11-Ruqyah: Kutafuta Shifaa Kwa Hijaamah

Ruqyah: Kinga Na Tiba Katika Shariy'ah

 

Kutafuta Shifaa Kwa Hijaamah

 

www.alhidaaya.com

 

 

Miongoni mwa mwongozo wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika kutafuta shifaa ya maradhi mbali mbali, ni kufanya hijaamah kama alivyosema:

خَيرُ ما تَداوَيتُم به الحِجامةُ

((Lilokuwa bora kabisa kwa tiba zenu ni Hijaamah)) [Hadiyth ya Samurah bin Jundub – As-Silsilah Asw-Swahiyhah (1053)]

 

Hijaamah inajulikana kama ni chuku au kuumikwa; nayo ni kuvutwa damu chafu yenye madhara kutoka sehemu kadhaa za mwilini kwa kuchanjwa kisha kuvutwa hiyo damu kwa pembe au aina ya kikombe cha gilasi.

 

Hadiyth kadhaa zimetaja umuhimu wa kutafuta shifaa kwa hijaamah, baadhi yake zimetaja na mengineyo kama kayyah (tiba ya kuchomwa moto kwa chuma), na pia  asali ambayo imeshatangulia kutajwa, na, Qiswtw Al-Bahr (au Qiswtw Al-Hind) hinnah n.k.

 

Qistw Al-Bahr au Qistw Al-Hind ni aina ya vijiti ambavyo vinasagwa kutoa unga wake na kutumiwa kama dawa ya maradhi mbali mbali.

 

  

Zifautazo ni Hadiyth chache za kuhusu tiba kwa hijaamah:

 

Kila Malaika mbinguni alimuusia Rasuli wa  Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ummah wake wafanye hijaamah, pindi alipokuwa katika safari ya Al-Israa Wal-Mi’raaj. Na ikabainishwa kuwa tarehe za kupaswa kufanywa hijaamah ni tarehe kumi na saba, kumi na tisa, na ishirini na moja ya miezi ya Hijriy.

 

Hadiyth ya ‘Abdullaah bin ‘Abbaas na Ibn Mas‘uwd (Radhwiya Allaahu 'anhumaa):

 

خَيرُ يومٍ تَحْتَجِمُونَ فيه سبعُ عَشْرةَ، و تِسعُ عشْرةَ، وإِحدَى و عِشرينَ. وما مَرَرْتُ بِمَلأٍ من الملائِكةِ لَيلةَ أُسْرِيَ بِي إِلَّا قالُوا : عليكَ بِالحِجامةِ يَا مُحمَّدُ

((Siku bora kabisa za kufanya hijaamah kwenu ni tarehe kumi na saba, kumi na tisa na ishirini na moja, na sijampitia Malaika yeyote yule usiku wa Israa isipokuwa walisema: Himiza kufanya hijaamah yaa Muhammad)) [Swahiyh Al-Jaami' (3332)]

 

 

عَنْ ابْنِ عَبَّاسٍ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا) عَنْ النَبِيِّ (صَلَّى الله عَلَيْهِ وَسَلَّم ) قَالَ: ((الشِّفَاءُ فِي ثَلاَثَةٍ:  شَرْبَةِ عَسَلٍ وَشَرْطَةِ مِحْجَمٍ وَكَيَّةِ نَارٍ وَأَنْهَى أُمَّتِي عَنْ الْكَيِّ ))

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Shifaa inapatikana kutokana na matatu; kinywaji cha asali, hijaamah [kuumikwa, chuku], na kayyah (tiba ya kuchomwa moto kwa chuma), lakini nakataza Ummah wangu na kayyah) [Al-Bukhaariy]

 

 

Tanbihi kuhusu kayyah (tiba ya kuchomwa moto kwa chuma).

 

Ingawa tiba hii ameitaja Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) lakini mwenyewe akasema kuwa anaikataza. ‘Ulamaa wameona kwamba imekusudiwia itumike tiba hii pale inapokuwa ni dharura tu, baada ya kushindwa kupata aina nyinginezo za matibabu. Na kwa sababu kuchomwa moto ni katika aina adhabu ya moto, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amewasifu wenye kutawakali kwa Allaah (‘Azza wa Jalla) (kuliko wale wenye kutafuta kinga). [Fataawaa Al-Lajnah Ad-Daaimah (1445), Mawqi’  Ar-Rasmiy li-Imaam Ibn Baaz]

 

 

عَنْ أَنَسٍ رضى الله عنه أَنَّهُ سُئِلَ عَنْ أَجْرِ الْحَجَّامِ، فَقَالَ احْتَجَمَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم حَجَمَهُ أَبُو طَيْبَةَ، وَأَعْطَاهُ صَاعَيْنِ مِنْ طَعَامٍ، وَكَلَّمَ مَوَالِيَهُ فَخَفَّفُوا عَنْهُ، وَقَالَ: ((إِنَّ أَمْثَلَ مَا تَدَاوَيْتُمْ بِهِ الْحِجَامَةُ وَالْقُسْطُ الْبَحْرِيُّ ‏))‏ وَقَالَ: ‏((لاَ تُعَذِّبُوا صِبْيَانَكُمْ بِالْغَمْزِ مِنَ الْعُذْرَةِ، وَعَلَيْكُمْ بِالْقُسْطِ))

Kutoka kwa Anas (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba aliulizwa kuhusu ujira wa mtu anayewafanyia watu hijaamah. Akasema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alifanyiwa hijaamah na Abuu Twayyibah akampa swaa’aah mbili (pishi mbili) za chakula, akazungumza na mabwana zake kuwaomba wampunguzie gharama au kodi waliyokuwa wakimtoza kila siku. Kisha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Dawa bora kabisa yenu kutumia ni kufanya hijaamah, na Qistw Al-Bahr)). Akasema: ((Msiwatese watoto wenu kwa kutibu tezi za koo au kimio kwa kubinya kaakaa (sakafu) ya mdomo na tumieni Qistw))  [Al-Bukhaariy – Kitaab Atw-Twibb]

 

  

كان إذا اشْتَكَى أحدٌ رأسَهُ قال: ((اذْهَبْ فَاحْتَجِمْ))، و إذا اشْتَكَى رِجْلَهُ قال: ((اذْهَبْ فَأخْضِبْها بِالحِنَّاءِ))

Ilikuwa pindi mtu anapolalamika kuumwa kichwa, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: ((Nenda ukafanye hijaamah)) na alipolalamika mtu mguu wake alisema: ((Nenda kaupake hinnah)) [Hadiyth ya Salmah Umm Raafi’ Mtumishi wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) – Swahiyh Al-Jaami’ (4671), As-Silsilah Asw-Swahiyhah (2059)]

 

 

Nyakati na siku bora za kufanya hijaamah:

 

 عَنِ ابْنِ عُمَرَ، قَالَ يَا نَافِعُ قَدْ تَبَيَّغَ بِيَ الدَّمُ فَالْتَمِسْ لِي حَجَّامًا وَاجْعَلْهُ رَفِيقًا إِنِ اسْتَطَعْتَ وَلاَ تَجْعَلْهُ شَيْخًا كَبِيرًا وَلاَ صَبِيًّا صَغِيرًا فَإِنِّي سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم يَقُولُ: ((الْحِجَامَةُ عَلَى الرِّيقِ أَمْثَلُ وَفِيهِ شِفَاءٌ وَبَرَكَةٌ وَتَزِيدُ فِي الْعَقْلِ وَفِي الْحِفْظِ فَاحْتَجِمُوا عَلَى بَرَكَةِ اللَّهِ يَوْمَ الْخَمِيسِ وَاجْتَنِبُوا الْحِجَامَةَ يَوْمَ الأَرْبِعَاءِ وَالْجُمُعَةِ وَالسَّبْتِ وَيَوْمَ الأَحَدِ تَحَرِّيًا وَاحْتَجِمُوا يَوْمَ الاِثْنَيْنِ وَالثُّلاَثَاءِ فَإِنَّهُ الْيَوْمُ الَّذِي عَافَى اللَّهُ فِيهِ أَيُّوبَ مِنَ الْبَلاَءِ وَضَرَبَهُ بِالْبَلاَءِ يَوْمَ الأَرْبِعَاءِ فَإِنَّهُ لاَ يَبْدُو جُذَامٌ وَلاَ بَرَصٌ إِلاَّ يَوْمَ الأَرْبِعَاءِ أَوْ لَيْلَةَ الأَرْبِعَاءِ))

Ibn ‘Umar amesema: Ee Naafi’! Damu inanichemka, nitafutie mfanya hijaamah, lakini ukiweza tafuta mtu mpole na si mzee au kijana kwani nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Hijaamah ni bora linapokuwa tumbo ni tupu kwani mna shifaa na barakah na inazidisha uwerevu na kuhifadhi kumbukumbu. Basi fanyeni hijaamah kwa barakah za Allaah siku za Alkhamiys, na epukeni hijaamah Jumatano, Ijumaa, Jumamosi na Jumapili. Fanyeni hijaamah Jumatatu na Jumanne kwani  hiyo ni siku ambao Allaah Alimpa afya (Nabiy) Ayyuwb kutokana na balaa (la maradhi), na alimsibu balaa la maradhi siku ya Jumatano, na ukoma na ubarasi hautokei isipokuwa Jumatano, au usiku wa Jumatano)) [Ibn Maajah – As-Silsilah Asw-Swahiyhah (766)]

 

 

 

 

 

 

 

Share