05-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Hajj Na 'Umrah: Shuruti Za Kuwajibisha Hajj

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Hajj Na ‘Umrah

 

05-Shuruti Za Kuwajibisha Hajj

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Nazo ni sifa ambazo ni lazima mtu awe nazo ili atakiwe kufanya Hajj kwa njia ya waajib. Mwenye kukosa moja ya shuruti hizi, basi Hajj si lazima kwake. Shuruti ni tano: Uislamu, akili, kubaleghe, uungwana na uwezo.

 

Ibn Qudaamah amesema: “Hatujui katika haya yote mvutano wowote”. [Al-Mughniy (3/218) na Nihaayat Al-Muhtaaj (2/375)]

 

-  Uislamu na akili, haya ni masharti mawili ya kuswihi Hajj pia. Hajj ya kafiri au mwendawazimu haiswihi.

 

- Ama kubaleghe na uungwana, haya ni masharti mawili ya kutosheleza Hajj pia, lakini si masharti ya kuswihi Hajj. Na lau mtoto mdogo au mtumwa watahiji, basi Hajj yao itaswihi. Ni kwa Hadiyth ya mwanamke aliyemnyanyua mtoto mdogo mbele ya Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akauliza: Je huyu ana Hajj? Akasema:

((نعم، ولك الأجر))

((Na’am, na wewe una malipo)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1336), Abu Daawuwd (1736) na An-Nasaaiy (5/120)]

 

Lakini kwa mujibu wa kauli yenye nguvu, ufaradhi wa Hajj hauondoki kwa mtoto au mtumwa. Ni kwa Hadiyth isemayo:

 

((من حج ثم عتق فعليه حجة أخرى، ومن حج وهو صغير ثم بلغ فعليه حجة أخرى))

((Aliyehiji kisha akaachwa huru, basi ni juu yake Hajj nyingine, na aliyehiji udogoni kisha akabaleghe, basi ni juu yake Hajj nyingine)). [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh. Imekharijiwa na Ibn Khuzaymah (3050), Al-Haakim (1/481) na Al-Bayhaqiy (5/179). Angalia Al-Irwaa (4/59)]

 

-  Ama uwezo, huu unakuwa ni sharti ya uwajibu tu. Lau mtu asiye na uwezo atajilazimisha kwa mbinde na tabu akahiji, basi Hajj yake ni swahiyh inayotosheleza. Ni kama mtu aliyejilazimisha kuswali au kufunga kwa tabu naye hawajibikiwi na Swalaah au Swawm, lakini zitaswihi. [Al-Mughniy (3/214)]

 

 

 

Share