02-Hadiyth Za Ramadhwaan Na Mafunzo: Milango Ya Jannah Hufunguliwa Milango Ya Moto Hufungwa

 

Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo

 

02-Milango Ya Jannah Hufunguliwa Milango Ya Moto Hufungwa

 

 

 

 

عن أبي هريرة رضي الله عنه قال: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: (( إِذَا دَخَلَ رَمَضَانُ فُتِّحَتْ أَبْوَابُ الجَنَّةِ ، وَغُلِّقَتْ أَبْوَابُ جَهَنَّمَ ، وَسُلْسِلَتِ الشَّيَاطِينُ )

 

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu)  akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)    amesema: ((Ikiingia Ramadhwaan, milango ya Jannah hufunguliwa, milango ya Moto hufungwa, na mashaytwaan hutiwa minyonyoro)) [Al Bukhaariy (3277) na Muslim (1079)]

 

 

Mafunzo:

 

 

Hadiyth hii inatakikana ichukuliwe kwa ufahamu huu ulioelezewa kwa uhalisia wake kwamba milango ya Jannah hufunguliwa na kuachwa wazi, milango ya moto hufungwa, na mashaytwaan hutiwa minyonyoro wasiweze kufurukuta. Asili ni kuchukuliwa kwa mwonekano huu mpaka ije dalili ya kupindua maana kusudiwa.

 

 

Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) aliulizwa swali lisemalo: “Hadiyth hii ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)   inasema mashaytwaan hufungwa pingu na kutiwa minyororo katika mwezi huu lakini pamoja na hayo tunawaona watu wakipandwa na mashaytwaan na pia wakimwasi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  mchana wa mwezi huu? Vipi mashaytwaan watiwe minyororo na baadhi ya watu waendelee kupandwa na mashaytwaan na kuasi?”

 

Sheikh alijibu akisema: “Yaliyotajwa katika Hadiyth hii ni mambo ya ghaibu. Wajibu wetu sisi ni kuyasadiki, kuyakubali na kutojaribu kuzungumzia yaliyo nyuma yake. Hivi kunakuwa ni salama zaidi kwa Dini ya mtu na salama zaidi kwa hatima yake”.

‘Ulamaa wengine wanasema kuwa jawabu la swali kama hilo linakuwa kama ifuatavyo:

 

Kwanza: Hufungwa kwa wafungaji swawm iliyo kidhi vigezo na masharti, si swawm tu mradi swawm. Mfungaji wa swawm kama hii hana kinga dhidi ya shaytwaan.

 

 

Pili: Kuna sababu nyinginezo nyingi za kufanyika maasia na shari. Si shaytwaan tu ndiye chanzo cha shari zote bali nafsi khabithi, desturi mbaya na mashaytwaan wa kibinaadamu ni sababu pia za maasia.

 

Tatu: Wanaofungiwa ni mashaytwaan sugu wabaya. Ama mashaytwaan wa kawaida wasio na athari kubwa kwa watu, hao hawafungwi. Na hii ndio sababu ya kupungua sana maasia katika mwezi wa Ramadhwaan kulinganisha na miezi mingineyo.

 

‘Ulamaa wengine wanasema kuwa kutiwa pingu mashaytwan kuna maanisha kushindwa kwao kuwarubuni wafungaji swawm na kuwazainia matamanio.

 

Wengine wanasema kuwa shaytwaan aliyefungwa anaweza pia kusababisha adha, lakini adha yake si kama ya yule aliye huru.

 

 

Ama hikma ya kufunguliwa milango ya Jannah na kufungwa milango ya moto, ‘Ulamaa wanasema ni kuwa katika mwezi huu wa Ramadhwaan, nyoyo za Waumini huchangamkia kheri na matendo mema yanayokuwa sababu ya kufunguliwa milango hiyo, na hujizuia na maasia na madhambi ambako kunakuwa ni sababu ya kufungwa milango ya moto. Na hii ni ishara kubwa juu ya utukufu na fadhila za mwezi huu wa Ramadhwaan.

 

 

 

Share