02-Zawadi Kwa Wanandoa: Nguzo Za 'Aqd Na Sharti Zake

 

 

 

Zawadi Kwa Wanandoa

 

02- Nguzo Za 'Aqd Na Sharti Zake 

 

أركان العقد وشروطه

 

 

 

'Aqd inakamilika kwa kukamilika kwa masharti yafuatayo:

 

a) Idhini ya Walii.

b) Kuridhika kwa bibi harusi mtarajiwa.

c) Kutimia kwa tamko la ndoa yaani Ijaab na Qabuul (yaani iijab na qubuul iliyounganishwa kwa tamko la ndoa au yenye kufidisha maana hiyo).

d) Kuwepo kwa mashahidi wawili waadilifu.

e) Kubalighi na kuwa na utambuzi baina ya wanandoa, hivyo haifai kuwepo kwa ndoa ikiwa mmoja wapo ni mwendawazimu au mdogo kwa umri na bado hajabaleghe.

  

'Aqd hii inalazimika kwa pande zote mbili husika, ila katika baadhi ya hali kama vile mwanamke kudanganywa na kughuriwa na mwanamme au mwanamme kuoa mwanamke asiyezaa kisha akagundua kuwa hazai na hakujua hilo kabla, katika hali hii anayo haki ya kuvunja 'Aqd.

 

Na kwa hali hiyo hiyo ni kujionesha mwanamme kuwa ni mchaji Allaah na mtu mwenye msimamo kisha baada ya muda ukadhihirika ukweli kuwa ni muovu na ni mtu mpotevu hana sifa hizo za mwanzo, hapa vile vile itavunjika 'Aqd yao.

 

Na kwa mfano huo huo ni kuoa kwa mwanamme msichana akitegemea kuwa ni bikra kisha ikadhihirika kuwa sio bikra, au akaona aibu nyingine iliyokuwa ni dhahiri na ya wazi kabisa au maradhi yenye kuchukiza.

 

 

Imepokewa kutoka kwa Ka’ab bin Zaid kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam)  alioa mwanamke wa kabila la Banii Ghafaar, alipokwenda kwake na baada ya kuweka nguo zake na kukaa katika kitanda na kuona baina ya kitovu na mbavu weupe ambao ulimuondoa na kukaa mbali nae na kuondoka kitandani, kisha akamwambia: “Chukua nguo zako.” na hakuchukua alichompa  (katika mahari.)” (Ahmad)

 

 

Amesema 'Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allahu 'anhu)  kwa yule bwana aliyeoa mwanamke nae (mwanamme) hazai, ‘Mwambie kuwa wewe huzai na mpe uhuru wa kuchagua.’

 

Share