06-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Mjumuisho: Mlango Wa Adhkaar Na Du’aa

 

بُلُوغُ الْمَرام

Buluwgh Al-Maraam

 

كِتَابُ اَلْجَامِعِ

Kitabu Cha Mjumuisho

 

بَابُ اَلذِّكْرِ وَالدُّعَاءِ

06-Mlango Wa Adhkaar Na Du’aa

 

 

 

 

1331.

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضى الله عنه قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏{يَقُولُ اَللَّهُ ‏تَعَالَى‏: أَنَا مَعَ عَبْدِي مَا ذَكَرَنِي، وَتَحَرَّكَتْ بِي شَفَتَاهُ} أَخْرَجَهُ ابْنُ مَاجَهْ، وَصَحَّحَهُ ابْنُ حِبَّانَ، وَذَكَرَهُ اَلْبُخَارِيُّ تَعْلِيقًا

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Allaah (تعالى)   Anasema: “Mimi Niko katika dhana ya mja wangu[1] anaponitaja na midomo yake inatikisika kwa sababu Yangu.” [Imetolewa na Ibn Maajah na akaisahihisha Ibn Hibbaan. Al-Bukhaariy ameitaja kuwa ni Mu’allaq]

 

 

 

1332.

وَعَنْ مُعَاذِ بْنِ جَبَلٍ‏ رضى الله عنه‏ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏{مَا عَمِلَ ابْنُ آدَمَ عَمَلاً أَنْجَى لَهُ مِنْ عَذَابِ اَللَّهِ مِنْ ذِكْرِ اَللَّهِ} أَخْرَجَهُ ابْنُ أَبِي شَيْبَةَ، وَالطَّبَرَانِيُّ بِإِسْنَادٍ حَسَنٍ

Kutoka kwa Mu’aadh bin Jabal (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mwana Aadam hajatenda amali yenye kumuokoa zaidi na adhabu ya Allaah kuliko kumdhukuru  Allaah.” [Imetolewa na Ibn Abuu Shaybah na Atw-Twabaraaniy kwa isnaad nzuri]

 

 

 

1333.

وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضى الله عنه قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ‏ صلى الله عليه وسلم ‏{مَا جَلَسَ قَوْمٌ مَجْلِسًا، يَذْكُرُونَ اَللَّهَ إِلَّا حَفَّتْ بِهِمُ الْمَلَائِكَةُ، وَغَشِيَتْهُمُ الرَّحْمَةُ، وَذَكَرَهُمُ اللَّهُ فِيمَنْ عِنْدَهُ} أَخْرَجَهُ مُسْلِم ٌ

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Watu hawakai wakamdhukuru Allaah isipokuwa Malaika Huwazunguka,[2] na rahmah huwaenea na utulivu huwateremkia, na Allaah Huwataja kwa walioko Kwake.” [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

1334.

وَعَنْهُ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏{مَا قَعَدَ قَوْمٌ مَقْعَدًا لَمْ يَذْكُرُوا اَللَّهَ، وَلَمْ يُصَلُّوا عَلَى اَلنَّبِيِّ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏إِلَّا كَانَ عَلَيْهِمْ حَسْرَةً يَوْمَ اَلْقِيَامَةِ} أَخْرَجَهُ اَلتِّرْمِذِيُّ، وَقَالَ: "حَسَنٌ"

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Watu hawakai kikao chochote na ikatokea hawamdhukuru Allaah katika kikao hicho wala hawamswalii Nabiy[3] (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) isipokuwa kitakuwa ni majuto kwao Siku ya Qiyaamah.” [Imetolewa na At-Tirmidhiy na amesema Hadiyth hii ni Hasan]

 

 

 

1335.

وَعَنْ أَبِي أَيُّوبَ رضى الله عنه قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏{مَنْ قَالَ: لَا إِلَهَ إِلَّا اَللَّهُ، وَحْدَهُ لَا شَرِيكَ لَهُ عَشْرَ مَرَّاتٍ، كَانَ كَمَنْ أَعْتَقَ أَرْبَعَةَ أَنْفُسٍ مِنْ وَلَدِ إِسْمَاعِيلَ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa Abuu Ayyuwb (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Atakayesema

لَا إِلَهَ إِلَّا اَللَّهُ، وَحْدَهُ لَا شَرِيكَ لَهُ

Hapana mwabudiwa wa haki ila Allaah, peke yake hana mshirika

 

Ni kama mwenye kuacha huru nafsi nne katika wana wa Ismaa’iyl.”[4] [Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

1336.

وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضى الله عنه قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏{مَنْ قَالَ: سُبْحَانَ اَللَّهِ وَبِحَمْدِهِ مِائَةَ مَرَّةٍ حُطَّتْ خَطَايَاهُ، وَإِنْ كَانَتْ مِثْلَ زَبَدِ اَلْبَحْرِ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Atakayesema:

سُبْحَانَ اَللَّهِ وَبِحَمْدِهِ

Kutakasika ni kwa Allaah na Kuhimidiwa ni Kwak

e

Mara mia kwa siku atafutiwa dhambi zake hata kama ni mfano wa povu la bahari.” [Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

1337.

وَعَنْ جُوَيْرِيَةَ بِنْتِ اَلْحَارِثِ قَالَتْ: قَالَ لِي رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏{لَقَدْ قُلْتُ بَعْدَكِ أَرْبَعَ كَلِمَاتٍ، لَوْ وُزِنَتْ بِمَا قُلْتِ مُنْذُ اَلْيَوْمِ لَوَزَنَتْهُنَّ: سُبْحَانَ اَللَّهِ وَبِحَمْدِهِ، عَدَدَ خَلْقِهِ، وَرِضَا نَفْسِهِ، وَزِنَةَ عَرْشِهِ، وَمِدَادَ كَلِمَاتِهِ} أَخْرَجَهُ مُسْلِمٌ

Kutoka kwa Juwayriyah bint Al-Haarith[5] (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliniambia: “Nimesema maneno manne baada yako lau yangelinganishwa na uliosema tangu leo, ya kwangu yangeyashinda:[6]

 

سُبْحَانَ اَللَّهِ وَبِحَمْدِهِ، عَدَدَ خَلْقِهِ، وَرِضَا نَفْسِهِ، وَزِنَةَ عَرْشِهِ، وَمِدَادَ كَلِمَاتِهِ

Kutakasika ni kwa Allaah, na kuhimidiwa ni Kwake, kwa idadi ya viumbe Vyake na radhi ya nafsi Yake na uzito wa ‘Arshi Yake na wingi wa (kuandikia) maneno Yake.” [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

1338.

وَعَنْ أَبِي سَعِيدٍ اَلْخُدْرِيِّ‏ رضى الله عنه قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏{اَلْبَاقِيَاتُ اَلصَّالِحَاتُ: لَا إِلَهَ إِلَّا اَللَّهُ، وَسُبْحَانَ اَللَّهِ، وَاَللَّهُ أَكْبَرُ، وَالْحَمْدُ لِلَّهِ، وَلَا حَوْلَ وَلَا قُوَّةَ إِلَّا بِاَللَّهِ} أَخْرَجَهُ النَّسَائِيُّ، وَصَحَّحَهُ اِبْنُ حِبَّانَ، وَالْحَاكِمُ

Kutoka kwa Abuu Sa’iyd Al-Khudriy (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Amali njema yenye kubakia:[7]

 

لَا إِلَهَ إِلَّا اَللَّهُ، وَسُبْحَانَ اَللَّهِ، وَاَللَّهُ أَكْبَرُ، وَالْحَمْدُ لِلَّهِ، وَلَا حَوْلَ وَلَا قُوَّةَ إِلَّا بِاَللَّهِ

Hapana mwabudiwa wa haki ila Allaah, na Kutakasika ni kwa Allaah, na Allaah ni Mkubwa, na sifa njema ni za Allaah na hapana uwezo wala nguvu ila vyote vinatokana na Allaah.”

 

[Imetolewa na An-Nasaaiy na akaisahihisha Ibn Hibbaan na Al-Haakim]

 

 

 

1339.

وَعَنْ سَمُرَةَ بْنِ جُنْدُبٍ رضى الله عنه قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏{أَحَبُّ اَلْكَلَامِ إِلَى اَللَّهِ أَرْبَعٌ، لَا يَضُرُّكَ بِأَيِّهِنَّ بَدَأْتَ: سُبْحَانَ اَللَّهِ، وَالْحَمْدُ لِلَّهِ، وَلَا إِلَهَ إِلَّا اَللَّهُ، وَاَللَّهُ أَكْبَرُ} أَخْرَجَهُ مُسْلِمٌ

Kutoka kwa Samurah bin Jundub (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Maneno yapendwayo mno kwa Allaah ni manne hakitakudhuru lolote utakaloanza

سُبْحَانَ اَللَّهِ، وَالْحَمْدُ لِلَّهِ، وَلَا إِلَهَ إِلَّا اَللَّهُ، وَاَللَّهُ أَكْبَرُ

Kutakasika ni kwa Allaah, sifa njema ni za Allaah, Hapana mwabudiwa wa haki ila Allaah, Allaah ni Mkubwa.” [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

1340.

وَعَنْ أَبِي مُوسَى اَلْأَشْعَرِيِّ رضى الله عنه قَالَ: قَالَ لِي رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏{يَا عَبْدَ اَللَّهِ بْنَ قَيْسٍ! أَلَّا أَدُلُّكَ عَلَى كَنْزٍ مِنْ كُنُوزِ اَلْجَنَّةِ؟ لَا حَوْلَ وَلَا قُوَّةَ إِلَّا بِاَللَّهِ} مُتَّفَقٌ عَلَيْه ِ

زَادَ النَّسَائِيُّ: {وَلَا مَلْجَأَ مِنَ اللَّهِ إِلَّا إِلَيْهِ}

Kutoka kwa Abuu Muwsaa Al-Ash’ariyy (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Ee Abdullaah bin Qays! Nikujulishe hazina za Jannah?[8]

لَا حَوْلَ وَلَا قُوَّةَ إِلَّا بِاَللَّهِ

Hapana uwezo wala nguvu ila vyote vinatokana na Allaah.” [Bukhaariy, Muslim]

An-Nasaaiy ameongezea:

لَا مَلْجَأَ مِنَ اللَّهِ إِلَّا إِلَيْهِ

Hakuna pa kukimbilia ila ni kwake (Allaah).”

 

 

 

1341.

وَعَنِ النُّعْمَانِ بْنِ بَشِيرٍ ‏رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا‏ عَنِ النَّبِيِّ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏قَالَ: {إِنَّ اَلدُّعَاءَ هُوَ اَلْعِبَادَةُ} رَوَاهُ اَلْأَرْبَعَةُ، وَصَحَّحَهُ اَلتِّرْمِذِيُّ

وَلَهُ مِنْ حَدِيثِ أَنَسٍ بِلَفْظِ: {اَلدُّعَاءُ مُخُّ اَلْعِبَادَةِ}

وَلَهُ مِنْ حَدِيثِ أَبِي هُرَيْرَةَ رَفَعَهُ: {لَيْسَ شَيْءٌ أَكْرَمَ عَلَى اَللَّهِ مِنَ الدُّعَاءِ} وَصَحَّحَهُ اِبْنُ حِبَّانَ، وَالْحَاكِمُ

Kutoka kwa An-Nu’maan bin Bashiyr (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Hakika du’aa ndio ‘ibaadah.”[9] [Imetolewa na Al-Arba’ah (At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah) na akaisahihisha At-Tirmidhiy]

 

Naye amepokea kutoka katika Hadiyth ya Anas kwa tamshi: “Du’aa ni ubongo wa ‘ibaadah.”

 

Vile vile amepokea katika Hadiyth ya Abuu Hurayrah Marfuw’: “Hakuna kitu kilicho kitukufu kwa Allaah kuliko du’aa.” Na akaisahihisha Ibn Hibbaan na Al-Haakim

 

 

 

1342.

وَعَنْ أَنَسٍ رضى الله عنه قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏{اَلدُّعَاءُ بَيْنَ اَلْأَذَانِ وَالْإِقَامَةِ لَا يُرَدُّ} أَخْرَجَهُ النَّسَائِيُّ، وَغَيْرُهُ، وَصَحَّحَهُ اِبْنُ حِبَّانَ، وَغَيْرُهُ

Kutoka kwa Anas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Du’aa baina ya Adhaan na Iqaamah hairudishwi.”[10] [Imetolewa na An-Nasaaiy na wengine na akaisahihisha Ibn Hibbaan na wengine]

 

 

 

1343.

وَعَنْ سَلْمَانَ رضى الله عنه‏ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏{إِنَّ رَبَّكُمْ حَيِيٌّ كَرِيمٌ، يَسْتَحِي مِنْ عَبْدِهِ إِذَا رَفَعَ إِلَيْهِ يَدَيْهِ أَنْ يَرُدَّهُمَا صِفَرًا} أَخْرَجَهُ اَلْأَرْبَعَةُ إِلَّا النَّسَائِيَّ، وَصَحَّحَهُ اَلْحَاكِمُ

Kutoka kwa Salmaan (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Hakika Rabb Wenu ni mwenye hayaa Mkarimu Anamstahi mja Wake anapoinua mikono yake Kwake kuirudisha patupu.”[11] [Imetolewa na Al-Arba’ah (At-Tirmidhiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah) isipokuwa An-Nasaaiy na akaisahihisha Al-Haakim]

 

 

 

1344.

وَعَنْ عُمَرَ‏ رضى الله عنه قَالَ: {كَانَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏إِذَا مَدَّ يَدَيْهِ فِي اَلدُّعَاءِ، لَمْ يَرُدَّهُمَا، حَتَّى يَمْسَحَ بِهِمَا وَجْهَهُ} أَخْرَجَهُ اَلتِّرْمِذِيُّ

وَلَهُ شَوَاهِدُ مِنْهَا: حَدِيثُ اِبْنِ عَبَّاسٍ: عَنْ أَبِي دَاوُدَ وَمَجْمُوعُهَا يَقْتَضِي أَنَّهُ حَدِيثٌ حَسَنٌ

Kutoka kwa ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ): “Alikua anaponyoosha mikono yake katika du’aa hairudishi hadi aipangusie uso wake.”[12] [Imetolewa na At-Tirmidhiy]

Nayo ina ushahidi mwingi ikiwemo Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) iliyoko kwa Abuu Daawuwd na wengineo. Jumla ya ushahidi wote unapelekea kuwa hii ni Hadiyth Hasan.

 

 

 

1345.

وَعَنِ ابْنِ مَسْعُودٍ رضى الله عنه قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏{إِنَّ أَوْلَى اَلنَّاسِ بِي يَوْمَ اَلْقِيَامَةِ، أَكْثَرُهُمْ عَلَيَّ صَلَاةً} أَخْرَجَهُ اَلتِّرْمِذِيُّ وَصَحَّحَهُ اِبْنُ حِبَّانَ

Kutoka kwa Ibn Mas-‘uwd (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Atakayekuwa karibu zaidi nami siku ya Qiyaamah ni yule anayeniswalia kwa wingi zaidi.”[13] [Imetolewa na At-Tirmidhiy na akaisahihisha Ibn Hibbaan]

 

 

 

1346.

وَعَنْ شَدَّادِ بْنِ أَوْسٍ‏ رضى الله عنه قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ‏ صلى الله عليه وسلم ‏{سَيِّدُ اَلِاسْتِغْفَارِ، أَنْ يَقُولَ اَلْعَبْدُ: اَللَّهُمَّ أَنْتَ رَبِّي، لَا إِلَهَ إِلَّا أَنْتَ، خَلَقْتَنِي، وَأَنَا عَبْدُكَ، وَأَنَا عَلَى عَهْدِكَ وَوَعْدِكَ مَا اِسْتَطَعْتُ، أَعُوذُ بِكَ مِنْ شَرِّ مَا صَنَعْتُ، أَبُوءُ لَكَ بِنِعْمَتِكَ عَلَيَّ، وَأَبُوءُ لَكَ بِذَنْبِي، فَاغْفِرْ لِي; فَإِنَّهُ لَا يَغْفِرُ اَلذُّنُوبَ إِلَّا أَنْتَ} أَخْرَجَهُ اَلْبُخَارِيُّ

Kutoka kwa Shaddaad bin Aws (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Bwana wa Istighfaar[14] ni mja kusema:

 

اَللَّهُمَّ أَنْتَ رَبِّي، لَا إِلَهَ إِلَّا أَنْتَ، خَلَقْتَنِي، وَأَنَا عَبْدُكَ، وَأَنَا عَلَى عَهْدِكَ وَوَعْدِكَ مَا اِسْتَطَعْتُ، أَعُوذُ بِكَ مِنْ شَرِّ مَا صَنَعْتُ، أَبُوءُ لَكَ بِنِعْمَتِكَ عَلَيَّ، وَأَبُوءُ لَكَ بِذَنْبِي، فَاغْفِرْ لِي; فَإِنَّهُ لَا يَغْفِرُ اَلذُّنُوبَ إِلَّا أَنْتَ

Ee Allaah, Wewe ni Rabb wangu, hapana mwabudiwa wa haki ila Wewe, umeniumba mimi na mimi ni mja Wako, nami niko juu ya  ahadi Yako, na agano Lako, kiasi cha uwezo wangu, najikinga Kwako kutokana na shari ya nilichokifanya, nakiri  Kwako kwa kunineemesha, na nakiri kwa madhambi yangu, basi nakuomba unighufurie  kwani hakuna wa kughufuria  madhambi ila Wewe.” [Imetolewa na Al-Bukhaariy]

 

 

 

1347.

وَعَنِ ابْنِ عُمَرَ ‏رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا‏ قَالَ: {لَمْ يَكُنْ رَسُولُ اَللَّهِ‏ صلى الله عليه وسلم ‏يَدَعُ هَؤُلَاءِ اَلْكَلِمَاتِ حِينَ يُمْسِي وَحِينَ يُصْبِحُ: اَللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ اَلْعَافِيَةَ فِي دِينِي، وَدُنْيَايَ، وَأَهْلِي، وَمَالِي، اَللَّهُمَّ اسْتُرْ عَوْرَاتِي، وَآمِنْ رَوْعَاتِي، وَاحْفَظْنِي مِنْ بَيْنِ يَدَيَّ، وَمِنْ خَلْفِي، وَعَنْ يَمِينِي، وَعَنْ شِمَالِي، وَمِنْ فَوْقِي، وَأَعُوذُ بِعَظَمَتِكَ أَنْ أُغْتَالَ مِنْ تَحْتِي} أَخْرَجَهُ النَّسَائِيُّ، وَابْنُ مَاجَهْ، وَصَحَّحَهُ اَلْحَاكِمُ

Kutoka kwa Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) hakuwa anaacha maneno haya anapochwewa[15] na anapopambazuka:

 

اَللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ اَلْعَافِيَةَ فِي دِينِي، وَدُنْيَايَ، وَأَهْلِي، وَمَالِي، اَللَّهُمَّ اسْتُرْ عَوْرَاتِي، وَآمِنْ رَوْعَاتِي، وَاحْفَظْنِي مِنْ بَيْنِ يَدَيَّ، وَمِنْ خَلْفِي، وَعَنْ يَمِينِي، وَعَنْ شِمَالِي، وَمِنْ فَوْقِي، وَأَعُوذُ بِعَظَمَتِكَ أَنْ أُغْتَالَ مِنْ تَحْتِي

“Ee Allaah, hakika nakuomba msamaha na Al’-Aafiyah (hifadhi, amani, salama) duniani na Aakhirah, na ahli wangu, na mali yangu. Ee Allaah nisitiri aibu zangu na nitulize khofu yangu. Ee Allaah, nihifadhi mbele yangu, na nyuma yangu, na kulia kwangu, na kushoto kwangu, na juu yangu, na najikinga kwa Uadhimu Wako kwa kutekwa chini yangu.”

 

[Imetolewa na An-Nasaaiy na Ibn Maajah na akaisahihisha Al-Haakim]

 

 

 

1348.

وَعَنِ ابْنِ عُمَرَ ‏رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا‏ قَالَ: كَانَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏يَقُولُ: {اَللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنْ زَوَالِ نِعْمَتِكَ، وَتَحَوُّلِ عَافِيَتِكَ، وَفَجْأَةِ نِقْمَتِكَ، وَجَمِيعِ سَخَطِكَ } أَخْرَجَهُ مُسْلِمٌ

Kutoka kwa Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa akisema:

 

اَللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنْ زَوَالِ نِعْمَتِكَ، وَتَحَوُّلِ عَافِيَتِكَ، وَفَجْأَةِ نِقْمَتِكَ، وَجَمِيعِ سَخَطِكَ

“Ee Allaah! Najilinda Kwako kutokana na kuondoka neema Zako,[16] kubadilika uzima wangu, na adhabu yako ya ghafla, najilinda Kwako kutokana na hasira Zako zote.” [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

1349.

وَعَنْ عَبْدِ اَللَّهِ بْنِ عُمَرَ ‏رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا‏ قَالَ: { كَانَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏يَقُولُ: اَللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنْ غَلَبَةِ اَلدَّيْنِ، وَغَلَبَةِ اَلْعَدُوِّ، وَشَمَاتَةِ اَلْأَعْدَاءِ} رَوَاهُ النَّسَائِيُّ، وَصَحَّحَهُ اَلْحَاكِمُ

Kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa akisema:

 

اَللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنْ غَلَبَةِ اَلدَّيْنِ، وَغَلَبَةِ اَلْعَدُوِّ، وَشَمَاتَةِ اَلْأَعْدَاءِ

“Ee Allaah! Najilinda Kwako kushindwa na madeni, kushindwa na adui[17] na kuchekwa na maadui.” [Imetolewa na An-Nasaaiy na akaisahihisha Al-Haakim]

 

 

 

1350.

وَعَنْ بُرَيْدَةَ رضى الله عنه قَالَ: {سَمِعَ اَلنَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم ‏رَجُلاً يَقُولُ: اَللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ بِأَنِّي أَشْهَدُ أَنَّكَ أَنْتَ اَللَّهُ لَا إِلَهَ إِلَّا أَنْتَ، اَلْأَحَدُ اَلصَّمَدُ، اَلَّذِي لَمْ يَلِدْ، وَلَمْ يُولَدْ، وَلَمْ يَكُنْ لَهُ كُفُوًا أَحَدٌ.‏ فَقَالَ" لَقَدْ سَأَلَ اَللَّهُ بِاسْمِهِ اَلَّذِي إِذَا سُئِلَ بِهِ أَعْطَى، وَإِذَا دُعِيَ بِهِ أَجَابَ} أَخْرَجَهُ اَلْأَرْبَعَةُ، وَصَحَّحَهُ اِبْنُ حِبَّانَ

Kutoka kwa Buraydah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alimsikia mtu anaomba:

 

اَللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ بِأَنِّي أَشْهَدُ أَنَّكَ أَنْتَ اَللَّهُ لَا إِلَهَ إِلَّا أَنْتَ، اَلْأَحَدُ اَلصَّمَدُ، اَلَّذِي لَمْ يَلِدْ، وَلَمْ يُولَدْ، وَلَمْ يَكُنْ لَهُ كُفُوًا أَحَدٌ

“Ee Allaah! Hakika mimi nakuomba kuwa mimi nashuhudia kuwa Wewe ni Allaah, hapana mwabudiwa wa haki ila Wewe, Wewe Peke Yako, Mkusudiwa wa yote, Ambaye Hakuzaa wala Hakuzaliwa na wala hakuna mfano Wake chochote.”

 Akasema Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ): Kwa hakika amemuomba Allaah kwa Jina lake ambalo Akiombwa nalo Hutoa[18] na Akiombwa kwalo Hujibu.” [Imetolewa na Al-Arba’ah (At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah) na akaisahihisha Ibn Hibbaan]

 

 

 

1351.

وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ‏ رضى الله عنه‏ قَالَ: {كَانَ رَسُولُ اَللَّهِ‏ صلى الله عليه وسلم ‏إِذَا أَصْبَحَ، يَقُولُ: اَللَّهُمَّ بِكَ أَصْبَحْنَا، وَبِكَ أَمْسَيْنَا، وَبِكَ نَحْيَا، وَبِكَ نَمُوتُ، وَإِلَيْكَ اَلنُّشُورُ} وَإِذَا أَمْسَى قَالَ مِثْلَ ذَلِكَ ; إِلَّا أَنَّهُ قَالَ: {وَإِلَيْكَ اَلْمَصِيرُ} أَخْرَجَهُ اَلْأَرْبَعَةُ

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa anapopambazuka anasema:

 

اَللَّهُمَّ بِكَ أَصْبَحْنَا، وَبِكَ أَمْسَيْنَا، وَبِكَ نَحْيَا، وَبِكَ نَمُوتُ، وَإِلَيْكَ اَلنُّشُورُ

 

“Ee Allaah! Kwako tumepambazuka na Kwako tunakuchwa, Kwako tunaishi, na Kwako tutakufa,[19] na Kwako tutafufuliwa.”

Na anapofikia jioni akisema vivo hivyo isipokuwa mwisho husema

وَإِلَيْكَ اَلْمَصِيرُ

Na marejeo ya mwisho ni Kwako.

[Imetolewa na Al-Arba’ah (At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah)]

 

 

 

1352.

وَعَنْ أَنَسٍ رضى الله عنه قَالَ: {كَانَ أَكْثَرُ دُعَاءِ رَسُولِ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏رَبَّنَا آتِنَا فِي اَلدُّنْيَا حَسَنَةً، وَفِي اَلْآخِرَةِ حَسَنَةً، وَقِنَا عَذَابَ اَلنَّارِ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa Anas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Du’aa ya Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliyokuwa akikithiri mno kuisoma ilikuwa ni:

 

رَبَّنَا آتِنَا فِي اَلدُّنْيَا حَسَنَةً، وَفِي اَلْآخِرَةِ حَسَنَةً، وَقِنَا عَذَابَ اَلنَّارِ

Ee Rabb! Tupe mema duniani na (Tupe) mema Aakhirah[20] na Utukinge na adhabu ya moto.”[21] [Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

1353.

وَعَنْ أَبِي مُوسَى اَلْأَشْعَرِيِّ‏ رضى الله عنه ‏ قَالَ: {كَانَ اَلنَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم ‏يَدْعُو: اَللَّهُمَّ اغْفِرْ لِي خَطِيئَتِي، وَجَهْلِي، وَإِسْرَافِي فِي أَمْرِي، وَمَا أَنْتَ أَعْلَمُ بِهِ مِنِّي، اَللَّهُمَّ اِغْفِرْ لِي جِدِّي، وَهَزْلِي، وَخَطَئِي، وَعَمْدِي، وَكُلُّ ذَلِكَ عِنْدِي، اَللَّهُمَّ اِغْفِرْ لِي مَا قَدَّمْتُ، وَمَا أَخَّرْتُ، وَمَا أَسْرَرْتُ، وَمَا أَعْلَنْتُ، وَمَا أَنْتَ أَعْلَمُ بِهِ مِنِّي، أَنْتَ اَلْمُقَدِّمُ وَالْمُؤَخِّرُ، وَأَنْتَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Kutoka kwa Abuu Muwsaa Al-Ash’ariyy (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa anaomba du’aa hii:

 

اَللَّهُمَّ اغْفِرْ لِي خَطِيئَتِي، وَجَهْلِي، وَإِسْرَافِي فِي أَمْرِي، وَمَا أَنْتَ أَعْلَمُ بِهِ مِنِّي، اَللَّهُمَّ اِغْفِرْ لِي جِدِّي، وَهَزْلِي، وَخَطَئِي، وَعَمْدِي، وَكُلُّ ذَلِكَ عِنْدِي، اَللَّهُمَّ اِغْفِرْ لِي مَا قَدَّمْتُ، وَمَا أَخَّرْتُ، وَمَا أَسْرَرْتُ، وَمَا أَعْلَنْتُ، وَمَا أَنْتَ أَعْلَمُ بِهِ مِنِّي، أَنْتَ اَلْمُقَدِّمُ وَالْمُؤَخِّرُ، وَأَنْتَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ

“Ee Allaah! Nighufurie makosa yangu, ujahili (ujinga) wangu, na israaf (upindukaji mipaka) katika mambo yangu, Unayoyajua Wewe kutoka kwangu. Ee Allaah! Nighufurie niliyoyafanya kwa kudhamiria, na niliyoyafanya kwa kukosea, na makosa yangu yote. Ee Allaah! Nighufurie niliyoyatanguliza na niliyoyachelewesha, na niliyoyaficha, na niliyoyadhihirisha, na ambayo Wewe Unayajua kuliko mimi, Wewe ni Mwenye kutanguliza, na Wewe ni mwenye kuchelewesha. Wewe ni Muweza juu ya kila kitu.” [Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

1354.

وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ‏ رضى الله عنه قَالَ: {كَانَ رَسُولُ اَللَّهِ‏ صلى الله عليه وسلم ‏يَقُولُ: اَللَّهُمَّ أَصْلِحْ لِي دِينِي اَلَّذِي هُوَ عِصْمَةُ أَمْرِي، وَأَصْلِحْ لِي دُنْيَايَ اَلَّتِي فِيهَا مَعَاشِي، وَأَصْلِحْ لِي آخِرَتِي اَلَّتِي إِلَيْهَا مَعَادِي، وَاجْعَلْ اَلْحَيَاةَ زِيَادَةً لِي فِي كُلِّ خَيْرٍ، وَاجْعَلْ اَلْمَوْتَ رَاحَةً لِي مِنْ كُلِّ شَرٍّ} أَخْرَجَهُ مُسْلِمٌ

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa akisema:

 

اَللَّهُمَّ أَصْلِحْ لِي دِينِي اَلَّذِي هُوَ عِصْمَةُ أَمْرِي، وَأَصْلِحْ لِي دُنْيَايَ اَلَّتِي فِيهَا مَعَاشِي، وَأَصْلِحْ لِي آخِرَتِي اَلَّتِي إِلَيْهَا مَعَادِي، وَاجْعَلْ اَلْحَيَاةَ زِيَادَةً لِي فِي كُلِّ خَيْرٍ، وَاجْعَلْ اَلْمَوْتَ رَاحَةً لِي مِنْ كُلِّ شَرٍّ

“Ee Allaah! Nitengenezee Dini yangu ambayo ndio hifadhi ya mambo yangu, na Nitengenezee dunia yangu ambayo ndani yake ni maisha yangu. Na nitengenezee Aakhirah yangu ambayo ndio marejeo kwangu. Yafanye maisha ni ziada kwangu katika kila kheri, na mauti ni raha yangu kutokana na kila shari.”[22] [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

1355.

وَعَنْ أَنَسٍ رضى الله عنه قَالَ: {كَانَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏يَقُولُ:" اَللَّهُمَّ اِنْفَعْنِي بِمَا عَلَّمْتَنِي، وَعَلِّمْنِي مَا يَنْفَعُنِي، وَارْزُقْنِي عِلْمًا يَنْفَعُنِي} رَوَاهُ النَّسَائِيُّ، وَالْحَاكِمُ

وَلِلتِّرْمِذِيِّ: مِنْ حَدِيثِ أَبِي هُرَيْرَةَ نَحْوُهُ، وَقَالَ فِي آخِرِهِ: {وَزِدْنِي عِلْمًا، وَالْحَمْدُ لِلَّهِ عَلَى كُلِّ حَالٍ، وَأَعُوذُ بِاَللَّهِ مِنْ حَالِ أَهْلِ اَلنَّارِ} وَإِسْنَادُهُ حَسَنٌ

Kutoka kwa Anas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa akisema:

 

اَللَّهُمَّ اِنْفَعْنِي بِمَا عَلَّمْتَنِي، وَعَلِّمْنِي مَا يَنْفَعُنِي، وَارْزُقْنِي عِلْمًا يَنْفَعُنِي

 

“Ee Allaah! Ninufaishe kwa Ulichonifundisha, Unifundishe kitakachonifaa na Uniruzuku elimu itakayoninufaisha.”[23] [Imetolewa na An-Nasaaiy na Al-Haakim]

At-Tirmidhiy amepokea kutoka katika Hadiyth ya Abuu Hurayrah mfano wake mwisho wake akasema:

 

وَزِدْنِي عِلْمًا، وَالْحَمْدُ لِلَّهِ عَلَى كُلِّ حَالٍ، وَأَعُوذُ بِاَللَّهِ مِنْ حَالِ أَهْلِ اَلنَّارِ

“Na Unizidishie elimu. Kuhimidiwa ni kwa Allaah kwa hali zote, na najilinda kwa Allaah kwa hali ya watu wa motoni.” [Isnaad yake ni Hasan]

 

 

 

1356.

وَعَنْ عَائِشَةَ ‏رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا‏ أَنَّ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم ‏عَلَّمَهَا هَذَا اَلدُّعَاءَ: {اَللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ مِنَ الْخَيْرِ كُلِّهِ، عَاجِلِهِ وَآجِلِهِ، مَا عَلِمْتُ مِنْهُ وَمَا لَمْ أَعْلَمْ، وَأَعُوذُ بِكَ مِنَ الشَّرِّ كُلِّهِ، عَاجِلِهِ وَآجِلِهِ، مَا عَلِمْتُ مِنْهُ وَمَا لَمْ أَعْلَمْ، اَللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ مِنْ خَيْرِ مَا سَأَلَكَ عَبْدُكَ وَنَبِيُّكَ، وَأَعُوذُ بِكَ مِنْ شَرِّ مَا عَاذَ بِهِ عَبْدُكَ وَنَبِيُّكَ، اَللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ اَلْجَنَّةَ، وَمَا قَرَّبَ إِلَيْهَا مِنْ قَوْلٍ أَوْ عَمَلٍ، وَأَعُوذُ بِكَ مِنَ النَّارِ، وَمَا قَرَّبَ مِنْهَا مِنْ قَوْلٍ أَوْ عَمَلٍ، وَأَسْأَلُكَ أَنْ تَجْعَلَ كُلَّ قَضَاءٍ قَضَيْتَهُ لِي خَيْرًا} أَخْرَجَهُ اِبْنُ مَاجَهْ، وَصَحَّحَهُ اِبْنُ حِبَّانَ، وَالْحَاكِمُ

 

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alimfundisha du’aa hii:

 

اَللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ مِنَ الْخَيْرِ كُلِّهِ، عَاجِلِهِ وَآجِلِهِ، مَا عَلِمْتُ مِنْهُ وَمَا لَمْ أَعْلَمْ، وَأَعُوذُ بِكَ مِنَ الشَّرِّ كُلِّهِ، عَاجِلِهِ وَآجِلِهِ، مَا عَلِمْتُ مِنْهُ وَمَا لَمْ أَعْلَمْ، اَللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ مِنْ خَيْرِ مَا سَأَلَكَ عَبْدُكَ وَنَبِيُّكَ، وَأَعُوذُ بِكَ مِنْ شَرِّ مَا عَاذَ بِهِ عَبْدُكَ وَنَبِيُّكَ، اَللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ اَلْجَنَّةَ، وَمَا قَرَّبَ إِلَيْهَا مِنْ قَوْلٍ أَوْ عَمَلٍ، وَأَعُوذُ بِكَ مِنَ النَّارِ، وَمَا قَرَّبَ مِنْهَا مِنْ قَوْلٍ أَوْ عَمَلٍ، وَأَسْأَلُكَ أَنْ تَجْعَلَ كُلَّ قَضَاءٍ قَضَيْتَهُ لِي خَيْرًا

“Ee Allaah! Nakuomba kheri zote za dunia na Aakhirah, ninazozijua na nisizozijua. Najilinda Kwako na shari zote za dunia na Aakhirah, ninazozijua humo na nisizozijua. Ee Allaah! Nakuomba kheri aliyokuomba mja Wako na Nabiy Wako, na najilinda Kwako na shari aliyokuomba mja Wako na Nabiy Wako. Ee Allaah! Nakuomba Jannah na kinachokaribisha Jannah kwa kauli au kitendo, na najilinda Kwako na moto na kinachokaribisha motoni kwa kauli au kitendo. Nakuomba Ufanye kila hukumu Uliyohukumu kwangu iwe ya kheri.” [Imetolewa na Ibn Maajah na akaisahihisha Ibn Hibbaan na Al-Haakim]

 

 

 

1357.

وَأَخْرَجَ اَلشَّيْخَانِ عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضى الله عنه قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏{كَلِمَتَانِ حَبِيبَتَانِ إِلَى اَلرَّحْمَنِ، خَفِيفَتَانِ عَلَى اَللِّسَانِ، ثَقِيلَتَانِ فِي اَلْمِيزَانِ، سُبْحَانَ اَللَّهِ وَبِحَمْدِهِ ، سُبْحَانَ اَللَّهِ اَلْعَظِيمِ}

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Kuna maneno mawili yanapendwa mno na Ar-Rahmaan, mepesi katika ulimi, mazito katika mizani:

سُبْحَانَ اَللَّهِ وَبِحَمْدِهِ ، سُبْحَانَ اَللَّهِ اَلْعَظِيمِ

Kutakasika ni kwa Allaah na Kuhimidiwa ni Kwake, Kutakasika ni kwa Allaah Mtukufu.”[24] [Bukhaariy, Muslim]

 

[1] Katika Hadiyth hii Allaah (عز وجل)  Anatangaza kuwa yu Pamoja na mja Wake si kwa kiwiliwili chake bali kwa elimu yake na kwa uweza Wake. Allaah Yupo katika ‘Arshi Yake.

[2] Tunajifunza kupitia Hadiyth hii tukufu kuwa Malaika wanavizungukia vikao vya kumdhukuru Allaah na huenezwa rahmah za Allaah ndani yake. Allaah (عز وجل) Anaweza kukumbukwa kupitia vikao hivi, kwa kumuomba Yeye tu na kusoma Qur-aan.

[3] Hadiyth nyingine inasema hivi: “Atawaadhibu, na Akipenda Atawasamehe.” Maneno haya ya kumdhukuru Allaah na kumswalia Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) ni ya lazima kufanywa.

[4] Hadiyth hii na Hadiyth za mfano huu, zenye maneno ya kuwa atakayefanya hivi na vile, atapata malipo haya na yale na kughufuriwa madhambi yake. Kuna rai tofauti kwa Wanazuoni kwa maana haswa ya Hadiyth hizi. Baadhi wanaona kuwa malipo yatalipwa kwa yule atakayefanya matendo yale siku zote, wakati Wanazuoni wengine hawahusishi sharti hili. Wanaona kuwa atakayefanya jambo lile la kulipwa ni vizuri ajizuie na madhambi makubwa kwanza. Hii ina maana ya kuwa matendo yale mazuri yatafuta madhambi madogo tu na sio makubwa. Wanazuoni wengine wanaona kuwa hayaingiliani kuwa ni madhambi madogo na makubwa, bali ni suala tu la malipo ayapatayo mtu. Baadhi ya Wanazuoni wana muono kuwa madhambi madogo yanaghufuriwa na kufutika kwa mambo mema ayafanyayo mtu, ama madhambi makubwa kifutio chake ni kutubia na kuomba maghfirah wa Allaah.

[5] Juwayriyah: Huyu ni Ummul-Mu’uminiyn, alikuwa katika mateka wa vita vya Al-Murais. Alikuwa ni katika fungu la hisa la Thaabit bin Qays bin Shammas, ambaye alikubaliana naye kumuuzia uhuru wake. Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alimlipa na akamuoa. Baada ya hapo Swahaba wakawaacha huru jamaa za Juwayriyah wakisema: “Hizi ni Shariy’ah za Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ).” Alikuwa ni mwanamke mwenye msaada mkubwa kwa watu wake. Alifariki mwaka 56 Hijriyyah.

 

[6] Maelezo ni kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliondoka na kumuacha Juwayriyah akiendelea na ‘ibaadah. Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliporudi katika ‘ibaadah wakati wa Dhwuhaa alimuona Juwayriya akiendelea na ‘ibaadah. Wakati huo Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akamtajia maneno yale.

 

[7] Maelezo mengi yanaonesha kuwa malipo ya matendo yote ya utiifu kwa Allaah na kufanya wema, yatabakia katika amali za aliyefanya matendo hayo. Miongoni mwa hayo ni maneno haya manne yaliyotajwa katika Hadiyth hii.

[8] Ina maana ya kuwa malipo ya kusema maneno haya ni makubwa, malipo yenyewe Allaah Ameyahifadhi Jannah. Kama zilivyo hazina zozote zenye thamani kubwa zinahifadhiwa katika sehemu yenye usalama.

[9] Du’aa ni sehemu ya ‘ibaadah. Kadhalika inaweza kuwa na maana kuwa Du’aa katika aayah ya Allaah:

 

وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ ۚ إِنَّ الَّذِينَ يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِي سَيَدْخُلُونَ جَهَنَّمَ دَاخِرِينَ﴿٦٠﴾

“Na Rabb wenu Amesema: Niombeni, Nitakuitikieni. Hakika wale wanaotakabari katika kuniabudu wataingia Jahanam wadhalilike” [Al Ghaafir: 60] ina maana ‘Niabudu nami Nitajibu du’aa zako…’

 

[10] Tunabainishiwa hapa kuwa kuna baadhi ya muda du’aa zinajibiwa, kama vile katikati ya usiku na baada ya Swalaah ya fardhi. Watu walimuuliza Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) ni nini cha kuomba katikati ya Adhana na Iqaamah. Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliwaambia wamuombe Allaah al-‘aafiyah (afya na salama) katika maisha yao ya kila siku na Iymaan yao katika kuyaendea mambo yao ya Dini.

 

[11] Katika Hadiyth hii tunajifunza kuwa ni Sunnah kunyanyua mikono wakati wa kuomba du’aa

 

[12] Kutokana na mapokezi ya Hadiyth hii ni kuwa baada ya kumaliza du’aa ni vizuri kupangusa uso kwa matumbo ya mkono.

[13] Kwa hakika kumswalia Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) ni du’aa kwa Allaah ya kumuombea rahmah Nabiy wake (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) katika kongamano la Malaika, na ni tendo kubwa la ki’ibaadah. Baada ya du’aa tukufu ya

لاَ إله الاَّ الله

 inafuatiwa na ‘ibaadah ya kumuombea Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) wetu na kumswalia.

 

[14] Du’aa hii imeitwa kuwa ni bwana wa Istighfaar (kuomba maghfirah). Ina hisia kubwa ya mja kujidhalilisha kwa Bwana wake apate kile anachokiomba.

[15] Al-‘Aafiyah ni neno linalojumuisha  Allaah (عزّ وجلّ)  kumjaalia mja Wake salama na kumpa amani, na kumlinda na maradhi, balaa, majanga, madhara, misukosuko, na kila aina za shari za wanaadam na majini na kubakia salama katika Dini yake na Aakhirah yake. Katika Dini ni ile hali ya kuacha madhambi na bid’ah, au kupuuzia majukumu ya mtu ya Dini au kuyaacha moja kwa moja. Al-‘Aafiyah kwa familia ni kutokupata maradhi, na mahitaji makubwa ya matamanio ya dunia. Al-‘Aafiyah katika utajiri na mali ni mtu kuokolewa na yanayoangamiza. Katika Hadiyth hii na du’aa Allaah Anatulinda na majanga yote yanayotokana na kukosa Al-‘Aafiyah. Tukizingatia kuwa mwana Aadam amezungukwa na maadui wake wengi kutokana na mashaytwaan wa kibin Aadam na mashaytwaan wa kijini, mwana Aadam ni kama kondoo katikati ya mbwa mwitu; kama hana ulinzi kutoka kwa Allaah, hawezi kujilinda yeye mwenyewe.

[16] Neema za Allaah zinaondoshwa na madhambi ya mtu. Kwa maneno mengine, kama kwamba maneno yaliyo katika du’aa hii ni kama kumuomba Allaah Atukinge na ubaya wa matendo yetu. Kwa hakika haya ni maneno tunayofundishwa na Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) na sio ya kuwa yeye ndie aliyekuwa muhitaji zaidi kwani hakuwa na dhambi.

 

[17] Kuzidiwa na madeni na ile hali ya kuwa mtu anashindwa tena kuyalipa madeni yale na hali hii huondoa hata nia ya kulipa deni lenyewe. Kwa hakika mwenye niyyah halisi ya kulipa deni lake Allaah Atamsahilishia njia ya kulilipa na kumpa nguvu ya kulipa kama ilivyotajwa katika Hadiyth. Ama kushindwa na maadui ni ile hali ya mtu kushindwa kujitetea au kulipa kisasi cha uadui uliofanywa.

[18] Katika lugha ya Kiarabu kuomba ina maana ya kuomba jambo fulani makhsusi, wakati du’aa ni ya jumla jamala (kuomba chochote). Vile vile kumuomba Allaah kitu, inatakiwa kutumiwa maneno yale yale yaliyokuja katika Hadiyth ambayo yatapata hadhi zaidi ya kujibiwa au kukubaliwa.

[19] Inasemwa, ‘Kulala ni nusu ya mauti’. Kutokana na uhusiano uliyopo wa maneno haya. Muda wowote mtu anapolala, ni kama anarejesha roho yake katika asili yake. Vivyo hivyo, neno la Kiarabu اَلْمَصِيرُ (mwisho wa kitu) limetumika katika Hadiyth hii (mwisho wako) kwa yule anayejitayarisha kulala. Mfano huo huo, mtu anapoamka, kama kwamba anarejesha uhai baada ya kifo. Katika lugha ya Kiarabu اَلنُّشُورُ (ufufuo) umetumika katika Hadiyth hii kwa maana ya (ufufuo wako) kwa yule ambaye anaamka kutoka usingizini.

[20] حَسَنَةً Mema ya maisha haya yanahusisha vitu vizuri vyema kama vile: mwenza wa maisha (mke/mume), Taqwah, watoto wema, utajiri na kujitosha, matumizi mazuri ya elimu ya mtu, n.k. mema ya Aakhirah ni mja kuingia Jannah, na mengine mfano wake kama vile kuwa mbali na wasiwasi, hesabu ya mtu kuwa nyepesi na kuokolewa na moto. Hadiyth iliyopokelewa na Abuu Hurayrah kwamba mtu anamuomba Allaah na anajikinga na moto mara saba, nao moto unamuomba Allaah kwa kusema: ‘Mja wako fulani anaomba ulinzi wako dhidi yangu, hivyo mpe ulinzi wako.’

 

[21] Al-Baqarah aayah ya 201

[22] Katika du’aa hii, uzuri wa maisha yote mawili ni yenye kutafutwa. Haina maana kuwa mtu aombee kifo chake. Bali matamanio aina gani ya kifo ikibidi yawe, ambayo ayatampa mja malazi na makazi mazuri baada ya hapo kutokana na kila jambo la shari kabla ya kufa katika maisha haya na baada yake (kaburini).

[23] Hadiyth hii inatufungua macho kuwa tuombe elimu yenye manufaa, na tuombe kwa Allaah na tujikinge na elimu isiyokuwa na manufaa. Elimu isiyokuwa na manufaa n ile isiyokuwa na manufaa na wewe katika Aakhirah yako.

[24] Imaam Al-Bukhaariy alihitimisha Swahiyh Al-Bukhaariy kwa kutaja Hadiyth hii. Kwa kufuata mfano wake waandishi wengi na wakusanyaji wengi wamemaliza Hadiyth kwa Hadiyth hii. Hadiyth hii inathibitisha kuwepo kwa Miyzaan (kipimo cha kupima matendo ya siku ya hukumu) kama yalivyotajwa kwa uwazi katika Qur-aan. Kuna mgongano wa rai miongoni mwa Wanazuoni katika upimaji wa matendo ya watu. Baadhi ya Wanazuoni wana muono kuwa hata ile rekodi ya matendo ya watu itapimwa, kama ilivyothibitishwa na Hadiyth ya “Bitaqa” iliyoripotiwa na Ahmad, Tirmidhiy, Ibn Maajah na wengineo. (Silsilah Ahadiyth Asw-Swahiyhah 1/212 namba 135). Wanazuoni wengine wana rai kwamba kila tendo lina maana yake, kwa maana kila tendo litapimwa kivyake, kama ilivyothibitishwa na Hadiyth ya mwisho katika Buluwgh Al-Maraam (namba 1358). Hadiyth hii inatuelezea upana wa rahmah ya Allaah, kuwa anatoa malipo makubwa sana kwa matendo madogo sana, na watu kusamehewa kwa makosa yao mara kwa mara.

 

 

Ee Allaah! Al-Ghafuwr na Ar-Rahiym, Muokoe mja wako katika asiyoyaona na Mkubalie Tawbah yake kwa huruma yako. Aamiyn, Ee Allaah! Mhifadhi wa dunia na Aakhirah. Ee Allaah! Msamehe madhambi ya mwandishi wa kitabu hiki Aamiyn.

 

 

Share