05-Hadiyth Za Ramadhwaan Na Mafunzo:Swawm Ni Ngao
Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo
05-Swawm Ni Ngao
عن عثمان بن عفان رضي الله عنه، قال: سمعت رسول الله صلى الله عليه وسلم يقول: الصِّيامُ جُنَّةٌ من النَّارِ ، كَجُنَّةِ أحدِكمْ من القِتالِ))
Imepokelewa toka kwa ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhwiya Allaahu 'anhu) akisema: “Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Swiyaam ni ngao dhidi ya moto, kama ngao ya mmoja wenu katika mapigano)) [Ibn Maajah, amiesahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh Ibn Maajah (1336), Swahiyh Al-Jaami’ (3879)]
Mafunzo:
Bila shaka makusudio makuu ya wenye akili ni kufuzu kwa kuingia Jannah (Peponi) na kuepushwa na moto wa Jahannam. Allaah (‘Azza wa Jalla) Anatuambia:
فَمَنْ زُحْزِحَ عَنِ النَّارِ وَأُدْخِلَ الْجَنَّةَ فَقَدْ فَازَ
Basi atakayewekwa mbali na moto na akaingizwa Jannah kwa yakini amefuzu. [Aal-‘Imraan: 185]
Na Anatuambia tena:
قُلْ إِنَّ الْخَاسِرِينَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنفُسَهُمْ وَأَهْلِيهِمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۗ أَلَا ذَٰلِكَ هُوَ الْخُسْرَانُ الْمُبِينُ ﴿١٥﴾
Sema: “Hakika waliokhasirika ni wale waliokhasiri nafsi zao na ahli zao Siku ya Qiyaamah. Tanabahi! Hiyo ndio khasara bayana.” [Az-Zumar: 15]
Hakuna mafanikio makubwa zaidi kuliko mtu kuingia Jannah (Peponi), na hakuna khasara kubwa zaidi kama mtu kuishilia motoni. Na haya ndiyo wanayoyaendea mbio watu wenye akili; kulipapia kila lile litakalowafikisha Jannah, na kujiepusha kwa nguvu zao zote na kila lile linalopelekea motoni.
Na swawm ni ‘ibaadah ambayo Allaah (‘Azza wa Jalla) Ameifanya kuwa ni kinga na ngao kwa mwenye Swawm. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametuambia katika Hadiyth:
عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ رضي الله عنه قَالَ : قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم: ((مَنْ صَامَ يَوْماً فِي سَبِيلِ اللَّهِ بَعَّدَ اللَّهُ وَجْهَهُ عَنْ النَّارِ سَبْعِينَ خَرِيفًا )) مسلم
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayefunga Swawm siku moja kwa ajili ya Allaah, Allaah Atamweka mbali uso wake na moto masafa ya miaka sabini)) [Muslim 2/208]
Na hii ni siku moja tu. Vipi ikiwa Mwislamu atafunga siku 100 kwa mfano wa siku kama hiyo katika maisha yake?! Mwislamu anaweza kuisikia Hadiyth kama hii lakini asiitie akilini au kuipa uzito. Lakini Mwislamu mwerevu na mjanja, kwa vile amejua kwamba akifunga siku kama hiyo atabaidishwa mbali na moto kwa urefu huo, basi mara moja huichangamkia na kuifunga siku kama hiyo hata angalau mara moja katika umri wake wote.
Na siku ya Qiyaamah, Waislamu wengi watajuta na kuhuzunika kutokana na kuiachilia nafasi kama hii na zinginezo ambazo zilikuwa ni kochokocho hapa duniani wakati watakapoona malipo makubwa yakitolewa kwa Waislamu wenzao werevu walioitumia kila nafasi ya kujichumia mambo ya kheri.
Hivyo basi ndugu yangu Mwislamu, wakati bado tunao wa kuweza kujichumia mengi ya kutufaa huko Aakhirah kuliko kupoteza umri wetu katika mambo yasiyo na faida.
Ngao hii ya swawm dhidi ya moto kwa mfungaji, ni lazima iwe ni ngao ya kumzuia mfungaji huyo na maasia hapa duniani, ili iweze kuwa ni ngao kwake dhidi ya moto Siku ya Qiyaamah. Ikiwa haitomkinga na maasia hapa duniani, basi haiwezi kumkinga na moto siku hiyo. Ni lazima imkinge hapa duniani na maneno machafu, matusi, masengenyo na matendo yote mabaya.
Baadhi ya watangu wema wamesema: “Masengenyo huitoboa Swawm, na istighfaar huikarabati, na mwenye kuweza miongoni mwenu asije na Swawm yenye kuvuja, basi afanye.”
Hakika mwenye Swawm amefungamanishwa na malipo na fadhla kutoka kwa Mola wake (‘Azza wa Jalla). Hivyo basi, awe na pupa ya kuzipata thawabu hizi kwa kutimiza masharti yake na kujiepusha na vizuizi vyake ili apate mradi tarajiwa wa kuepushwa na moto wa Jahannam.