00-Aayah Na Mafunzo: Fadhila Za Suwrah Al-Faatihah

Aayah Na Mafunzo

 

Al-Faatihah

 

Fadhila Za Suwrah Al-Faatihah

 

 

Hii ni Suwrah iliyokuwa Adhimu na bora, kuliko Suwrah zote za Qur-aan, nayo ni miongoni mwa Suwrah zenye majina mengi na miongoni mwa majina yake ni: Al-Faatihah, Ummul-Qur-aan, AlhamduliLLaah, Asw-Swalaah, Ash-Shifaa, Ar-Ruqyah, Sab‘ul-Mathaaniy, Ummul-Kitaab. Haijateremka katika Tawraat wala katika Injiyl wala katika Zaburi mfano wake.

Utukufu na Fadhila za Suwratul-Faatihah unaelezewa katika Hadiyth nyingi, baadhi yake ni hizi zifuatazo:

 

Hadiyth Ya Kwanza:

Abuu Sa’iyd bin Al-Mu’allaa (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia kwamba:  Nilikuwa nikiswali, akaniita Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) nikawa sikumuitikia mpaka nilipomaliza kuswali. Kisha nikamwendea akaniambia: “Kimekuzuia nini usinijie?”  Nikasema:  Ee Rasuli wa Allaah, nilikuwa naswali. Akasema: “Kwani Allaah Hakusema: “Enyi walioamini! Muitikieni Allaah na Rasuli Anapokuiteni kwenye yale yenye kukuhuisheni.” [Al-Anfaal (8: 24)]. Kisha akasema: “Nitakufundisha Suwrah tukufu kabisa katika Qur-aan kabla hukutoka Msikitini.” Akanikamata mkono, alipotaka kutoka Msikitini, nikamwambia: ee Rasuli wa Allaah, ulisema utanifundisha Suwrah tukufu kabisa katika Qur-aan. Akasema: “Naam, AlhamduliLLaahi Rabbil-‘Alaamiyn, hizo ni (Aayaat) Saba zinazokaririwa (kusomwa) na Qur-aan Adhimu niliyopewa.” [Al-Hijr (15: 87) Al-Bukhaariy]

 

Hadiyth Ya Pili:

Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia kwamba: Baadhi ya Swahaaba (wakiwa safarini) walifika karibu na kabila fulani la Waarabu, wakakataa kuwapokea. Walipobakia katika hali hiyo, huku mkuu wao alitafunwa na nyoka (au nge). Wakasema: Je, mna dawa yoyote au tabibu? Wakajibu: Nyinyi mmekataa kutupokea kwa hiyo hatutamtibu mgonjwa wenu hadi mtulipe! Wakakubali kuwapa kundi la kondoo. Mmoja wa Swahaaba akaanza kumsomea Suwratul-Faatihah huku akikusanya mate na kumtemea (mahali alipotafunwa). Mgonjwa akapona kisha watu wake wakawaletea kondoo lakini wakasema. Tusiwachukue mpaka tumuulize Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Walipomuuliza alicheka akasema: “Mmejuaje kuwa Suwratul-Faatihah ni ruqya? Chukueni na nigaieni sehemu yangu.” [Al-Bukhaariy]

 

Hadiyth Ya Tatu:

Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhumaa)  amehadithia kwamba: Jibriyl ('Alayhis-Salaam) alipokuwa na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisikia sauti kutoka juu. Jibriyl ('Alayhis-Salaam) akatazama juu akasema: “Huu mlango wa mbinguni umefunguliwa na haujapatapo kufunguliwa isipokuwa leo.” Malaika akateremka humo akasema: “Huyu Malaika ameteremka ardhini, hajapatapo kuteremka kamwe isipokuwa leo.” Akasalimia kisha   akasema: “Pokea bishara ya nuru mbili ulizopewa ambazo hakuna Nabiy aliyepewa kabla yako; Ufunguo wa Kitabu (Al-Faatihah), na Aayah (mbili) za mwisho wa Suwratul-Baqarah.  Hutosoma herufi humo ila utapewa barakah zake ziliomo.” [Muslim]

 

Hadiyth Ya Nne:

Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Atakayeswali Swalaah bila ya kusoma humo mama wa Qur-aan (Suwratu Al-Faatihah) huwa haikutimia (ina kasoro).” Alikariri mara tatu: “Haikutimia.” Mtu mmoja alimwambia Abuu Hurayrah: (Hata) tukiwa nyuma ya Imaam? Akasema: Isome mwenyewe (kimya kimya) kwani nilimsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “Allaah (تعالى) Amesema: Nimeigawa Swalaah baina Yangu na mja Wangu nusu mbili, mja Wangu atapata yale aliyoyaomba. Mja anaposema: Himidi Anastahiki Allaah Rabb wa walimwengu, Allaah  (Ta’aalaa) Husema: Mja Wangu kanihimidi.  Na anaposema: Ar-Rahmaan, Mwenye kurehemu, Allaah (Ta’aalaa) Husema: Mja wangu kanisifu na kunitukuza kwa wingi, na anaposema: Mfalme wa siku ya malipo, Allaah (Ta’aalaa) Husema: Mja wangu kaniadhimisha. Na mara moja alisema: Mja wangu ameniaminisha. Na anaposema: Wewe Pekee tunakuabudu na Wewe Pekee tunakuomba msaada, Husema: Hii ni baina Yangu na mja Wangu na mja Wangu atapata kile alichokiomba. Na anaposema: Tuongoze njia iliyonyooka, njia ya wale Uliowaneemesha, si ya walioghadhibikiwa wala waliopotea, Husema: Hii ni ya mja Wangu na mja Wangu atapata kile alichokiomba.” [Muslim, Maalik, At-Tirmidhiy, Abu Daawuwd, An-Nasaaiy na Ibn Maajah]  

 

Hadiyth Ya Tano:

‘Ubaadah bin Swaamit (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia kwamba  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakuna Swalaah kwa asiyesoma (ndani yake) Ufunguo wa Kitabu.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

  

 

Share