10-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Hajj Na 'Umrah: Muhtasari Wa Vitendo Vya Hajj Ya Mwenye Kufanya Tamattu’u

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Hajj Na ‘Umrah

 

10-Muhtasari Wa Vitendo Vya Hajj Ya Mwenye Kufanya Tamattu’u

 

Alhidaaya.com

 

 

 

[Hajj inajuzu kwa moja ya aina tatu: Ifraad, au Tamattu’u au Qiraan ambazo tutazifafanua mbeleni. Tamattu’u ni bora na nyepesi zaidi, nayo inamfaa zaidi Hujaji toka nchi yetu (Misri)]

 

Hakuna shaka yoyote kuwa Muislamu ana pupa ya Hajj yake kuwa na sifa sawa na Hijjah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa waalihii wa sallam) ili iwe na uhakika zaidi wa kukubaliwa, na imkurubishe zaidi katika kuzipata fadhla za Hajj zilizotajwa nyuma.

 

Hivyo basi, ninayaandika hapa kwa muhtasari matendo ya “Hajj ya Tamattu’u” toka katika mjumuiko wa Hadiyth za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam), kisha nitafuatishia mfululizo huu kwa kuvichambua vitendo hivyo na vigawanyo vyake kwa upande wa nguzo, waajibaat, mustahabbu na kadhalika. Hivyo nasema:

 

 

Kabla Ya Safari

 

1- Aliyepata uwezo wa kuhiji, na akaweka azima na nia ya mwisho ya kuitekeleza Hajj, basi aharakie kutubia toba safi ya kweli kwa maasia yake, ajitahidi kutoka ndani ya duara la kudhulumu watu kwa kuwarejeshea wenyewe haki zao, ajitahidi kulipa madeni yake kiasi awezavyo, ajitahidi kuwafurahisha wazazi wake na kupata ridhaa yao, awaombe radhi jamaa zake kama kuna kitu kati yake na wao, na awaachie watoto na wote anaowakimu kimaisha cha kuwaendeshea maisha muda wote wa kutokuwepo yeye.

 

2- Awe na pupa ya kuhakikisha kuwa gharama zake za kuhijia ni za chumo halali. Atahadhari na fedha zenye utata wa uhalali au uharamu, au mali haramu (ya kupora) ili awe karibu zaidi na kukubaliwa Hajj yake.

 

3- Ajitahidi kuongozana na msafara wa watu wema wenye utashi wa kheri, wenye kuchukia shari na watakaomsaidia. Kama itakuwa wepesi kupata msafara wa ‘Ulamaa wenye kuhangaikia watu, basi itakuwa bora zaidi.

 

4- Atoke kwenda safari yake akiwajibika na adabu za kisharia katika safari, na hiyo ni katika miezi ya Hajj.

 

Kuhirimia

 

5-  Anapofika katika Miyqaat, atavua nguo zake, atakoga kama anavyooga janaba, na atajitia manukato mazuri zaidi atakayokuwa nayo. Mwanamke atafanya hivyo hivyo hata kama atakuwa na hedhi au nifasi. Kubakia harufu ya manukato kwenye nguo au mwili baada ya kuhirimia hakuna neno kwao wote wawili (mwanaume na mwanamke).

 

6- Mwanaume atavaa mavazi ya Ihraam (vipande viwili), na mwanamke atavaa nguo yoyote aipendayo.

 

7- Ukiingia wakati wa Swalaah yake ya Faradhi ataswali, na kama haukuingia, ataswali rakaa mbili kwa niya ya Sunnah ya wudhuu. Akimaliza, atanuwia kuhirimia ‘Umrah baada ya kupanda kipando chake (gari, meli, ndege, mnyama n.k) na atamhimidi Allaah na kupiga Takbiyr akielekea Qiblah, kisha aseme:

 

((لبيك اللهم عمرة))

 

8- Atakayekuwa ndani ya ndege, atahirimia atakapokuwa mkabala na Miyqaat, kwa ndege kuwa juu ya eneo hilo. Atakuwa ashajiandaa kabla ya kuhirimia kwa kuoga, kujitia manukato na kuweka tayari mavazi ya Ihraam.

 

9- Anapohirimia ‘Umrah kwa sauti atalabbi:

 

((لبيك اللهم لبيك، لبيك لا شريك لك لبيك، إن الحمد والنعمة لك والملك، لا شريك لك))

 

Mwanaume atanyanyua sauti yake akiitikia Talbiyah, na mwanamke atanyanyua kwa kiasi tu cha mwanamke aliye pembeni yake kumsikia.

 

10– Aliyehirimia anatakiwa akithirishe Talbiyah na hususan zinapobadilika hali na nyakati kama anapopanda kwenye mnyanyuko au anaposhuka kwenye mteremko, au usiku unapoingia au mchana. Mwanamke ataleta Talbiyah hata kama ana hedhi, na Talbiyah haikatishwi isipokuwa pale anapoanza Twawaaf. [Kwa kuwa yuko kwenye ‘Umrah. Ama mwenye kufanya “Ifraad”, au mwenye kufanya “Qiraan”, hawa hawakatishi Talbiyah mpaka pale wanapoanza kutupia Jamarat Al-‘Aqabah]

 

 

Kuingia Makkah Na Kutufu

 

11- Anapofika Makkah, aharakie kwenda Al-Masjid Al-Haraam, atangulie kuliendea Jiwe Jeusi, aliguse kwa mkono wake wa kulia na alibusu – kama itakuwa wepesi - na kama haikuwezekana ataligusa na ataubusu mkono wake. Kama hakuweza kuligusa, ataashiria kwa mkono wake, atapiga Takbiyr na hatoubusu mkono wake. Ni vizuri asiwasonge watu akawaudhi, na yeye akapata adha yao.

 

12- Kisha atatufu – Al Ka-’abah ikiwa kushotoni kwake -, na anapofika katika Nguzo ya Al-Yamaaniy (Ar-Ruknu Al-Yamaaniy), ataigusa bila kuibusu kama itakuwa wepesi. Anapokuwa kati ya Nguzo ya Al-Yamaaniy na Jiwe Jeusi atasema:

 

((رَبَّنَا آتِنَا فِي الدُّنْيَا حَسَنَةً وَفِي الْآخِرَةِ حَسَنَةً وَقِنَا عَذَابَ النَّارِ))

 

Anapolifikia Jiwe Jeusi, anakuwa ametimiza mzunguko mmoja, na atafanya kando yake aliyoyafanya mwanzoni, kisha ataendelea na Twawaaf mpaka akamilishe mizunguko saba.

 

13- Mwanamume – si mwanamke - anatakikana apitishe sehemu ya nguo yake ya juu (ridaa) chini ya kwapa lake la kulia na ncha zake mbili azitupie juu ya bega lake la kushoto kuanzia mwanzo wa Twawaaf hadi mwisho wake. Ataharakiza mwendo katika mizunguko mitatu ya kwanza tu, na iliyobaki minne atazunguka kwa mwendo wa kawaida.

 

14- Akimaliza Twawaaf ataswali rakaa mbili nyuma ya Maqaam Ibraahiym. Atasoma katika rakaa mbili Suwrat Al-Kaafiruwn na Suwrat Al-Ikhlaas.

 

15- Kisha atakwenda kunywa maji ya Zamzam na atajimwagia kichwani.

 

16- Halafu atarudi tena kwenye Jiwe Jeusi na ataligusa ikiwa itakuwa wepesi kwake.

 

 

Kusai (kwenda) Kati Ya Swafaa Na Marwah

 

17- Kisha atatoka kwenda sehemu ya Kusai. Anapokaribia Swafaa atasoma:

 

 

إِنَّ الصَّفَا وَالْمَرْوَةَ مِن شَعَائِرِ اللَّـهِ

na atasema:

 

 "أبدأ بما بدأ الله به"

((Ninaanza kwa Aliloanza nalo Allaah)).

 

18- Atapanda juu ya Swafaa mpaka aione Al-Ka-‘abah na aielekee na aseme:

 

((لا إِلَهَ إِلاَّ اللهُ وَحْدَهُ لَا شَرِيْكَ لَهُ، لَهُ الـمُلْكُ ولَهُ الـحَمْدُ، وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيءٍ قَديرٌ، لَا إلَهَ إِلاَّ اللهُ وَحْدَهُ، أَنْجَزَ وَعْدَهُ، وَنَصَرَ عَبْدَهُ، وهَزَمَ الأَحْزَابَ وَحْدَهُ))

Ataomba atakacho, na atafanya hivyo mara tatu.

 

 

19- Kisha atateremka toka Swafaa kwenda Marwah akitembea. Kati ya alama (taa) mbili za kijani, mwanamume atakwenda matiti (mchakamchaka) na si mwanamke.

 

20- Anapofika Marwah, atafanya kama alivyofanya juu ya Swafaa. Na hii itakuwa ni raundi moja ya kwanza. Kisha atateremka kwenda Swafaa, na ataendelea hivyo hivyo mpaka akamilishe raundi saba (kwenda ni raundi na kurudi ni raundi).

 

 

Kujivua Na Ihraam

 

21- Anapomaliza Kusai, atanyoa nywele zake au atazipunguza. Kupunguza hapa ni bora zaidi na hasa hasa ikiwa wakati wa Hajj umekurubia. Mwanamke hanyoi bali hupunguza.

 

Kisha atavaa nguo zake za kawaida, na kila lililokuwa marufuku kwake baada ya kuhirimia kama kujimai, linakuwa halali mpaka utakapowadia wakati wa kuanza Hajj. [Hadi hapo ‘ibaadah ya ‘Umrah itakuwa imemalizika]

 

Siku Ya Tarwiyah

 

22- Inapofika tarehe nane ya Dhul-Hijjah (Siku ya Tarwiyah), atajiandaa kuhirimia kama ilivyotangulia – toka nyumbani kwake Makkah - kisha atahirimia Hajj kwa kusema:

 

لبيك اللهم بحجة

na ataleta Talbiyah.

 

Akihofia jambo fulani linaweza kumzuia asiweze kuitimiza Hajj yake, basi anaweza kuweka sharuti kwa kusema:

 

 وإن حبسني حابس فمحلي حيث حبستني

Na kama kitanizuia kizuizi, basi pangu pa kuvua Ihraam ni pale Utakaponizuia”.

 

 

23- Kisha atatoka kwenda Minaa wakati wa Dhuhaa (jua linapopanda) na atalala huko Minaa. Ataswali huko Adhuhuri, Alasiri, Magharibi, ‘Ishaa na Alfajiri kwa kupunguza bila kukusanya.

 

 

Siku ya ‘Arafah

 

24- Jua linapochomoza – tarehe tisa (‘Arafah) - atatembea toka Minaa hadi ‘Arafah. Atashukia Namirah, na atakaa hapo mpaka jua litakapopinduka (Adhuhuri) kama itakuwa ni wepesi.

 

25- Jua linapopinduka, atakusanya Adhuhuri na Alasiri kwa pamoja kwa kupunguza (rakaa mbili mbili) kwa Adhana moja na Iqaamah mbili – pamoja na imam - bila Sunnah. (Zitaswaliwa zote katika wakati wa Swalaah ya Adhuhuri).

 

26- Kisha baada ya kuswali, ataacha mengine yote akae kuleta adhkaar, kuomba du’aa, na kunyenyekea kwa Allaah Ta’aalaa katika eneo hilo la ‘Arafah huku akinyanyua mikono yake, akiwa ameelekea Qiblah – na si kuelekea Kilima- na atasimama hivi mpaka jua lizame.

 

27- Jua linapozama, atateremka kwa taratibu na upole.

 

 

Kutoka ‘Arafah Kwenda Muzdalifah Na Kulala Huko

 

28- Kisha atatembea hadi Muzdalifah. Akifika huko, atakusanya Magharibi na ‘Ishaa kwa pamoja kwa Adhana moja na Iqaamah mbili bila Sunnah. (Zitaswaliwa zote katika wakati wa Swalaah ya ‘Ishaa)

 

29- Atalala Muzdalifah mpaka Alfajiri, na hatoswali Sunnah za usiku.

 

30- Ataswali Alfajiri mwanzoni mwa wakati kwa Adhana moja na Iqaamah moja. Kisha atasimama juu ya Al-Mash-‘ar Al-Haraam (Mlima mashuhuri Muzdalifah) ataelekea Qiblah, ataomba, ataleta Takbiyrah, na ataleta Tahliyl (Laa ilaaha illa Allaah) mpaka unjano wa asubuhi ukomae.

 

31- Wanawake madhaifu na wengineo, wanaruhusika kuondoka Muzdalifah baada ya usiku wa manane mwezi unapotoweka.

 

Siku Ya Kuchinja (Yawm An-Nahr) Na Kwenda Minaa Na Kutupia (vijiwe) Jamarah

 

 

32- Kisha ataondoka toka Muzdalifah kwenda Minaa asubuhi inapovaa unjano kabla jua halijachomoza. Ataharakisha mwendo zaidi akifika Bonde la Muhassar.

 

33- Akifika Minaa, ataikata Talbiyah wakati anapoanza kutupia Jamaratul Aqabah – nayo ni ya mwisho kuelekea Makkah - kwa vijiwe saba mfululizo kimoja baada ya kingine. Atapiga Takbiyr kwa kila kijiwe, na kutupia kunakuwa baada ya jua kuchomoza.

 

34- Anapomaliza kutupia Jamaratul Aqabah, ataruhusiwa kuyafanya yote yaliyokuwa marufuku isipokuwa kujimai. [Hii inaitwa Tahallul ya kwanza. Atavaa nguo aitakayo, atakata kucha na atajitia manukato]

 

35- Kisha atachinja mnyama wake Minaa au Makkah, na anaruhusiwa kuchinja siku yoyote katika Masiku Matatu ya Tashriyq.  Kama hana fedha ya kununulia mnyama, atafunga siku tatu katika Hajj na nyingine saba baada ya kurudi kwao.

 

36- Halafu atanyoa kichwa chake, na mwanamke atapunguza nywele zake hata kwa kiasi cha pingili ya kidole.

 

Kurudi Makkah Na Twawaaf Ya Ifaadhwah

 

37- Halafu atarudi Makkah, atatufu mara saba, na atasai kati ya Swafaa na Marwah. [Kwa kuwa anafanya Tamattu’u, ama mwenye kufanya Qiraan, huyo hatufu isipokuwa Twawaaf moja tu].

 

Anaweza kuahirisha Twawaaf siku ya mwisho ya Tashriyq. Akitufu, kila kitu kitakuwa halali hata kujimai pia. [Hii ndio Tahallul kubwa]

 

38- Mwanamke akiwa na hedhi – wakati wa kufanya ‘amali za Hajj -, atafanya mambo yote isipokuwa Twawaaf, ataiakhirisha mpaka atwaharike kama ataweza.

 

39- Ikiwa atapata uzito na tabu kama atasubiri atwaharike – kama ashakuwa amebuku tarehe ya safari ya kurudi au akahofia madhara kama atabakia - basi atatufu akiwa na hedhi yake kwa mujibu wa kauli sahihi zaidi ya ‘Ulamaa, kwa kuwa huo ndio upeo wa mwisho wa uwezo wake.

 

Kwenda Minaa

 

40- Kisha baada ya Kutufu na Kusai, atarudi tena Minaa ili kulala huko Masiku ya Tashriyq (Usiku wa tarehe 11, 12, na 13).

 

 

Masiku Ya Tashriyq Na Kutupia Jamaraat Tatu Siku Za Tarehe Kumi Na Moja Na Kumi na Mbili

 

41- Kisha atatupia Jamaraat tatu tarehe kumi na moja – baada ya Adhuhuri hata mpaka usiku - kila nguzo ataitupia vijiwe saba huku akipiga Takbiyr kwa kila kijiwe. Ataanzia Jamarat ndogo, kisha ya katikati. Atasogea mbele baada ya kila Jamarah, ataelekea Qiblah na aombe du’aa ndefu – ikiwa itakuwa wepesi - kisha ataliendea Jamarah la Aqabah atalitupia vijiwe saba, na hatosimama kuomba du’aa baada yake. Kijiwe ambacho hakitagonga Jamarah au kuingia shimoni, basi hakihesabiwi.

 

42- Kisha tarehe kumi na mbili atafanya vile vile alivyofanya siku iliyopita ya tarehe kumi na moja.

 

Akimaliza kutupia vijiwe – tarehe kumi na mbili - akitaka ataharakisha kuondoka, na atashuka toka Minaa, na akitaka atachelewesha kuondoka na atalala Minaa usiku wa tarehe kumi na tatu, na kuchelewesha ni bora zaidi.

 

Kutupia Tarehe Kumi Na Tatu (Siku Ya Mwisho Ya Tashriyq)

 

43- Akiamua kulala usiku wa tarehe kumi na tatu, au jua likazama siku ya tarehe kumi na mbili na yeye bado yuko Minaa, basi ni lazima alale Minaa ili kutupia vijiwe Jamaraat tatu tarehe kumi na tatu kama alivyofanya siku mbili zilizotangulia baada ya Adhuhuri.

 

Twawaaf Ya Kuaga Kabla Ya Safari

 

44- Mwenye kuhiji akitaka kusafiri kurudi nchini kwake, asitoke mpaka atufu Twawaaf ya kuaga. Ataifanya ni ahadi yake ya mwisho na Makkah. Ama mwenye hedhi na nifasi, hao wanaruhusiwa wasifanye Twawaaf ya kuaga.

 

45- Imestahabiwa kwa Hujaji azuru Al-Masjid An-Nabawiy huko Al-Madiynah, na kuuzuru si katika ‘amali za Hajj kama wanavyodhani watu wengi.

 

46- Halafu atarejea nchini kwake. Akifika, atawachinjia watu wake, mafukara na masikini ng’ombe au ngamia kama itakuwa wepesi. Kama hakuweza hilo, basi si lazima. Allaah Ta’aalaa Ndiye Ajuaye Zaidi.

 

 

 

Share