229-Aayah Na Mafunzo: Hukmu Ya Khul’u Ni Kurudisha Mahari Kutokuvuka Mipaka

Aayah Na Mafunzo

Al-Baqarah

Hukmu Ya Khul’u Ni Kurudisha Mahari Kutokuvuka Mipaka

 

 

الطَّلَاقُ مَرَّتَانِ ۖ فَإِمْسَاكٌ بِمَعْرُوفٍ أَوْ تَسْرِيحٌ بِإِحْسَانٍ ۗ وَلَا يَحِلُّ لَكُمْ أَن تَأْخُذُوا مِمَّا آتَيْتُمُوهُنَّ شَيْئًا إِلَّا أَن يَخَافَا أَلَّا يُقِيمَا حُدُودَ اللَّـهِ ۖ فَإِنْ خِفْتُمْ أَلَّا يُقِيمَا حُدُودَ اللَّـهِ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِمَا فِيمَا افْتَدَتْ بِهِ ۗ تِلْكَ حُدُودُ اللَّـهِ فَلَا تَعْتَدُوهَا ۚ وَمَن يَتَعَدَّ حُدُودَ اللَّـهِ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ ﴿٢٢٩﴾

229. Talaka ni mara mbili. Hivyo kuzuia kwa mujibu wa shariy’ah au kuachia kwa ihsaan. Wala si halali kwenu kuchukua chochote katika mlivyowapa wanawake, isipokuwa wote wawili wakikhofu kuwa hawatoweza kusimamisha mipaka ya Allaah. Mtakapokhofu kuwa wote wawili hawatoweza kusimamisha mipaka ya Allaah; basi hakuna lawama juu yao katika ambacho amejikombolea kwacho. Hiyo ni mipaka ya Allaah basi msitaadi. Na atakayetaadi mipaka ya Allaah basi hao ndio madhalimu.

 

Mafunzo:

 

Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) amehadithia kwamba: Mke wa Thaabit bin Qays alimfuata Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: Ee Rasuli wa Allaah,  Thaabit bin Qays simlaumu katika tabia wala Dini, lakini mimi nakhofia ukafiri katika Uislamu (kutokutekeleza haki zake). Basi Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Utamrejeshea shamba lake?” Akasema: Ndio. Akasema kumwambia Qays: “Kubali shamba na umtaliki.” [Al-Bukhaariy (5273)].

Khul‘u: kujivua kutoka katika ndoa na kurudisha mahari.

 

Kutaadi mipaka ya Allaah amekataza pia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) aliposema: “Allaah Ameweka mipaka, hivyo msipindukie, na Ametoa maamrisho hivyo msiyadharau, na kuyaharamisha baadhi ya mambo, hivyo msifanye makosa. Ameacha baadhi ya mambo bila ya kuyawekea shariy’ah kwa kuwahurumia, si kwa sababu Aliyasahau, basi msiulizie khabari zake.” [Ad-Daaraqutwniy (4/298)]

 

Share