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), basi inapasa kutahadhari kutokumshirikisha nayo kwa vyovyote vile na kwamba hata ikiwa kinachochinjwa ni kiasi kidogo vipi, basi huwa ni shirki na khatari yake ni kumuingiza mtu motoni kama ilivyonukuliwa katika Kitaab At-Tawhiyd Hadiyth: 

 

((دَخَلَ الْجَنَّةَ رَجُلٌ فِي ذُبَابc وَدَخَلَ النَّار رَجُلٌ فِي ذُبَاب)): قَالُوا: وَكَيْفَ ذَلِكَ يَا رَسُولَ الله؟ قَالَ: ((مَرَّ رَجُلانِ علَى قَوْمٍ لَهُمْ صَنَمٌ لاَ يَجُوزُهُ أحَدٌ حَتَّى يُقَرِّبَ لَهُ شَيْئاً، فَقَالُوا لإَحَدِهِمَا: قَرِّبْ، قَالَ: لَيْسَ عِنْدِي شَيْءٌ أُقَرِّبَهُ، قَالُوا بِه: قَرِّبْ وَلَوْ ذُباَبًا، فَقَرَّبَ ذُبَاباً، فَخَلُّوا سَبِيْلَهُ، فَدَخَلَ النَّارَ، وَقَالُوا لِلآخر: قَرِّبْ، فَقَالَ: مَا كُنْتُ لأُقَرِّبَ لأحَدٍ شَيْئًا دُونَ الله عَزَّ وَجَلَّ. فَضَرَبُوا عُنقَهُ، فَدَخَلَ الْجَنَّةَ)) 

((Mtu mmoja ameingia Jannah kwa nzi, na ameingia motoni mtu kwa ajili ya nzi)).  Wakasema: Vipi hivyo ee Rasuli wa Allaah? Akasema: ((Watu wawili walipitia mbele ya watu walikuwa na sanamu lao, hapiti mtu hadi ajikurubishe kwa kuchinja. Wakamwambia mmoja wao: Jikurubishe! [Chinja!]  Akasema:  Sina kitu cha kujikurubisha. Wakasema: Jikurubishe japo kwa nzi.  Akajikurubisha kwa nzi. Wakamwachia apite njia akaingia motoni.  Wakawambia mwengine: Jikurubishe! Akasema: Sikuwa najikurubisha [nachinja] kwa yeyote pasi na Allaah ‘Azza wa Jalla. Wakampiga shingo [wakamuua] akaingia Jannah)). [Ahmad, Sharh Kitaab At-Tawhiyd li-Ibn  Baaz, na Majmuw’ Al-Fataawaa Ibn Baaz] 

 

Shaykh Fawzaan bin Swaalih Al-Fawzaan (Hafidhwahu Allaah) akifafanua Hadiyth hiyo anasema:  

 

“[Mtu wa kwanza] Ametoa udhuru kutokuwa na kitu. Hakusema ‘hakika kuchinja pasi na Allaah haijuzu au ni munkari’ – Tunajikinga kwa Allaah.  Na hii inafahamika kwamba lau angelikuwa ana  mnyama wa kuchinja angelichinja. Wakamwambia: jikurubishe walau kwa nzi! Akajikurubisha kwa nzi, yaani akafanya hivyo kwa ajili ya sanamu wakamwachia apite njia, akaingia motoni kwa sababu ya shirki. Amejikurubisha pasi na Allaah, na 'ibra (zingatio) hapa ni niyyah na kusudio wala si kuhusu kinachochinjwa. Na kwamba hakuchukia jambo hili wala hakujiepusha nalo, bali ametoa udhuru kutokuwa na kitu na kwa hivyo amengia Motoni – Tunajikinga kwa Allaah. 

 

Na wakamwambia mwengine: Jikurubishe! Akasema: Sikuwa ni mwenye kuchinja chochote kwa ajili ya asiyekuwa Allaah ‘Azza wa Jalla.

 

Amejiepusha na amechukia shirki. Wakampiga shingo yake, kwa maana wamemuua akaingia Jannah kwa sababu ya Tawhiyd. Hivyo basi, katika Hadiyth hii tukufu kuna mafunzo muhimu:

 

Kwanza: Hadiyth inaruhusu kuelezea habari za ummah zilizopita na kuelezea ilivyothibiti kwa ajili ya kuwaidhi na zingatio. 

 

Pili: Katika Hadiyth kuna dalili ya kuharamishwa kujikurubisha kwa kuchinja pasi na Allaah, na mwenye kujikurubisha pasi na Allaah, atakuwa ametenda shirki kwa sababu mtu aliyeua nzi ameingia motoni hata ikiwa ni kitu kichafu cha kutemwa (kidogo, duni mno). Na mtu wa pili amechukia shirki na amejiepusha japokuwa ilikuwa ni kitu cha kuchukizwa (duni) akaingia Jannah. 

 

Tatu: Kama alivyosema Shaykh (Rahimahu Allaah) kuhusu mas-alah ya niyyah ya 'amali za moyo, japokuwa ni kitu kichafu cha kutemwa (kidogo, duni mno) lakini itambulike kuwa niyyah ni 'amali ya moyo. 

 

Nne: Kama alivyosema Shaykh (Rahimahu Allaah) kuhusu wepesi wa bin Aadam kukaribia Jannah na moto ni kama alivyosema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Jannah iko karibu zaidi kwa mmoja wenu kuliko nyuzi za viatu vyake, na moto kama hivyo)). [Al-Bukhaariy]

 

Huyu amepigwa shingo yake (ameuliwa) akaingia Jannah. Na yule wamemwachia njia akaingia motoni.  

 

Tano: Kwamba mtu aliyeua  nzi alikuwa Muumini, akaingia motoni kwa sababu ya kujikurubisha kwake kwa nzi, kwa sababu angelikua kafiri, angeliingia motoni kwa kufru yake si kwa kujikurubisha kwa nzi. Akadhihirisha kwamba alikuwa Muumini, na mas-alah haya ni khatari sana! Basi wako wapi wanaochinja kwa ajili ya makaburi, na majini, na mashaytwaan, na kwa ajili ya ardhi, na wachawi?

 

Akaonyesha kwamba shirki kubwa kabisa inamtoa mtu nje ya Dini japokuwa ikiwa ni kitu chepesi. Hivyo basi, suala la Tahwiyd na  ‘Aqiydah hayasamehewi hayo.” [Sharh Kitaab At-Tawhiyd – Baab maa jaa-a fiy adhdhab-h li-ghayri-LLaah]  

 

 

 

 

Share