12-Hadiyth Za Ramadhwaan Na Mafunzo: Fadhila Za Kuchelewesha Suhuwr (Daku)

 

Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo

 

12-Fadhila Za Kuchelewesha Suhuwr (Daku)

 

 

 

 عَنْ أَنَسٍ، عَنْ زَيْدِ بْنِ ثَابِتٍ ـ رضى الله عنه ـ قَالَ تَسَحَّرْنَا مَعَ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم ثُمَّ قَامَ إِلَى الصَّلاَةِ‏.‏ قُلْتُ : كَمْ كَانَ بَيْنَ الأَذَانِ وَالسَّحُورِ؟ قَالَ:   قَدْرُ خَمْسِينَ آيَةً‏ .‏

 

Imepokelewa toka kwa Anas aliyepokea toka kwa Zayd bin Thaabit (Radhwiya Allaahu 'anhu)   kuwa alisema: “Tulikula daku pamoja na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), kisha akanyanyuka kwenda katika Swalaah. Nikauliza: Kulikuwa na muda gani baina ya iqaamah na suhuwr (daku)? Akasema: “Kama Aayah khamsini hivi” [Al-Bukhaariy]

 

Mafunzo:

 

 

Hadiyth hii ni dalili ya kuwa imesuniwa kuchelewesha kula suhuwr (daku) hadi muda kidogo kabla ya Swalatul Fajr, kwani kitambo cha Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Zayd kumaliza kula daku na kuingia katika Swalaa kilikuwa ni kiasi cha kusoma mtu Aayah khamsini (50) za Qur-aan Tukufu kwa kisomo cha wastani; si cha haraka wala cha kuvuta sana. Na hii inaonyesha kwamba wakati wa Swalaah uko karibu na wakati wa kuanza siku mpya ya Swawm.

 

Lakini pamoja na hivyo, inajuzu kula suhuwr (daku) katikati ya usiku kama saa sita au saba, au hata kabla ya hapo kwa mujibu wa hali ya kila mmoja ingawa ni kinyume na Sunnah.

 

 

Mwislamu akila daku mapema, anaweza kulala na kupitwa na Swalaah ya Alfajiri pamoja na mengi ya kheri yanayopatikana nyakati za mwisho za usiku Alizoziita Allaah (‘Azza wa Jalla) katika Qur-aan  الاسحار,   neno ambalo السحور  (daku) limenyambulika toka hapo.

 

Mla suhuwr (daku) anatakikana ale kidogo kiasi cha kushiba. Asijaze tumbo, kwani kutamletea uvivu na uzito utakaosababisha kushindwa kufanya mengi ya kheri. Hata tembe chache tu za tende zinatosha kwa daku.

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

 

(( سحور المؤمن التمر))

((Suhuwr (Daku) ya Muumini ni tamr (tende))). [Abuu Daawuwd, na isnadi yake imenyooka]

 

 

 

Hadiyth hii pia inaonyesha kuwa imesuniwa suhuwr (daku) kuwa tende, au mlo pamoja na tende.

 

Sunnah hii wengi wameghafilika nayo wakidhani kuwa tende ni wakati wa kufungulia Swawm pekee.

 

 

 

 

 

 

 

 

Share