25-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Hajj Na 'Umrah: Kulala Muzdalifah Usiku Wa Yawm An-Nahr

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Hajj Na ‘Umrah

 

25-Kulala Muzdalifah Usiku Wa Yawm An-Nahr

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

Hukmu yake

 

Fuqahaa wamekhitalifiana kuhusu hukmu ya kusimama Muzdalifah (ambayo pia huitwa Jam-‘u) na kulala hapo katika kauli tatu:

 

Ya kwanza:

 

Ni nguzo, na atakayekosa kusimama hapo, basi kaikosa Hajj. Ni madhehebu ya Ibn ‘Abbaas, Ibn Az-Zubayr, An-Nakh-’iy, Ash-Sha-’abiy, ‘Alqamah na Ahlu Adh-Dhwaahir. Kuna kidokezo katika madhehebu ya Maalik kuhusu hili, na ni chaguo la Ibn Al-Qayyim (Rahimahu-Allaah). [Al-Mughniy (3/376), Al-Muhallaa (7/118), Bidaayatul Mujtahid (1/376) na Zaad Al-Ma’aad (3/253)]

 

Dalili zao ni:

 

1- Kauli Yake Ta’aalaa:

((فَإِذَا أَفَضْتُم مِّنْ عَرَفَاتٍ فَاذْكُرُوا اللَّـهَ عِندَ الْمَشْعَرِ الْحَرَامِ ۖ))

((Basi mtakapomiminika kutoka ‘Arafaat mdhukuruni Allaah kwenye Al-Mash-’aril Haraam)). [Al-Baqarah (2:198)]

 

Kuna ‘Ulamaa wanaosema kuwa Al-Mash-’arul Haraam ni Jabali ambalo liko Muzdalifah lijulikanao kama “Quzah”, na wengine wamesema ni eneo lote la Muzdalifah.

 

2- Hadiyth ya ‘Urwah bin Al-Mudhwarras kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

 

((من شهد صلاتنا هذه ووقف معنا حتى ندفع وقد وقف بعرفة قبل ذلك ليلاً أو نهاراً فقد أتم حجه وقضى تفثه))

((Aliyehudhuria Swalaah yetu hii [Swalaatul Fajr], akasimama pamoja nasi mpaka tukaondoka, na akawa alisimama ‘Arafah kabla ya hayo usiku au mchana, basi ameitimiza Hajj yake na ametekelezaNusuk zake)). [Hadiyth Swahiyh. Imetajwa nyuma kidogo]

 

3- Ni kitendo cha Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) ambacho ni kama kibainisho cha aliloamuriwa katika Aayah Tukufu.

 

Ya pili:

 

Ni waajib, na mwenye kuacha ni lazima achinje na Hajj yake ni sahihi. Kauli hii ni madhehebu ya Jumhuri ya ‘Ulamaa. Dalili zao ni:

 

1- Kauli ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam):

 

((الحج عرفة، من جاء قبل أن يطلع الفجر فقد أدرك))

((Hajj ni ‘Arafah. Atakayekuja kabla ya kuchomoza Alfajiri basi ameipata)).  [Al-Mughniy (3/417) na Az-Zaad (2/253)]

 

Hii ina maana kuwa atakayesimama ‘Arafah kabla ya kuchomoza Alfajiri kwa kitambo kidogo, basi Hajj yake ni sahihi. Na kama kusimama Muzdalifah kungekuwa ni nguzo, basi Hajj yake isingeswihi.

 

2- Kama ingelikuwa ni nguzo, basi wanaume na wanawake wangeifanya wote kwa pamoja. Na kwa kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliwaamuru akina mama watangulie mbele usiku, imejulikana kuwa si nguzo.

 

Wamejibu kuhusu Aayah (iliyotajwa 198 Al-Baqarah) na Hadiyth ya ‘Urwah bin Al-Mudhwarras wakisema kuwa kilichotamkwa ndani ya viwili hivyo si nguzo, kwani lau mtu atalala Muzdalifah, na asimdhukuru Allaah wala kuswali hapo, basi Hajj yake ni sahihi.. Kisha, kulala si lazimisho la kumdhukuru Allaah Ta’aalaa wala kuswali Swalaah ya Alfajiri, kwa kuwa ikiwa atateremka toka ‘Arafah mwishoni mwa usiku wa tarehe 10, ataweza hayo.

 

Hivyo basi, tunalazimika kulichukulia hilo [la kulala Muzdalifah] kama ima ni jambo la waajib, au jambo bora, au jambo mustahabu. [Ikhtiyaaraat Ibn Qudaamah Al-Fiqhiyyah cha Al-Ghaamidiy (1/678)]

 

Ninasema: “Kwa mujibu wa hoja hii, muradi wa kuitimiza Hajj katika Hadiyth ni utimizaji ambao hata kama haupo, basi jambo litakuwa ni sawa lakini pamoja na uharamu. Linalotoa mwega kwa hayo niyasemayo ni kuwa atakayeipata ‘Arafah na Muzdalifah lakini hakutufu Twawaaful Ifaadhwah, basi Hajj yake inakuwa haikutimia kwa Ijma’a ya ‘Ulamaa. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

Na kauli isemayo kusimama na kulala Muzdalifah ni waajib, ndio kauli sawa na yenye nguvu zaidi. Lakini sitosema lolote kuhusu lazimisho la kuchinja mnyama wa kufidia kosa la kutosimama, kwa kuwa kiasli, mali ya Muislamu ni haramu isipokuwa kwa haki, na hili hujulikana kwa dalili. Na haiswihi kuleta Qiyaas cha kafara hata kama hili ni kinyume na Jumhuri ya ‘Ulamaa”.

 

Ya tatu:

 

Ni Sunnah. Hii ni kauli dhaifu, nayo ni riwaya toka kwa Ahmad.

 

Faida

 

Mpaka wa muda wa wajibu wa kulala

 

[Raddu Al-Mukhtaar (2/241), Haashiyatul ‘Adwaa (1/475), Mughnil Muhtaaj (1/498) Al-Mughniy (3/417) na Al-Furuw’u (3/510)]

 

Mahanafiy wanasema kuwa mwenye kupata kiasi cha kitambo kidogo cha kutokea kuchomoza Alfajiri –Yawm An-Nahr (Tarehe 10)- mpaka jua kutoka hapo Muzdalifah, basi amekipata kisimamo cha Muzdalifah, ni sawa kama alilala hapo au la. Na kama hakupata kitambo hicho, basi ni lazima achinje isipokuwa tu kama alishindwa kutokana na udhuru, hapo hatowajibikiwa kuchinja.

 

‘Ulamaa wa Kimaalik wanasema ni muda wa kumtua mnyama mzigo sehemu yoyote ya usiku kitambo cha kati ya kuwasili kwake hadi kuchomoza Alfajiri.

 

Ama Mashaafi’iy na Mahanbali, wao wanasema ni lazima asimame kiasi cha kitambo cha kuanzia anapowasili hadi usiku wa manane –kama atafika hapo kabla ya usiku wa manane- na ikiwa atafika hapo baada ya usiku wa manane basi kitamtosha kitambo kifupi kabla ya kuchomoza Alfajiri.

 

Ninasema: “Linaloonekana ni kuwa waajib ni kulala Muzdalifah mpaka Alfajiri, ni sawa alifika huko kabla ya usiku wa manane au baada yake, kwa kuwa kulala maana yake ni kusalia huko mpaka Alfajiri. Lakini wanawake madhaifu na wengineo, wanaruhusiwa kuondoka hapo baada ya usiku wa manane. Matamshi ya Hadiyth kadhaa yanadokeza hilo [la kuruhusiwa kuondoka] kama Hadiyth ya ‘Aaishah aliyesema: ((Tulishuka Muzdalifah, na Sawdah akamwomba ruksa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) ili sisi [wanawake] tuondoke kabla ya mminyano wa watu. Yeye alikuwa mzito wa kutembea na Rasuli akamruhusu. Akaondoka kabla ya mminyano wa watu…)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1681) na Muslim (1290]

 

Hadiyth hii iko wazi ikibainisha kuwa ambaye hana ruksa [au udhuru], basi ni lazima abakie Muzdalifah mpaka asubuhi, kwa kuwa ni kitendo kwa mkabala wa ruksa.

 

Vile vile Hadiyth ya Asmaa: ((Kwamba yeye alishuka Muzdalifah, akasimama muda hivi akiswali, kisha akasema: Ee mwanangu kipenzi! Je, mwezi umezama? Nikasema: Hapana. Akaswali tena muda hivi kisha akasema: Ee mwanangu kipenzi! Je, mwezi umezama? Nikasema: Na’am. Akasema: Basi ondokeni. Tukaenda mpaka tukatupia vijiwe Al-Jamarah, halafu akarejea, akaswali Alfajiri nyumbani kwake [Minaa]. Nikamwambia: We vipi! Mimi sioni ila tumewahi sana kuondoka [Muzdalifah]. Akasema: Ee mwanangu kipenzi! Hakika Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amewaruhusu wanawake)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1679) na Muslim), na anayezungumza hapa na Asmaa ni mwachwa huru wake au mtumishi wake ‘Abdallah]

 

Na toka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaah ‘anhumaa) [akiwa kijana mdogo wakati huo] amesema: ((Mimi ni katika ambao Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliwatanguliza mapema pamoja na wakeze ambao afya zao si imara)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1678) na Muslim (1293)]

 

Hadiyth hizi na nyinginezo zinatuhabarisha kuwa ulalaji wa wajibu ni mpaka Alfajiri isipokuwa kwa wanawake wenye afya dhaifu na nguvu kidogo. Hawa wanaruhusiwa kushuka toka hapo kabla ya Alfajiri baada ya mwezi kutoweka.

 

Faida

 

Ruksa ya kutolala Muzdalifah ni mahsusi kwa wanawake wenye afya dhaifu na nguvu kidogo pamoja na watoto wadogo. Je, wanawake kiujumla wanaingia kwenye ruksa hii, au ni kwa madhaifu tu kati yao?

 

Nukta hii ni ya kuitafiti. Inavyoonekana ni kuwa inawahusu wanawake madhaifu tu, kwa kuwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliwatanguliza wake zake madhaifu na ‘Aaishah akabaki pamoja naye. Sawdah alimwomba ruksa ya kuondoka mapema kwa kuwa alikuwa mnene na mzito wa kutembea. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

Mambo yaliyosuniwa Muzdalifah na kuondoka kutoka hapo

 

1- Ni kuswali Magharibi na ‘Ishaa kwa pamoja katika wakati wa ‘Ishaa (Jam-‘u Taakhiyr) hapo hapo Muzdalifah.

 

2- Adhana moja na Iqaamah mbili kwa Swalaah mbili.

 

3- Kuacha Sunnah zote baina ya Swalaah mbili.

 

4- Kulala mpaka Alfajiri bila kusimama usiku kuswali.

 

5- Kuswali Alfajiri mwanzoni mwa wakati wake kwa Adhana moja na Iqaamah moja.

 

6- Kusimama juu ya kilima cha Muzdalifah, kuelekea Qiblah na kuomba du’aa, pamoja na kuleta Tahmiyd, Takbiyr na Tahlilyl mpaka papambazuke kabisa.

 

7- Kuondoka kwa utaratibu toka Muzdalifah kabla jua halijachomoza.

 

8- Kukaza mwendo kidogo katika eneo la Batwn Muhassir isipokuwa kama amepanda gari ambayo yeye si dereva, hapo hawezi kufanya hivyo. Lakini inakuwa vyema anuwie kwa moyo wake lau angeliweza kuchakarisha mwendo hapo, basi angeuchakacharisha. [Batwn Muhassir ni eneo kati ya Minaa na Muzdalifah. Limeitwa hivyo kwa kuwa ndovu wa jeshi la Abrahah walinyon’gonyea hapo na kuishiwa nguvu kabisa. Na huenda kutokana na hilo, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa akikaza mwendo kama ilivyo desturi yake mwahala pa watu walioshushiwa adhabu]

 

9- Aende Jamarah (kurusha vijiwe) kwa njia nyingine tofauti na ile aliyoipita akielekea ‘Arafaat (ikiwezekana).

 

 

Share