07-Hadiyth Za Ramadhwaan Na Mafunzo: Mlango Wa Rayyan Peponi Wataingia Wenye Swawm

 

Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo

 

07-Mlango Wa Rayyan Peponi Wataingia Wenye Swawm

 

 

 

 

 عَنْ سَهْلِ بْنِ سَعْدٍ رضى الله عنه عَنِ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم قَالَ: (( فِي الْجَنَّةِ ثَمَانِيَةُ أَبْوَابٍ، فِيهَا باب يُسَمَّى الرَّيَّانَ لاَ يَدْخُلُهُ إِلاَّ الصَّائِمُونَ ‏)) البخاري

Imepokelewa toka kwa Sahl bin Sa’d (Radhwiya Allaahu 'anhu)  kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Peponi kuna milango minane. Humo kuna mlango uitwao Rayyaan, hawauingii isipokuwa Asw-Swaaimuwn (wafungaji)) [Al-Bukhaariy]

 

 

Mafunzo:

 

 

Mlango huu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameuweka maalumu kwa ajili ya wafungaji (Swawm) tu. Wafungaji peke yao ndio watakaopita kwenye mlango huu. Umeitwa Rayyaan kutokana na wingi wa mito inayopita kuelekea kwake pamoja na maua na matunda mazuri yenye kuuzunguka.

 

Pia umeitwa hivyo kwa kuwa mwenye kuufikia, kitamwondokea kiu kikali cha Siku ya Qiyaamah, na kisha atadumu milele na hali ya kutohisi kiu.

 

Aidha, umeitwa hivi kwa kuwa ni jazaa kwa wafungaji kutokana na kiu na njaa iliyokuwa ikiwakabili wakati wa swawm yao, nao wakasubiri na kuitii amri ya Mola wao mpaka wakati wa kufungua Swawm, na hususan kwa wale wenye kuishi kwenye nchi za joto kali.

 

Na hapa Hadiyth imegusia tu kiu kutokana na neno "ري" linalonyambuka toka “Ar Rayyaan” kwa kuwa mara nyingi kiu kinakuwa kikimsumbua zaidi mfungaji kuliko njaa, na mwana Aadam anaweza kusota kwa muda mrefu bila ya kula lakini hawezi kusota na kiu kwa zaidi ya wiki moja.

 

Kutokana na hali hiyo, mlango huu umewekwa spesheli na Allaah ('Azza wa Jalla) kwa wafungaji kwa ajili ya kuwakirimu kutokana na Swawm yao waliyoifanya hapa duniani na tabu ya kiu iliyowasumbua.

 

Lakini je wahusishwa hapa ni wale wenye kufunga Swiyaam za Ramadhwaan pekee?

 

‘Ulamaa wanatuambia kwamba wahusishwa hapa ni wale waliofunga Ramadhwaan pamoja na kushikamana na Swawm za Sunnah kama za Jumatatu na Alkhamisi, Ayyamul-biydwh (Masiku meupe) na kadhalika.

 

Lakini pia kuna mushkel mwingine wa kuunganisha kati ya Hadiyth hiyo na Hadiyth ifuatayo:

 

عَنْ عُمَرَ ‏ رضى الله عنه ‏ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏{ مَا مِنْكُمْ مِنْ أَحَدٍ يَتَوَضَّأُ، فَيُسْبِغُ اَلْوُضُوءَ، ثُمَّ يَقُولُ: أَشْهَدُ أَنْ لَا إِلَهَ إِلَّا اَللَّهُ وَحْدَهُ لَا شَرِيكَ لَهُ، وَأَشْهَدُ أَنَّ مُحَمَّدًا عَبْدُهُ وَرَسُولُهُ، إِلَّا فُتِحَتْ لَهُ أَبْوَابُ اَلْجَنَّةِ" } أَخْرَجَهُ مُسْلِم

Kutoka kwa ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Hakuna yeyote miongoni mwenu anayetawadha vizuri, kisha akasema: “Ash-hadu an laa ilaaha illa Allaah Wahdahu laa shariyka Lahu, wa ash-hadu anna Muhammad ‘Abduhuu wa Rasuwluhu” (Nashuhudia kuwa hapana mwabudiwa wa haki ila Allaah, Peke Yake, hana mshirika, na ninashuhudia kuwa Muhammad ni mja Wake na Rasuli Wake) ila   atafunguliwa milango minane ya Jannah.” [Imetolewa na Muslim na At-Tirmidhiy]

 

 

Hapa swali linakuja:

 

“Je, kiwa mtu huyu si katika wafungaji (Swawm), vipi aachiliwe milango yote minane ukiwemo mlango wa “Rayyaan” wakati mlango huu ni kwa wafungaji tu?”

 

Jibu linasema:

 

“Ni kweli atakuwa na uhuru kamili wa kuingia mlango wowote autakao. Lakini mlango wa “Rayyaan” hatouchagua, bali atachagua mwingine wowote. Kwa kuwa hapo, wataitwa wafungaji, wakishajitokeza wataambiwa waingie kwenye mlango huo kisha utafungwa. Hii ni kwa Hadiyth nyingine ifuatayo:  

 

عَنْ سَهْلٍ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((إِنَّ فِي الْجَنَّةِ بَابًا يُقَالُ لَهُ الرَّيَّانُ يَدْخُلُ مِنْهُ الصَّائِمُونَ يَوْمَ الْقِيَامَةِ لَا يَدْخُلُ مِنْهُ أَحَدٌ غَيْرُهُمْ يُقَالُ أَيْنَ الصَّائِمُونَ فَيَقُومُونَ لَا يَدْخُلُ مِنْهُ أَحَدٌ غَيْرُهُمْ فَإِذَا دَخَلُوا أُغْلِقَ فَلَمْ يَدْخُلْ مِنْهُ أَحَدٌ ))

Imepokelewa kutoka kwa Sahl (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakika katika Jannah kuna mlango unaitwa Rayyaan, wataingia humo siku ya Qiyaamah wenye kufunga (Swawm), hatoingia yeyote mwingine. Itasemwa: “Wako wapi waliokuwa wakifunga? Watasimama kuingia hatoingia yeyote mwengine, watakapoingia, utafungwa, basi hatoingia mwengine)) [Al-Bukhaariy 1763, Muslim 1947]

 

Kadhalika, milango mingine inayobaki pia ina watu wake. Kila mtu ataitwa kwa mujibu wa ubobezi wake kwenye ‘amali fulani. Haya yanathibitishwa na Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

عن أَبِي هُرَيْرَةَ، أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ: ((مَنْ أَنْفَقَ زَوْجَيْنِ فِي سَبِيلِ اللَّهِ نُودِيَ فِي الْجَنَّةِ: يَا عَبْدَ اللَّهِ هَذَا خَيْرٌ فَمَنْ كَانَ مِنْ أَهْلِ الصَّلاَةِ دُعِيَ مِنْ بَابِ الصَّلاَةِ وَمَنْ كَانَ مِنْ أَهْلِ الْجِهَادِ دُعِيَ مِنْ بَابِ الْجِهَادِ وَمَنْ كَانَ مِنْ أَهْلِ الصَّدَقَةِ دُعِيَ مِنْ بَابِ الصَّدَقَةِ وَمَنْ كَانَ مِنْ أَهْلِ الصِّيَامِ دُعِيَ مِنْ بَابِ الرَّيَّانِ))‏ ‏.‏ فَقَالَ أَبُو بَكْرٍ الصِّدِّيقُ:  يَا رَسُولَ اللَّهِ مَا عَلَى مَنْ يُدْعَى مِنْ هَذِهِ الأَبْوَابِ مِنْ ضَرُورَةٍ فَهَلْ يُدْعَى أَحَدٌ مِنْ هَذِهِ الأَبْوَابِ كُلِّهَا؟  قَالَ:  نَعَمْ وَأَرْجُو أَنْ تَكُونَ مِنْهُمْ ))

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mwenye kutoa dinari mbili fiy SabiyliLLah (katika njia ya Allaah) basi ataitwa: “Ee mja wa Allaah! Hii ni kheri.” Atakayekuwa ni katika watu wa Swalaah, basi ataitwa toka mlango wa Swalaah, na atakayekuwa ni katika watu wa Jihaad, ataitwa toka mlango wa Jihaad, na atakayekuwa ni katika watu wa Swadaqah, ataitwa toka mlango wa Swadaqah, na atakayekuwa ni katika watu wa Swiyaam, ataitwa toka mlango wa Ar-Rayyaan)) Abu Bakr Asw-Swiddiyq akasema: “Ee Rasuli wa Allaah! Hivi ni lazima mtu aitwe katika mlango mmojawapo tu kati ya milango hii? Je, hivi mtu anaweza kuitwa aingie milango yote?” Akasema: ((Naam! Na nataraji uwe miongoni mwao)) [Muwatwah bin Maalik Kitaab Al-Jihaad]

 

 

 

Share