11-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Hajj Na 'Umrah: Nguzo Za Hajj: Nguzo Ya Kwanza Ya Hajj: Kuhirimia (Al-Ihraam)

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Hajj Na ‘Umrah

 

11-Nguzo Za Hajj:

Nguzo Ya Kwanza Ya Hajj: Kuhirimia (Al-Ihraam)

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Matendo yaliyotangulia yanagawanyika katika nguzo, yaliyo wajibu (waajibaat) na yaliyosuniwa (mustahabbaat).

 

Nguzo za Hajj kwa mujibu wa Jumhuri ya ‘Ulamaa ni nne: Kuhirimia, Kusimama ‘Arafah, Twawaaf ya Ifaadhwah na Kusai kati ya Swafaa na Marwah. [Kwa Ash-Shaafi’iy nguzo hizi ni sita. Ni hizi nne pamoja na kunyoa au kupunguza, na kupangilia kati ya nguzo. Ama kwa Hanafiy ni nguzo mbili: Kusimama ‘Arafah na Twawaaf ya Ifaadhwah]

 

Nguzo Ya Kwanza Ya Hajj: Kuhirimia (Al-Ihraam)

 

Kuhirimia ni kutia niya ya Hajj au ‘Umrah toka kwenye Miyqaat inayotambulika kisharia. Ni nguzo kati ya nguzo za Hajj kwa mujibu wa Jumhuri ya ‘Ulamaa, na ni sharti ya kuswihi Hajj kwa Mahanafiy. Allaah Ta’aalaa Amesema:

((وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ))

((Na hawakuamrishwa isipokuwa wamwabudu Allaah wenye kumtakasia Dini, wenye kujiengua na upotofu kuelemea Dini ya haki)). [Al-Bayyinah (98:5)]

 

Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

((إنما الأعمال بالنيات))

((Hakika si jinginelo, ‘amali ni kwa niya)). [Hadiyth Swahiyh. Imetajwa mara nyingi nyuma)).

 

 

Aina Za Ihraam (Kuhirimia)

 

Hajj hufanywa kwa miundo mitatu:

 

1- Ifraad: Ni Hujaji kunuwia Hajj tu wakati anapohirimia kwa kusema:

 

 لبيك اللهم بحج

kisha atafanya ‘amali za Hajj tu.

 

2-  Qiraan: Ni Hujaji kunuwia Hajj na ‘Umrah kwa pamoja kwa kusema:

لبيك حجا وعمرة

na atazifanya zote mbili hizo (Hajj na ‘Umrah) katika ‘amali (nusuk) moja, au aingize Hajj ndani ya ‘Umrah kabla ya Twawaaf.

 

Jumhuri wamesema: Viwili vinaingiliana. Atatufu Twawaaf moja na atasai Sai moja, na hilo litamtosheleza kwa Hajj na ‘Umrah.

 

‘Ulamaa wa Kihanafiy wanasema atatufu Twawaaf mbili na atasai Sai mbili, na mwenye kufanya Qiraan ni lazima achinje mnyama kwa Ijma’a ya ‘Ulamaa kama itakavyokuja mbeleni.

 

3- Tamattu’u: Ni kunuwia mwenye kuhji ‘Umrah tu katika miezi ya Hajj kwa kusema:

 

 لبيك عمرة

na atakwenda Makkah, atafanya ‘amali za ‘Umrah na atajivua Ihraam. Atakaa Makkah akiwa hana Ihraam, kisha atahirimia Hajj na atafanya Manaasiki za Hajj, na hiyo ni katika mwaka huo huo.

 

Mwenye kufanya Tamattu’u ni lazima pia achinje mnyama kwa Ijma’a ya ‘Ulamaa.

 

Dalili za uhalali wa ‘amali hizi tatu

 

1-  Hakuna khilafu yoyote kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alipoanza Hajj, Hajj ilikuwa inajuzu kwa aina zake hizi tatu tulizozitaja. Na ndivyo hivi hivi walivyofanya Swahaba zake ambao wako waliofanya Tamattu’u, waliofanya Qiraan, na waliofanya Ifraad. Kwa kuwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliwachaguza katika hilo kama ilivyokuja katika Hadiyth ya ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa) anayesema: Tulitoka pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akasema:

 

((من أراد منكم أن يهل بحج وعمرة فليفعل، ومن أراد أن يهل بحج فليهل، ومن أراد أن يهل بعمرة فليهل..))

((Anayetaka miongoni mwenu kunuwia Hajj na ‘Umrah, basi afanye, na anayetaka kunuwia Hajj, basi anuwie, na anayetaka kunuwia ‘Umrah, basi anuwie…)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1211)]

 

2- Kisha Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliwahamisha – baada ya chaguzi hizi - kwenda kwenye Tamattu’u bila kuwakazia hilo [kuwashadidia]. ‘Aaishah anasema:..Tukateremka Sarif [Sehemu karibu na At-Tan-’iym], akawatokea Swahaba wake akasema:

((من لم يكن منكم أهدى، فأحب أن يجعلها عمرة فليفعل، ومن كان معه هدي فلا))

((Ambaye miongoni mwenu hakuja na mnyama wa kudhwahi na akataka kuifanya ‘Umrah, basi afanye, na yule mwenye mnyama asifanye)). Akasema (‘Aaishah): “Basi kuna waliolitekeleza hilo na kuna walioliacha katika Swahaba Wake [ambao hawakuwa na wanyama]”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1560) na Muslim (1211), na ziada ni yake]

 

Na katika Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alipowasili Dhiy Tuwaa – sehemu karibu na Makkah - na akalala hapo, alipopambaukiwa asubuhi aliwaambia:

((من شاء أن يجعلها عمرة فليجعلها عمرة))

((Anayetaka kuifanya [Hajj yake] ‘Umrah basi aifanye ‘Umrah)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1564) na Muslim (1240)]

 

3- Kisha akawaamuru – kwa ambaye hakuswaga mnyama kati yao - waivunje Hajj na kuifanya ‘Umrah na wavue Ihraam. Toka kwa ‘Aaishah amesema: Tulitoka pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) na hatuoni [ndani ya akili zetu] isipokuwa tunahiji tu. Tulipofika Makkah, tulitufu Nyumba. Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akamwamuru kila ambaye hajaswaga mnyama avue Ihraam. Akasema: Akavua Ihraam kila ambaye hakuswaga mnyama, na wakeze hawakuswaga mnyama, wakavua Ihraam…. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1561) na Muslim (1211)]

 

Na katika riwaya ya Ibn ‘Abbaas: …Akawaamuru waifanye (Hajj) ‘Umrah. Hilo likawapa ukakasi mkubwa sana, wakasema: Ee Rasuli wa Allaah, ni vuo lipi la Ihraam [Tahallul ipi? Ya kuruhusiwa baadhi ya yaliyokatazwa tu]? Akasema: ((Vuo la yote [Tahallul ya kuruhusiwa kufanya marufuku zote])). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1564) na Muslim (1240)]

 

Ninasema: “Kwa ajili ya awamu hizi tatu zilizotangulia, ‘Ulamaa wamekhitalifiana kuhusiana na usharia wa ‘amali hizi tatu:

 

Jumhuri ya Salaf na Makhalaf wanasema kuwa ‘amali hizi tatu; Ifraad, Qiraan na Tamattu’u, zote zinajuzu, na kwamba uwanja ni mpana, hata baadhi yao wamenukulu Ijma’a kuhusu hilo. [Angalia Al-Majmuw’u (7/144), Al-Mughniy (3/276), na Ma’aalimu As-Sunan cha Al-Khattwaabiy (2/301). An-Nawawiy amesema baada ya kueleza khilafu za baadhi ya Swahaba katika suala hili katika Sharhu Muslim: “Ijma’a imepatikana baada ya hili juu ya kujuzu Ifraad, Tamattu’u na Qiraan bila ya ukaraha” ]

 

Kisha wakakhitalifiana hawa – baada ya kukubaliana juu ya uhalali na usharia wake -  ni ipi ‘amali bora zaidi kati ya hizi tatu? Hili litakuja kugusiwa mbeleni.

 

Lakini baadhi ya ‘Ulamaa wengine wanaona kuwa ni waajib kufanya Tamattu’u kwa ambaye hakuswaga mnyama, na kwamba akitufu na akasai, basi atavua Ihraam kwa lazima. Na haya ni madhehebu ya Ibn ‘Abbaas na Abu Muwsaa Al-Ash-‘Ariy. Pia ni kauli ya Ahlu Adh-Dhwaahir, na imeungwa mkono na Ibn Hazm, kisha Ibn Al-Qayyim kwa tafiti mbili muhimu. [Rejea Al-Muhallaa (7/99 na zinazofuatia) na Zaad Al-Ma’aadiy (2/77) na zinazofuatia]

 

Wamelitolea dalili hilo kwa amri aliyoitoa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kwa Swahaba zake ya kuvunja Hajj kwenda kwenye ‘Umrah na kulifanya hilo ni waajib wa lazima kwao. Hilo lilikuwa na ukakasi mkubwa kwao, jambo linaloonyesha kuwa walifahamu kuwa amri hiyo ni ya waajib, na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akakasirika walipojivuta vuta na kumuuliza tena kama inavyoeleza Hadiyth ya ‘Aaishah: ‘Aliyy akaingia naye amekasirika mno. Nikasema: Nani amekukasirisha ee Rasuli wa Allaah, Allaah Amwingize motoni?. Akasema:

((أو ما شعرت أني أمرت الناس بأمر فإذا  هم يترددون..))

((Hivi hujui kwamba nimewaamuru watu amri, na ghafla wao wanasitasita..)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1210) na Ahmad (6/175)]

 

Wametolea dalili pia kwa kauli yake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalhii wa sallam) walipomuuliza kuhusu agizo la kuvunja Hajj alilowapa: “Je ni kwa mwaka wetu huu tu au milele abadan?” Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi akaingiza vidole vyake ndani ya vingine akasema:

((دخلت العمرة في الحج إلى يوم القيامة، لا بل لأبد أبد، لا بل لأبد أبد))

((‘Umrah imeingia ndani ya Hajj hadi Siku ya Qiyaamah, hapana bali milele na milele, hapana bali milele na milele)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1218)]

 

Ibn ‘Abbaas alikuwa akijadiliana na watu kitaaluma suala hili mpaka kufikia kusema: Ninawaambieni: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema, na nyinyi mnasema: Amesema Abu Bakr na ‘Umar. Mawe yamekurubia kuwashukieni toka mbinguni.. [Musnad Ahmad (1/337)/ Al-Faqiyhu Al-Mutafaqqih (1/145), na Jaami’u Bayaan Al-‘Ilm (2/239)]

 

Kwa kuwa Abu Bakr na ‘Umar walikuwa wanaona kuwa Ifraad ni bora zaidi kuliko Tamattu’u kama tutakavyozungumzia hili mbeleni.

 

Na kiini cha dhana ya madhehebu haya ni kuwa, anayetaka kuhiji na akafika Miyqaat, kama hana mnyama wa kuchinja, basi ni waajib kwake ahirimie ‘Umrah pekee na hapana budi [yaani awe mwenye kufanya Tamattu’u]. Na kama atahirimia Hajj, au Qiraan ya Hajj na ‘Umrah, ni wajibu kwake avunje Ihraam yake kuwa ‘Umrah na avue Ihraam anapoimaliza, kisha aanze kunuwia Hajj kwa Ifraad toka Makkah.

 

Na kama amemswaga mnyama, basi atafanya Qiraan akinuwia:

((لبيك بعمرة وحج معا))

[Angalia Al-Muhallaa (7/99)]

 

Ni Ipi Bora Zaidi Kati Ya ‘Amali Hizi Tatu?

 

Na kwa msingi wa kujuzisha Jumhuri  ‘amali hizi tatu, wamekhitalifiana kwa kauli mbalimbali kuhusu ni ipi iliyo bora zaidi. Na sababu ya kukhitilafiana huku, ni mvutano kuhusu Hajj ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam): Je, alifanya Ifraad, au Qiraan, au Tamattu’u?

 

[1] Kauli ya kwanza: Ifraad ni bora zaidi 

 

Ni madhehebu ya Maalik, Dhwaahir na Ash-Shaafi’iy, nayo imesimuliwa toka kwa ‘Umar, ‘Uthmaan, Ibn ‘Umar, Jaabir na ‘Aaishah.   [Al-Mudawwanah (1/360), Al-Ummu (2/143) na Al-Majmuw’u (7/145 na zinazofuatia)]

 

Hoja zao ni:

 

1- Yaliyothibiti toka kwa Jaabir, Ibn ‘Umar, Ibn ‘Abbaas na ‘Aaishah kuwa: ((Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alinuwia Hajj. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1562) na Muslim (1211) toka kwa ‘Aaishah]

 

Na katika riwaya: “Alinuwia Hajj kwa Ifraad.”

 

2- Makhalifa Waongofu (Radhwiya Allaah ‘anhum) walifanya Ifraad ya Hajj baada ya Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) na wakaendelea kufanya hivyo. Na ndivyo alivyofanya Abu Bakr, ‘Umar na ‘Uthmaan. Wamekhitalifiana alivyofanya ‘Aliyy.

 

3- Kwamba ‘Umar amesema: Ipambanueni Hajj yenu na ‘Umrah yenu, kwani hiyo ni ukamilifu zaidi wa Hajj yenu na ukamilifu zaidi wa ‘Umrah yenu. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1217), na Maalik (778)]

 

4- ‘Uthmaan (Radhwiya Allaah ‘anhu) alipotajiwa Tamattu’u ya ‘Umrah kisha Hajj alisema: ((Tamattu’u ni utimilisho zaidi kwa Hajj na ‘Umrah, visifanyike viwili katika mwezi wa Hajj [‘Umrah ifanyike peke yake nje ya mwezi wa Hajj]. Na lau mtaichelewesha ‘Umrah hii ili muizuru Nyumba hii mara mbili, basi ingekuwa bora zaidi, kwani Allaah Ta’alaa Ametanua wigo katika kheri)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Ahmad (1/92) na Ibn Jariyj (2/207) kwa Sanad Swahiyh]

 

5- Ni kwamba Ifraad haipasi ndani yake kuchinja kwa Ijma’a ya ‘Ulamaa na hiyo ni kutokana na kukamilika kwake kinyume na Tamattu’u na Qiraan.

 

6- Ni kwamba umma wote umekubaliana – hivi ndivyo walivyosema wao - kuwa inajuzu Ifraad bila ya umakuruhu kinyume na Tamattu’u na Qiraan, hivyo Ifraad imekuwa ni bora zaidi.

 

 [2] Kauli ya pili: Qiraan ni bora zaidi

 

Haya ni madhehebu ya Hanafiy na Ath-Thawriy, na riwaya toka kwa Ahmad –kwa aliyeswaga mnyama -, na hoja zao ni:

 

1- Imethibiti kuwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa sallam) alinuwia Hajj na ‘Umrah. Kama Hadiyth ya Anas aliposema: Nimemsikia Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akisema:

لبّيك عمرةً وحجّاً

 

[Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (4354) na Muslim (1222).

 

2- Ni neno la ‘Aliyy bin Abiy Twaalib kumwambia ‘Uthmaan wakati alipokataza Qiraan: Hutaki jingine lolote isipokuwa kukataza jambo ambalo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alilifanya? ‘Uthmaan akamwambia: Tuache sisi na jambo letu. Akasema: Hakika mimi siwezi kukuacha. ‘Aliy alipoona mambo hivyo, alinuwia yote mawili. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1569) na Muslim (1222)]

 

3- Mwenye kufanya Qiraan ni lazima achinje, na chinjo hilo si la kufidia au kuunga kosa, bali ni chinjo la ‘ibaadah, na ‘ibaadah inayofungamana na kiwiliwili na mali ni bora zaidi kuliko inayohusiana na kiwiliwili tu.

 

4- Mwenye kufanya Qiraan anachakarikia ‘ibaadah, na hilo ni bora zaidi kuliko kuichelewesha.

 

5- Qiraan inawezesha kufanyika ‘Umrah katika wakati wa Hajj, na hilo ni utukuko zaidi.

 

 

[3] Kauli ya tatu: Tamattu’u ni bora zaidi

 

Ni madhehebu ya Ahmad bin Hanbal, Ahlu Adh-Dhwaahir na Ibn Al-Qayyim, na moja kati ya kauli mbili za Ash-Shaafi’iy. Imesimuliwa toka kwa Ibn ‘Umar, Ibn ‘Abbaas, Ibn Az-Zubayr, ‘Aaishah na kundi la Salaf [Al-Mughniy (3/260), Al-Majmuw’u (7/150-152), Al-Muhallaa (7/99) na Zaad Al-Ma’aadiy (2/177)]

 

 

Hoja zao ni:

 

1- Hadiyth ya ‘Aaishah: ((Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alifanya Tamattu’u kwa (kuanza) ‘Umrah kisha (kumalizia) Hajj, na watu wakafanya Tamattu’u pamoja naye.

 

Az-Zuhriy amesema: Ni kama vile alivyonielezea Saalim toka kwa Ibn ‘Umar toka kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam).   [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1692) na Muslim (1237). Inavyoonekana ni kuwa Tamattu’u inayokusudiwa kwayo hapa ni Qiraan kama alivyosema Sheikh wa Uislamu]

 

2- Toka kwa ‘Imraan bin Huswayn amesema: Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alifanya Tamattu’u, nasi tukafanya Tamattu’u pamoja naye. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy kwa maana yake (1572) na Muslim (1226) na tamko ni lake].

 

3- Toka kwa Abu Jamrah amesema: Nilifanya Tamattu’u na watu wakanikataza nisifanye hilo. Nikamuuliza Ibn ‘Abbaas, naye akaniamuru kufanya. Nikaona usingizini kana kwamba mtu ananiambia: Hajj Mabruwr na ‘Umrah Mutaqabbalah. Nikamweleza Ibn ‘Abbaas naye akasema: “Sunnah ya Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam.). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1567) na Muslim (1243)]

 

4- Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliwaamuru Swahaba wake  wakati walipotufu Nyumba wavue Ihraam, na waifanye ‘Umrah – kama ilivyotangulia -. Akawahamisha toka kwenye Ifraad na Qiraan na kuwapeleka kwenye Tamattu’u, na yeye hakuwahamisha isipokuwa kwenye zuri zaidi.

 

5- Hadiyth ya Jaabir aliyesema: Tulihiji pamoja na Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) siku alipomswaga ngamia pamoja naye. Watu walishatia niya ya Hajj kwa Ifraad. Akawaambia:

 

((حلوا من إحرامكم بطواف البيت، وبين الصفا والمروة، ثم أقيموا حلالا حتى إذا كان يوم التروية فأهلوا بالحج، واجعلوا التي قدمتم بها متعة)). قالوا: كيف نجعلها متعة وقد سمينا الحج؟ قال: ((افعلوا ما أمرتكم به، فلولا أني سقت الهدي لفعلت مثل الذي أمرتكم به))

((Vueni Ihraam baada ya Kutufu Nyumba, na [baada ya Kusai] baina ya Swafaa na Marwah, kisha kaeni bila Ihraam mpaka inapofika Siku ya Tarwiyah nuwieni Hajj, na yafanyeni mliyoyatenda kabla kuwa ni Mut-‘ah (Qiraan))). Wakasema: Vipi tutayafanya Mut-‘ah na sisi tumeiita Hajj?”Akasema: ((Fanyeni niliyokuamrisheni, na lau si mimi kumswaga mnyama, ningefanya mfano wa niliyokuamrisheni)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1568) na Muslim (1216)]

 

5- Tamattu’u imetajwa kiuainisho katika Kitabu cha Allaah Ta’aalaa:

((فَمَن تَمَتَّعَ بِالْعُمْرَةِ إِلَى الْحَجِّ فَمَا اسْتَيْسَرَ مِنَ الْهَدْيِ))

((basi mwenye kufanya Tamattu’u kwa kutekeleza ‘Umrah kwanza kisha Hajj, achinje mnyama aliye mwepesi)). [Al-Baqarah (2:196)]

 

Lakini ‘amali zingine mbili hazikutajwa.

 

7- Mwenye kufanya Tamattu’u, zinamkusanyikia kwa pamoja Hajj na ‘Umrah katika miezi ya Hajj zikiwa kamili na zikiwa nyepesi.

 

8- Kauli yake (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) hutangulizwa kabla ya kitendo chake kukitokea ukinzani.

 

[4] Kauli ya nne: Uchanganuzi

 

Ni chaguo la Sheikh wa Uislamu Ibn Taymiyah (Rahimahu-Allaah) na muhtasari wa maneno yake: [Majmuw’u Al-Fataawaa (26/85-91)]

 

(a) Ikiwa atafanya Ifraad ya Hajj peke yake kwa safari moja, na ‘Umrah kwa safari nyingine, basi inakuwa ni bora zaidi kuliko kufanya Qiraan na Tamattu’u katika safari moja mahususi, na hii inakuwa kama alifanya ‘Umrah kabla ya miezi ya Hajj. Na hii ndio Ifraad aliyoifanya Abu Bakr na ‘Umar, na alikuwa anawachagulizia watu kuifanya, na pia ‘Aliyy.

 

(b) Ama akitaka kukusanya ‘amali mbili (Hajj na ‘Umrah) kwa safari moja, na akafika Makkah katika miezi ya Hajj ilhali hakuswaga mnyama, basi Tamattu’u ni bora zaidi kwake.

 

(c) Na akitaka kukusanya ‘amali mbili kwa safari moja na akaswaga mnyama, basi Qiraan ni bora zaidi kwa kufuata alivyofanya Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) ambapo alifanya Qiraan na akaswaga mnyama.

 

Kisha ni lipi bora kati ya viwili: Aswage mnyama na afanye Qiraan, au afanye Tamattu’u bila kuswaga mnyama na avue Ihraam?

 

Amesema: “Hapa ni mahala pa ijtihaad kutokana na kukinzana Alilomchagulia Allaah Ta’aalaa Nabiy Wake na lile ambalo Nabiy Wake aliwachagulia Swahaba Zake”. Na yeye Rahimahu-Allaah amelipendelea zaidi la kwanza.

 

Ninasema: “Uchanganuzi huu unakubalika sana. Ndanimwe, Ibn Taymiyah ameitumia kila nassi katika nususi zilizopokelewa katika mahala pake mwafaka. Kisha akaijaalia aina bora zaidi kwa mujibu wa ugumu wake na uzito wake. Ni kama Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alivyomwambia ‘Aaishah wakati aliposema:

 

يَا رَسُولَ الله، يَصْدُرُ النَّاسُ بِنُسُكَيْنِ وَأصْدُرُ بِنُسُكٍ؟ فَقال: َإِذَا طَهُرْتِ فَاخْرُجِي إِلَى التَّنْعِيمِ فَأهِلِّي، ثُمَّ ائْتِينَا بِمَكَانِ كَذَا، وَلَكِنَّهَا عَلَى قَدْرِ نَفَقَتِكِ أوْ نَصَبِكِ"

Ee Rasuli wa Allaah, watu watarudi wamefanya Nusuk mbili [Hajj na ‘Umrah] na mimi nitarudi nimefanya Nusuk moja tu [Hajj]. Akamwambia: “Ukitwaharika, basi toka uende At-Tan-‘iym unuwie, halafu njoo mahala fulani utatukuta, lakini malipo ni kwa kadiri ya pesa unayotumia au tabu unayopata”  [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1787) na Muslim (1211)]

 

Kadhalika, ameziweka aina bora zaidi kwa mujibu wa kuswaga mnyama, na yote hayo yametajwa katika Sunnah.  Na kwa ajili hiyo, Ibn Taymiyah hakuingia kwenye wimbi la machafuko kama walivyoingia Fuqahaa wengi kutokana na kuona kwao kuwa kilicho bora ndicho hicho hicho na hakuna kingine zaidi yake.

 

Pamoja na hayo yote, sidharau nguvu ya kauli ya waliosema kuwa Tamattu’u ndio bora zaidi bali ni waajib pia. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”.

 

Wakazi Wa Haram Hawana Isipokuwa Ifraad

 

Allaah Ta’aalaa Amesema:

 

((فَمَن تَمَتَّعَ بِالْعُمْرَةِ إِلَى الْحَجِّ فَمَا اسْتَيْسَرَ مِنَ الْهَدْيِ ۚ فَمَن لَّمْ يَجِدْ فَصِيَامُ ثَلَاثَةِ أَيَّامٍ فِي الْحَجِّ وَسَبْعَةٍ إِذَا رَجَعْتُمْ ۗ تِلْكَ عَشَرَةٌ كَامِلَةٌ ۗ ذَٰلِكَ لِمَن لَّمْ يَكُنْ أَهْلُهُ حَاضِرِي الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ))

((Basi mwenye kufanya Tamattu’u kwa kutekeleza ‘Umrah kwanza kisha Hajj, achinje mnyama aliye mwepesi. Na asiyepata basi afunge Swiyaam siku tatu katika Hajj na saba mtakaporejea. Hizo ni kumi kamili. Hayo ni kwa ajili ya yule ambaye watu wake hawaishi karibu na Al-Masjidil-Haraam)). [Al-Baqarah (2:196)]

 

Hapa Allaah Mtukufu Ameruhusu kufanya Tamattu’u kwa mtu ambaye hana watu karibu na Al-Masjid Al-Haraam, yaani, mtu ambaye makazi yake hayako Makkah au Al-Haram – kwa mujibu wa kauli sahihi zaidi - kwa kuwa Tamattu’u imewekwa kwa ajili yake kwa vile hana watu, na mkazi wa Makkah ana watu wake, hivyo yeye hana hilo la kufanya Tamattu’u. Haya ni madhehebu ya Ibn ‘Abbaas na Abu Haniyfah, na yanatiliwa nguvu na Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas ambayo inaeleza:

 

 ثُمَّ أَمَرَنَا عَشِيَّةَ التَّرْوِيَةِ أَنْ نُهِلَّ بِالْحَجِّ، فَإِذَا فَرَغْنَا مِنَ الْمَنَاسِكِ جِئْنَا فَطُفْنَا بِالْبَيْتِ وَبِالصَّفَا وَالْمَرْوَةِ فَقَدْ تَمَّ حَجُّنَا، وَعَلَيْنَا الْهَدْىُ كَمَا قَالَ اللَّهُ تَعَالَى {فَمَا اسْتَيْسَرَ مِنَ الْهَدْيِ فَمَنْ لَمْ يَجِدْ فَصِيَامُ ثَلَاثَةِ أَيَّامٍ فِي الْحَجِّ وَسَبْعَةٍ إِذَا رَجَعْتُمْ} [البقرة: 196] إِلَى أَمْصَارِكُمْ. الشَّاةُ تَجْزِى، فَجَمَعُوا نُسُكَيْنِ فِى عَامٍ بَيْنَ الْحَجِّ وَالْعُمْرَةِ، فَإِنَّ اللَّهَ تَعَالَى أَنْزَلَهُ فِى كِتَابِهِ وَسَنَّهُ نَبِيُّهُ - صلى الله عليه وسلم - وَأَبَاحَهُ لِلنَّاسِ غَيْرَ أَهْلِ مَكَّةَ، قَالَ اللَّهُ {ذَلِكَ لِمَنْ لَمْ يَكُنْ أَهْلُهُ حَاضِرِي الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ))

((Kisha akatuamuru jioni ya [Siku ya] Tarwiyah tuhirimie Hajj. Tulipomaliza Manaasik, tulikuja tukatufu Nyumba, na [tukasai] Swafaa na Marwah, Hajj yetu ikatimia na tukawajibikiwa kuchinja kama Alivyosema Allaah Ta’aalaa:  

 

((فَمَا اسْتَيْسَرَ مِنَ الْهَدْيِ ۚ فَمَن لَّمْ يَجِدْ فَصِيَامُ ثَلَاثَةِ أَيَّامٍ فِي الْحَجِّ وَسَبْعَةٍ إِذَا رَجَعْتُمْ))

((achinje mnyama aliye mwepesi. Na asiyepata basi afunge Swiyaam siku tatu katika Hajj na saba mtakaporejea)).. kwenye miji yenu. Kondoo anatosha. Wakakusanya Nusuki (‘amali) mbili katika mwaka mmoja kati ya Hajj na ‘Umrah, kwani Allaah Mtukufu Ameiteremsha katika Kitabu Chake na Nabiy Wake (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akaiwekea sharia, na Akawaruhusu watu ambao si wakazi wa Makkah kuifanya. Allaah Amesema:

 

((ذَٰلِكَ لِمَن لَّمْ يَكُنْ أَهْلُهُ حَاضِرِي الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ))

((Hayo ni kwa ajili ya yule ambaye watu wake hawaishi karibu na Al-Masjidil-Haraam)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1572)]

 

 

Ninasema: “Msingi wa madhehebu haya ni kuwa kiwakilishi kionyeshi (demonstrative pronoun) katika Kauli Yake Ta’aalaa katika Aayah   (ذَٰلِكَ)

“Hayo”na katika neno la Ibn ‘Abbaas katika Hadiyth

 

 (أَنْزَلَهُ فِى كِتَابِهِ وَسَنَّهُ نَبِيُّهُ) 

“Ameiteremsha”, kinarudi kwa Tamattu’u, nalo liko bayana”.

 

Na inafaa pia kirudi kwa mnyama, na maana ya Aayah inakuwa: Mwenye kufanya Tamattu’u, basi ni lazima achinje kama si katika wakazi wa Makkah, na kama ni mkazi, basi si wajibu kuchinja. Na haya ndiyo yaliyosemwa na Maalik, Ash-Shaafi’iy na Ahmad, na Ibn Hazm ameunga mkono.

 

Je, inajuzu kuingiza Hajj ndani ya ‘Umrah?

 

[Al-Majmuw’u (7/168) na Ash-Sharhu Al-Mumti’u]

 

Mtu akihirimia ‘Umrah peke yake katika miezi ya Hajj, kisha akaona vyema achanganye na Hajj afanye Qiraan, basi anaweza kufanya hilo kwa mujibu wa kauli ya Jumhuri (kinyume na Hanafiy) kwa sharti iwe kabla ya kuanza kutufu, na kama ameanza kutufu ijapokuwa kwa hatua moja, basi haijuzu kuingiza Hajj ndani ya ‘Umrah.

 

Dalili ya hilo ni kuwa ‘Aaishah alipopata hedhi huko Sarif baada ya kuhirimia ‘Umrah, Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alimwamuru anuwie Hajj akimwambia:

 

((طوافك بالبيت وبالصفا والمروة، يسعك لعمرتك وحجك))

((Kutufu kwako Nyumba, na Swafaa na Marwah, kunakutosheleza wewe ‘Umrah yako na Hajj yako)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1211)]

 

Na hii ni dalili ya kuwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kumwamuru ‘Aaishah kunuwia Hajj, hakukuwa ni kuibatilisha ‘Umrah yake.  

 

Lakini, mtu anaweza kusema: Dalili imetokea katika hali inayofanana na dharura kwa kuwa ‘Aaishah hakuweza kukamilisha ‘Umrah yake akiwa na hedhi. Hivyo dalili hapa inakuwa mahsusi zaidi kuliko tukio lenyewe. Hapa kidogo kuna kijiukakasi. Na hili linatiliwa nguvu na Rasuli kumwamuru mtu aliyehirimia Hajj na hana mnyama wa kuchinja aifanye Hajj yake kuwa ‘Umrah. Hivyo vipi tuifanye ‘Umrah kuwa Hajj nako ni kinyume na aliloamuru?

 

 

Je, Inajuzu Kuingiza ‘Umrah Ndani Ya Hajj?

 

[Al-Majmuw’u (7/170), Al-Mughniy (3/512), Al-Mabsuwtw (4/180) na Majmuw’u Al-Fataawaa (26/88)]

 

- Ama akihirimia Hajj, kisha akaingiza ndani yake ‘Umrah, haitoswihi na hawi ni mwenye kufanya Qiraan. Ni kauli ya Maalik, Ash-Shaafi’iy katika kauli yake mpya na Ahmad. Imekhitariwa na Sheikh wa Uislamu.

 

- Lakini Abu Haniyfah amejuzisha kwa kujengea juu ya asili yake. Anasema: “Kazi ya mwenye kufanya Qiraan ni zaidi ya mwenye kufanya Ifraad. Akihirimia Hajj na akaingiza ndani yake ‘Umrah, anakuwa ni mwenye kufanya Qiraan na lazima atufu mara mbili na asai mara mbili”.

 

Ninasema: “Na mimi napondokea kwenye kauli ya Abu Haniyfah – si kutokana na hoja aliyoitoa - bali kwa Hadiyth ya ‘Aaishah isemayo:

 

أهل رسول الله صلى الله عليه وسلم بالحج)

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alihirimia Hajj [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1562) na Muslim (1211).

 

Pamoja na Hadiyth Marfuu ya Ibn ‘Umar isemayo:

 

((أتاني آت من ربي، فقال: صل في هذا الوادي المبارك وقل: عمرة في حجة))

((Alinijia mwenye kunijia [Jibriyl] toka kwa Mola wangu akasema: Swali katika bonde hili [la Al-‘Aqiyq] lililobarikiwa na sema: ‘Umrah ndani ya Hajj). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1534), Abu Daawuwd (1783) na Ibn Maajah (2976)]

 

Imekhitariwa na Al-‘Allaamah Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu-Allaah).

 

Je, Inaswihi Niya Ya Kuhirimia Bila Kuainisha?

 

Mwenye kuhirimia bila kutaja aina yoyote kati ya ‘amali hizi tatu (Ifraad, Qiraan au Tamattu’u) kwa kutokujua, au akahirimia mithili ya Ihraam ya mtu anayejua, basi hilo linajuzu, na Ihraam yake ni sahihi kwa mujibu wa kauli ya Jumhuri ya ‘Ulamaa kinyume na Maalik. Ni kwa Hadiyth ya Abu Muwsaa: Kwamba ‘Aliyy alimwendea Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) na Rasuli alimuuliza: Umesema nini ulipohirimia?. ‘Aliyy akasema: Nimesema:

 

لبيك بإهلال كإهلال النبي صلى الله عليه وسلم

((Labbayka kwa niya kama niya ya Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa sallam)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1734) na Muslim (1221)]

 

Haijuzu Kuvuka Miyqaat Bila Kuhirimia

 

[Angalia Al-Majmuw’u (7/212-215)]

 

Aliyepita Miyqaat – ilhali amekusudia kuhiji au kufanya ‘Umrah - basi haijuzu kwake kuivuka bila kuhirimia. Ni Ijma’a ya ‘ Ulamaa wote. Kama ataivuka kisha akahirimia baada yake basi atapata dhambi kwa kufanya hivyo, na dhambi haiondoki mpaka arudi kwenye Miyqaat ahirimie tena kisha akamilishe ‘ibaadah yake. Si lazima achinje mnyama kama alirudi kwenye Miyqaat kabla hajaanza kufanya ‘amali yoyote ni sawa ikiwa Nguzo kama Kusimama ‘Arafah au Kusai, au Sunnah kama Twawaaf ya Quduwm. Haya ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy, Ath-Thawriy, Abu Yuwsuf, Muhammad na Abu Thawr.

 

Maalik, Ibn Al-Mubaarak na Ahmad wamesema kuchinja hakutenguki (hakuondoki) kwa kurudi kwake.

 

Abu Haniyfah kasema kama atarudi huku akipiga Talbiyah basi hatochinja, na akirudi kimya kimya basi lazima achinje.

 

Na Ibn Al-Mundhir amesimulia toka kwa Hasan na An-Nakh-‘iy kuwa aliyevuka Miyqaat halazimiki kuchinja chochote. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

Na kama hakurudi kwenye Miyqaat, basi ‘ibaadah yake ni sahihi, na lazima achinje kwa mujibu wa kauli ya Jumhuri.

                                                          

Kuhirimia Kabla Ya Kufika Miyqaat

 

[Al-Majmuw’u (7/205) kwa mabadilisho kidogo]

 

Salaf katika Swahaba na waliowafuatia wenye kutambulika vyema kwa misimamo imara ya dini, wamekubaliana wote kwa sauti moja kuwa inajuzu kuhirimia kwenye Miyqaat na kabla ya Miyqaat.

 

Lakini Daawuwd amesema haijuzu kuhirimia kabla yake na Ihraam haitoswihi (akifanya mtu hivyo). Kauli hii inamrudi yeye mwenyewe kwa kuwepo Ijma’a hiyo. Na pamoja na hivyo, ni makruhu kuhirimia kabla ya Miyqaat kwa mujibu wa kauli sahihi zaidi. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

Mwenye Kupita Miyqaat Mbili

 

Raia wa nchi za Sham au raia wa Misri akipita Miyqaat ya watu wa Madiynah kabla hajafika Al-Juhfah (Miyqaat yake ya asili), basi haijuzu kwake kuchelewesha Ihraam, bali inampasa ahirimie toka Dhul Hulayfah (ambayo ni ya watu wa Madiynah) kwa mujibu wa kauli ya Jumhuri. Ni kwa ujumuishi wa neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam):

 

((ولمن أتى عليهنَّ من غير أهلهنَّ))

((Na kwa yule atakayeingia humo katika wasio wakazi wake)). [Hadiyth Swahiyh. Imetajwa nyuma kidogo kwenye mlango wa Miyqaat]

 

Abu Haniyfah na Maalik wanaona kuwa si waajib kwake, bali inajuzu akawize kuhirimia hadi afike Miyqaat yake kwa kuwa ndiyo ya asili. Hili pia limekhitariwa na Sheikh wa Uislamu. Lakini la kwanza (la kuhirimia hapo hapo) ni la akiba zaidi (kuliko kukawiza hadi afike Miyqaat yake).

 

Mwenye Kuhirimia Kuweka Shuruti Ya Kuvua Ihraam Kutokana Na Udhuru Wa Kumzuia Kukamilisha Hajj

 

Inajuzu kwa aliyehirimia aweke shuruti – wakati anapohirimia - la kuvunja Ihraam yake wakati wowote likimzuia jambo kukamilisha ‘amali yake ya Hajj kama ugonjwa au mfano wake kwa kusema:

((اللهم محلي حيث حبستني))

((Ee Allaah, pangu pa kuvua Ihraam ni pale Utakaponizuia)).

 

Ni kwa Hadiyth ya ‘Aaishah aliyesema: ((Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliingia kwa Dhwubaa’ah binti Az-Zubayr akamwambia: (([Huenda] ulitaka kuhiji)). Akasema: Wa-Allaahi, najihisi kuumwa sana. Akamwambia: ((Hiji, na ushurutishe, na sema:

اللهم محلي حيث حبستني

((Ee Allaah, pangu pa kuvua Ihraam ni pale Utakaponizuia)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5089) na Muslim (1207)]

 

Akishurutisha, basi itajuzu ajivue na Ihraam yake likitokea la kumzuia asiendelee, na hatochinja mnyama. Na kama hakushurutisha na likatokea la kumzuia asiendelee, basi ni lazima achinje kutokana na Neno Lake Ta’aalaa:

 ((فَإِنْ أُحْصِرْتُمْ فَمَا اسْتَيْسَرَ مِنَ الْهَدْيِ))

((Na kama mkizuilika, basi chinjeni wanyama walio wepesi kupatikana)). [Al-Baqarah (2:196)]

 

 

 

 

Share