12-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Nikaah: Mlango Wa Kunyonya (Mtoto Kunyonyeshwa Na Asiye Mamake)

بُلُوغُ الْمَرام

Buluwgh Al-Maraam

 

كِتَابُ اَلنِّكَاحِ

Kitabu cha Nikaah (Ndoa)

 

بَابُ اَلرَّضَاعِ

12-Mlango Wa Kunyonya (Mtoto Kunyonyeshwa Na Asiye Mamake)

 

 

 

 

 

963.

عَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ {لَا تُحَرِّمُ اَلْمَصَّةُ وَالْمَصَّتَانِ} أَخْرَجَهُ مُسْلِمٌ

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Kunyonya mara moja na mbili hakuharamishi.”[1] [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

964.

وَعَنْهَا قَالَتْ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  {اُنْظُرْنَ مَنْ إِخْوَانُكُنَّ، فَإِنَّمَا اَلرَّضَاعَةُ مِنْ اَلْمَجَاعَةِ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ 

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Angalieni vizuri ndugu zenu ni nani.[2] Hakika kunyonyesha (kunakoleta udugu) ni kutokana na kumaliza njaa (ya mtoto).” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

965.

وَعَنْهَا قَالَتْ: {جَاءَتْ سَهْلَةُ بِنْتُ سُهَيْلٍ. فَقَالَتْ: يَا رَسُولَ اَللَّهِ! إِنَّ سَالِمًا مَوْلَى أَبِي حُذَيْفَةَ مَعَنَا فِي بَيْتِنَا، وَقَدْ بَلَغَ مَا يَبْلُغُ اَلرِّجَالُ. قَالَ: "أَرْضِعِيهِ. تَحْرُمِي عَلَيْهِ"}  رَوَاهُ مُسْلِمٌ

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema: “Sahlah bint Suhayl[3] alikuja kwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akasema: Ee Rasuli wa Allaah! Saalim[4] muachwa huru wa Abuu Hudhayfah[5] yuko pamoja nasi nyumbani mwetu na amefikia yanayofikiwa na wanaume. Nabiy akasema: “Mnyonyeshe utakuwa haraam kwake.”[6] [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

966.

وَعَنْهَا: {أَنْ أَفْلَحَ أَخَا أَبِي الْقُعَيْسِ جَاءَ يَسْتَأْذِنُ عَلَيْهَا بَعْدَ اَلْحِجَابِ. قَالَتْ: فَأَبَيْتُ أَنْ آذَنَ لَهُ، فَلَمَّا جَاءَ رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  أَخْبَرْتُهُ بِاَلَّذِي صَنَعْتُ، فَأَمَرَنِي أَنْ آذَنَ لَهُ عَلَيَّ. وَقَالَ: "إِنَّهُ عَمُّكِ"} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema: “Aflah (mjomba aliyenyonya naye) nduguye Abuu Al-Qu’ays,[7] aliomba ruhusa kuingia kwangu baada ya kuteremka Aayah ya hijaab. Nikakataa kumruhusu. Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alipokuja nilimueleza nililotenda, akaniamurisha nimruhusu na akaniambia: “Huyo ni ami yako.”[8] [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

967.

وَعَنْهَا قَالَتْ: {كَانَ فِيمَا أُنْزِلُ فِي اَلْقُرْآنِ: عَشْرُ رَضَعَاتٍ مَعْلُومَاتٍ يُحَرِّمْنَ، ثُمَّ نُسِخْنَ بِخَمْسٍ مَعْلُومَاتٍ، فَتُوُفِّيَ رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  وَهِيَ فِيمَا يُقْرَأُ مِنَ اَلْقُرْآنِ} رَوَاهُ مُسْلِمٌ

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema: “Miongoni mwa Aayah za Qur-aan zilizoteremka ilikuwa ni Aayah hii: “Manyonyesho kumi yanayojulikana yanafanya mtu kuwa maharimu wa mnyonyeshaji.” Kisha zikafutwa kwa manyonyesho matano yanayojulikana….” [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

968.

وَعَنِ اِبْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا {أَنَّ اَلنَّبِيَّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  أُرِيدُ عَلَى اِبْنَةِ حَمْزَةَ. فَقَالَ: "إِنَّهَا لَا تَحِلُّ لِي، إِنَّهَا اِبْنَةُ أَخِي مِنْ اَلرَّضَاعَةِ} وَيَحْرُمُ مِنْ اَلرَّضَاعَةِ  مَا يَحْرُمُ مِنْ اَلنَّسَبِ. مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ 

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kuwa: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alipewa binti wa Hamzah. Alisema: Yeye si halaal kwangu kumuoa, yeye ni binti ya ndugu yangu wa kunyonya, na yale[9] yanayoharamishwa katika kunyonya yanaharamishwa katika nasaba.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

969.

وَعَنْ أُمِّ سَلَمَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  {لَا يُحَرِّمُ مِنْ اَلرَّضَاعَةِ إِلَّا مَا فَتَقَ اَلْأَمْعَاءَ، وَكَانَ قَبْلَ اَلْفِطَامِ} رَوَاهُ اَلتِّرْمِذِيُّ، وَصَحَّحَهُ هُوَ وَالْحَاكِمُ 

Kutoka kwa Ummi Salamah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Haiharamishi katika kunyonya ila kiasi kilichopenya matumboni na ikawa kabla ya kuachishwa kunyonya.” [Imetolewa na At-Tirmidhiy na akaisahihisha At-Tirmidhiy na Al-Haakim]

 

 

 

970.

وَعَنِ اِبْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: {لَا رَضَاعَ إِلَّا فِي اَلْحَوْلَيْنِ} رَوَاهُ اَلدَّارَقُطْنِيُّ وَابْنُ عَدِيٍّ مَرْفُوعًا وَمَوْقُوفًا، وَرَجَّحَا اَلْمَوْقُوفَ 

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema: “Hakuna kunyonyesha isipokuwa ile miaka miwili ya mwanzo.” [Imetolewa na Ad-Daaraqutwniy na Ibn ‘Adiyy  ikiwa ni Marfuw’ na Mawquwf, wameitilia nguvu kuwa ni Mawquwf]

 

 

 

971.

وَعَنِ اِبْنِ مَسْعُودٍ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ  قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  {لَا رَضَاعَ إِلَّا مَا أَنْشَزَ اَلْعَظْمَ، وَأَنْبَتَ اَللَّحْمَ} رَوَاهُ أَبُو دَاوُدَ 

Kutoka kwa Ibn Mas-‘uwd (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Hakuna kunyonyesha ila yanayoimarisha mfupa na kuotesha nyama.” [Imetolewa na Abuu Daawuwd]

 

 

 

972.

وَعَنْ عُقْبَةَ بْنِ اَلْحَارِثِ، {أَنَّهُ تَزَوَّجَ أُمَّ يَحْيَى بِنْتَ أَبِي إِهَابٍ، فَجَاءَتْ اِمْرَأَةٌ. فَقَالَتْ: قَدْ أَرْضَعْتُكُمَا، فَسَأَلَ اَلنَّبِيَّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  فَقَالَ: "كَيْفَ وَقَدْ قِيلَ ؟ " فَفَارَقَهَا عُقْبَةُ. وَنَكَحَتْ زَوْجًا غَيْرَهُ} أَخْرَجَهُ اَلْبُخَارِيُّ

Kutoka kwa ‘Uqbah bin Al-Haarith[10] anasema kuwa: Yeye alimuoa Ummi Yahya[11] binti Abuu Ihaab. Akaja mwanamke mmoja akasema: “Nimekunyonyesheni wewe na huyo mkeo.” Akaja akamuuliza Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) jambo hilo. Akasema: “Itakuwaje (unasita) na imeshasemwa (kuwa amewanyonyesha?)”[12] ‘Uqbah akamtaliki yule mke akaolewa na mtu mwingine.[13] [Imetolewa na Al-Bukhaariy]

 

 

 

973.

وَعَنْ زِيَادِ اَلسَّهْمِيِّ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ  قَالَ: {نَهَى رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  أَنْ تُسْتَرْضَعَ اَلْحَمْقَى} أَخْرَجَهُ أَبُو دَاوُدَ وَهُوَ مُرْسَلٌ، وَلَيْسَتْ لِزِيَادٍ صُحْبَةٌ 

Kutoka kwa Ziyaad As-Sahmiyy[14] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amekataza watu wasiwape wapumbavu kuwanyonyeshea watoto wao.” [Imetolewa na Abuu Daawuwd nayo ni mursal na Ziyaad si Swahaba]

 

[1] Hadiyth hii inatujulisha kuwa kitendo cha kunyonya ziwa la mwanamke mara moja au mbili halithibitisha umaharim. Hadiyth iliyopokewa na ‘Aaishah anaeleza kuwa ili kuthibitisha makatazo hayo mwanamke anatakiwa anyonyeshe kwa uchache mara tano.

[2] Ilitokea wakati fulani mtu alikuwa amekaa karibu na Mama ‘Aaishah. Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) hakupenda hali hiyo. ‘Aaishah alimjulisha kuwa yule aliyekaa naye alikuwa ni nduguye kwa kunyonya. Baada ya kusikia hivi Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akalitolea ufafanuzi suala hili la kunyonya kwa watoto pamoja utotoni.

 

[3] Sahlah binti wa  Suhayl bin ‘Amr Al-Qushariyah alikuwa wa kabila la Banuu ‘Aamir bin Lu’ayy. Alisilimu mapema na alihama pamoja na Abuu Hudhayfah kuenda Uhabeshi na akamzalia Muhammad bin Abiy Hudhayfah.

[4] Huyu ni Saalim bin Ma’qil muachwa huru wa Abuu Hudhayfah. Alilelewa na mwanamke wa Ki-answaar akiitwa Layla au Thubayta, binti wa Ya’ar, pindi Abuu Hudhayfah alipomuoa alikuja pamoja na Saalim ambaye Abuu Hudhayfah alimfanya katika watu wake. Saalim alihudhuria Badr na Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliwaamurrisha Maswahaba zake wasikilize Qur-aan kutoka kwa watu wane na miongoni mwa hao watu wane Saalim alikuwemo. Alikuwa na mazowea ya kuwaongoza Muhajiruwna, akiwemo ‘Umar,  katika Swalaah Msikiti wa Quba kabla ya Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) kuwasili Madiynah. Hadiyth hii inamhusu Sahlah bint Suhayl. ‘Ulamaa wote wakiwemo Taabi’iyna na Fuqahaa wana msimamo kuwa mtu mkubwa hanyonyeshwi. Na wana msimamo kuwa Hadiyth hii ni Mansuwkh (Hukumu yake imefutwa)

 

[5] Inasemekana kuwa jina lake lilikuwa ni Muhaashim au Hishaam bin ‘Utbah bin Rabiy’ah bin ‘Abd Shams. Alikuwa ni Swahaba maarufu aliyehudhuria Badr, Uhud na vita vyote muhimu. Aliuwawa katika vita vya Al-Yamaamah akiwa na umri wa miaka 53.

 

[6] ‘Ulamaa wengi wamekubaliana na rai kuwa kunyonyesha kunakofanya uharaam wa watu wawili ni ule wa miaka miwili ya mwanzo wa umri wa mtoto. Ama kadhia hii ya Saalim katika Hadiyth hii ni maalum, haitumiki kwa mtu mwingine yeyote.

[7] Jina lake kamili ni Abul-Ja’d Aflah, muachwa huru wa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) au muachwa huru wa Ummu Salamah. Kaka yake  Abul-Qu’ays alikuwa akiitwa Al-Ja’d au Wail bin Aflah Al-Ash’ari, hivyo basi jina la kaka yake Aflah ni sawa sawa na jina la baba yake. ‘Aaishah alikuwa na wajomba wawili wa kunyonya, miongoni mwao akiwemo kaka zake Abuu Bakr kwa kunyonya ambao walifariki katika zama za Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) na wa pili alikuwa ni Aflah ambaye ni kwa kaka wa baba yake kwa kunyonya.

 

[8] Mwanamke ananyonyesha maziwa yake, atakuwa ni mama halisi wa mtoto, kama kwamba yeye ndiye aliyemzaa na baba halikadhalika ataonekana hivyo. Na ichukuliwe hivyo kwa watoto wote watakaonyonya nao pamoja nao katika makatazo ya maharim kuoana.

[9] Yatupasa kufahamu kuwa mtoto anaelekea kwa mama yake aliyemyonyesha. Hata hivyo mama huyo hatokuwa na uhusiano wa ndugu wa damu wa mtoto yule. Uharaam huu utakuwa na wenzake walionyonya.

[10]Alikua akiitwa Sirwa’ta ‘Uqbah bin Al-Haarith bin ‘Aamir bin Nawfal bin ‘Abd Manaaf Al-Makkiy. Alikuwa ni Swahaba miongoni mwa waliosilimu siku ya Fat-h Makkah. Aliishi hadi miaka ya hamsini ya Hijrah.

 

[11] Jina lake ni Ghaniyah, binti wa Abiy Ihaab bin ‘Uwair At-Tamiymiy. Inasemekana kuwa jina lake lilikuwa Zaynab vile vile.

[12] Hadiyth hii inatufahamisha kuwa tukitaka kuthibitisha uhusiano wa walionyonyeshwa pamoja (ukaka na udada), ushahidi wa mtu mmoja unatosha kuthibitisha. Hili linaonesha vile vile kuwa ushahidi utakaotolewa na mwanamke, katika mas-ala yanayohusiana na mwanamke, ana nguvu zaidi kuliko itakayotolewa na mwanamume.

 

[13] Imeandikwa katika kitabu At-Taqriyb kuwa alikuwa ni Taabi’ wa kizazi cha tatu na anajulikana kama ni thiqah (madhubuti). Ameripoti Hadiyth ambayo ni Mursal. Na inasemekana kuwa ni muacha huru wa ‘Amr bin Al-‘Aasw. Waandishi wote wa Usudul Al-Ghaba na Al-Isti’aba hakutajwa miongoni mwa Maswahaba.

 

[14] Hind bin ‘Utbah bint Rabiy’ah bin ‘Abd Shams alisilimu mwaka wa Fat-h Makkah baada ya mume wake kusilimu katika mwaka huo huo wa Fat-h Makkah. Kifo cha baba yake ‘Utbah mjomba wake Shaybah na kaka yake Al-Waliyd huko Badr vilimshtua sana na alifurahi sana pindi Hamza alipouawawa katika vita vya Uhud.

Share