02-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swiyaam: Fadhila Za Swiyaam Na Faida Zake

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swiyaam

 

02-Fadhila Za Swiyaam Na Faida Zake

 

Alhidaaya.com

 

 

 

(a) Swiyaam ni katika twa’a adhwimu za kujikurubisha kwazo kwa Allaah Ta’aalaa ambazo Muumini hulipwa thawabu zisizo na mipaka. Kwa ‘ibaadah hii, dhambi alizozifanya mtu nyuma hufutwa, hubaidishwa kati ya uso wake na kati ya moto, hustahiki mja kuingia Peponi kupitia mlango maalumu ulioandaliwa kwa ajili ya wafungaji, na mja atafurahi kwayo atakapokutana na Mola wake.

 

1- Toka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu Anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

 

((قال الله عز وجل: كل عمل ابن آدم له إلا الصيام فإنه لي وأنا أجزي به، والصيام جنة، فإذا كان يوم صوم أحدكم فلا يرفث ولا يصخب ولا يجهل، فإن شاتمه أحد أو قاتله قليقل: إني صائم –مرتين- والذي نفس محمد بيده لخلوف فم الصائم أطيب عند الله يوم القيامة من ريح المسك، وللصائم فرحتان يفرحهما: إذا أفطر فرح بفطره، وإذا لقي ربه فرح بصومه))

((Allaah ‘Azza wa Jalla Amesema: Kila ‘amali ya mwanadamu ni yake, isipokuwa Swiyaam, hakika Swiyaam yanihusu Mimi tu, na Mimi Ndiye Ninasimamia malipo yake. Na Swiyaam ni ngao, na itakapokuwa siku ya Swiyaam ya mmoja wenu, basi asitamke maneno machafu, wala asipayuke na kupaza sauti, wala asifanye mambo ya ovyo. Na ikiwa mtu atatafuta sababu ya kutukanana naye, au kupigana naye basi aseme: Hakika mimi niko kwenye Swiyaam –mara mbili-. Naapa kwa Ambaye nafsi ya Muhammad iko Mkononi Mwake, hakika harufu mbaya ya kinywa cha mfungaji, itanukia vizuri zaidi kwa Allaah Siku ya Qiyaamah kuliko harufu ya misk. Na mfungaji ana furaha mbili anazozifurahia: anapofungua hufurahi kwa kufuturu kwake, na atakapokutana na Mola wake atafurahi kwa Swawm yake)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1904) Muslim (1151) na wengineo]

 

2- Toka kwa Abu Hurayrah amesema: “Amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam):

((من صام رمضان إيمانا واحتسابا، غفر له ما تقدم من ذنبه))

((Atakayefunga Ramadhwaan kwa iymaan na kutarajia malipo [toka kwa Allaah], hughufiriwa dhambi zake zilizotangulia)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1900) Muslim (760) na wengineo]

 

3- Toka kwa Sa’iyd Al-Khudriy amesema: “Amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘ alayhi wa aalihii wa sallam):

((لا يصوم عبد يوما في سبيل الله إلا باعد الله بذلك اليوم وجهه عن النار سبعين خريفا))

((Hafungi mja siku yoyote katika Njia ya Allaah isipokuwa Allaah Ataubaidisha uso wake kwa siku hiyo na moto miaka 70)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2840), Muslim (1153) na wengineo]

 

4- Toka kwa Sahl bin Sa’ad kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

((إن في الجنة بابا يقال له الريان يدخل منه الصائمون يوم القيامة لا يدخل منه أحد غيرهم يقال: أـين الصائمون؟ فيقومون لا يدخل منه أحد غيرهم، فإذا دخلوا أغلق فلم يدخل منه أحد))

((Hakika Peponi kuna mlango uitwao Ar-Rayyaan,, wataingia kupitia kwao wafungaji Siku ya Qiyaamah, haingii yeyote kupitia kwao zaidi yao. Patanadiwa: Wako wapi wafungaji? Watasimama, haingii kupitia kwao yeyote zaidi yao. Wanapoingia, utafungwa, na hatoingia yeyote kupitia kwao)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1896), Muslim (1152) na wengineo]

 

(b) Swiyaam ni chuo cha tabia na mwenendo ambapo Muumini anajifunza humo mambo mengi. Swiyaam ni Jihaad ya nafsi, ni mapambano dhidi ya hawaa na vishawishi viovu vya Shaytwaan ambavyo vinaweza kumtokezea. Pia mtu hujizoesha kwayo kuwa na tabia ya subra kwa vitu ambavyo hawezi kuvipata, na anapokabiliwa na matukio ya kutisha na kuogofya na misukosuko. Kadhalika, hufundisha nidhamu na utiifu, hukuza kwa mtu mhemko wa huruma na udugu, na hisia ya mshikamano na ushirikiano unaowaunganisha Waislamu. [Al-Fiqhu Al-Islaamiy wa Adillatuh (2/566-568)]

 

Share