21-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Zakaah: Hukmu Kiujumla Katika Zakaah

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Zakaah

 

21-Hukmu Kiujumla Katika Zakaah

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Je, Yatosheleza Kutoa Thamani (pesa) Badala Ya Kitu Chenyewe Kilichowajibikiwa Zakaah?

 

‘Ulamaa wana madhehebu mawili katika kutoa thamani katika Zakaah:

 

La kwanza: Hilo halijuzu. Ni madhehebu ya Maalik, Ash-Shaafi’iy, Ahmad na Daawuwd. [Al-Mudawwanah (1/258), Al-Majmuw’u (5/428-429) na Al-Mughniy (2/565)]

 

Hoja yao ni:

 

1- Sharia imeeleza na kuainisha cha waajib katika Zakaah, hivyo haijuzu kutoka nje ya kiainishwa, kama isivyojuzu katika wanyama wa kudhwahi [kuchinja wasiotajwa kama paa], wala katika manufaa, wala katika kafara.

 

2- Kauli ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam):

((في خمس وعشرين من الإبل بنت مخاض، فإن لم تكن بنت مخاض فابن لبون))

((Katika ngamia ishirini na tano [atolewe] binti makhaadh, na kama hakuna binti makhaadh, basi [atolewe] ibn labuwn)). [Imekharijiwa nyuma]

 

Wamesema: Kama thamani ingejuzu, basi angebainisha.

 

3- Neno lake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kwa yule ambaye amewajibikiwa kumtoa jadha‘a:

((تقبل منه الحقة ويجعل معها شاتين أو عشرين درهما))

((Hukubaliwa toka kwake hiqqah na aongeze juu yake mbuzi wawili, au dirhamu ishirini)). [Imekharijiwa nyuma]

 

Wamesema: Lau thamani ingelikuwa inatosheleza, basi asingemkadiria, bali amewajibisha tofauti kwa mujibu wa thamani.

 

4- Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

((فرض زكاة الفطر صاعا من تمر، أو صاعا من شعير..))

((Amefaradhisha Zakaatul Fitwr pishi ya tende, au pishi ya shayiri..)). [Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1504) na Muslim (984)]

 

Wamesema: Hapa hakutaja thamani, na kama thamani ingejuzu, basi angeeleza, kwani haja inaweza kupelekea hilo.

 

5- Pale Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alipomwambia Mu’aadh wakati alipomtuma kwenda Yemen:

((خذ الحب من الحب، والشاة من الغنم، والبعير من الإبل، والبقرة من البقر))

((Chukua nafaka kutoka nafaka, na mbuzi kutoka ghanam, na ngamia kutoka ngamia, na ng’ombe kutoka ng’ombe)). [Imekharijiwa na Abu Daawuwd (1099), Ibn Maajah (1814), Al-Haakim (1/546), Al-Bayhaqiy (4/112) na Ad-Daaraqutwniy (2/99). Kuna ulaini katika Sanad yake]

 

6- Zakaah ni waajib kwa ajili ya kuondosha dhiki ya masikini, na kutoa shukurani kwa neema ya mali. Na dhiki ziko nyingi, hivyo basi, inatakikana uwajibu uanuwaike ili umfikie masikini kwa aina zote ambazo zitaondosha dhiki yake, na kuishukuru neema kupatikane kwa faraja itokanayo na kile kile ambacho Allaah Amemneemesha mtu.

 

La pili: Inajuzu kutoa thamani (pesa). Ni madhehebu ya Abu Haniyfah, Ath-Thawriy katika madhehebu ya Al-Bukhaariy, kauli ya nguvu katika madhehebu ya Ash-Shaafi’iy na riwaya toka kwa Ahmad. Hoja yao ni: [Al-Mabsuwtw (2/156) na Al-Majmuw’u (2/429)]

 

1- Yaliyosimuliwa toka kwa Mu’aadh bin Jabal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba aliwaambia watu wa Yemen: ((Nileteeni vitambaa vya vazi la khamiysw au nguo za kuvaliwa badala ya shayiri na mahindi nichukue kutoka kwenu, kwani hilo ni jepesi zaidi kwenu na lenye kuwafaa zaidi Muhaajiriyna Madiynah)).  [Al-Bukhaariy kasema ni Mu’allaq (3/336), na Al-Haafidh kasema ni Mawswuwl katika At-Taghliyq (3/12) kwa Sanad Dhwa’iyf kutokana na kukatika kwake]

 

2- Wametoa dalili ya kutosheleza ibn labuwn badala ya binti makhaadh, na kutosheleza hiqqah na juu yake dirhamu 20 badala ya jadha‘a. (Na hizi ni dalili mbili; ya pili na ya tatu ya madhehebu ya kundi la kwanza).

 

Wamesema, katika hili  thamani inachukulika.

 

3- Makusudio ya kutoa Zakaah ni kumkidhia masikini mahitaji, na kumkidhia ni kwa kumpatia pesa, na pia kumpatia kitu. Na huenda kumwondoshea dhiki ya uhitaji kwa pesa kukawa na manufaa zaidi.

 

Kila kundi limejitahidi kuzijibu dalili za kundi jingine na kutilia nguvu mwelekeo wake. Ninaloliona lina nguvu zaidi kwa upande wangu ni lile lililokhitariwa na Sheikh wa Uislamu Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah), nalo ni kuchukulia ukati na kati katika mlango huu. Hakujuzisha ikawa ndio mwisho, wala hakuzuia ikawa ndio basi. Anaona inajuzu kutoa pesa (thamani) lakini kujuzu huko kufungamane na haja, maslaha na haki.

 

Na kama hakuna haja wala maslaha muhimu, basi lenye nguvu kwake ni kuwa hairuhusiwi kutoa pesa. Mwelekeo wake huu ni qaaidah ya kukusanya kati ya dalili tofauti. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi. [Majmuw’u Al-Fataawaa (25/80-82)]

 

Nini hukmu ya kuwahisha Zakaah kabla ya kupitiwa na mwaka?

 

Umejua kwamba mali ikifikia kiwango, basi si waajib kuitolea Zakaah mpaka mwaka ukamilike. Lakini ikiwa mwenye mali anataka kuitolea Zakaah kabla ya kutimia mwaka, hapa ‘Ulamaa wana kauli mbili:

 

Ya kwanza: Inajuzu. Ni madhehebu ya Abu Haniyfah, Ash-Shaafi’iy, Ahmad na kundi la Masalaf. [Al-Mabsuwtw (2/176), Al-Ummu (2/20), Al-Majmuw’u (6/86) na Al-Mughniy (2/470)]

 

Dalili zao ni:

1- Yaliyosimuliwa ya kuwa Al-‘Abbaas alimuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kuhusu kuwahisha Zakaah yake kabla ya muda wake. ((Rasuli akamruhusu hilo)). [Abu Daawuwd (1624), At-Tirmidhiy (678), Ibn Maajah (1795) na wengineo. Al-Albaaniy kasema ni Hadiyth Hasan katika Al-Irwaa (857)].

 

2- Yaliyosimuliwa kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alimwambia ‘Umar:

((إنا كنا تعجلنا صدقة العباس لعامنا هذا عام أول))

((Hakika sisi tulikuwa tumeiwahisha Zakaah ya Al-‘Abbaas katika mwaka wetu huu, mwaka wa kwanza)). [Angalia iliyotangulia]

 

3- Huo ni uwahishaji wa mali ambayo sababu ya uwajibu wake imeshapatikana (nayo ni kukamilika kiwango), kabla ya uwajibu wake wa kiwakati. Ni kama kuharakisha kulipa deni kabla ya kufika muda wake, kutoa kafara ya kiapo baada ya kuapa na kabla ya kuvunja kiapo, na kafara ya kuua baada ya kujeruhi kabla ya roho kutoka.

 

Ya pili: Ni marufuku. Ni madhehebu ya Maalik (lakini amelijuzisha kama zimebakia siku chache za kukamilika mwaka). Pia ni kauli ya Rabiy-‘a, Daawuwd na Ibn Hazm. [Al-Mudawwanah (1/284), Bidaayatul Mujtahid (1/232) na Al-Muhallaa (6/95)]

 

Dalili zao ni:

 

1- Hadiyth Marfuw’u ya Ibn ‘Umar: ((Hakuna Zakaah katika mali mpaka yapitiwe na mwaka)). [At-Tirmidhiy (631), Abu Daawuwd (1573), Ibn Maajah (1792), Ad-Daaraqutwniy (198) na Al-Bayhaqiy (4/104). Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika Al-Irwaa (787)]

 

2- Hadiyth ya Abu Bakr As-Swiddiyq: ((Ni kuwa alikuwa hachukui katika mali Zakaah mpaka yapitiwe na mwaka)). [Muswannaf ‘Abdur Razzaaq (7024)]

 

3- Ni kwamba mwaka ni sharti katika kuwajibika Zakaah. Hivyo haijuzu kutolea Zakaah mapema kama kiwango.

 

4- Ni kuwa Zakaah ina wakati wake. Hivyo haijuzu kuitanguliza kabla ya wakati kama ilivyo kwa Swalaah.

 

Kauli yenye nguvu

 

Inajuzu kutoa Zakaah kabla ya kupita mwaka kwa kuwa hakuna dalili ya kuzuia hilo. Ama Hadiyth (ya Ibn ‘Umar) “Hakuna Zakaah katika mali mpaka yapitiwe na mwaka”, ni kuwa Hadiyth inafahamisha tu kwamba si wajibu kutoa Zakaah kabla ya mwaka kutimilia, na hakuna ndani yake kinachozuia kuiwahisha.

 

Ama wanaposema: “Zakaah ina wakati wake maalum na haijuzu kuitanguliza kabla ya wakati huo”, basi sisi tunawaambia kuwa wakati unapoingia kwenye kitu, na ukanasibiana na kumfariji mtu, basi inatakikana (mhusika) auharakishe (kumfariji) badala ya kujifariji yeye binafsi. Ni kama deni la muda. Ama kupimia na Swalaah, hilo halijuzu kwa kuwa ‘ibaadah hazifanyiwi vipimo zenyewe kwa zenyewe, na kufananishia nyakati za Swalaah haiwezekaniki, na hivyo ni lazima zisivuke zaidi ya hapo. Allaah Ndiye Mjuzi zaidi”.

 

 

Share