06-Aayah Na Mafunzo: Maana Ya Njia Iliyonyooka

Aayah Na Mafunzo

Al-Faatihah

Maana Ya Njia Iliyonyooka

 

 

 

اهْدِنَا الصِّرَاطَ الْمُسْتَقِيمَ ﴿٦﴾

6. Tuongoze njia iliyonyooka.

 

 

Mafunzo:

 

Hadiyth Ya Kwanza:

 

An-Nawaas bin Sam’aan  (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Allaah (Ta’aalaa) Amepiga mfano; Swiraatw (njia) iliyonyooka, imezungukwa pande zote na kuta mbili na kila ukuta una milango iliyo wazi na imefunikwa na mapazia. Na katika lango la swiraatw kuna mlinganiaji akiita: “Enyi watu! Ingieni nyote katika swiraatw na msipite pembeni.” Na juu ya swiraatw, mlinganiaji mwengine anamuonya mtu yeyote anayetaka kufungua hiyo milango akiwaambia: Masikitiko kwenu! Msiufungue! Kwani  mkifungua mtapita ndani! Kwani Asw-Swiraatw ni Uislaam, na kuta mbili ni mipaka Aliyoiweka Allaah. Na milango iliyofunguliwa ni yaliyoharamishwa na Allaah. Na huyo Daa’iy (mlinganiaji) juu ya lango la Swiraatw ni Kitaabu cha Allaah, na Daa’iy juu ya swiraatw ni maonyo ya Allaah yaliyo ndani ya kila nafsi ya Muislaam.”  [Ahmad, ameisahihisha Al-Albaaniy; Swahiyh Al-Jaami’ (3887)]

 

 

Hadiyth Ya Pili:

Jaabir (Radhwiya Allaahu 'anhu)  amehadithia kwamba: Tulikuwa tumekaa pamoja na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akachora mstari mbele yake, akachora mistari miwili kuliani, na mistari miwili kushotoni kisha akaweka mkono wake katika njia ya katikati akasema: “Hii njia ya Allaah” Kisha akasoma: “Na kwamba hii njia Yangu iliyonyooka, basi ifuateni, na wala msifuate njia (nyinginezo) zitakufarikisheni na njia Yake.” [Ahmad, Swahiyh Ibn Maajah (11)] 

 

 

Share