09-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Hajj Na 'Umrah: Picha Halisi Ya Hijjah ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Hajj Na ‘Umrah

 

09-Picha Halisi Ya Hijjah ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)   

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

Toka kwa Ja’afar bin Muhammad toka kwa baba yake amesema: ((Tuliingia kwa Jaabir bin ‘Abdillaah nikamwambia: Nielezee kuhusu Hijjah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam). Akaashiria kwa mkono wake akakunja (hesabu) tisa, akasema: Hakika Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikaa miaka tisa hakuhiji. Kisha katika mwaka wa kumi, watu walitangaziwa kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) atakwenda kuhiji. Watu wengi mno wakaja Madiynah, na wote wanataka kumfanya Rasuli wa Allaah kigezo kwa kutenda kama atakavyotenda. Tukatoka pamoja naye mpaka tukafika Dhul-Hulayfah, na Asmaa bint ‘Umays akajifungua Muhammad bin Abiy Bakr. Akatuma mtu kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amuulizie nini afanye? Akasema:

 

((اغتَسِلي، واستَثْفِري بثوبٍ، وأَحْرِمي))

((Oga, ufunge utupu wako vizuri kwa kitambaa, kisha hirimia )).

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akaswali Msikitini, kisha akampanda Al-Qaswaa (ngamia wake), akaenda naye mpaka ngamia alipokaa naye sawa juu ya Al-Baydaa [alihirimia Hajj]. Niliangalia upeo wa macho yangu mbele yake nikaona watu kati ya waliopanda wanyama na wenye kutembea kwa miguu, na kulia kwake hivyo hivyo, kushoto kwake hivyo hivyo, na nyuma yake hivyo hivyo, na Rasuli wa Allaah yuko baina yetu huku Qur-aan inamteremkia, na yeye anajua taawiyl yake. Na chochote alichokifanya nasi pia tulikifanya. Rasuli akanyanyua sauti kuleta Talbiyah [Tawhiyd] akisema:

 

لبيك اللهم لبيك، لبيك لا شريك لك لبيك إن الحمد والنعمة لك والملك لا شريك لك

“Nimekuitikia haraka ee Allaah nimekuitikia haraka. Nimekuitikia haraka, Huna mshirika, nimekuitikia haraka. Hakika Himdi na Neema ni Zako pamoja na Ufalme, Huna mshirika”.

 

Na watu wakaitikia kwa sauti [huku baadhi yao] wakiongeza au wakibadili tamko la Rasuli, na Rasuli wa Allaah hakuwasemesha kitu, bali aliendelea kuleta Talbiyah yake. Jaabir (Radhwiya Allaah ‘anhu) akasema: Hatunuwii isipokuwa Hajj, hatujui ‘Umrah. Tukaenda pamoja naye hadi tukafika kwenye Nyumba (Al-Ka’abah), akaligusa Jiwe Jeusi kwa mkono wake, akaenda mwendo wa haraka mara tatu na akatembea mwendo wa kawaida mara nne [katika Kutufu]. Kisha akapenya watu akaenda Maqaam Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) akasoma

 

وَاتَّخِذُوا مِن مَّقَامِ إِبْرَاهِيمَ مُصَلًّى  

 

akaiweka Maqaam baina yake na Al-Ka’abah (akaswali katikati). Baba yangu alikuwa anasema na mimi najua kwa yakini kuwa kaliona toka kwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam):  Alikuwa anasoma katika rakaa mbili

 

قُلْ يَا أَيُّهَا الْكَافِرُونَ

Na,

قُلْ هُوَ اللَّـهُ أَحَدٌ

 

(Suwrah Al-Kaafiruwn na Suwrah Al-Ikhlaasw):

 

Kisha akarudi tena kwenye Jiwe Jeusi akaligusa kwa mkono wake, halafu alitoka kupitia mlangoni kuelekea As-Swafaa. Alipoikurubia As-Swafaa alisoma:

 

إِنَّ الصَّفَا وَالْمَرْوَةَ مِن شَعَائِرِ اللَّـهِ

na kusema:

"أبدأ بما بدأ الله به"

 

“Ninaanza kwa Alilolianzia kwalo Allaah”. Akaanzia As-Swafaa, akapanda juu yake mpaka akaweza kuiona Nyumba (Al-Ka’abah), akaelekea Qiblah, akamuwahidisha Allaah na akamkabirisha na kusema:

 

لا إِلَهَ إِلاَّ اللهُ وَحْدَهُ لَا شَرِيْكَ لَهُ، لَهُ الـمُلْكُ ولَهُ الـحَمْدُ، وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيءٍ قَديرٌ، لَا إلَهَ إِلاَّ اللهُ وَحْدَهُ، أَنْجَزَ وَعْدَهُ، وَنَصَرَ عَبْدَهُ، وهَزَمَ الأَحْزَابَ وَحْدَهُ

 

“Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah Mmoja Asiye na mshirika, ni Wake Ufalme na ni Yake Hamdi, na Yeye ni Mweza juu ya kila kitu. Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah Mmoja, Ametekeleza Ahadi Yake, Amemsaidia Mja Wake, na Ameyashinda makundi Peke Yake”.

 

Kisha akaomba du’aa baina ya maneno hayo, na akasema mfano wake mara tatu. Halafu akateremka kwenda Al-Marwah. Miguu yake ilipojikita barabara chini ya bonde aliharakisha mwendo mpaka tulipoanza kupanda, hapo alitembea mwendo wa kawaida hadi Al-Marwah. Akafanya juu ya Al-Marwah mithili ya aliyoyafanya juu ya As-Swafaa mpaka ulipofika mzunguko wake wa mwisho juu ya Al-Marwah alisema: Lau jambo langu lingenibainikia mapema [kuwa Tamattu’u ni bora zaidi] nisingelifanya Qiraan kwa kuja na mnyama, na ningeliifanya ‘Umrah. Basi yeyote kati yenu asiye na mnyama, basi avue Ihraam na aifanye ‘Umrah. Suraaqah bin Maalik bin Khuth-‘um alisimama na kusema: Ee Rasuli wa Allaah! Je, ni kwa mwaka wetu huu tu au hadi milele? Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akaviumanisha vidole vyake kimoja ndani ya kingine akasema: ‘Umrah imeingia ndani ya Hajj –mara mbili- hapana, bali milele milele. ‘Aliy akaja toka Yemen akiwa na ngamia wa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam), akamkuta Faatwimah ni mmoja kati ya waliovua Ihraam, amevaa nguo ya rangi na amejitia wanja. Akamshangaa sana kwa kufanya hivyo. Faatwimah akamwambia: Baba yangu ameniamuru kufanya hivi, na ‘Aliy alikuwa akizungumza kwa lahaja ya Kiiraqi. Nikaenda [Jaabir] kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) ili kumkwaza Faatwimah kutokana na jambo alilolifanya kwa kumuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kuhusu hayo ambayo Faatwimah ameyaeleza kuwa yeye amemwamuru. Nikamweleza kuwa mimi nimemshangaa sana kwa aliyoyafanya. Rasuli akasema: Amesema kweli, amesema kweli. Akaniuliza: Umesema nini ulipohirimia Hajj? Nikasema: Ee Allaah! Mimi ninahirimia kwa alilohirimia kwalo Rasuli Wako. Akasema: Mimi nina wanyama wa kuchinja, basi usivue Ihraam. [Jaabir] anaendelea kusema: Jumla ya wanyama wa kuchinja aliokuja nao ‘Aliy kutoka Yemen na ambao Nabiy alikuja nao ilikuwa mia moja. Watu wote wakavua Ihraam na wakapunguza nywele isipokuwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) pamoja na wale waliokuwa na wanyama. Ilipofika Siku ya Tarwiyah, walikwenda Mina na wakahirimia Hajj. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alimpanda mnyama wake, akaswali hapo Minaa Adhuhuri, Alasiri, Magharibi, ‘Ishaa na Alfajiri. Kisha alikaa kidogo mpaka jua likachomoza. Akaamuru afungiwe hema la manyoya eneo la Namirah. Rasuli wa Allaah (Swallah Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akaenda huku Maqureshi wakidhani kwamba atasimama kwenye Al-Mash-‘ar Al-Haraam kama walivyokuwa wanafanya wao enzi ya ujahilia. Lakini Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alipitiliza mpaka akafika karibu na ‘Arafah. Akakuta hema lake lishafungwa Namirah, na akashukia hapo. Na jua lilipopinduka, aliamuru aletewe Al-Qaswaa [ngamia wake], akatayarishwa, akampanda hadi chini ya bonde, na hapo aliwakhutubia watu. Akasema: Hakika damu zenu na mali zenu ni haramu juu yenu kama haramisho la Siku yenu hii, katika Mwezi wenu huu, na katika mji wenu huu. Jueni kwamba kila kitu katika mambo ya ujahilia nimekiweka chini ya miguu yangu [nimekisamehe, nimekifuta], na mauaji ya ujahilia yamesamehewa. Na mauaji ya kwanza ninayoyasamehe katika watu wetu waliouawa ni damu ya Ibn Rabiy-‘ah bin Al-Haarith, alikuwa anatafutiwa mama wa kumnyonyesha katika Baniy Sa’ad, Hudhayl wakamuua. Na riba ya ujahili imesamehewa, na riba ya kwanza ninayoisamehe ni riba yetu; riba ya ‘Abbaas bin ‘Abdil Muttwalib, riba yote hiyo imesamehewa na kufutwa. Basi mcheni Allaah katika wake zenu, kwani nyinyi mmewachukua kwa dhamana ya Allaah, na mmehalalishiwa tupu zao kwa Neno la Allaah. Na haki zao kwenu ni kuwa wasimwingize nyumbani kwenu yeyote msiyetaka aingie, na wakifanya hivyo, basi wapigeni pigo hafifu, na nyinyi mna wajibu kwao wa kuwakimu kwa chakula na nguo kwa mujibu wa ada na desturi. Na ka hakika mimi nimekuachieni kitu ambacho hamtopotea baada yake kama mtashikamana nacho;  Kitabu cha Allaah, na nyinyi mtaulizwa kuhusu mimi [kama nimefikisha Ujumbe au la], basi je mtajibu nini? Wakasema: Tunashuhudia kwamba wewe umefikisha, umetekeleza na umenasihi. Akasema huku amekinyanyua kidole chake cha shahada mbinguni na kukizungusha kwa watu: Ee Allaah Shuhudia, ee Allaah Shuhudia (mara tatu). Kisha akaadhini halafu akaqimu, akaswali Adhuhuri, halafu akaqimu akaswali Alasiri, na hakuswali baina ya Swalaah hizi Swalaah yoyote ya Sunnah. Kisha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alimpanda ngamia wake akaenda naye mpaka sehemu ya kisimamo, akamwelekeza upande wa miamba ya mawe, na njia ya watembeao kwa miguu ikawa mbele yake. Akaelekea Qiblah, na aliendelea kusimama mpaka jua likachwa, unjano wake ukapotea kidogo na mduara wake ukatoweka. Kisha akampandisha Usaamah nyuma ya ngamia wake, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akaanza kuondoka akiwa ameikaza barabara kamba ya ngamia wake [kumdhibiti asiende mbio] mpaka kichwa chake kikawa kinagusana na vishikio vya kupumzishia miguu ya mpandaji. Akawa anawaashiria watu kwa mkono wake wa kulia akiwaambia: Enyi watu! Nendeni taratibu. Nendeni kwa upole. Na kila anapofika kwenye kifusi cha mchanga, aliilegeza kamba ya ngamia kidogo ili aweze kupanda kwa usahali. Alikwenda hadi akafika Muzdalifah, akaswali hapo Magharibi na ‘Ishaa kwa adhana moja na iqaamah mbili, na hakuswali Sunnah yoyote kati ya Swalaah hizo mbili. Halafu Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akalala kwa ubavu mpaka Alfajiri ilipochomoza. Akaswali Swalaatul Fajr wakati As-Subh ilipowadia kwa adhana moja na iqaamah moja. Halafu akampanda Al-Qaswaa mpaka akafika Al-Mash-‘ar Al-Haraam [eneo la Mlima wa Qazah uliopo Muzdalifah], akaelekea Qiblah, akamwomba Allaah, akamkabirisha, akamhalilisha na akamuwahidisha. Aliendelea kusimama katika hali hiyo mpaka anga likawa la kinjano sana, kisha akaondoka kabla jua halijapanda. Rasuli akambeba Al-Fadwl bin ‘Abbaas nyuma ya ngamia wake. Al-Fadwl alikuwa na nywele nzuri, mweupe wa rangi, na mjamala wa sura. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alipoanza kuondoka, walipita mbele yake wanawake wenye kwenda haraka. Al-Fadhwl akaanza kuwaangalia na Rasuli wa Allaah (Swallah Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akauweka mkono wake kwenye uso wa Al-Fadhwl [kumzuia]. Al-Fadhwl akaugeuza uso upande mwingine apate kuangalia. Wakaendelea kwenda mpaka Rasuli akafika eneo la Muhassir, na hapo aliongeza mwendo wa ngamia wake. Kisha akapitia njia ya kati inayotokezea Al-Jamarat Al-Kubraa mpaka akalifikia guzo [Jamarah] lililopo mbele ya mti. Akalitupia vijiwe saba huku akileta Takbiyrah kwa kila kijiwe. Ukubwa wa kila kijiwe ni sawa na kijiwe cha kurusha kwa manati au kwa kidole. Alitupia toka ndani ya bonde. Kisha aliondoka hadi machinjioni, akachinja ngamia sitini na tatu kwa mkono wake, halafu alimpa ‘Aliy akachinja waliobakia na akamshirikisha katika wanyama wake. Halafu akaamuru kiletwe kipande cha nyama ya kila ngamia, vikatiwa kwenye jungu vikapikwa. Akala nyama hiyo yeye na ‘Aliy na wakanywa supu yake. Kisha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akampanda ngamia wake na kuelekea Al-Ka’abah, akaswali Adhuhuri Makkah. Akawaendea Baniy ‘Abdil Muttwalib wakiwa katika shughuli ya kuteka, kujaza mahodhi na kunywesha watu maji ya Zamzam, akawaambia: Tekeni maji enyi Baniy Al-Muttwalib. Na lau [si mimi kuhofia] watu kuwazidini nguvu na kukamata kazi yenu ya kunywesha watu maji, basi ningeliteka maji pamoja nanyi. Wakampa ndoo ya maji, akanywa nayo maji. 

 

 

Na ametuhadithia ‘Umar bin Hafsw bin Ghiyaath, ametuhadithia baba yangu, ametuhadithia Ja-‘afar bin Muhammad, amenihadithia baba yangu amesema: ((Nilimwendea Jaabir bin ‘Abdillaah nikamuuliza kuhusu Hijjah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam), akanihadithia sawa na alivyohadithia Haatim bin ‘Ismaaiyl, na akaongeza katika Hadiyth yake: “Abu Sayaarah alikuwa akiwapeleka Waarabu akiwa amepanda punda asiye na tandiko [enzi ya ujahilia]. Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alipopita Al-Mash-ar Al-Haraam akitokea Muzdalifah, Maqureshi walidhani atasimama na kushukia hapo. Rasuli akapita bila hata kusimama mpaka akawasili ‘Arafaat, akashukia hapo)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1218), Abu Daawuwd (1905), Ibn Maajah (3074), Ad-Daaramiy (1850) na wengineo]

 

 

 

Share