085-Aayah Na Mafunzo: Jibriyl ('Alayhis-Salaam) Amekuja Kukufundisheni Dini Yenu

Aayah Na Mafunzo

Aal-‘Imraan

Jibriyl ('Alayhis-Salaam) Amekuja Kukufundisheni Dini Yenu

www.alhidaaya.com

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَمَن يَبْتَغِ غَيْرَ الْإِسْلَامِ دِينًا فَلَن يُقْبَلَ مِنْهُ وَهُوَ فِي الْآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ ﴿٨٥﴾

Na yeyote anayetaka dini isiyokuwa ya Kiislamu basi haitokubaliwa kwake; naye katika Aakhirah atakuwa miongoni mwa waliokhasirika. [Aal-'Imraan: 85]

 

 

 

Mafunzo:

 

Umar (رضي الله عنه) amehadithia kwamba: Siku moja tulikuwa tumekaa na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) hapo alitokea mtu ambaye nguo zake zilikuwa nyeupe pepe na nywele zake zilikuwa nyeusi sana; hakuwa na alama ya machofu ya safari na wala hapakuwa na hata mmoja katika sisi aliyemtambua. Alienda akakaa karibu na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akaweka magoti yake karibu na magoti yake na akaweka viganja vyake juu ya mapaja yake kisha akasema; Ee Muhammad! Niambie kuhusu Uislamu.  Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Uislamu ni kukiri laa ilaaha illa Allaah na kwamba Muhammad ni Rasuli wa Allaah. Na kusimamisha Swalaah, kutoa Zakaah, kufunga Swiyaam Ramadhwaan na kwenda kuhiji (Makkah) ukiweza.” (Akasema yule mtu yaani Jibriyl) Umesema kweli. Tulipigwa na mshangao kwa kumuuliza kwake Rasuli na kumsadikisha.  Na akasema tena: Niambie kuhusu Iymaan.  Akasema “Ni kumwamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Rasuli Wake na Siku ya Qiyaamah, na kuamini ya kuwa kheri na shari zinatoka Kwake.” (Akasema Jibriyl): Umesema kweli. Akasema hebu nielezee kuhusu Ihsaan.  Akasema: “Ni kumuabudu Allaah kama vile unamuona na kama humuoni basi Yeye Anakuona” Akasema (Jibriyl):  Niambie    kuhusu Qiyaamah.  Akajibu: “Muulizwaji si mjuzi kama asivyo vilevile Muulizaji.” Kisha akamwambia: Nijulishe alama zake: Akajibu: “Kijakazi atazaa bibi yake, na utaona wachunga wenda miguu chini, wenda uchi (wasio na uwezo wa kumiliki hata mavazi), mafukara (wasiokuwa hata na sehemu ya kuishi kwa umaskini) wakishindana kujenga majumba ya fahari.” Kisha akaondoka (Jibriyl) na nilitulia kidogo (nikitafakari). Kisha akasema: “Ee 'Umar! Je, unamjua ni nani yule aliyekuwa akiuliza?” Nikasema: Allaah na Rasuli Wake wanajua zaidi.  Akasema: “Ni Jibriyl, alikuja kuwafundisha Dini yenu.” [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

 

Share