03-Wasiya Kumi Katika Mwisho Wa Suwrah Al-An’aam: Kutokuua Watoto

 

  Wasiya Kumi Katika Mwisho Wa Suwrah Al-An'aam  

 

03- Kutokuua Watoto

 

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَلَا تَقْتُلُوا أَوْلَادَكُم مِّنْ إِمْلَاقٍ ۖ نَّحْنُ نَرْزُقُكُمْ وَإِيَّاهُمْ ۖ

na wala msiwaue watoto wenu kutokana na umasikini. Sisi Tunakuruzukuni pamoja nao. [Al-An’aam: 151]

 

 

Makafiri walikuwa wakiwaua watoto wao ima kwa khofu ya kuwa hawatoweza kuwapatia chakula au kuwaua wasichana kwa sababu ya kuwadhalilisha. Siku ya Qiyaamah wataulizwa kuhusu dhulma hii, Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَإِذَا الْمَوْءُودَةُ سُئِلَتْ ﴿٨﴾

Na mtoto wa kike aliyezikwa hali akiwa yuhai atakapoulizwa.

 

 

بِأَيِّ ذَنبٍ قُتِلَتْ ﴿٩﴾

Kwa dhambi gani aliuliwa? [At-Takwiyr: 8-9]

 

 

Hadiyth za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

عَبْد اللَّه بْن مَسْعُود رَضِيَ اللَّه عَنْهُ أَنَّهُ سَأَلَ رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَآله وَسَلَّمَ ((أَيّ الذَّنْب أَعْظَم ؟)) قَالَ ((أَنْ تَجْعَل لِلَّهِ نِدًّا وَهُوَ خَلَقَك)) قُلْت ثُمَّ أَيّ  قَالَ ((أَنْ تَقْتُل وَلَدَك خَشْيَة أَنْ يُطْعَم مَعَك)) قُلْت ثُمَّ أَيّ ؟ قَالَ ((أَنْ تُزَانِي حَلِيلَة جَارك))  ثُمَّ تَلَا رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ   ((وَاَلَّذِينَ لَا يَدْعُونَ مَعَ اللَّه إِلَهًا آخَر وَلَا يَقْتُلُونَ النَّفْس الَّتِي حَرَّمَ اللَّه إِلَّا بِالْحَقِّ وَلَا يَزْنُونَ)) البخاري و مسلم

Kutoka kwa ‘Abdullaah bin Mas’uwd (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba alimuuliza Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): Dhambi gani kubwa? Akasema: ((Kumfanyia Allaah mshirika na hali Yeye Amekuumba)) Nikasema: Kisha ipi? Akasema: ((Kumuua mtoto wako kwa khofu ya kutoweza kumpatia chakula chake)) Nikasema kisha ipi? Akasema: ((Kuzini na mke wa jirani yako)) Kisha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasoma:

 

وَاَلَّذِينَ لَا يَدْعُونَ مَعَ اللَّه إِلَهًا آخَر وَلَا يَقْتُلُونَ النَّفْس الَّتِي حَرَّمَ اللَّه إِلَّا بِالْحَقِّ وَلَا يَزْنُونَ

Na wale ambao hawaombi pamoja na Allaah mwabudiwa mwengine na wala hawaui nafsi ambayo Allaah Ameiharamisha isipokuwa kwa haki [Al-Furqaan: 68]  [al-Bukhaariy na Muslim]

 

Ibn ‘Abbaas, Qataadah na As-Suddi na wengineo wamesema kuhusu: 

مِّنْ إِمْلَاقٍ

kutokana na umasikini

 

“Sio kuwaua kwa sababu nyinyi ni masikini. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema katika Suwratul-Israa:

 

وَلَا تَقْتُلُوا أَوْلَادَكُمْ خَشْيَةَ إِمْلَاقٍ ۖ نَّحْنُ نَرْزُقُهُمْ وَإِيَّاكُمْ ۚ إِنَّ قَتْلَهُمْ كَانَ خِطْئًا كَبِيرًا ﴿٣١﴾

Na wala msiue auladi wenu kwa kukhofia ufukara. Sisi Tunawaruzuku wao na nyinyi. Hakika kuwaua imekuwa ni hatia kubwa. [Al-Israa: 31]

 

Kutajwa wao kwanza kuwa Allaah Anawaruzuku kuna maana kwamba msikhofu umasikini kwa sababu ya kuwalisha watoto wenu, kwani hakika rizki yao inatoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).”

 

 

Share