Abu Hurayrah (رضي الله عنه)

 

 

 

Utangulizi

Hapana Muilsamu asiyemjua 'Abu Hurayrah' Abdur-Rahman bin Swakhr al Dausiy sahaba mtukufu – Allaah Awe radhi naye.

Kabla ya kusilimu alikuwa akijulikana kwa jina la Abdush-Shams, na baada ya Allaah Kumhidi na kuingia katika dini hii tukufu aliulizwa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam):

"Jina lako nani?"

Akajibu:

"Abdush-Shams."

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) akamuambia:

"Bali jina lako kuanzia leo ni Abdur-Rahman."

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) akasema:

"Sawa ewe Mtume wa Allaah."

Umaarufu wa jina la Abu Hurayrah ulianza tokea wakati wa ujana wake alipokuwa na paka mdogo aliyekuwa akimpenda sana, na wenzake wakambandika jina la Abu Hurayrah. Na jina hilo likavuma na kuenea sana. Na baada ya kujuana   na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) akawa naye akipenda sana kumuita kwa jina hilo na Abu Hurayrah, alikuwa akilifurahia sana jina hilo huku akisema:

"Kipenzi changu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) ananiita kwa jina hili."

 

Kusilimu kwake

Alisilimishwa na Sahaba maarufu Al Tufayl bin Amru Al Dausiy (Radhiya Allaahu 'anhu) lakini alibaki katika nchi yake ya Yemen na hakuondoka kwenda Madina mpaka katika mwaka wa sita baada ya Hijra alipoamua kusafiri pamoja na watu wengi wa kabila lake kuelekea Madina mji wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam).

Alipokuwa Madina, Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) alikuwa akipenda kumtumikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) na kumhudumia na alikuwa hambanduki. Msikiti ulikuwa makao yake makuu na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) alikuwa mwalimu na kiongozi wake mkuu.

 

Mama yake

Mama yake Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) alikataa kusilimu juu ya kuwa mwanawe alikuwa daima akimshikila huku akimfahamisha utukufu wa dini hii na kwamba ndiyo njia ya pekee itakayomuokoa na moto wa Jahannam na kumletea maisha mema hapa duniani na huko akhera. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) alikuwa na huzuni kubwa sana kwa sababu ya kukataa mama yake kusilimu, na siku moja alipokuwa akimsemesha akimtaka amuamini Allaah mmoja na Mtume wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam), mama yake alitamka neno baya juu ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) jambo lililomzidisha huzuni na kumuuma sana.

Akaenda kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) huku akiwa analia, na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) akamuuliza:

"Kipi kinachokuliza ewe Abu Hurayrah?"

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) akasema:

"Siku zote ninamlingania mama yangu asilimu lakini yeye anakataa. Na leo nilipokuwa nikimsemesha alitamka neno baya juu yako nikahuzunika sana. Tafadhali muombee Allaah Mtukufu aulainishe moyo wake aupende Uislamu."

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) akanyanyua mikono yake juu na kuomba:

"Mola wangu, 'mhidi' muongoze mama yake Abu Hurayrah."

Anasema Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu):

"Niliporudi nyumbani niliukuta mlango umefungwa na nikawa nasikia sauti ya maji. Nilipotaka kuingia, mama yangu akaniambia:

"Subiri ewe Abu  Hurayrah usiingie."

Baada ya kumaliza na kuvaa nguo zake akaniambia:

"Sasa ingia."

Nikaingia, akasema:

"Nashuhudia kuwa hapana Mola isipokuwa Allah, na kwamba Muhammad ni Mtume wake na mjumbe wake."

Nikarudi mbio kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) huku nikilia kwa furaha kama nilivokuwa nikilia wakati ule kwa huzuni nikasema:

"Pokea habari njema ewe Mtume wa Allaah, Allaah ameikubali dua yako na mama yangu keshaongoka na kusilimu."

Baada ya kusilimu mama yake, Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) alipata utulivu mkubwa ndani ya nafsi yake, akahisi kama kwamba mzigo mkubwa sana ameweza kuutuwa. Akaona kuwa sasa hapana jambo litakaloweza kumzuwia kujishughulisha na kutafuta elimu kwa moyo wake wote na nguvu zake zote.

 

Akimpenda sana mama yake

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) alikuwa akimpenda sana mama yake. Alikuwa kila anapotaka kutoka nje ya nyumba akisimama mbele ya chumba chake na kumuamkia:

"Assalaam alaykum wa Rahmatullahi wa Barakatuh ewe mama yangu."

Na mama yake hujibu:

"Wa alayka ssalaam wa Rahmatullahi wa Barakatuh ewe mwanangu."

Kisha Abu Hurayrah husema:

"Allaah Akurehemu kama ulivyonilea nilipokuwa mdogo."

Na mama yake husema:

"Na wewe Akurehemu kama unavyonipenda ukiwa mkubwa."

Na anaporudi nyumbani alikuwa akifanya hivyo hivyo.

Alikuwa akipenda sana kuwakumbusha watu kuwatendea mema wazazi wao na kuunganisha na kuuendeleza uhusiano wa ndugu na jamaa.

Siku moja aliona watu wawili wakitembea, mmoja wao akiwa mkubwa wa umri, akamuuliza yule mdogo:

"Nani huyu uliyefuatana naye?"

Akamuambia:

"Baba yangu."

Akamuambia:

"Basi usimuite kwa jina lake, wala usitembee mbele yake wala usikae kabla yake."

 

Akimpenda sana Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam)

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) alikuwa akimpenda sana Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) mapenzi yasiyoweza kuelezeka. Alikuwa hachoki kumtizama, na alikuwa akisema:

"Sijaona kitu kizuri kinachoufurahisha moyo kuliko kuungalia uso wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam). Kama kwamba jua linaangaza katika uso wake mtukufu."

Alikuwa akimshukuru Allaah kwa Kumjaalia kuwa pamoja naye na kuwa sahibu yake. Alikuwa akisema:

"Namshukuru Allaah kwa Kumhidi Abu Hurayrah. Namshukuru Allaah Aliyemfundisha Abu Hurayrah Qurani (Qur-aan). Namshukuru Allaah kwa Kumjaalia Abu Hurayrah kuwa sahibu yake Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam).”

 

Elimu yake

Kama alivyokua akimpenda Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam), Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) alikuwa pia akiipenda elimu na akaifanya kuwa ni lengo lake kubwa.

Anasema Zayd bin Thaabit (Radhiya Allaahu 'anhu):

"Siku moja mimi na Abu Hurayrah pamoja na sahibu yangu mmoja tulipokuwa msikitini tukimuomba Allaah na kumdhukuru, aliingia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) akasimama mbele yetu kisha akakaa pamoja na sisi. Tukanyamaza. Akasema:

"Endeleeni na yale mliyokuwa mkifanya."

Tukamuomba Allaah mimi na sahibu yangu kabla ya Abu Hurayrah. Kisha Mtume wa Allaah akamtaka Abu Hurayrah naye aombe, na Abu Hurayrah akanyanyua sauti yake akaomba:

"Mola wangu nakuomba na mimi unipe yote waliyotangulia kukuomba sahibu zangu, na nakuomba elimu isiyosahaulika."

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) akasema:

"Aamiyn."

Tukasema:

"Na sisi tunamuomba Allaah elimu isiyosahaulika."

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) akasema:

"Keshakutangulieni kijana wa kabila la Al Dawsiy (Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu))."

Maadui wa haki wanadai kuwa eti wanashangazwa vipi Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) ameweza kukusanya maelfu kwa maelfu ya hadithi katika miaka michache aliyoishi pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam), lakini ukweli uliothibiti kwa dalili ni kuwa katika vitabu sita maarufu vya Masunni na katika Muwata-a cha Imam Malik hadithi za Abu Hurayrah zilizopokelewa na kukubaliwa ndani yake idadi yake ni 2218 tu. Katika vitabu vya Sahih Al-Bukhaariy na Sahih Muslim mna hadithi 609 tu za Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) na walizokubaliana juu yake Al-Bukhaariy na Muslim ni 326, ziko wapi sasa hizo hadithi maelfu kwa maelfu?

Inajulikana kuwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) alisilimu mwaka wa saba baada ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) kuhajiri kwenda Madina na umri wake wakati ule ulikuwa miaka thelathini, na alikuwa akiishi as-Suffah (sehemu iliyoshikamana na msikiti wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) mahali walipokuwa wakiishi wageni masikini), na alikuwa daima pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam), hambanduki, kila anapokwenda alikuwa naye mpaka Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) alipofariki dunia.

Mtu aliyejitolea kutafuta elimu na kusikiliza hadithi za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) hatoshindwa kukusanya idadi hiyo ya hadithi.

Isitoshe Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) alikuwa na wanafunzi wengi waliopokea kutoka kwake hadithi hizo na kuzieneza, na miongoni mwa Hadithi alizozisimuliwa Abu Hurayrah zimo ndani yake maneno ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) aliyoyasikia yeye mwenyewe kutoka kinywani mwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) na nyngine ni juu ya matendo ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) na zipo hadithi ambazo Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) amesimulia juu ya aliyoyasikia kutoka kwa Masahaba wengine (Radhiya Allaahu 'anhu) yale ambayo Masahaba hao waliyasikia kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam).

Zipo pia hadithi nyingi zisizosihi isnadi, yaani hadithi alizosingiziwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kuwa amesimulia na ukweli ni kuwa yeye hakuzisimulia hadithi hizo. Tunamshukuru Allaah kwa Kutuletea maulamaa wa hadithi walioweza kuzichambua hadithi hizo na kutuletea zile zilizosihi tu na wakatujulisha juu ya zile zisizokuwa sahihi.

Imepokelewa kuwa siku moja Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) alimuendea Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) kumshitakia udhaifu wake wa kuhifadhi, na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) akamwambia: ‘‘Itandaze nguo yako’’, na alipoitandaza akamuombea dua kisha akamuambia; "Sasa jifunike nayo", akajifunika, na tokea siku ile hakusahau tena hadithi.

Hadithi hii imesimuliwa na Al-Bukhaariy na wengineo, na haimo ndani ya vitabu vya maulamaa wa Kisunni peke yao, bali imo hata ndani ya vitabu vya hadithi vya Kishia.

Imeandikwa katika kitabu cha ‘Al Kharaij’ (1/75) na katika ‘Bihar al Anwar’ (18/913) mlango wa ‘Miujiza ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) na kukubaliwa kwa dua zake’ kuwa; Abu Hurayrah alimwambia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam): ‘Mimi nasikia kutoka kwako hadithi nyingi kisha nazisahau’ Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) akamuambia; ‘Tandaza guo lako lote’, akatandaza kisha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) akauweka mkono wake ndani yake kisha akamwambia; ‘Jifunike nalo’,  ‘nikajifunika’ anasema Abu Hurayrah; ‘na tokea siku hiyo sijasahau tena hadithi’.

Wakati watu wa Madina walipokuwa wakijishughulisha na biashara na ukulima, Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) alijishughulisha na kujikurubisha kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) huku akihifadhi hadithi zake. Alikuwa akisema: "Sahibu zangu katika watu wa Makkah walikuwa wakijishughulisha na biashara masokoni, na sahibu zangu katika watu wa Madina walikuwa wakijishughulisha na kilimo, lakini mimi nilikuwa masikini niliyetumia muda wangu mwingi kukaa pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam). Nilikuwa nikihudhuria wasipohudhuria, na nikihifadhi wanaposahau. Na Wallahi lau kama si ile aya iliyomo ndani ya kitabu cha Allaah nisingehadithia hadithi yoyote. Allaah anasema: "Hakika wale wanaoficha Tuliyoyateremsha baada ya Sisi kuzibainisha kwa watu Kitabuni -- hao Anawalaani Allaah, na wanawalaani kila wenye kulaani." Al Baqarah- 159

 

Akiwapendelea wenzake elimu

Kama alivyokuwa akiipenda elimu, Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) alikuwa pia akiwapendelea wenzake waipate.

Siku moja alipokuwa akipita sokoni na kuona namna gani watu walivyokuwa wakijishughulisha na biashara pamoja na dunia, akawaambia:

"Uvivu ulioje mlio nao enyi watu wa Madina."

Wakasema:

"Uvivu gani uliotuona nao ewe Abu Hurayrah?"

Akasema:

"Urithi wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) unagawiwa na nyinyi mpo hapa? Kwa nini na nyinyi hamuendi mkachukua sehemu yenu?"

Wakasema:

"Ni wapi huko ewe Abu Hurayrah?"

Akasema:

"Msikitini."

Wakatoka mbio kuelekea msikitini, na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) alisimama pale akiwasuburi warudi, na walipomuona wakamuambia:

"Ewe Abu Hurayrah, tumekwenda msikitini tukaingia ndani lakini hatukuona chochote kikigawiwa."

Akawauliza:

"Na hamkumuona mtu yeyote msikitini?"

Wakasema:

"Ndiyo, tumeona watu wanasali na wengine wanasoma Qur-aan na wengine wanakumbushana katika mambo yaliyohalalishwa na yaliyoharamishwa…"

Akasema:

"Ole wenu! Huo ndio urithi wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam)."

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) aliishi wakati wa Makhalifa waongofu (Radhiya Allaahu 'anhu) na pia wakati wa ukhalifa wa Muawiya (Radhiya Allaahu 'anhu). Alitembelea nchi nyingi sana za Kiislamu katika wakati wake, lakini makao makuu yake yalikuwa Madina, mji wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam), mji alioupenda sana akaishi ndani yake sehemu kubwa ya maisha yake mpaka alipofariki dunia.

Mbali ya kuhudhuria darsa za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam), Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) alijifunza elimu kutoka kwa 'Umar bin Al-Khatwaab (Radhiya Allaahu 'anhu) na Masahaba wengi wakubwa na alihitimu Qur-aan  kutoka kwa sahaba maarufu Ubay bin Ka'ab (Radhiya Allaahu 'anhu).

 

Muujiza wa birika la maziwa

Kutokana na kujishughulisha kwake na darsa za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) pamoja na kutafuta elimu, Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) alipambana na matatizo ya kujipatia riziki yake.

Hebu tumsikilize Abu Hurayrah mwenyewe (Radhiya Allaahu 'anhu) akituhadithia:

"Nilikuwa nikishikwa na njaa nikawa wakati mwingine namsimamisha mmoja katika Sahaba wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) namuuliza juu ya tafsiri ya aya katika  Qur-aan wakati mimi naijua tafsiri hiyo, namuuliza ili anikaribishe nyumbani kwake nipate kuingiza chochote kinywani mwangu.  

Siku moja njaa kali ilinishika ikanibidi nifunge jiwe tumboni, nikasimama njiani, akapita mbele yangu Abu Bakar nikamuuliza juu ya aya katika kitabu cha Allaah, na nilimuuliza ili apate kunikaribisha tu lakini hakunikaribisha. Kisha akapita 'Umar bin Al-Khatwaab  nikamuuliza juu ya aya, naye pia hakunikaribisha. Mpaka alipopita Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) akafahamu juu ya njaa niliyonayo akaniambia:

"Ewe Abu Hurayrah."

Nikamuambia:

"Labbayka ewe Mtume wa Allaah."

Akaniambia:

“Nifuate.”

Nikamfuata na kuingia naye nyumbani. Akaona birika lenye maziwa ndani yake, akawauliza watu wa nyumba yake:

"Mumepata wapi maziwa haya?"

Wakasema:

"Mtu fulani ameleta."

Akasema:

"Ewe Abu Hurayrah, nenda kawaite watu wa 'Suffah' (Watu wa Suffah ni wageni mafakiri wasio na watu wala watoto wala mali pale Madina). Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) aliwajengea mahali karibu na msikiti.

Nikasema nafsini mwangu:

"Haya maziwa hayawezi kuwatosha watu wa Suffah."

Nilitamani ninywe angalau fundo moja ya maziwa yale ili nipate nguvu kabla ya kwenda kuwaita. Nikawasili kwa watu wa Suffah na kuwaita, wakaja na kukaa wote mbele ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) akaniambia:

"Chukua ewe Abu Hurayrah wape."

Nikaanza kuwapa. Kila mtu akanywa katika maziwa yale mpaka akashiba. Baada ya kuwamaliza nikampa birika Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) aliyeunyanyua uso wake kunitizama huku akitabasamu akaniambia:

"Tumebaki mimi na wewe."

Nikasema:

"Umesema kweli ewe Mtume wa Allaah."

Akaniambia:

"Kunywa."

Nikanywa, kisha akasema:

"Kunywa (bado)."

Nikaendelea kunywa huku akinitaka niendelee mpaka nilipomuambia:

"Naapa kwa yule aliyekuleta kwa haki, hamna tena nafasi tumboni mwangu."

Akakichukua kile chombo na kunywa maziwa yaliyobaki."

 

Alitajirika bila kubadilika

Haikupita miaka mingi tokea wakati ule, Waisalmu wakaanza kupata nguvu na kuteka miji mingi na kupata mali nyingi kutokana na ngawira zilizopatikana vitani, na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) naye pia akaweza kujijengea nyumba, akawa na mke na watoto sawa kama Waislamu wengine waliofaidika na mali za ngawira zilizowafikia kutoka nchi mbali mbali walizoteka.

Hata hivyo, yote hayo hayakuweza kubadilisha mwenendo na tabia za Sahaba huyu mtukufu (Radhiya Allaahu 'anhu), na pia hayakuweza kumsahaulisha zama zilizopita. Alikuwa akipenda kusema:

"Nilizaliwa yatima, nikahama nikiwa masikini. Nilifanya kazi kwa Busrah binti Ghazawan kwa malipo yaliyoniwezesha kupata chakula tu. Nilikuwa nikiwahudumia watu wake kuwapandisha farasi na kuwashusha na kuwaendesha, na sasa Allaah Ameniwezesha kumuoa Busrah. Namshukuru Allaah Aliyeisimamisha dini na kumfanya Abu Hurayrah kuwa kiongozi.

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) alichaguliwa zaidi ya mara moja na Muawiyah bin Abu Sufyan (Radhiya Allaahu 'anhu) kuwa gavana wa Madina, lakini ugavana huo haukumbadilisha mwenendo wake wala tabia zake njema.

 

Abu Hurayrah na  'Umar bin Al-Khatwaab (Radhiya Allaahu 'anhu)

Wakati wa ukhalifa wa Umar bin Khattab (Radhiya Allaahu 'anhu) alimpa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) ugavana wa nchi ya Bahrain. Na Ummar kama anavyojulikana alikuwa mtu mkali sana hasa anapomtawaza mtu kumpa ugavana kisha baada ya muda mtu huyo akaweza kutajirika. Inajulikana kuwa  'Umar bin Al-Khatwaab (Radhiya Allaahu 'anhu) ni mtu wa mwanzo duniani kuanzisha nidhamu ya 'Jieleze mali hii umepata vipi.'

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) alipopewa ugavana wa Bahrain aliweza kupata utajiri kwa njia za kihalali, kutokana na malipo kama wanavyolipwa magavana, na alizitumia pesa zake katika biashara mbali mbali za halali.

Hebu tumsikilize Abu Hurayrah mwenyewe akituhadithia juu ya mkasa wake na   'Umar  (Radhiya Allaahu 'anhu).

Anasema Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu):

"'Umar bin Al-Khatwaab  aliniambia kwa ghadhabu: 'Ewe adui wa Allaah na adui wa Kitabu Chake! Umeiba mali ya Allaah."

Nikamuambia:

"Mimi si adui wa Allaah wala si adui wa Kitabu Chake, bali ni adui wa maadui wa Allaah na adui wa maadui wa Kitabu Chake na wala sijaiba mali ya Allaah."

Akasema:

"Umepata wapi mali yote hii."

Nikamuambia:

"Kutokana na farasi wangu waliozaa na malipo niliyokuwa nikilipwa."

 Umar bin Al-Khatwaab akaniambia:

"Zipeleke zote katika nyumba ya hazina ya Waislamu."

Nikampa mali yote 'Umar bin Al-Khatwaab kisha nikanyanyua mikono yangu mbinguni nikasema:

"Mola wangu Msamehe Amiri wa Waislamu."

Hazikupita siku nyingi 'Umar bin Al-Khatwaab  (Radhiya Allaahu 'anhu) alimuita tena Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) na kumtaka arudi kuwa gavana wa Bahrain, lakini Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) alikataa.

 'Umar bin Al-Khatwaab   (Radhiya Allaahu 'anhu) akamuuliza:

"Kwa nini unakataa?"

Akasema:

"Ili heshima yangu isivunjwe na mali yangu isichukuliwe."

Kisha akasema:

"Na naogopa kuhukumu bila ya elimu na kusema bila ya huruma."

 

Ucha Mungu wake

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) alikusanya elimu na ucha Mungu. Alikuwa mchana akipenda kufunga na katika thuluthi za mwanzo za usiku kila siku alikuwa akinyanyuka kusali, na anapomaliza alikuwa akimuamsha mkewe ili naye apate kusali na yeye huenda kupumzika. Na katika theluthi ya mwisho ya usiku baada ya mkewe kumaliza kusali alikuwa akimuamsha binti yao. Na kwa ajili hii ibada ilikuwa ikiendelea usiku kucha ndani ya nyumba yake.

 

Mali yote nishaigawa

Binti wa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) siku moja alimuambia baba yake:

"Ewe baba yangu, shoga zangu wananicheka, wananiambia: "Kwa nini baba yako hakununulii dhahabu ukavaa kama wanawake wengine?"

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) akamuambia:

"Ewe binti yangu, waambie kuwa baba yangu ananiogopea moto wa Jahannam."

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) hakuwa akimnyima binti yake kwa ajili ya ubakhili au kwa sababu yoyote nyingine, kwani alikuwa mkarimu sana aliyekuwa akitumia mali yake yote katika njia ya Allaah.

Siku moja Marwaan bin Al-Hakam alimpelekea Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) Dinari mia za dhahabu, na siku ya pili Marwaan akamtuma mtu kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kumuambia:

"Mtumishi wangu jana alikosea alipokuletea dinari zile, nilimtuma ampelekee mtu mwengine akakuletea wewe."

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) akamuandikia Marwaan kumuambia:

"Pesa zote ulizoleta nishazitoa sadaka katika njia ya Allaah na sikubakisha nyumbani kwangu hata dinari moja. Kwa hivyo yatakapotokea malipo yangu kutoka katika nyumba ya hazina chukua  badala yake."

Si kweli kuwa Marwaan alikosea alipompelekea pesa zile, bali alitaka kumjaribu tu. Na alipofanya uchunguzi aligundua kuwa maneno ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) ni sawa kama alivyosema.

 

Kifo chake 

Alipoumwa maradhi yake ya mwisho zilienea habari katika mji wa Madina na vitongoji vyake kuwa mmojawapo wa Masahaba wakubwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) anaumwa sana.

Watu wengi walimiminika nyumbani kwake kumtembelea na kumuombea dua. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) alinyanyua kichwa chake na kuwatizama huku akilia. Na alipoulizwa kwa nini analia, akasema:

"Hakika mimi siililii dunia yenu hii, bali naililia safari ndefu na zawadi chache nilizochukua  Nimesimama katika njia panda. Mojawapo inaelekea Peponi na nyingine Motoni. Na mimi sijui njia ipi nitakayoelekea."

 Alipokuja Marwaan bin Al-Hakam kumtembelea katika maradhi yake hayo alimuambia:

"Allaah Atakupa uzima na utapona Insha-Allah."

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) akajibu:

"Mola wangu, mimi napenda kukutana nawe. Nakuomba na Wewe upende kukutana nami na uniharakishie."

Alifariki dunia kabla ya Marwaan kuondoka mjini hapo katika mwaka wa 59 Hijri akiwa na umri wa miaka 78, na alizikwa katika makaburi ya Al-Baqiy'i.

 

Baadhi ya sifa zake

1.    Masahaba wengi na maulamaa wengi wamemsifia sana Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) na wameisifia elimu yake:-

2.    Anasema Abu   Sa'iyd, al Khudry (Radhiya Allaahu 'anhu): "Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) amesema: "Abu Hurayrah ni chombo cha elimu."

3.    Amesema Imam Shaafi'iy: “Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) hodari wa kuhifadhi kupita wote wenye kuhifadhi hadithi katika wakati wake”.

4.    Imam Al-Bukhaariy naye amesema yafuatayo juu ya Abu Hurayrah: “Maulamaa wapatao mia nane wamepokea hadithi kutoka kwake, na alikuwa hodari wa kuhifadhi kupita watu wote wa elimu ya hadithi wa zama zake.”

5.   

Uwezo mkubwa wa kuhifadhi unatokana na baraka za ile dua aliyoombewa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam).

 

Marejeo:

Siyar aalam an-Nubalaa

Al Imam Adh-Dhahabiy

Suwaru min siyar as Sahabah

Abdul Hamid al Suhaybany

Rijaal hawla Ar-Rasuul

Dr. Khaalid Muhammad Khaalid

 

Share