27-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Hajj Na 'Umrah: Tahallul (Kujivua Ihraam) Ya Kwanza Na Ya Pili

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Hajj Na ‘Umrah

 

27-Tahallul (Kujivua Ihraam) Ya Kwanza Na Ya Pili

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Hajj ina tahallul mbili; ya kwanza na ya pili, nazo zinafungamana na kutupia Jamaratul ‘Aqabah, kunyoa na Twawaaful Ifaadhwah. ‘Ulamaa wamekhitalifiana kuhusu je tahallul ya kwanza inapatikana kwa kutupia hata kama hakunyoa, au kutupia pamoja na kunyoa?

 

Asli ya hili ni Hadiyth ya ‘Aaishah aliyesema: ((Nilimtia manukato Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kwa mikono yangu hii miwili wakati alipohirimia, na kwa kuvua kwake Ihraam (tahallul) wakati alipovua Ihraam kabla hajatufu)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1754) na Muslim (1189)]

 

Na ‘Aaishah hakuongozana naye wakati Rasuli alipoteremka toka Muzdalifah. Na imethibiti kiuhakika kuwa aliendelea kumpanda mnyama wake mpaka alipotupia Jamaratul ‘Aqabah, na hii inaonyesha kuwa ‘Aaishah alimtia manukato Rasuli baada ya kutupia. Lakini je, kumtia manukato kulikuwa kabla ya kunyoa au baada ya kunyoa?

 

Baadhi ya ‘Ulamaa wamesema: [Ash-Sharhul Mumti’u]

 

“Lau ingekuwa anavua Ihraam kwa kutupia tu, basi angelisema: “Na kwa kuvua kwake Ihraam kabla hajanyoa”. Yeye ameiweka tahallul baina ya Twawaaf na vitendo vya kabla yake ambavyo ni kutupia, kuchinja na kunyoa, na hususan Rasuli (Swallah Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

((إن معي الهدي فلا أحل حتى أنحر))

((Hakika mimi nina mnyama wa kuchinja, sivui Ihraam mpaka nichinje)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1566) na Muslim (1229)

 

Kuna Hadiyth nyingineyo isemayo:

((إذا رميتم وحلقتم فقد حل كل شيء إلا النساء))

((Mkitupia na mkanyoa, basi kila kitu kimehalalika isipokuwa wanawake))…lakini Hadiyth hii si Swahiyh. [Hadiyth Dhwa’iyf. Imekharijiwa na At-Twahaawiy (1/419), Al-Bayhaqiy (5/136) na Ahmad (6/143)]

 

Na wengine wamesema: Hujaji akitupia Jamaratul ‘Aqabah, kila kitu kinakuwa halali kwake isipokuwa wanawake hata kama hakunyoa. Wametoa dalili kwa riwaya ya Hadiyth iliyotangulia ya ‘Aaishah kwa tamko: ((Nilimtia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) manukato ya dhariyrah katika Hijjah ya Kuaga kwa mkono wangu kwa kuvua Ihraam na kuhirimia, wakati alipohirimia, na wakati alipotupia Jamaratul ‘Aqabah Yawm An-Nahr, kabla hajatufu Nyumba)). [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na Ahmad (6/200)]

 

Na kwa Hadiyth:

((إذا رميتم الجمرة فقد حل لكم كل شيء إلا النساء))

((Mkitupia Jamarah, basi kila kitu ni halali kwenu isipokuwa wanawake))..bila ziada ya ((وحلقتم)) na ((mkanyoa)). [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh. Angalia Al-Irwaa (4/236) na Asw-Swahiyhah (239)]

 

 

Haya ni madhehebu ya ‘Atwaa, Maalik, Abu Thawr na Abu Yuwsuf na riwaya toka kwa Ahmad. Ni chaguo la Ibn Qudaamah na mwelekeo wa Ibn Hazm ambaye pamoja na yote kasema: “Ni halali kwake hayo kwa kuingia tu wakati wa kutupia hata kama hakutupia”. [Al-Mughniy (3/439), Al-Muhallaa (7/139) na Hijjatun Nabiyy (uk. 81)]

 

Naye Ash-Shaafi’iy amesema kwamba tahallul ya kwanza inapatikana kwa mambo mawili kati ya matatu: Kutupia, kunyoa na kutufu, na tahallul ya pili inapatikana kwa la tatu (kutufu). [Al-Majmuw’u (8/205) na Fat-hul Baariy (3/684)]

 

Ama tahallul ya pili, hii hupatikana baada ya Twawaaful Ifaadhwah. Ni kwa Hadiyth ya Ibn ‘Umar: ((..kisha hakufanya [yaani Nabiy Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) jambo lolote marufuku kwake mpaka akamaliza Hajj yake, akachinja mnyama wake Yawm An-Nahr na akafanya Twawaaful Ifaadhwah kwenye Nyumba. Kisha akafanya kila kitu kilichozuiwa kwake….)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1227) na wengineo]

 

 

2- Kutupia Siku Ya Kwanza Na Ya Pili Ya Masiku Ya Tashriyq

Ni lazima katika siku hizi mbili za tarehe (11 na 12 Dhul Hijja) kutupia nguzo tatu kimpangilio; kwanza Al-Jamarat As-Sughraa (nguzo ndogo), kisha ya kati, na hatimaye Jamaratul Aqabah (nguzo kuu). Kila nguzo ataitupia vijiwe saba.

 

 

Wakati wa kutupia

 

Wakati wa kutupia katika siku hizi mbili unaanzia baada ya kupinduka jua, na haijuzu kabla yake kwa mujibu wa msimamo wa Jumhuri ya ‘Ulamaa. [Al-Mabsuwtw (4/23), Al-Muwattwa (1/409), Al-Furuw’u (3/518) na Al-Majmuw’u (8/211)]

 

Dalili ni:

 

1- Hadiyth ya Jaabir: ((Nilimwona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) anatupia Yawm An-Nahr [wakati wa] Dhuhaa. Ama baada ya hapo, ni baada ya kupinduka jua)).

 

Na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema: 

((خذوا عني مناسككم))

((Jifunzeni kutoka kwangu matendo yenu ya Hajj)). [Hadiyth Swahiyh. Imetajwa nyuma]

 

2- Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa akisubiria jua lipinduke ili atupie. Toka kwa Wabrah: ((Nilimuuliza Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaah ‘anhu): Wakati gani nitupie vijiwe? Akasema: Akitupia kiongozi wako  [wa Hajj] na wewe hapo tupia. Nikamuuliza tena swali hilo hilo. Akasema: Tulikuwa tunasubiria, na jua linapopinduka tunatupia)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1746)]

 

Na lau ingejuzu kabla jua kupinduka, basi Rasuli angefanya angalau mara moja ili kuonyesha kuwa inajuzu.

 

3- Lau kutupia kungekuwa kunajuzu kabla jua kupinduka, basi Rasuli angefanya kwa kuwa kufanya hivyo, ni kuileta ‘ibaadah mwanzoni mwa wakati wake, ni kuwawepesishia watu ‘ibaadah na kuwarefushia wakati. [Ash-Sharhul Mumti’u (7/384)]

 

Wakati uliosuniwa unaanza tokea kupinduka jua mpaka kuchwa. Ikiwa itakuwa uzito kutupia kabla ya Magharibi, basi hapana ubaya kutupia usiku  kama tulivyoeleza nyuma kuhusu kutupia Yawm An-Nahr.

 

Ama mwisho wa kutupia, madhehebu ya ‘Ulamaa ni mfano wa yale yale tuliyoyagusia katika kutupia Yawm An-Nahr. 

 

 

Picha ya utupiaji katika siku mbili

 

Toka kwa Saalim kwamba Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaah ‘anhumaa): ((Alikuwa anatupia Jamrat Ad-Dunyaa [iliyo karibu na Msikiti wa Khayf] kwa vijiwe saba na huleta Takbiyr kwa kila kijiwe, kisha husogea mbele mpaka akafika ndani ya bonde, halafu huelekea Qiblah kwa muda mrefu akiomba huku akinyanyua mikono yake miwili. Kisha hutupia Jamarat la kati halafu huelekea upande wa kushoto ndani ya bonde. Halafu hutupia Jamaratul ‘Aqabah tokea ndani ya bonde na wala hasimami mbele yake, na husema: Hivi ndivyo nilivyomwona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akifanya)).  [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1751)]

 

An-Nafrul Awwal

 

Hujaji akitupia vijiwe siku ya kwanza na ya pili ya Tashriyq, basi anaruhusika kwenda Makkah kama atapenda kuharakia kuondoka toka Minaa (Ta’ajjul). Siku hii huitwa Yawmu An-Nafril Awwal (Siku ya mguro wa kwanza kwenda Makkah). Na kwa mguro huu, kutupia siku ya tatu ya Tashriyq kutakuwa hakuko tena kwa makubaliano ya ‘Ulamaa wote. Na hii ni kwa Kauli Yake Ta’aalaa:

 

((فَمَن تَعَجَّلَ فِي يَوْمَيْنِ فَلَا إِثْمَ عَلَيْهِ وَمَن تَأَخَّرَ فَلَا إِثْمَ عَلَيْهِ ۚ لِمَنِ اتَّقَىٰ))

((Atakayeharakisha kuondoka katika siku mbili, basi hakuna dhambi juu yake; na atakayetaakhari basi hakuna dhambi juu yake; kwa mwenye kuwa na taqwa)). [Al-Baqarah (2:203)]

 

Katika madhehebu ya Jumhuri, Hujaji anatakiwa agure au aondoke (mguro wa kwanza) kabla jua kuchwa siku ya pili ya Masiku ya Tashriyq (tarehe 12). Na Mahanafiy wanasema anaweza kuondoka siku ya tatu ya Tashriyq kabla Alfajiri haijawadia.

 

 

3- Kutupia Siku Ya Tatu Ya Tashriyq

 

Ni waajib kutupia Jamaraat tatu katika siku hii kwa aliyebakia Minaa na hakugura kwenda Makkah (katika Mguro wa kwanza) baada ya jua kupinduka kwa mujibu wa kauli ya Jumhuri.  Lakini Abu Haniyfah amesema inajuzu kutupia kabla jua kupinduka baada ya Alfajiri, na Hadiyth ya Jaabir inamjibu.

 

Na wamekubaliana kuwa wakati wa mwisho wa kutupia katika siku hii ni kuchwa jua, na kwamba wakati wa kutupia ili kulipia siku zilizotangulia unamalizikia pia kwa kuchwa jua la siku ya tatu ya Tashriyq, kwa kuwa wakati wa Manaasik unatoka kwa kuchwa jua.

 

 

An-Nafru Ath-Thaaniy

 

Hujaji akitupia Jamaraat tatu katika siku ya tatu ya Tashriyq, -nayo ni siku ya nne ya masiku ya kuchinja- ataondoka Minaa kwenda Makkah. Hatakiwi akae Minaa baada ya kutupia. Na hii huitwa Yawmu An Nafri Ath-Thaaniy (Siku ya mguro wa pili).

 

 

Kutupiwa vijiwe na mtu mwingine

 

Aliyeshindwa kutupia mwenyewe kutokana na ugonjwa, au kuzuiliwa na mfano wake, basi atamwomba mtu mwingine amtupilie, kwa kuwa wakati wake ni mfinyu. Na huyu atakayemtupilia ni lazima awe kwanza ameshajitupilia mwenyewe.

 

Na haiswihi kuwatupia wanawake wenye nguvu zao na uwezo wa kutupa wala watoto. Ama Hadiyth ya Jaabir isemayo: ((Tulihiji pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam)  tukiwa pamoja na wanawake na watoto, nasi tukawatupilia))…Hadiyth hii ni Dhwa’iyf [Imekharijiwa na Ahmad (3/314), na mfanowe kwa At-Tirmidhiy (927), Ibn Maajah (3038) na Al-Bayhaqiy (5/256)]

 

 

Kulala Minaa Masiku ya Tashriyq Ni Waajib

 

Ni waajib kulala Minaa nyusiku za siku tatu za Tashriyq (au nyusiku mbili za tarehe 11 na 12) kwa anayeta’ajjal (anayeharakia) kwa mujibu wa kauli ya Jumhuri ya ‘Ulamaa. Wanasema ni lazima kuchinja mnyama kwa atakayeondoka huko bila udhuru kutokana na Hadiyth ya Ibn ‘Umar: ((Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alimruhusu ‘Abbaas alale Makkah siku za [kukaa] Minaa kwa ajili ya hodhi lake la kunyweshea maji [Mahujaji])). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1745) na Muslim (1315)]

 

Hadiyth hii ni dalili kuwa ni waajib kulala Minaa, na kulala ni katika Manaasik za Hajj. Kwa kuwa kutolewa ruksa kunahukumia mkabala wake ambao ni zuio, na ruksa imetolewa kwa udhuru uliotajwa. [Al-Mughniy (3/449), Al-Furuw’u (3/518) na Ash-Sharhul Mumti’u]

 

Mahanafiy wamesema ni Sunnah. Ni kauli pia ya Ash-Shaafi’iy na riwaya toka kwa Ahmad. [Al-Hidaayah (2/2/186) na Al-Inswaaf (3/47)]

 

Kauli ya kwanza ya Jumhuri kuwa ni waajib ndio sahihi zaidi. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

 

Share