20-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Zakaah: Zakaah Ya Rikaaz Na Madini

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Zakaah

 

20-Zakaah Ya Rikaaz Na Madini

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Maana ya الركاز  “Rikaaz” katika lugha ya kawaida ni kitu kilichohifadhiwa chini ya ardhi kama madini au mali au kinginecho.

 

Ama kisharia (kiistilahi), ni hazina ya mali iliyofukiwa chini enzi ya kale ambayo hutolewa bila gharama zozote wala kazi kubwa ikiwa ni dhahabu, au fedha au vinginevyo.

 

Ama madini katika lugha ya kawaida, ni kutokana na neno la Kiarabu العدن  kwa maana ya kukaa mahala muda mrefu, na pia ina maana ya kiini cha kitu.

 

Ama kiistilahi, ni kila kinachotoka ardhini ambacho kimeumbwa humo kutokana na mada nyinginezo, na kina thamani.

 

Kuna madini magumu ambayo huyeyushwa na kuchakatwa kwa moto kama dhahabu, fedha, chuma, shaba, risasi na zebaki. Pia yapo madini miminika kama petrol, lami na mfano wake.

 

Rikaaz na madini ina maana moja kwa Mahanafi lakini Jumhuri ya ‘Ulamaa wametofautisha kati ya viwili hivi kutokana na Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam):

((...والمعدن جبار، وفي الركاز الخمس))

((Na madini [atakayeumia au kudhurika kwenye mgodi] hakuna fidia, na katika rikaaz ni khumsi [moja ya tano = 20%])). [Al-Bukhaariy (1499) na Muslim (1710)]

 

Hapa Rasuli ametofautisha kati ya madini na rikaaz.

 

Atakayegundua (okota) hazina ya mali, nini afanye?

 

Atakayeokota au kugundua hazina ya mali, hakosi kuwa na moja ya hali tano:

 

[1] Aipate kwenye ardhi ambayo haikuguswa na mtu au ambayo haina mmiliki

 

Itakuwa ni halali yake. Atatoa Zakaah khumsi yake (moja ya tano), na nne zilizobaki atachukua yeye.

 

Imepokewa na ‘Amri bin Shu’ayb toka kwa baba yake toka kwa babu yake kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema – kuhusu hazina ya mali ambayo mtu mmoja aliipata kwenye magofu ya enzi ya ujahili -:

 

((إن وجدته في قرية مسكونة أو في سبيل ميتاء فعرفه، وإن وجدته في خربة جاهلية، أو في قرية غير مسكونة، ففيه، وفي الركاز الخمس))

((Ikiwa umeipata kwenye kijiji chenye watu, au katika njia inayopitwa sana na watu, basi itangazie. Na kama umeipata kwenye magofu ya enzi za ujahili, au katika kijiji kisicho na watu, basi ichukue, na katika rikaaz khumsi)). [Abu Daawuwd (1710), Ash-Shaafi’iy katika Musnadi wake (674), Ahmad (2/207), na Al-Bayhaqiy (4/155)]. Sanad yake ni Hasan.

 

 

[2] Aipate kwenye barabara inayopitwa na watu au kijiji chenye watu

 

Huyu ataitangazia. Akipatikana mwenyewe basi atamkabidhi, na kama hakupatikana, basi ni haki ya mgunduaji kwa mujibu wa Hadiyth iliyotangulia.

 

[3] Aipate kwenye milki ya mtu mwingine. Hapa ‘Ulamaa wana kauli tatu:

 

Ya kwanza:

 

Itakuwa ni ya mmiliki wa ardhi. Ni kauli ya Abu Haniyfah, Muhammad bin Al-Hasan, Qiyaas ya kauli ya Maalik, na riwaya toka kwa Ahmad.

 

Ya pili:

 

Itakuwa ya mgunduaji. Ni riwaya nyingine toka kwa Ahmad, na Abu Yuwsuf ameiridhia. Wamesema: Sababu ni kuwa hazina haimilikiwi kwa kumiliki nyumba, hivyo inakuwa ni mali ya aliyeigundua.

 

Ya tatu:

 

Ni kwa uchanganuzi huu: Ikiwa mmiliki wa ardhi au nyumba atakiri ni yake, basi itakuwa mali yake, na kama akisema si yake, basi itakuwa haki ya mmiliki wa kwanza. Ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy.

 

[Al-Mabsuwtw (2/214), Fat-hul Qadiyr (2/183), Al-Mughniy (3/49), Al-Ummu (2/41) na Al-Majmuw’u (6/40)]

 

[4] Aikute ndani ya mali iliyohamia kwake kwa kununua au mfano wake. Hapa kuna kauli mbili:

 

Ya kwanza:

 

Itakuwa ya aliyeipata baada ya kumiliki mali ikiwa mmiliki wa kwanza hakuidai. Ni madhehebu ya Maalik, Abu Haniyfah na mashuhuri toka kwa Ahmad.

 

Ya pili:

 

Itakuwa ya mmiliki wa kabla yake kama atasema ni yake, na kama hakusema itakuwa ni ya wa nyuma yake na kuendelea. Na kama mmiliki wake hakujulikana, basi itakuwa ni kama mali iliyopotea. Hii ni kauli ya Ash-Shaafi’iy.

[Al-Mabsuwtw (2/212), Al-Mudawwanah (1/290), Al-Mughniy (3/49), Al-Ummu (2/44), na Al-Majmuw’u (6/40)]

 

[5] Aikute kwenye eneo la vita

 

Ikiwa ataipata kwa mbinde akisaidiana na kundi la Waislamu, basi itakuwa ni ngawira na itabeba hukmu ya ngawira. Na kama aliweza mwenyewe kuipata bila kusaidiwa, hapa ‘Ulamaa wana kauli mbili:

 

Ya kwanza:

 

Ni ya alieipata. Ni madhehebu ya Ahmad, kwa kufananisha na kilichopatikana kwenye ardhi ambayo haikuguswa na mtu.

 

Ya pili: 

 

Mmiliki wa ardhi akijulikana na akawa adui anayeupiga vita Uislamu, basi atazuiliwa ardhi, na ardhi itakuwa ghanima. Na kama hakujulikana na ardhi haikuzuiliwa, basi itakuwa ni rikaaz. Ni madhehebu ya Maalik, Abu Haniyfah na Ash-Shaafi’iy kwa uchanganuzi kati yao.

[Al-Mughniy (3/50), Al-Mudawwanah (1/291), Al-Mabsuwtw (2/215) na Al-Majmuw’u (6/40)]

 

Si sharti kiwango kitimie au mwaka ukamilike kwa rikaaz

 

Kiwango na mwaka havishurutishwi katika rikaaz, bali hulazimu kutolewa Zakaah mara tu inapopatikana. Atatoa khumsi (moja ya tano = 20%) kutokana na kauli yake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam):

((في الركاز الخمس))

((Katika rikaaz khumsi)). [Muttafaqun ‘alayhi]

 

Hii ni kauli ya Jumhuri ya ‘Ulamaa.

 

Nani atapewa khumsi ya Rikaaz?

 

‘Ulamaa wamekhitalifiana katika kubainisha watu wa kupewa khumsi katika kauli mbili:

 

Ya kwanza:

 

Khumsi hutolewa kwa wastahiki wale wale wa Zakaah. Ni kauli ya Ash-Shaafi’iy na Ahmad ingawa amesema kuwa ikiwa ataitoa swadaqah kwa masikini itamtosheleza.

 

Dalili yao ni yaliyosimuliwa toka kwa ‘Abdullaah bin Bishr Al-Khath-’amiy ambaye alipokea toka kwa mtu wa jamii yake akiitwa Hajamah akisema: ((Niliangukiwa na gudulia kwenye parokia la kale huko Kufa kwenye makaburi ya Bishr, ndani yake kuna dirham elfu nne. Nikaenda nalo kwa ‘Aliy bin Abiy Twaalib, akaniambia nizigawanye mafungu matano, nami nikazigawa. ‘Aliy akachukua fungu moja (moja ya tano) kati yake, halafu akanipa nne ya tano. Nilipompa mgongo kuondoka aliniita na kuniuliza: Je, una majirani mafukara au masikini? Nikamwambia na’am. Akasema: Basi lichukue uwagawanyie kati yao)). [Imekharijiwa na ‘Abdur Razzaaq (7179), At-Twahaawiy katika Sharhul Ma’aaniy (3/304), na Al-Bayhaqiy (4/157) kwa Sanad Dhwa’iyf]

 

Na kwa vile rikaaz inanufaikiwa toka ardhini, imefananishwa na mazao ya kilimo.

 

 

2- Hutolewa kwa wastahiki wa “fay-u” (mali inayochukuliwa toka kwa makafiri bila mapigano). Ni kauli ya Abu Haniyfah, Maalik, na riwaya katika madhehebu ya Ahmad, na Ibn Qudaamah amesema ni kauli swahiyh.

 

Dalili yao ni yaliyosimuliwa toka kwa Ash-Sha’abiy akisema: ((Mtu mmoja alikuta dinari 1000 zimezikwa akitokea Madiynah. Akaenda nazo kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu), na ‘Umar akachukua khumsi yake dinari 200, na zilizobaki akamwachia mwenyewe.  ‘Umar akaanza kuzigawa dinari 200 kwa Waislamu waliokuwepo kwake mpaka akabakisha baki. Akauliza: Yuko wapi mwenye dinari? Akasimama na kumwendea, na ‘Umar akamwambia: Chukua dinari hizi, ni zako)). [Al-Amwaal cha Abu ‘Ubayd (874) kwa Sanad Dhwa’iyf]

 

Ushahidi hapa ni kuwa lau zingelikuwa ni Zakaah, basi angezihusisha na wastahiki wake tu, na asingezirudisha tena kwa aliyezipata.

 

Wamesema: Na kwa vile “fay-u” ni waajib kwa Dhimmiy (kafiri anayeishi nchi ya Kiislamu kwa kulipa kodi, na anapatiwa himaya na haki zote za nchi), na Zakaah si waajib kwake, na kwa vile pia ni mali inayogawanywa mafungu matano, mkono wa kafiri unaondoshwa [kwa mazingatio kuwa ilizikwa enzi ya ujahili], hivyo inafanana na khumsi ya ngawira.

 

Ninasema: “Dalili hizi mbili hazifai kutolea hoja. Hata Al-Albaaniy (Allaah Amrehemu) amesema: “Hakuna kwenye Sunnah lolote lenye kutoa ushahidi wa wazi kwa kauli moja juu ya nyingine. Na kwa ajili hiyo, nimekhitari katika (hukmu ya rikaaz) kuwa pa kupelekwa kutaachiwa kiongozi wa Waislamu aamue anavyoona yeye; ataiweka pale anapoona kuna maslaha zaidi ya nchi. Na hili pia ndilo alilolikhitari Abu ‘Ubayd katika Al-Amwaal”. [Tamaam Al-Minnah uk. 378]

 

Je, madini yanaingia kwenye hukmu ya Rikaaz?

 

Maalik na Ash-Shaafi’iy wanaona kuwa madini hayapaswi kutolewa chochote isipokuwa dhahabu na fedha.

 

Ama Jumhuri, wao wanasema kuwa madini kwa aina zake zote; dhahabu, fedha (silver), shaba, chuma, risasi, petroli na mengineyo, ni kama rikaaz ambayo ni lazima haki yake itolewe, ingawa wamekhitalifiana katika kiasi chake cha kutolewa. [Al-Mabsuwtw (2/295), Al-Mudawwanah (1/292), Al-Ummu (2/45) na Al-Mughniy (3/50)]

 

Kauli hii ndiyo yenye nguvu zaidi kutokana na ujumuishi wa Kauli Yake Ta’aalaa:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَنفِقُوا مِن طَيِّبَاتِ مَا كَسَبْتُمْ وَمِمَّا أَخْرَجْنَا لَكُم مِّنَ الْأَرْضِ ۖ وَلَا تَيَمَّمُوا الْخَبِيثَ مِنْهُ تُنفِقُونَ وَلَسْتُم بِآخِذِيهِ إِلَّا أَن تُغْمِضُوا فِيهِ ۚ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ حَمِيدٌ

((Enyi walioamini! Toeni katika vizuri mlivyochuma na katika ambavyo Tumekutoleeni kutoka katika ardhi. Na wala msikusudie vibaya kutoka humo mkavitoa na hali nyinyi wenyewe si wenye kuvichukuwa isipokuwa kwa kuvifumbia macho. Na jueni kwamba hakika Allaah ni Mkwasi, Mwenye kustahiki kuhimidiwa)). [Al-Baqarah (2:267)]

 

Na hakuna shaka kuwa mafuta (petrol) yanayojulikana kama dhahabu nyeusi, ni katika madini yenye thamani kubwa zaidi. Hivyo basi, haiswihi kutolewa nje ya hukmu hii. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

Kiasi cha uwajibu katika madini

 

Abu Haniyfah na maswahibu wake, Abu ‘Ubayd na wengineo, wanaona kuwa kiasi cha uwajibu katika madini ni khumsi kama rikaaz.

 

Lakini Jumhuri wanasema ni robo ya kumi (2.5%) kwa kufanyia Qiyaas na kiwango cha dhahabu na fedha.

 

Kiini cha makhitalifiano kati ya makundi haya mawili, ni kutofautiana kwao katika ufahamu wa maana ya rikaaz. Je, madini yanaingia kwenye rikaaz au hayaingii?

 

Baadhi ya Fuqahaa wamefafanua wakisema: “Ikiwa kinachopatikana ni kingi kulinganisha na kazi na gharama, basi hapo wajibu ni khumsi (20%). Na kama ni kidogo kulinganisha na kazi na gharama, basi wajibu ni robo ya kumi (2.5%)”. [Angalia Fiqhu Az Zakaah (1/471) na kurasa zinazofuatia]

 

Na mtu ana haki ya kusema kuwa madini hayana Zakaah –isipokuwa dhahabu na fedha- kutokana na Hadiyth inavyosema:

((والمعدن جبار، وفي الركاز الخمس))

((Na madini [atakayeumia au kudhurika kwenye mgodi] hakuna fidia, na katika rikaaz ni khumsi [moja ya tano = 20%])).

.. ambapo maana ya (المعدن جبار)  ni kwamba hakuna Zakaah kwenye madini kwa dalili ya kukutanika kwake na neno    ((و في الركاز الخمس)) Isitoshe, rikaaz ni mali iliyotayari ambayo huchukuliwa bila gharama wala tabu yoyote kinyume na madini ambayo yanahitaji gharama na kazi kubwa ya kuyatoa, na kwa ajili hiyo Zakaah imeondoshwa kwa madini.

 

Ingawa yamkinika pia muradi wa neno lake (المعدن جبار)  kuwa kwa maana ya mwenye kumkodi mtu wa kumchimbia madini, mgodi ukamfunika akafa, basi hakuna fidia. Inatiliwa nguvu na kukutanishwa na neno lake:

 ((البئر جبار، والعجماء جبار))

((Kisima hakina fidia, na mnyama hana fidia)). [Kwa maana kuwa mtu akianguka kwenye kisima cha mtu akaumia au mtu akamkodi kumchimbia kikamwangukia, basi hakuna kulipwa fidia. Au mnyama wa mtu akaharibu mali au akamdhuru mtu bila ya uzembe wa mmiliki wake, basi hakuna fidia].

 

 

Share