12-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Hajj Na 'Umrah: Sunnah Za Kuhirimia

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Hajj Na ‘Umrah

 

12-Sunnah Za Kuhirimia

 

Alhidaaya.com

 

 

 

1- Kuoga kabla ya kuhirimia

 

Ni kwa Hadiyth ya Zayd bin Thaabit kwamba ((Yeye alimwona Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amevua nguo kwa ajili ya kuhirimia na akaoga)). [Hadiyth Hasan. Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (831)]

 

Mwanamke ataoga hata kama ana hedhi au nifasi. Katika Hadiyth ya Jaabir: ((Mpaka tukafika Dhul Hulayfah, na Asmaa bint ‘Umays akamzaa Muhammad bin Abiy Bakr. Akatuma mtu kwenda kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amuulizie nini afanye? Akasema (Rasuli):

((اغتسلي واستثفري بثوب وأحرمي))

((Oga, na funga vizuri kwa kitambaa sehemu ya damu [utupu], kisha hirimia)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim]

 

2- Kujitia manukato mwilini kabla ya kuhirimia

 

Ni kwa Hadiyth ya ‘Aaishah aliyesema: ((Nilikuwa nikimtia manukato Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kwa ajili ya kuhirimia kwake wakati anapohirimia, na kwa ajili ya kuvua kwake Ihraam  kabla hajatufu Nyumba)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1539) na Muslim (1189)]

 

Kadhalika, mwanamke hujitia manukato. Ni kwa Hadiyth ya ‘Aaishah aliyesema: ((Tulikuwa tunatoka pamoja na Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) hadi Makkah, kisha tunavipaka vipaji vyetu vya uso kwa uturi wenye harufu nzuri wakati wa kuhirimia. Na mmoja wetu anapotokwa jasho ulikuwa unavuja juu ya uso wake na Rasuli anauona, na wala hatukatazi)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (1839) na Al-Bayhaqiy (5/48)]

 

Ninasema: “Ama baada ya kuhirimia, haitojuzu kutumia manukato yoyote kwa Ijma’a ya ‘Ulamaa kama alivyonukulu An-Nawawiy katika Al-Majmuw’u (7/270)”.

 

3- Mwanaume ahirimie kwa vipande viwili vyeupe vya nguo cha chini na cha juu (izari na ridaa)

 

Toka kwa Ibn ‘Abbaas amesema: ((Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliondoka Madiynah baada ya kuzichana vizuri nywele zake na kujitia mafuta, na akavaa kipande chake cha chini cha nguo (izaar) na cha juu (ridaa) yeye pamoja na Swahaba wake)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1545)]

 

Na toka kwa Ibn ‘Abbaas kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

((البسوا من ثيابكم البياض، فإنها من خير ثيابكم، وكفنوا بها موتاكم))

((Vaeni katika nguo zenu nyeupe, kwani hizo ni katika nguo zenu bora zaidi, na wakafinieni kwazo maiti zenu)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (999) na Abu Daawuwd (3860)]

 

Ama mwanamke, yeye atavaa nguo yoyote aipendayo, lakini hatovaa niqabu wala glovu kama itakavyokuja mbeleni katika mambo yaliyokatazwa. Nguo yake haihusishwi na rangi maalum kama nyeupe na kadhalika kama wanavyoitakidi akina mama wengi na hususan Wamisri. ((‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa) alikuwa anavaa nguo ya rangi nyekundu, akiwa amehirimia)). [Isnaad yake ni Swahiyh. Ibn Hajar katika Al-Fat-h (3/405) ameiegemeza kwa Sa’iyd bin Mansuwr na akasema: “Isnaad yake ni Swahiyh”]

 

4- Kuswali katika Bonde la Al-‘Aqiyq kwa mwenye kupita hapo

 

Hili ni bonde lililo karibu na Al-Baqiy’u, na kuna umbali wa maili nne kati yake na Madiynah. [Fat-hul Baariy (3/359)]

 

‘Umar amesema: ((Nimemsikia Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akisema wakati yuko Bonde la Al-‘Aqiyq:

 

((أتاني الليلة آت من ربي، فقال: صل في هذا الوادي المبارك وقل: عمرة في حجة))

((Alinijia usiku mwenye kunijia [Jibriyl] toka kwa Mola wangu akasema: Swali katika bonde hili [la Al-‘Aqiyq] lililobarikiwa na sema: ‘Umrah ndani ya Hajj)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1534) na wengineo. Tumeitaja nyuma]

 

 

5- Kuswali katika Msikiti wa Dhul Hulayfah kwa mwenye kupita hapo

 

Ni kwa Hadiyth ya Ibn ‘Umar aliyesema: ((Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa anaswali rakaa mbili hapo Dhul Hulayfah)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1184)]

 

Na Hadiyth ya Jaabir inasema: ((Alipofika Dhul-Hulayfah aliswali, kisha aliendelea kubaki kimya mpaka akafika Al-Baydaa)). [Hadiyth Hasan. Imekharijiwa na An-Nasaaiy (2756)]

 

Angalizo:

 

Jumhuri wamechukulia toka Hadiyth ya Ibn ‘Umar kuwa ni mustahabu kuswali rakaa mbili kwa ajili ya kuhirimia. An-Nawawiy amesema katika kuisherehesha: “Katika yanayopatiwa faida ndani yake ni kuwa imestahabiwa kuswali rakaa mbili wakati mtu anapotaka kuhirimia, na ataziswali kabla ya kuhirimia, na zitakuwa ni Sunnah. Haya ndiyo madhehebu yetu na madhehebu ya ‘Ulamaa wote isipokuwa yale aliyoyasimulia Al-Qaadhwiy na wengineo toka kwa Al-Hasan Al-Baswriy kuwa imestahabiwa iwe baada ya Swalaah ya Faradhi. Amesema: “Kwa kuwa yeye amesimulia kwamba rakaa hizi mbili zilikuwa ni Swalaat As-Subhi. Lakini la sawa ni kauli ya Jumhuri, navyo ndivyo Hadiyth inavyoonyesha”.

 

Ninasema: “Bali Hadiyth inavyoonyesha ni kwamba Swalaah imestahabiwa kwa ajili ya Masjid na si kwa ajili ya kuhirimia. Haya yanatiliwa nguvu na Hadiyth ya Ibn As-Samatw: ((Kwamba yeye alitoka pamoja na ‘Umar hadi Dhul-Hulayfah. Akaswali rakaa mbili, nami nikamuuliza kuhusu hilo akasema: Hakika mimi nafanya kama nilivyomwona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam)). [Hadiyth Hasan. Imekharijiwa na Ahmad]

 

Hapa kuhirimia hakukutajwa, bali faida zinazoweza kupatikana kutokana na Hadiyth hiyo ni yale yanayokuja baada yake:

 

6- Kutia niya ya kuhirimia baada ya Swalaah ya Faradhi au ya Sunnah

 

Lililo bora ni kuhirimia baada ya mtu kuswali Swalaah ya Faradhi au ya Sunnah kutokana na Hadiyth zilizotangulia. Hili linatiliwa nguvu pia na Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas: ((Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliswali Adhuhuri Dhul-Hulayfah kisha akaitisha ngamia. Alipokaa juu yake na kutulia naye sawa juu ya mwinuko wa Al-Baydaa alihirimia Hajj)). [Hadiyth Hasan. Imekharijiwa na Ad-Daaramiy (1912), Abu Daawuwd (1752) na Ahmad (2982)]

 

Ninasema: “Linaloonekana ni kuwa Swalaah aliyoiswali Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kabla hajahirimia ilikuwa ni Swalaah ya Adhuhuri. Inajulikana kwamba Nabiy alikuwa akipunguza Swalaah hapo Dhul-Hulayfah –kama tulivyoeleza katika Swalaah ya Msafiri- hivyo aliswali rakaa mbili”.

 

Tumeshaitaja Hadiyth ya Rasuli isemayo:

 

((أتاني آت من ربي، فقال: صل في هذا الوادي المبارك وقل: عمرة في حجة))

((Alinijia mwenye kunijia [Jibriyl] toka kwa Mola wangu akasema: Swali katika bonde hili [la Al-‘Aqiyq] lililobarikiwa na sema: ‘Umrah ndani ya Hajj((. [Hadiyth Swahiyh. Imetajwa nyuma]

 

Na Swalaah hii aliyoamuriwa inawezekana ikawa ya Faradhi au ya Sunnah. Na kwa ajili hiyo, Sheikh wa Uislamu Ibn Taymiyah amesema: “Kama anaswali Faradhi, atahirimia baada yake, na kama haswali basi kuhirimia hakuna Swalaah yake maalumu, na hili ndilo lenye nguvu”. [Majmuw’u Al-Fataawaa (26/108) na mfano wake katika Al-Muhallaa cha Ibn Hazm (7/90)]

 

7- Kuleta tahmiyd, tasbiyh na takbiyr –juu ya mnyama- kabla ya kuhirimia

 

Ni kwa yaliyomo kwenye Hadiyth ya Anas: ((…kisha akapanda mpaka ngamia akatulia naye sawa juu ya mwinuko wa Al-Baydaa, hapo alimhimidi Allaah, akasabbih na akakabbir, kisha akahirimia Hajj na ‘Umrah)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy na Abu Daawuwd (1779)].

 

8- Kuelekea Qiblah wakati wa kuhirimia

 

Toka kwa Naafi’i amesema: ((Ibn ‘Umar alipokuwa anaswali asubuhi Dhul-Hulayfah, alikuwa anaagiza aletewe mnyama wake kisha humpanda. Anapotulia naye sawa, huelekea Qiblah na kuleta Talbiyah, na husema kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa sallam) alifanya hivyo)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1553)]

 

9- Kunyanyua sauti wakati wa kuitikia Talbiyah

 

Ni kwa Hadiyth ya As-Saaib bin Khallaad aliyesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

((جاءني جبريل فقال: يا محمد، مر أصحابك أن يرفعوا أصواتهم بالتلبية))

((Jibriyl alinijia na kuniambia: Ee Muhammad! Waamuru Swahaba wako wanyanyue sauti zao kuitikia Talbiyah)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (830), Abu Daawwd (1197), An-Nasaaiy (5/162) na Ibn Maajah (2922)]

 

Jumhuri wanasema agizo hili ni la Sunnah, na Adh-Dhwaahiriyyah wanasema ni la Wajibu. [Haashiyat As-Sanadiy (5/162)]

 

Toka kwa Jaabir na Abu Sa’iyd wamesema: ((Tulikuja pamoja na Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) na sisi tunapaza sauti ya nguvu kuitikia Talbiyah)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1148)]

 

Je, mwanamke atanyanyua sauti yake kuitikia Talbiyah?

 

‘Ulamaa wote kwa sauti moja wanasema kuwa mwanamke hafanyiwi Talbiyah na mwingine kwa niaba, bali ni lazima ailete yeye mwenyewe. [At-Tirmidhiy ameyanukulu haya katika Al-Jaami’u (849). Ama Hadiyth ya Jaaabir isemayo: ((Tulikuwa tunaleta Talbiyah kwa niaba ya wanawake, na tunatupia viguzo kwa niaba ya watoto)) Hadiyth hii ni Dhwa’iyf, haifai]

 

Lakini je, mwanamke atanyanyua sauti yake kuleta Talbiyah?

 

Wengi wamesema hatonyanyua sauti yake kwa Talbiyah. [Hata Ibn ‘Abdul Barri amenukuu Ijma’a juu ya hili. Lakini hili limetenguliwa na kauli ya ‘Aaishah na wengineo kama tutakavyo kuja kuona]

 

Wametoa hoja kwa haya yafuatayo:

 

1- Mwanamke ameamuriwa kujisitiri, hivyo ni makruhu kwake kunyanyua sauti kuhofia watu kufitinika naye.

 

2- Ni kauli yake Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam):

 

((التسبيح للرجال والتصفيق للنساء))

((Tasbiyh ni kwa wanaume na kupiga vikofi kwa wanawake)). [Hadiyth Swahiyh. Imetajwa katika mlango wa Swalaah]

 

Hivyo basi, Hadiyth inadulisha kuwa hatonyanyua sauti yake kwa kuleta Talbiyah kwa kulinganisha na hali yake katika Swalaah.

 

3- Yanayosimuliwa toka kwa Ibn ‘Umar kuwa amesema: ((Mwanamke hapandi juu ya Swafaa na Marwah, na hanyanyui sauti yake katika kuleta Talbiyah)). Hadiyth hii ni Dhwa’iyf. [Imekharijiwa na Al-Bayhaqiy katika Sunan zake (5/46)]

Lakini wengineo wakiongozwa na ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa) wanasema mwanamke hunyanyua sauti yake kwa dalili zifuatazo:

 

1- Kwa ujumuishi wa kauli ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam):

 

((جاءني جبريل فقال: يا محمد، مر أصحابك أن يرفعوا أصواتهم بالتلبية))

((Jibriyl alinijia na kuniambia: Ee Muhammad! Waamuru Swahaba wako wanyanyue sauti zao kuitikia Talbiyah)). [Hadiyth Swahiyh. Imetajwa nyuma kidogo]

 

Na hilo limejumuishwa kwa wote wanawake na wanaume, na ndilo alilolifahamu ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa).

 

2- Toka kwa ‘Abdur Rahmaan bin Al-Qaasim toka kwa baba yake amesema: ((Mu’aawiyah alitoka usiku wa An-Nafar [tarehe 12], akasikia sauti ya Talbiyah na kuuliza: Nani huyu? Wakamjibu: Ni ‘Aaishah, amenuwia ‘Umrah toka At-Tan-’iym. ‘Aaishah akaelezwa hilo naye akasema: Lau angeniuliza ningemweleza)). [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na Ibn Abiy Shaybah katika Al-Muswannaf (1/4/389)]

 

Ibn Hazm amesema kwenye Al-Muhallaa (7/93): “Watu walikuwa wakiyasikia maneno ya Wamama wa Waumini na hakukuwa na ukakasi wowote kwa hilo. Watu wamesimulia kutoka kwao na wao wakiwa katika umri wa miaka 20 na zaidi ya hapo, na hakuna yeyote aliyekhalifu kujuzu hilo na kustahabiwa kwake”.  

 

Kisha akaandika athar zinazogusia hilo.

 

Ninasema: “Kauli nyoofu zaidi kuhusu hili ni ya Sheikh wa Uislamu Ibn Taymiyah (26/115) isemayo: “Na mwanamke atanyanyua sauti yake kiasi cha kusikia swahiba wake pembeni”.

 

Mwenye Hedhi Na Mwenye Nifasi Huhirimia Na Huleta Talbiyah

 

Tumeshaeleza nyuma kuwa mwenye hedhi na mwenye nifasi hawazuiliwi kuhirimia Hajj, na kuwa imesuniwa kwao kuoga. Aidha, wawili hao hunuwia Hajj baada ya kuoga. Toka kwa ‘Aaishah amesema: ((Asmaa bint ‘Umays alipata nifasi kwa kumzaa Muhammad bin Abiy Bakr huko Ash-Shajarah, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akamwamuru aoge na atie niya)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1209), Abu Daawuwd (1744) na Ibn Maajah (2911)]

 

Na Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alimwambia ‘Aaishah -alipopata hedhi-:

 

((افعلي ما يفعل الحاج غير أن لا تطوفي بالبيت))

((Fanya (yote) ayafanyayo mwenye kuhiji isipokuwa tu usitufu Nyumba)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (294) na Muslim (1211)]

 

Ash-Shaafi’iy amesema katika Al-Ummu (2/134): Pamoja na Talbiyah katika ayafanyayo Hujaji.

 

 

 

Share