24-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Hajj Na 'Umrah: Nguzo Ya Nne Ya Hajj: Kusimama ‘Arafah

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Hajj Na ‘Umrah

 

24-Nguzo Ya Nne Ya Hajj: Kusimama ‘Arafah

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

Muradi wa Kusimama ‘Arafah ni kuwepo Hujaji katika ardhi ya ‘Arafah kwa mujibu wa shuruti na ahkaam zilizotajwa.

 

Hukmu yake

 

Kusimama ‘Arafah ni nguzo ya kimsingi kati ya nguzo za Hajj. Sifa yake pekee tofauti na nguzo nyingine ni kuwa atakayepitwa na kisimamo hiki basi ameikosa Hajj.

 

Kuwa kwake nguzo kumethibiti kwa dalili zisizo na chembe ya shaka toka kwenye Qur-aan, Sunnah na Ijma’a.

 

(a) Kwenye Qur-aan

 

Allaah Ta’alaa Amesema:

((ثُمَّ أَفِيضُوا مِنْ حَيْثُ أَفَاضَ النَّاسُ))

((Kisha miminikeni kutoka pale wamiminikapo watu)). [Al-Baqarah (2:199)]

 

Aayah hii imethibiti kuwa iliteremka kuwaamuru watu wasimame ‘Arafah. Toka kwa ‘Urwah toka kwa baba yake toka kwa ‘Aaishah ((Kuwa Aayah hii iliteremka kuwazungumzia “Al-Hums”. Amesema: Walikuwa wanamiminika toka Jam-‘u [Muzdalifah], wakaamuriwa wamiminike toka ‘Arafaat)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1665) na Muslim (1219)]

 

“Al-Hums” ni Maqureysh na kizazi chao. Walikuwa enzi ya ujahilia wakimiminika toka Muzdalifah (Jam-‘u), na watu wakimiminika toka ‘Arafaat. Wameitwa hivyo kutokana na ushadidiaji na ukereketwa wa iymaan yao.

 

(b) Kwenye Sunnah

 

Kuna Hadiyth nyingi. Iliyo mashuhuiri zaidi ni Hadiyth ya ‘Abdur Rahmaan bin Ya-‘amar ((Kuwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alimwamuru mpiga mbiu anadi:

((الحج عرفة، من جاء ليلة جمع قبل طلوع الفجر فقد أدرك الحج))

((Hajj ni ‘Arafah. Atakayekuja usiku wa Jam-‘u [Muzdalifah] kabla ya kuchomoza Alfajiri, basi hakika ameipata Hajj)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (1933), At-Tirmidhiy (590), An-Nasaaiy (5/264) na Ibn Maajah (3015)]

 

(c) Kwenye Ijma’a

 

‘Ulamaa wengi wamenukuu Ijma’a ya kuwa Kusimama ‘Arafah ni nguzo kati ya nguzo za Hajj, na mwenye kupitwa na kisimamo hicho, basi ni lazima ahiji mwaka kesho. [Bidaayatul Mujtahid (1/335)]

 

Wakati Wake

 

1- Jumhuri ya ‘Ulamaa wanasema wakati wa Kusimama ‘Arafah unaanzia baada ya kupinduka jua (Adhuhuri ya) Siku ya ‘Arafah (tarehe 9). [Al-Badaai’u (2/125) na Al-Mughniy (3/414)]

 

Ni kutokana na kitendo cha Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) ambaye hakusimama ‘Arafah ila baada ya jua kupinduka kama ilivyoeleza Hadiyth ndefu ya Jaabir. Na Rasuli kasema:

((خذوا عني مناسككم))

((Jifunzeni kutoka kwangu matendo yenu ya Hajj)).

 

Lakini Imaam Ahmad (Rahimahu-Allaah) amesema kuwa wakati wa kusimama unaanzia tokea Alfajiri ya Siku ya ‘Arafah. Na dalili yake ni Hadiyth ya ‘Urwah bin Mudhwarras kuwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

 

((من شهد صلاتنا هذه ووقف معنا حتى يدفع وقد وقف بعرفة قبل ذلك ليلاً أو نهاراً فقد تم حجه وقضى تفثه))

((Aliyehudhuria Swalaah yetu hii [Swalaatul Fajr], akasimama pamoja nasi mpaka akaondoka, na akawa alisimama ‘Arafah kabla ya hapo usiku au mchana, basi Hajj yake imetimia na ametimiza Nusuk zake)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na

Abu Daawuwd (1950), At-Tirmidhiy (891), An-Nasaaiy (5/263) na Ibn Maajah (3016). Angalia Al-Irwaa (1066)]

 

Lakini neno lake “mchana” halikuainisha wakati maalum, na wakati huo unaainishwa na kitendo cha Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam), na muradi unakuwa ni baada ya jua kupinduka. Na hili ndilo la akiba na salama zaidi. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

2- Mwenye kusimama ‘Arafaat mchana, basi ni lazima avute muda wa kubakia hapo hadi baada ya kuchwa jua. Na kama ataondoka hapo kabla ya Magharibi, basi Abu Haniyfah, Ash-Shaafi’iy na Ahmad wanasema kuwa Hajj yake ni sahihi lakini ni lazima achinje ili aunge sehemu ya usiku aliyoipunguza ambayo ilikuwa ijumuishwe na sehemu ya mchana ktk Kisimamo. [Al-Badaai’u (3/1098), Al-Majmuw’u (8/123) na Al-Mughniy (3/370)]

 

Riwaya toka kwa Ash-Shaafi’iy inasema si lazima achinje. Ahlu Adh-Dhwaahir wamesema hivyo hivyo. [Al-Muhallaa (7/8)]

 

Na hii ndio kauli yenye nguvu. Lakini Maalik amesema kuwa Hajj yake haiswihi mpaka akusanye baina ya usiku na mchana katika kusimama kwake. [Al-Mudawwanah, Bidaayatul Mujtahid (1/375)]

 

Na hoja yake ni Hadiyth ya Ibn ‘Umar amesema: ((Mwenye kuipata ‘Arafaat kwa usiku basi ameipata Hajj, na aliyepitwa na ‘Arafaat usiku, basi Hajj imempita. Basi huyo avue Ihraam kwa ‘Umrah, na ni lazima ahiji mwaka ujao)). [Hadiyth Swahiyh Marfuw’u. Imekharijiwa na Maalik katika Al-Muwattwa (886 ikiwa Mawquwf) na Ad-Daara Qutwniy (2/241) Marfuw’u]

 

Hadiyth hii imejibiwa ikiambiwa kuwa usiku umehusishwa kwa kuwa kupitwa na kisimamo kunafungamana nao. Na kiini cha inachodulisha ni:

 

3- Kiasi kinachotosheleza Kusimama ni Hujaji asimame sehemu ya usiku kabla ya Alfajiri –japo kwa muda mfupi- na kama Alfajiri itachomoza kabla hajasimama, basi ataikosa Hajj. Hili limegusiwa vile vile na Hadiyth iliyotangulia ya ‘Urwah bin Mudhwarras. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

 

 

Sunnah Na Adabu Za Kusimama ‘Arafah Na Kuondoka (kumiminika) Kutoka Hapo

 

1- Kusimama pembeni mwa miamba ya mawe

 

Hujaji anaruhusiwa kusimama sehemu yoyote ya eneo la ‘Arafah. Lakini imesuniwa asimame pembeni au mbele ya miamba ya mawe iliyotandazika chini ya Jabal Ar-Rahmah. Jabali hili liko katikati ya ardhi ya ‘Arafaat. Kufanya hivi ni kwa Hadiyth ya Jaabir: ((..mpaka akafika sehemu ya kisimamo, akamwelekeza ngamia wake Al-Qaswaa upande wa miamba ya mawe, na njia ya watembeao kwa miguu ikawa mbele yake..)).

 

An-Nawawiy amesema: “Na hiki ndicho Kisimamo kilichostahabiwa. Ama kitendo kilichozoeleka kufanywa na watu wa kawaida wasio na uelewa wa dini cha kupanda juu ya Jabali hilo na kudhani kuwa Hajj haiswihi ila kwa kufanya hivyo, basi hilo ni kosa”.

 

2,3- Kuelekea Qiblah na kunyanyua mikono miwili kuomba du’aa

 

Ni kwa Hadiyth ya Jaabir: ((Na akaelekea Qiblah…)). Na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

 

((خير الدّعاء يوم عرفة، وخير ما قلت أنا والنبيّون من قبلي: لا إله إلّا الله وحده لا شريك له، له الملك وله الحمد، وهو على كلّ شيءٍ قدير))

((Du’aa bora na ya kheri zaidi ni ya Siku ya ‘Arafah. Na bora na la kheri zaidi nililolisema Mimi na Manabii walionitangulia ni: Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah Peke Yake Asiye na mshirika, ni Wake Ufalme, na ni Yake Himdi, Naye ni Mweza juu ya kila kitu)). [Hadiyth Hasan. Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (3585), na Ibn Abiy Shaybah (1/369). Angalia As-Swahiyhah (1503)]

 

Kuna matamshi mengi ya du’aa ya ‘Arafah yaliyopokelewa toka kwa Nabiy (Swallah Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam), lakini Asaaniyd Zake ni Layyin. [Angalia Zaadul Ma’aad (2/237)]

 

 

4- Kuleta Talbiyah

 

Ni kwa Hadiyth ya Sa’iyd bin Jubayr. Amesema: ((Tulikuwa pamoja na Ibn ‘Abbaas, akaniambia: Ee Sa’iyd! Mbona siwasikii watu wakileta Talbiyah? Nikamwambia: Wanamwogopa Mu’aawiyah. Ibn ‘Abbaas akatoka ndani ya hema lake akasema: “Labbayka Allaahumma Labbayka”, hakika wao wameiacha Sunnah kwa kumchukia ‘Aliyy (Radhwiya Allaah ‘anhu)). [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Haakim (1/464-465) na Al-Bayhaqiy (5/103). Angalia kitabu cha Hijjatun Nabiyy (uk. 74)]

 

Ninasema: “Ingawa Ibn Taymiyah (26/136) amesema kwamba kuleta Talbiyah ‘Arafah hakukuripotiwa toka kwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) bali kumenukuliwa toka kwa Makhalifa Waongofu na wengineo, lakini Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas –ikiwa ni Swahiyh- inakuwa ni hoja dhidi yake. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.

 

Angalizo

 

Hivi ndivyo inavyotakikana iwe hali ya Hujaji anapokuwa ‘Arafah. Alete adhkaar na du’aa, ahudhurishe moyo, asome Qur-aan, awe mnyenyekevu, ajinyenyekeze na ajikurubishe kwa Allaah Subhaanah.

 

Hakika ni hasara kubwa kuwaona baadhi ya Mahujaji katika Siku hii ya ‘Arafah wakiipitisha Siku hii kwa kufanya mambo ya kipumbao yasiyo na faida, kucheza na kuzungumza na wenzi wao mambo yasiyo na ulazima. Na hata wengine wanafikia ujasiri wa kucheza karata, kuvuta sigara,  kusikiliza nyimbo na muharramaat zingine. Tunajilinda kwa Allaah na hali hii ya kutojali kitu.

 

 

5- Hujaji asifunge Swawm

 

Ni kwa Hadiyth ya Maymuwnah: ((Kwamba watu walishakia kama Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amefunga Siku ya ‘Arafah. Nikampelekea maziwa –naye kasimama sehemu ya Kisimamo-, akayanywa na watu wanatizama)).  [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1989) na Muslim (1124)]

 

 

6- Kuteremka toka ‘Arafah kwa utulivu na utaratibu baada ya kuchwa jua

 

Ni kwa neno lake Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) –wakati alipoteremka toka ‘Arafah baada ya kuchwa jua-:

((أيها الناس عليكم السكينة، فإن البر ليس بالابضاع))

((Enyi watu! Fanyeni utulivu, kwani wema si kwa kukimbizana)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1671), Muslim (1218) na An-Nasaaiy (5/257)]

 

Lakini kama atapata njia wazi mbele yake, basi anaweza kuchakarisha mwendo kidogo. Ni kwa Hadiyth: ((Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa anatembea mwendo wa hatua pana, na kama njia iko wazi, aliharakisha mwendo kidogo)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1666) na Muslim (1286)]

 

 

7- Kutembea kwa miguu kwenda Muzdalifah sambamba na kuleta Talbiyah

 

Hadiyth husika imelielezea hili nyuma kuzungumzia mwahala pa kuleta Talbiyah.

 

 

 

Share