Matunda Ya Imani

 

Matunda ya Imani

 

Alhidaaya.com

 

Imekusanywa na: Muhammad Al-Ma'awiy

 

 

 

Himdi Anastahiki Rabb wa viumbe vyote, Yeye Ndiye Mlinzi wa Waumini wa kweli. Ninashuhudia kwamba hapana mwabudiwa wa haki ila Allaha na wala Hana mshirika, Yeye Ndiye Aliyewaahidi wenye Ikhlaasw kwa ufanisi na neema za milele. Na ninashuhudia kuwa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni Rasuli wa Allah, naye amekuja na ukweli wa wazi kabisa pamoja, akiwa ni mwenye kuwaongoza watu katika njia hiyo, mwenye kuleta bishara njema na kuonya walimwengu. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

آمَنَ الرَّسُولُ بِمَا أُنزِلَ إِلَيْهِ مِن رَّبِّهِ وَالْمُؤْمِنُونَ ۚ كُلٌّ آمَنَ بِاللَّـهِ وَمَلَائِكَتِهِ وَكُتُبِهِ وَرُسُلِهِ لَا نُفَرِّقُ بَيْنَ أَحَدٍ مِّن رُّسُلِهِ ۚ وَقَالُوا سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا ۖ غُفْرَانَكَ رَبَّنَا وَإِلَيْكَ الْمَصِيرُ ﴿٢٨٥﴾

 “Rasuli ameamini yaliyoteremshwa kwake kutoka kwa Rabb wake na Waumini (pia). Wote wamemwamini Allaah, na Malaika Wake, na Vitabu Vyake, na Rusuli Wake. (Nao husema): Hatutofautishi baina ya yeyote kati ya Rusuli Wake. Na wakasema: Tumesikia na tumetii, tunakuomba maghfirah Rabb wetu na Kwako ni mahali pa kuishia.” [ Al-Baqarah: 285].

 

Enyi ndugu zangu Waumini! Hakika Allaah (‘Azza wa Jalla) Ameumba viumbe ili wamtii na wamuabudu, Naye Hataki kutoka kwetu riziki wala Haitaji wamlishe.

 

Kwani Yeye Allaah (‘Azza wa Jalla) Ndiye Mwenye kuruzuku, Mwenye nguvu madhubuti kabisa. Na daraja kubwa ya Imani ni kumuamini Allaah (‘Azza wa Jalla) na Malaika Wake, na Vitabu Vyake na Rusuli Wake na Siku ya Mwisho. Qur-aan imetubainishia sifa za Waumini wa kweli kama ifuatavyo:

 

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللَّـهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ﴿٢﴾ الَّذِينَ يُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ﴿٣﴾ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُؤْمِنُونَ حَقًّا ۚ لَّهُمْ دَرَجَاتٌ عِندَ رَبِّهِمْ وَمَغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ﴿٤﴾

 

Hakika Waumini ni wale ambao Anapotajwa Allaah, nyoyo zao zinajaa khofu na wanaposomewa Aayaat Zake huwazidishia iymaan, na kwa Rabb wao wanatawakali. Ambao wanasimamisha Swalaah na katika yale Tuliyowaruzuku hutoa. Hao ndio Waumini wa kweli!  Wana daraja (za Jannah) kwa Rabb wao na maghfirah na riziki karimu. [Al-Anfaal: 2-4]

 

 

Wenye Imani walijua hakika hii na hivyo kuijaza mioyo yao Imani kwa Allaah (‘Azza wa Jalla) Peke Yake, ambaye mkononi Mwake umo Ufalme wote; na Yeye ni Mwenye uweza juu ya kila kitu. Na kama inavyoeleweka kuwa Muumini mkamilifu ni yule mwenye kutekeleza wajibu wa Allaah (‘Azza wa Jalla) na mwenye kumtegemea Yeye katika kila jambo na anapotajwa Allaah (‘Azza wa Jalla) basi nyoyo zao hujawa na hofu na Aayah Zake zinaposomwa Imani yao huongezeka na pia huwa na yakini juu ya yakini. Hivyo, huwafanya wawe ni bishara njema kwa ahadi Yake na kuogopa adhabu Yake.

 

Imani katika nafsi ya Muumini inapanda na kuwa juu ya kila kitu na hivyo na mafungamano ya karibu na Allaah (‘Azza wa Jalla), hivyo kutoweza kushughulishwa na kitu chochote ambacho kinaweza kumtoa katika Imani hiyo. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

رِجَالٌ لَّا تُلْهِيهِمْ تِجَارَةٌ وَلَا بَيْعٌ عَن ذِكْرِ اللَّـهِ وَإِقَامِ الصَّلَاةِ وَإِيتَاءِ الزَّكَاةِ ۙ يَخَافُونَ يَوْمًا تَتَقَلَّبُ فِيهِ الْقُلُوبُ وَالْأَبْصَارُ ﴿٣٧﴾

“Wanaume ambao haiwashughulishi tijara wala uuzaji na kumdhukuru Allaah na kusimamisha Swalaah na kutoa Zakaah wanakhofu Siku zitapopinduka humo nyoyo na macho.” [An-Nuwr: 37]

 

Hivi ndivyo watu wa Imani walivyoshikia Imani yao na kuwa na uhusiano na Rabb wao na kufanya amali katika kumridhisha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa viungo vyao na mioyo yao. Yalikuwa mafungamano ya watu hawa kwa ndugu zao Waumini ni mafungamano ya ndugu kwa nduguye, anampenda kwa ajili ya Allaah na kumchukia kwa ajili ya Allaah, anampa kwa ajili ya Allaah na kumyima kwa ajili ya Allah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Hilo ni kuhakikisha kauli ya Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

“Mwenye kupenda kwa ajili ya Allaah na kuchukia kwa ajili ya Allaah, na kutoa kwa ajili ya Allaah na kuzuia kwa ajili ya Allaah, hakika yeye atakuwa amekamilisha Imani yake.”

 

Hivyo, mafungamano baina ya Waumini yalikuwa ni mahusiano baina ya viungo katika mwili mmoja. Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anapigia mfano kuhusu hilo pale aliposema:

“Mfano wa Waumini katika kupendana na kurehemeana kwao na kuhurumiana kwao ni sawa na mwili mmoja, kikishtakia kiungo kimoja basi mwili mzima utakosa usingizi na kushikwa na homa” [Al-Bukhaariy].

 

Rehema inajenga mahusiano baina yao, na mapenzi na mahaba yanawajumlisha pamoja na kuzifunga pamoja nyoyo zao. Hivyo wakawa kama ilivyotaja Qur-aan:

 

مُّحَمَّدٌ رَّسُولُ اللَّـهِ ۚ وَالَّذِينَ مَعَهُ أَشِدَّاءُ عَلَى الْكُفَّارِ رُحَمَاءُ بَيْنَهُمْ ۖ تَرَاهُمْ رُكَّعًا سُجَّدًا يَبْتَغُونَ فَضْلًا مِّنَ اللَّـهِ وَرِضْوَانًا ۖ سِيمَاهُمْ فِي وُجُوهِهِم مِّنْ أَثَرِ السُّجُودِ ۚ  

“Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) ni Rasuli wa Allaah. Na wale walio pamoja naye ni wakali zaidi dhidi ya makafiri; wanahurumiana baina yao. Utawaona wakirukuu na wakisujudu wakitafuta fadhila na radhi kutoka kwa Allaah. Alama zao dhahiri zi katika nyuso zao kutokana na athari za sujudu.” [ Al-Fat-h: 29]

 

Na kwa sifa hizi zilizotajwa waliweza kuhakikisha katika nafsi zao mafunzo ya Dini yao na muongozo wa Nabiy wao, wakawa ni wenye kuamrisha mema na kukataza maovu, na pia kuusiana kwa haki na kuusiana kusubiri na wanasaidiana katika wema na taqwa ya Allaah (‘Azza wa Jalla) na wala hawashirikiani katika maovu na uadui. Muumini anatambua haki ya nduguye Muumini katika kuyalinda mali yake, heshima yake, na cheo chake na kumtetea juu ya Dini yake wala hawakiuki mipaka baadhi yao kwa wengine wala hawaudhiani kwa maneno wala matendo, hivyo kuhakikisha kauli ya Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pale aliposema:

“Muumini ni yule ambaye watu hupata usalama kwake na Muislamu ni yule ambaye Waislamu wenziwe husalimika na mdomo wake na mkono wake” [At-Tirmidhiy na An-Nasaaiy kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhum)]. Na katika riwaayah nyengine: “Na Muhaajir ni yule anaye yahama maovu”.

 

Enyi ndugu zangu watukufu! Hakika katika sifa nyeti na za kipekee za Waumini walio wakweli ni kushindana katika Njia ya Allaah na kujitolea mhanga kwa nafsi na mali yake katika kuhakikisha ushindi na kupata shahada kwa ajili ya haki na Dini. Kwa ajili hiyo, hawahepi katika vita wala hawabaki nyuma katika matukio na kwa hayo hapana tofauti baina ya wakongwe wao wala wadogo kati yao, na wanaume na wanawake wao na mifano ya hiyo katika historia ni mingi iliyo mashuhuri na maarufu. Ni ushujaa wa kipekee na kujitolea mhanga kukubwa.

 

Enyi Waislamu! Hakika Waumini wa kweli kwa Allaah (‘Azza wa Jalla) wanakua na starehe na neema ya azima yenye nguvu katika kupambana na matukio tofauti. Hakika wao wanachukua fursa ya kuigeuza hofu kuwa utulivu na amani na kupigania maisha kwa maslahi ya haki na kheri. Na wanabadilisha kuharibikiwa kwa kuleta ushindi na kufaulu, na kushindwa kwa kufikia kufuzu na ufanisi. Hawa ndio Waumini wa kweli na haki.

 

 Enyi Waislamu! Hakika Imani - Na hii ndio sehemu yake ya kihakika katika Ummah huu – taklifu yake ni kuu na tukufu. Ni wajibu iwe na dhumuni la kimatendo kama methodolojia na tabia ambayo itasimama juu ya nguzo zake na kuwekwa katika vigezo vyake na kusimama kwenye njia bainifu na hivyo kuitafsiri katika yanayojiri hivi sasa. Anasema Allaah (‘Azza wa Jalla):

 

وَمَن يَعْمَلْ مِنَ الصَّالِحَاتِ مِن ذَكَرٍ أَوْ أُنثَىٰ وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَأُولَـٰئِكَ يَدْخُلُونَ الْجَنَّةَ وَلَا يُظْلَمُونَ نَقِيرًا ﴿١٢٤﴾

“Na atakayefanya mema akiwa mwanamume au mwanamke hali yeye ni Muumini; basi hao wataingia Jannah na wala hawatodhulumiwa watu kadiri ya kitone cha kokwa ya tende.” [ An-Nisaa: 124).

 

Enyi waja wa Allaah (‘Azza wa Jalla), hizi ni baadhi ya sifa za Waumini katika mahusiano yao na Rabb wao na mafungamano mazuri na ndugu zao, na kushindana katika mambo ya Dini yao. Hivyo, ni vyema kuzitaja na kuzikumbuka sifa hizo na kupata mazingatio na mawaidha ndani yake na ni juu yetu kushikamana na Dini yetu na kuiga maadili na tabia za Nabiy wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kuifuata Sunnah yake kwa kadri ya uwezo wetu wala tusiipuuze wala kuikejeli na kuifanyia mzaha.

 

Hivyo mcheni Allaah haki ya kumcha wala msife isipokuwa katika Uislamu na turudi kwa Rabb wetu na tutubu kwa makosa na madhambi tunayoyafanya mchana na usiku, kwani Yeye ni Mwingi wa kughufuria na kusamehe.

 

Tunamuomba Allaah (‘Azza wa Jalla)Atutakabalie 'amali zetu na Atuepeushie na makosa pamoja na madhambi na Atupatie mema na mazuri hapa ulimwenguni na mema na mazuri Kesho Aakhirah na Atuepushe moto wa Jahanamu. Aamiyn.

 

 

 

Share