153-Aayah Na Mafunzo: Kuomba Msaada Kwa Subira Na Swalaah

Aayah Na Mafunzo

Al-Baqarah

Kuomba Msaada Kwa Subira Na Swalaah

 

 

  

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَعِينُوا بِالصَّبْرِ وَالصَّلَاةِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ مَعَ الصَّابِرِينَ ﴿١٥٣﴾

153. Enyi walioamini! Tafuteni msaada kwa subira na Swalaah; hakika Allaah Yu pamoja na wanaosubiri.

 

 

Mafunzo:

 

Miongoni mwa fadhila za subira na Swalaah: Swuhayb bin Sinaan (رضي الله عنه) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Ajabu ya jambo la Muumin kwamba kila jambo lake ni kheri. Na halipatikani hili isipokuwa kwa Muumin. Anapofikwa na jambo zuri hushukuru nayo ni kheri kwake na anapofikwa na jambo lenye madhara husubiri nayo ni kheri kwake.” [Muslim: (2999)]

 

Pia, Abuu Faraas Rabiy'ah bin Ka'ab Al-Aslamiy (رضي الله عنه) ambaye alikuwa mtumishi wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amehadithia: Nililala na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) usiku mmoja nikamletea maji ya kutawadha, akaniambia: “Omba utakacho!” Nikasema: Nataka kuandamana na wewe Jannah! Akasema: “Hutaki lolote lingine?” Nikasema: Ni hilo tu. Akasema: “Basi nisaidie (ili hilo liwezekane) kwa kuzidisha kusujudu (Kuswali).” [Muslim] 

 

 

Share