077-Asbaabun-Nuzuwl: An-Nisaa Aayah 077: أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ قِيلَ لَهُمْ كُفُّوا أَيْدِيَكُمْ وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ

أسْبابُ النُّزُول

Asbaabun-Nuzuwl

 

Sababu Za Kuteremshwa (Baadhi Ya Aayaat Za Qur-aan)

 

Imekusanywa na: Alhidaaya.com

 

 

An-Nisaa   077-Je, huoni wale walioambiwa: “Zuieni mikono yenu…

 

 

أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ قِيلَ لَهُمْ كُفُّوا أَيْدِيَكُمْ وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ فَلَمَّا كُتِبَ عَلَيْهِمُ الْقِتَالُ إِذَا فَرِيقٌ مِّنْهُمْ يَخْشَوْنَ النَّاسَ كَخَشْيَةِ اللَّـهِ أَوْ أَشَدَّ خَشْيَةً ۚ وَقَالُوا رَبَّنَا لِمَ كَتَبْتَ عَلَيْنَا الْقِتَالَ لَوْلَا أَخَّرْتَنَا إِلَىٰ أَجَلٍ قَرِيبٍ ۗ قُلْ مَتَاعُ الدُّنْيَا قَلِيلٌ وَالْآخِرَةُ خَيْرٌ لِّمَنِ اتَّقَىٰ وَلَا تُظْلَمُونَ فَتِيلًا ﴿٧٧﴾

Je, huoni wale walioambiwa: Zuieni mikono yenu (msipigane) na simamisheni Swalaah na toeni Zakaah. Basi walipoandikiwa amri kupigana, mara kundi miongoni mwao linawaogopa watu kama kumwogopa Allaah au woga zaidi. Na husema: Rabb wetu!  Kwa nini Umetuamrisha kupigana? Lau Ungelituakhirishia hadi muda kidogo hivi! Sema: Starehe za dunia ni chache; na Aakhirah ni bora zaidi kwa mwenye taqwa; wala hamtodhulumiwa kadiri ya uzi wa kokwa ya tende. [An-Nisaa (4:77)]

 

Sababun-Nuzuwl:

 

Aayah hii imeteremshwa kama alivyohadithia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما)  kwamba: ‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf na Swahaba wenzake  (رضي الله عنهم)  walipokuwa Makkah walimwendea Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na kumwambia: Ee Rasuli wa Allaah! Tulipokuwa washirikina tulikuwa kwenye ‘izzah (hadhi na utukufu) lakini sasa tumeingia Uislamu tumekuwa madhalili. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Hakika mimi nimeamrishwa kusamehe basi msifanye qitaal (vita).” Kisha Allaah Alipomuamrisha Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kuhajiri Madiynah, Alimuamrisha Jihaad na qitaal (dhidi ya washirikina), basi (wao Waislamu) wakasita. Hapo ikateremshwa Aayah hii. [An-Nasaaiy na Al-Haakim]  

 

 

 

Share