067-Aayah Na Mafunzo: Kisa Cha Al-Baqarah (Ng’ombe)

Aayah Na Mafunzo

Al-Baqarah

Kisa Cha Al-Baqarah (Ng’ombe)

 

 

وَإِذْ قَالَ مُوسَىٰ لِقَوْمِهِ إِنَّ اللَّـهَ يَأْمُرُكُمْ أَن تَذْبَحُوا بَقَرَةً ۖ قَالُوا أَتَتَّخِذُنَا هُزُوًا ۖ قَالَ أَعُوذُ بِاللَّـهِ أَنْ أَكُونَ مِنَ الْجَاهِلِينَ ﴿٦٧﴾

67. Na pindi Muwsaa alipowaambia kaumu wake: “Hakika Allaah Anakuamuruni mchinje ng’ombe.” Wakasema: “Unatufanyia mzaha?” Akasema: “Najikinga kwa Allaah kuwa  miongoni mwa wajinga.”  

 

قَالُوا ادْعُ لَنَا رَبَّكَ يُبَيِّن لَّنَا مَا هِيَ ۚ قَالَ إِنَّهُ يَقُولُ إِنَّهَا بَقَرَةٌ لَّا فَارِضٌ وَلَا بِكْرٌ عَوَانٌ بَيْنَ ذَٰلِكَ ۖ فَافْعَلُوا مَا تُؤْمَرُونَ ﴿٦٨﴾

68. Wakasema: “Tuombee kwa Rabb wako Atubainishie ni ng’ombe wa aina gani huyo?” (Muwsaa) Akasema: “Hakika Yeye (Allaah) Anasema kwamba ng’ombe mwenyewe si mpevu wala si mchanga, bali ni wa katikati baina ya hao, basi fanyeni mnavyoamrishwa.”

 

قَالُوا ادْعُ لَنَا رَبَّكَ يُبَيِّن لَّنَا مَا لَوْنُهَا ۚ قَالَ إِنَّهُ يَقُولُ إِنَّهَا بَقَرَةٌ صَفْرَاءُ فَاقِعٌ لَّوْنُهَا تَسُرُّ النَّاظِرِينَ ﴿٦٩﴾

69. Wakasema: “Tuombee kwa Rabb wako Atubainishie rangi yake?” (Muwsaa) Akasema: “Hakika Yeye (Allaah) Anasema kwamba ni ng’ombe wa rangi ya njano iliyoiva mno, rangi yake huwapendeza wanaotazama.”

 

 قَالُوا ادْعُ لَنَا رَبَّكَ يُبَيِّن لَّنَا مَا هِيَ إِنَّ الْبَقَرَ تَشَابَهَ عَلَيْنَا وَإِنَّا إِن شَاءَ اللَّـهُ لَمُهْتَدُونَ ﴿٧٠﴾

70. Wakasema: “Tuombee kwa Rabb wako Atubainishie ni ng’ombe wa aina gani huyo? Kwa hakika ng’ombe wametutatiza na hakika sisi In-Shaa-Allaah  tutakuwa wenye kuongoka.”

 

قَالَ إِنَّهُ يَقُولُ إِنَّهَا بَقَرَةٌ لَّا ذَلُولٌ تُثِيرُ الْأَرْضَ وَلَا تَسْقِي الْحَرْثَ مُسَلَّمَةٌ لَّا شِيَةَ فِيهَا ۚ قَالُوا الْآنَ جِئْتَ بِالْحَقِّ ۚ فَذَبَحُوهَا وَمَا كَادُوا يَفْعَلُونَ ﴿٧١﴾

71. (Muwsaa) Akasema: ”Hakika Yeye (Allaah) Anasema kwamba ni ng’ombe ambaye hakutiishwa; kwa kulima ardhi wala kwa kumwagilia maji shamba; ni kamilifu hana dosari.” Wakasema: “Sasa umekuja na haki.” Basi wakamchinja na hawakuwa wenye kukaribia kufanya hivyo. 

 

وَإِذْ قَتَلْتُمْ نَفْسًا فَادَّارَأْتُمْ فِيهَا ۖ وَاللَّـهُ مُخْرِجٌ مَّا كُنتُمْ تَكْتُمُونَ ﴿٧٢﴾

72. Na pindi mlipoiua nafsi, kisha mkakhitilafiana kwayo, na Allaah ni Mwenye kutoa hayo mliyokuwa mkiyaficha.

 

فَقُلْنَا اضْرِبُوهُ بِبَعْضِهَا ۚ كَذَٰلِكَ يُحْيِي اللَّـهُ الْمَوْتَىٰ وَيُرِيكُمْ آيَاتِهِ لَعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ ﴿٧٣﴾

73. Tukasema: “Mpigeni (huyo maiti) kwa baadhi ya sehemu yake (huyo ng’ombe).” Hivyo ndivyo Allaah Anavyohuisha wafu na Anakuonyesheni Aayaat (miujiza, dalili) Zake huenda mkatia akilini.

 

 

Mafunzo:

 

Kuhusu Aayah (76- 73); kulikuweko na mtu aliyepooza (asiyekuwa wa kawaida) na alikuwa na mali nyingi. Hakuwa na mrithi isipokuwa jamaa yake mmoja. Mrithi huyo alimuua huyo bwana ili apate kurithi mali. Kisha akachukua mwili wake akautupa nje na nyumba ya mtu mmoja kumsingizia. Siku ya pili  akadai kulipiza kisasi, pakatokea mzozano na watu walikaribia kuuana. Mwishowe wakasema “Mnaye Rasuli wa Allaah mwendeeni.” Walipomwendea Nabiy Muwsaa akawaambia: “Hakika Allaah Anakuamuruni mchinje ng’ombe.” Wakafanya ugumu wa kutii amri hii kwa kubishana na wakazidi kufanyiwa ugumu kumtafuta ng’ombe mwenye sifa fulani. Wasingebishana basi ingewatosheleza kuchinja ng’ombe yoyote yule.  Ng’ombe mwenye sifa hizo akapatikana kwa mtu mmoja pekee naye akataka alipwe dhahabu iliyojaza ngozi ya ng’ombe. Wakamlipa na wakamchinja na kisha wakachukua sehemu ya ng’ombe kumpigia huyo mtu aliyeuliwa, akazindukana na wakamuuliza nani aliyemuua? Akamuashiria mrithi wake, basi hakuruhusiwa tena kumrithi. [Tafsiyr Ibn Kathiyr]  

 

 

Share