021-Asbaabun-Nuzuwl: Al-Anbiyaa Aayah 101: إِنَّكُمْ وَمَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ حَصَبُ جَهَنَّمَ أَنتُمْ لَهَا وَارِدُونَ

أسْبابُ النُّزُول

Asbaabun-Nuzuwl

 

Sababu Za Kuteremshwa (Baadhi Ya  Suwrah Na Aayaat Za Qur-aan)

 

Imekusanywa na: Alhidaaya.com

 

 021-Suwrah Al-Anbiyaa Aayah: 101  

 

 

Kauli Zake Allaah (سبحانه وتعالى):

 

إِنَّكُمْ وَمَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ حَصَبُ جَهَنَّمَ أَنتُمْ لَهَا وَارِدُونَ ﴿٩٨﴾ لَوْ كَانَ هَـٰؤُلَاءِ آلِهَةً مَّا وَرَدُوهَا ۖ وَكُلٌّ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿٩٩﴾ لَهُمْ فِيهَا زَفِيرٌ وَهُمْ فِيهَا لَا يَسْمَعُونَ ﴿١٠٠﴾ إِنَّ الَّذِينَ سَبَقَتْ لَهُم مِّنَّا الْحُسْنَىٰ أُولَـٰئِكَ عَنْهَا مُبْعَدُونَ ﴿١٠١﴾ لَا يَسْمَعُونَ حَسِيسَهَا ۖ وَهُمْ فِي مَا اشْتَهَتْ أَنفُسُهُمْ خَالِدُونَ ﴿١٠٢﴾ لَا يَحْزُنُهُمُ الْفَزَعُ الْأَكْبَرُ وَتَتَلَقَّاهُمُ الْمَلَائِكَةُ هَـٰذَا يَوْمُكُمُ الَّذِي كُنتُمْ تُوعَدُونَ ﴿١٠٣﴾

Hakika nyinyi na yale mnayoyaabudu badala ya Allaah ni vichochezi vya moto wa Jahannam, nyinyi mtauingia. Lau wangelikuwa hawa ni waabudiwa wanaostahiki kuabudiwa basi wasingeliuingia; lakini wote humo ni wenye kudumu. Kwao humo, ni kupumua kwa mngurumo nao humo hawatosikia lolote. Hakika wale ambao umewatangulia wema Wetu, hao watabaidishwa nao (moto). Hawatosikia mvumo wake. Nao watadumu katika ambayo zimetamani nafsi zao. Haitowahuzunisha mfazaiko mkubwa kabisa; na Malaika watawapokea (wakiwaambia): Hii ni ile Siku yenu mliyokuwa mkiahidiwa. [Al-Anbiyaa: 98-103]

 

 

Sababun-Nuzuwl: 

 

 حدثنا عبيد بن رجال حدثنا الحسن بن علي حدثنا يحيى بن آدم حدثنا أبو بكر بن عياش ثنا عاصم عن أبي رزين عن أبي يحيى  عن ابنِ عبَّاسٍ قال : آيةٌ في كتابِ اللهِ عزَّ وجلَّ لا يسألُني النَّاسُ عنها ولا أدري أعرَفوا ولا يسألوني عنها فسُئلَ ما هيَ قال : لمَّا نزلَت : (إِنَّكُمْ وَمَا تَعْبُدُونَ مِنْ دُونِ اللَّهِ حَصَبُ جَهَنَّمَ أنْتُمْ لَهَا وَارِدُونَ) شقَّ ذلكَ علَى أهلِ مكَّةَ ، وقالوا : شتمَ محمَّدٌ آلهتَنا ، فجاءَهم ابنُ الزِّبَعْرَى فقال : ما شأنكُم ؟ قالوا : شتمَ محمَّدٌ آلهتَنا . قال : - وما قال ؟ قالوا : قال : (إِنَّكُمْ وَمَا تَعْبُدُونَ مِنْ دُونِ اللَّهِ حَصَبُ جَهَنَّمَ أنْتُمْ لَهَا وَارِدُونَ) قال : ادعوه لي ، فدعا محمَّدًا صلَّى اللهُ عليهِ وعلَى آلِه وسلَّمَ فقال ابنُ الزِّبَعْرَى : يا محمَّدٌ هذا شَيءٌ لآلهتِنا خاصَّةً أم لكلِّ ما عُبِدَ مِن دونِ اللهِ ؟ قال : بل لكلِّ ما عُبِدَ مِن دونِ اللهِ عزَّ وجلَّ . قال : فقال خصَمْناهُ وربُّ هذهِ البِنيَةِ يا محمَّدٌ ألستَ تزعمُ أنَّ عيسَى عبدٌ صالحٌ وعُزَيرًا عبدٌ صالحٌ والملائكةُ عبادٌ صالحونَ ؟ قال : بلَى . قال : فهذهِ النَّصارَى تعبدُ عيسَى وهذهِ اليهودُ تعبدُ عُزَيرًا وهذهِ بنو مَليحٍ تعبدُ الملائكةَ ، قال : فضجَّ أهلُ مكَّةَ ، فنزلَت (إِنَّ الَّذِينَ سَبَقَتْ لَهُمْ مِنَّا الْحُسْنَى أُولَئِكَ عَنْهَا مُبْعَدُونَ) قال : ونزلَت (وَلَمَّا ضُرِبَ ابْنُ مَرْيَمَ مَثَلًا إِذَا قَوْمُكَ مِنْهُ يَصِدُّونَ) وهو الضَّجيجُ

Ametuhadithia ‘Ubayd bin Rijaal, ametuhadithia Al-Hasan bin ‘Aliy, ametuhadithia Yahyaa bin Aadam, ametuhadithia Abu Bakr bin ‘Ayyaash, ametuhadithia ‘Aaswim toka kwa Abiy Raziyn toka kwa Abiy Yahyaa toka kwa Ibn ‘Abbaas, amesema: Aayah katika Kitabu cha Allaah (عز وجل), watu hawaniulizi kuhusu Aayaah hiyo (nini sababu ya kuteremshwa kwake), na sijui kama wameijua, na wala hawaniulizi kutaka kujua. Akaulizwa ni Aayah ipi hiyo? Akasema: Ilipoteremka:

((إِنَّكُمْ وَمَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ حَصَبُ جَهَنَّمَ أَنتُمْ لَهَا وَارِدُونَ))

((Hakika nyinyi na yale mnayoyaabudu badala ya Allaah ni vichochezi vya moto wa Jahannam, nyinyi mtauingia)) [Al-Anbiyaa (21:98)].

 

Khabari hiyo ilikuwa ni nzito mno kwa watu wa Makkah, wakasema: Muhammad amewatusi miungu yetu. Bin Az-Ziba-‘araa akawaendea na kuwauliza: Mna shida gani? Wakasema Muhammad amewatusi miungu yetu. Akawauliza: Kasema nini? Wakamwambia amesema:

 

((إِنَّكُمْ وَمَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ حَصَبُ جَهَنَّمَ أَنتُمْ لَهَا وَارِدُونَ))

((Hakika nyinyi na yale mnayoyaabudu badala ya Allaah ni vichochezi vya moto wa Jahannam, nyinyi mtauingia)).

 

Akawaambia: Niitieni aje kwangu. Wakamwitia Muhammad (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam). Ibn Az-Ziba-‘araa akamuuliza: Ee Muhammad! Je, jambo hili ni kwa miungu yetu tu au kwa kila kinachoabudiwa badala ya Allaah? Akasema: “Bali kwa kila kinachoabudiwa badala ya Allaah (عز وجل)”  Akasema: Tushamshinda! Naapa kwa Bwana wa nyumba hii. Ee Muhammad! Si wewe unaedai kuwa ‘Iysaa ni mja mwema? Na ‘Uzayr mja mwema? Na Malaika Waja Wema? Akasema: “Na’am, ni kweli.” Akamwambia: Basi hawa Manaswara wanamwabudu ‘Iysaa, na hawa Mayahudi wanamwabudu ‘Uzayr, na hawa Baniy Milayh wanawaabudu Malaika. Watu wa Makkah wakashangilia kwa kelele [kuona kuwa hoja nzito]. Hapo ikashuka:

 

إِنَّ الَّذِينَ سَبَقَتْ لَهُم مِّنَّا الْحُسْنَىٰ أُولَـٰئِكَ عَنْهَا مُبْعَدُونَ

((Hakika wale ambao umewatangulia wema Wetu, hao watabaidishwa nao (moto)). [Al-Anbiyaa (21:101)]

 

Na ikashuka pia:

((وَلَمَّا ضُرِبَ ابْنُ مَرْيَمَ مَثَلًا إِذَا قَوْمُكَ مِنْهُ يَصِدُّونَ))

((Na mwana wa Maryam aliponukuliwa kama mfano, tahamaki watu wako wanaupigia kelele na kushangilia)). [Az-Zukhruf (43:57)]

 

[Al-Imaam At-Twahaawiy amesema katika kitabu cha Mushkilul Aathaar Mujallad wa kwanza ukurasa wa 431][1]

 

 

[1] Baadhi Ya Wapokezi:

 

  • Abu Yahyaa, ni Miswda’u. ‘Ammaar Ad-Duhniy kasema: “Miswda’u alikuwa anamjua Ibn ‘Abbaas”. Ibn Hibaan kasema katika Adh-Dhwu’afaa: “Alikuwa akienda kinyume na Riwaayah zilizothibiti, na anabaki pweke na Riwaayah zilizo Munkar”, akikhtasir toka Tahdhiyb At-Tahdhiyb. Naye ni katika wapokezi wa Muslim. Inaonyesha kuwa Hadiyth yake inashuka chini ya kiwango cha Uhasan, lakini inafaa katika Hadiyth Shawaahid (zenye matini moja na maana moja lakini zimesimuliwa na Maswahaba wawili tofauti) na Mutaaba’aat (zenye matini moja na maana moja lakini zimesimuliwa na Swahaba huyo huyo mmoja).

 

  • Abu Raziyn ni Mas-‘uwd bin Maalik. Abu Zur-‘atah amemthibitisha kama ilivyo katika Tahdhiyb At-Tahdhiyb.

 

 

  • ‘Ubayd bin Rijaal. Huyu, Muhammad bin Ayyuwb Al-Madhwaahiriy ameandika wasifu wake katika Taraajumu Sharhi Ma’aaniy Al-Aathaar, lakini kamweleza kwa ufinyu mno. Lakini katika Al-Ikmaal Mujallad wa nne ukurasa wa 33, ‘Ubayd bin Muhammad bin Muwsaa muuza nguo na mwadhini anajulikana kama ‘Ubayd bin Rijaal ambaye anasimulia toka kwa Yahyaa bin Bukayr na Ahmad bin Swaaleh na wengineo. Abu Twaalib Al-Haafidh, Al-Miswriyy na wengineo wamesimulia kutoka kwake.

 

  • Al-Mu’alliq ameongeza: “Ibn Yuwnus ‘Ubayd bin Muhammad Muwsaa muuza nguo na mwadhini alikuwa na kun-ya ya Abul Qaasim akijulikana kama ‘Ubayd bin Rijaal mpaka mwisho wa aliyoyaeleza”.

Na katika Tabswiyrul Muntabah imeelezwa kwamba ‘Ubayd bin Rijaal ambaye ni Sheikh wa At-Twabaraaniy amemsikia Yahyaa bin Bukayr.

 

Ninasema: “Jina lake ni Muhammad bin Muhammad bin Muwsaa muuza nguo na mwadhini, na ‘Ubayd ndio laqabu yake. Inavyoonyesha ni kuwa hali yake imefichika kwa kuwa hajathibitishwa. Watu wengi wamesimulia toka kwake lakini Hadiyth imekuja bila kupitia kwake kama tutakavyokuja kuona katika Suwrat Az-Zukhruf In Shaa Allaah”.

Na kama ilivyo kwa At-Twabaraaniy katika Al-Kabiyr Mujallad wa 12 ukurasa 153 amesema (Rahimahu-Allaah): “Ametuhadithia Mu’aadh bin Al-Muthannaa, amehadithia ‘Aliy bin Al-Madiyniy, amehadithia Yahyaa bin Aadam toka kwa Abu Bakr bin ‘Ayyaash toka kwa ‘Aaswim bin Bihidlah toka kwa Abu Raziyn toka kwa Ibn ‘Abbaas”, kisha akaitaja. Lakini amedondoshwa kutoka kwake Abu Yahyaa. Hivyo hiyo inazingatiwa kuwa ni kasoro kwa Hadiyth iliyotangulia, lakini kasoro yenyewe si ya kudhuru kwa kuwa waliomwongeza (waliomtaja) Abu Yahyaa ni wengi”.

 

Njia (Sanad) ya pili ya Hadiyth:

 

Al-Imaam At-Twahaawiy (Rahimahu-Allaah) amesema katika Mujallad wa kwanza ukurasa wa 432: “Ametuhadithia Ahmad bin Daawuwd, ametuhadithia Ibraahiym bin Muhammad bin ‘Ar-‘arah, ametuhadithia Yaziyd bin Abiy Hakiym, ametuhadithia Hakam bin Abaan toka kwa ‘Ikrimah toka kwa Ibn ‘Abbaas”, kisha akataja mfanowe katika ukurasa wa 137.

 

Baadhi Ya Wapokezi:

 

Ahmad bin Daawuwd Ibn Muwsaa. Ibn Yuwnus na Ibn Al-Jawziy wamemthibitisha kama ilivyo katika Taraajum Al-Akhbaar, na wapokezi waliosalia ni katika wapokezi wa At-Tahdhiyb, amewashusha ngazi ya kuifanya Hadiyth yake kuwa Hasan. Hivyo Hadiyth kwa njia (upokezi) ya kwanza ni Swahiyh Lighayrihi. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

 

Njia ya tatu (Sanad) hadi kwa Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما)

 

Al-Imaam At-Twahaawiy (Rahimahu-Allaah) amesema katika Mushkilul Aathaar Mujallad wa kwanza ukurasa wa 431: ”Ametuhadithia Abu Umayyah, ametuhadithia Muhammad bin As Swalt, ametuhadithia Abu Kudaynah toka kwa ‘Atwaa bin As-Saaib toka kwa Sa’iyd bin Jubayr toka kwa Ibn ‘Abbaas”, kisha akataja mfanowe.

 

Al-Khatwiyb ameitaja Hadiyth hii katika Al-Faqiyhu wal Mutafaqqihu katika ukurasa wa 70 toka kwa Sheikh wake Abu Sa’iyd Muhammad bin Muwsaa As-Swayrafiy. “Ametuhadithia Abul ‘Abbaas Muhammad bin Ya’aquwb Al-Aswamm, ametuhadithia Abu Umayyah At-Twarsuwsiy”, wakaitaja baadhi ya wapokezi ambao wanahitaji kuchunguzwa. Abu Umayyah ndiye Muhammad bin Ibraahiym At-Twarsuwsiy Al-Haafidh (aliyehifadhi Hadiyth nyingi, mutuwn na asaaniyd). Ibn Hibaan amesema kuwa aliingia Misri na kuwasomea Hadiyth toka kichwani bila kitabu na kukosea. Nami hainifurahishi kutoa dalili kwa kutumia Hadiyth zake isipokuwa zile tu alizozielezea toka kwenye kitabu chake.

 

Na ‘Atwaa bin As-Saaib hifdhi yake ilidorora, na Abu Kudaynah si katika waliopokea toka kwake kabla ya mdororo huo, lakini yeye ni mutaabi’u (mshiriki) kama unavyoona. Yeye na Muhammad bin Ibraahiym kama Hadiyth haikutolewa toka kitabu chake, basi wawili hawa wanafaa katika Shawaahid na Mutaaba’aat.

 

Njia (Sanad) ya nne hadi kwa Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما):

 

Al-Imaam Abu ‘Abdillaah Al-Haakim (Rahimahu-Allaah) amesema katika Mujallad wa pili ukurasa 384: “Ametuhadithia Abul ‘Abbaas Qaasim bin Al-Qaasim As-Sayyaariy, ametuhadithia Muhammad bin Muwsaa bin Haatim, ametuhadithia ‘Aliy bin Al-Hasan bin Shaqiyq, ametuhadithia Al-Husayn bin Waaqid toka kwa Yaziyd An-Nahwiy toka kwa ‘Ikrimah toka kwa Ibn ‘Abbaas”, akataja mfanowe. Amesema Isnaad yake ni swahiyh, na wala hawakumkhariji.

 

Muhammad bin Muwsaa bin Haatim ndiye Al-Qaashaaniy (mchoraji wa kauri) katika Lisaan Al-Miyzaan inayoeleza kuwa msimulizi toka kwake ni Al-Qaasim As-Sayyaariy ambaye amesema: “Mimi sihusiki na agano lake”. Ibn Abiy Sam-’aan amesema: “Muhammad bin ‘Aliy Al-Haafidh alikuwa akimwelezea kwa picha hasi”.

           

 

 

 

Share