26-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Hajj Na 'Umrah: Jamaraat (Kurusha Vijiwe) Minaa

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Hajj Na ‘Umrah

 

26-Jamaraat (Kurusha Vijiwe) Minaa

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

Taarifu yake

 

الرمي katika lugha ni kutupa kitu kwa kasi. Na الجمرات أو الجمار ni vijiwe vidogo.

 

Umoja wake (singular) ni جمرة ambazo ni changarawe.

 

Hukmu yake

 

Jumhuri ya ‘Ulamaa wanasema Kutupia Jamaraat ni waajib na haijuzu kuacha, na mwenye kuacha ni lazima achinje mnyama.

 

 

Dalili ya kuwa ni waajib

 

1- Hadiyth ya Jaabir aliyesema: ((Nilimwona Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) anatupia vijiwe akiwa juu ya mnyama wake Siku ya An-Nahr [tarehe 10] na anasema:

 

((لتأخذوا عني مناسككم، فإني لا أدري لعلي لا أحج بعد حجتي هذه))

((Jifunzeni kutoka kwangu Manaasik zenu, kwani hakika mimi sijui, huenda nisihiji baada ya Hijjah yangu hii)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1297), An-Nasaaiy (3062) na Abu Daawuwd (1970)]

 

2- Neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam):

 

((إنما جعل الطواف بالبيت وبالصفا والمروة ورمي الجمار لإقامة ذكر الله))

((Hakika si jinginelo, Kutufu Nyumba, Kusai baina ya As-Swafaa na Al-Marwah na Kutupia vijiwe kumewekwa kwa ajili ya kumdhukuru Allaah)). [Isnaad yake ni Dhwa’iyf. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (1888), At-Tirmidhiy (902) na Ahmad (4/64)]

 

3- Ni ‘amali ambayo baada yake inafuatia kuvua Ihraam (Tahallul), hivyo imekuwa ni waajib ili iwe ni kitenganishi kati ya kuvua Ihraam na kuwa ndani ya Ihraam.

 

Sehemu Vilipo Viguzo Vinavyotupiwa Vijiwe Na Idadi Yake

 

Viguzo vinavyotupiwa vijiwe ni vitatu:

 

1- Jamarat Al-‘Aqabah Al-Kubraa (Guzo Kuu). Hili ni la kwanza upande wa Makkah, na linakuwa upande wa kushoto kwa anayeingia Minaa.

 

2- Al-Jamarat Al-Wustwaa (la kati).    Linafuatia baada ya Jamarat Al-‘Aqabah upande wa Muzdalifah.

 

3- Al-Jamarat As-Swughraa (dogo). Linafuatia baada ya Masjid Al-Khayf Minaa.

 

Ukubwa wa vijiwe

 

Imestahabiwa ukubwa wa vijiwe vya kutupia uwe mfano wa kijiwe kinachorushwa kwa kidole (au manati), yaani ukubwa wa punje kubwa ya haragwe. Baadhi wamesema ni kubwa kuliko njegere (chickpeas) na chini ya hazeli (hazelnut).

 

Katika Hadiyth ya Jaabir: ((..Kisha akapita njia ya kati inayotokezea kwenye Al-Jamarat Al-Kubraa [Guzo kuu] mbele ya mti, akalitupia kwa vijiwe saba, analeta Takbiyr kwa kila kijiwe anachotupa mithili ya kijiwe cha kukivurumisha kwa kidole…)).

 

Na Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliamuru aokotewe vijiwe vya kutupia, akaokotewa vijiwe saba vya ukubwa wa kuvurumisha kwa kidole, na akaanza kuvipangusa vumbi kwenye kiganja chake, na akasema:

 

((بأمثال هؤلاء فارموا، وإياكم والغلو في الدين، فإنما أهلك من كان قبلكم الغلو في الدين))

((Kwa mithili ya [ukubwa wa] hivi tupieni, na nawatahadharisheni na uchupaji mipaka na kufanya ifraatw katika Diyn, kwani uchupaji na ifraatw katika Diyn uliwaangamiza waliopita kabla yenu)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na An-Nasaaiy (5/268), Ibn Maajah (3029) na Ahmad (1/215, 347)]

 

Sijui tuseme nini kwa wayafanyayo baadhi ya wajinga wanaotupia Jamaraat kwa viatu. Tunamwomba Allaah Ayatengeneze mambo ya Waislamu na Awaeleweshe Sunnah Tukufu ya Nabiy wao.

 

Ni wapi vijiwe huokotwa?

 

Hujaji anaweza kuokota vijiwe sehemu yoyote aitakayo, kwa kuwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) hakuainisha mahala maalumu pa kuokotea kama ilivyo katika Hadiyth iliyotangulia ya Ibn ‘Abbaas. Hii pia ni kauli ya Ahmad na ‘Atwaa, na imekhitariwa na Ibn Al-Mundhir na Ibn Taymiyah (Allaah Awarehemu).

 

Ash-Shaafi’iy amependelea Hujaji avichukue toka Muzdalifah. [Al-Majmuw’u (8/155)].

 

Hili limesimuliwa toka kwa Ibn ‘Umar na Sa’iyd bin Jubayr.

 

Ninasema: “Lakini uzito bila shaka haufichiki, na jambo lina wasaa”.

 

Je, inajuzu kutumia vijiwe zaidi ya mara moja?

 

Jumhuri wanasema inajuzu kutumia vijiwe ambavyo ameshavitupia mwanzo lakini pamoja na ukaraha. Ibn Hazm amesema inajuzu bila ukaraha. Amesema (Rahimahul Laah) katika Al-Mughniy (7/288): “Ama kutupia kwake kwa vijiwe ambavyo ameshavitupia, hilo halikukatazwa na Qur-aan wala Sunnah”. 

 

Na hii pia ni kauli ya Abu Haniyfah na Maswahibu wake.  

 

Na ikisemwa kuwa imesimuliwa toka kwa Ibn ‘Abbaas akisema: ((Kuwa vijiwe vya kutupia viguzo vilivyotaqabaliwa kati yake huondoshwa [na Malaika], na ambavyo havikutaqabaliwa kati yake huachwa, na kama si hivyo, vingekuwa mlima wa kuziba njia)) Tunasema: “Na’am. Ikiwa utupaji wa vijiwe hivi wa mtu fulani haukutaqabaliwa na wa mwingine umetaqabaliwa, ni sawa na mtu aliyetoa swadaqah kitu fulani na Allaah Asimtaqabalie, kisha kitu kile kile akimiliki mtu mwingine akitolee swadaqah na Allaah Amtaqabalie”.

 

Vijiwe havioshwi

 

Ash-Shaafi’iy (Rahimahul Laah) amestahabisha kuviosha vijiwe vya kutupia Jamaraat, lakini hakuna dalili juu ya hilo. Ibn Al-Mundhir kasema: “Hakuna Hadiyth yoyote inayojulikana kuwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliviosha au kuamuru vioshwe, na hakuna faida yoyote kuviosha”.

 

Pia ‘Atwaa, Ath-Thawriy, Maalik na ‘Ulamaa wengi wanasema havioshwi.

 

Ash-Shaafi’iy amesema: “Tumesimuliwa toka kwa Twaawuws kuwa alikuwa anaviosha”.

 

Ninasema: “Linaloonekana ni kuwa hakuna usharia wa kuviosha. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.

 

Kutupia juu ya kipando

 

Inajuzu Hujaji kutupia viguzo akiwa juu ya kipando (mnyama, gari, pikipiki n.k). Ni kwa Hadiyth ya Qudaamah bin ‘Abdullaah amesema: ((Nilimwona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akitupia Jamaratul ‘Aqabah Yawm An-Nahr [tarehe 10] juu ya ngamia wake mwekundu aliyechanganya weupe, hapigwi mtu [aliye mbele yake], wala hafukuzwi, wala haambiwi kaa kando, kaa kando)). [Hadiyth Hasan. Imekharijiwa na An-Nasaaiy (5/270), At-Tirmidhiy (903) na Ibn Maajah (3035)]

 

Wakati wa kutupia na idadi yake

 

Siku za kutupia ni nne.

 

Yawm An-Nahr (Tarehe 10 Dhul Hijjah), na masiku matatu yanayofuatia ambayo huitwa Masiku ya At-Tashriyq (11, 12 na 13 Dhul Hijjah).

 

Katika Yawm An-Nahr, Hujaji atatupia vijiwe saba kwenye Jamarat Al-‘Aqabah Al-Kubraa (Guzo kuu) peke yake.

 

Na katika Masiku Matatu ya At-Tashriyq, atatupia kwa mpangilio kwa kila siku Al-Jamarat As-Swughraa (Guzo dogo), kisha guzo la kati na kisha guzo kuu Jamarat Al-‘Aqabah. Kila guzo atatupia vijiwe saba. Hivyo idadi jumla ya vijiwe atakavyovitupia itakuwa ni 70; vijiwe saba Yawm An-Nahr, na 21 katika kila siku ya Masiku ya At-Tashriyq [7 + (21 × 3) = 70].

 

Ikiwa Hujaji ataharakia kuondoka (atafanya “Ta’ajjul”) kwa kutoweza kungojea hadi tarehe 13 –na hili anaruhusiwa- basi idadi ya vijiwe kwake itakuwa ni 49 [7 + (21×2) = 49].

 

1- Kutupia Yawm An-Nahr

 

Tushasema nyuma kuwa ni waajib kutupia Jamaratul ‘Aqabah tu Yawm An-Nahr kwa vijiwe saba. Lakini, ni kutokea wapi hutupiwa vijiwe?

 

Imesuniwa Hujaji atupie kutoka katikati ya Bonde (Batwn Al-Waadiy) ambapo Makkah inakuwa kushotoni kwake na Minaa kuliani mwake kama ataweza kufanya hivyo. Ni kwa kitendo cha Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kama ilivyoeleza Hadiyth ya Jaabir, na kwa Hadiyth ya Ibn Mas’uwd isemayo: ((Kwamba yeye alipotupia Jamaratul ‘Aqabah aliingia ndani ya bonde, na alipokuwa sambamba na mti, alisimama mbele yake, akatupia vijiwe saba, na kwa kila kijiwe akaleta Takbiyr, kisha akasema: Kutokea hapa –Naapa kwa Yule Ambaye hapana mola isipokuwa Yeye tu- alisimama ambaye aliteremshiwa Suwrat Al-Baqarah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1750) na Muslim (1296)]

 

Na kama haikuwa wepesi –na hususan katika zama zetu za sasa- basi hapana ubaya atupie toka mahala popote anapoweza.

 

Wakati wa kutupia

 

Toka kwa Jaabir (Radhwiya Allaah ‘anhu) amesema: ((Nilimwona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akitupia Yawm An-Nahr wakati wa Dhuhaa, na ama baada ya hapo ni baada ya kupinduka jua)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy ikiwa Mu’allaq Majzuwman (3/677) na Muslim (1299).

 

Kwa hiyo Sunnah, asitupie Jamararul ‘Aqabah Yawm An-Nahr [tarehe 10] ila baada ya kuchomoza jua. Na hili si waajib kwa Jumhuri ya ‘Ulamaa.

 

Ama yaliyosimuliwa toka kwa Ibn ‘Abbaas kwamba: ((Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alitutanguliza mabarobaro wa Baniy Al-Muttwalib usiku wa Muzdalifah juu ya punda akawa anatupiga piga migongo yetu akituambia:

((أبني لا ترموا الجمرة حتى تطلع الشمس))

 ((Enyi wanangu! Msitupie vijiwe mpaka jua lichomoze)), Hadiyth hii ni Dhwa’iyf. [Imekharijiwa na Abu Daawuwd (1940), An-Nasaaiy (5/271) na Ibn Maajah (3025). Ina Asaaniyd ambazo zina walakin. Al-Haafidh amesema ni Swahiyh katika Al-Fat-h (3/528) kwa Asaaniyd zake, na pia Al-Albaaniy katika kitabu cha Hijjatun Nabiy uk. 80.]

 

Kwani, ikiwa atachelewesha kutupia mpaka muda wa kabla ya kuchwa jua, basi inajuzu ingawa hilo kwa mujibu wa Ijma’a ya ‘Ulamaa halikustahabiwa. [At-Tamhiyd cha Ibn ‘Abdil Barr (17/255)]

 

Kama itamwia mtu uzito kutupia kabla jua kuchwa, basi anaruhusiwa kutupia japokuwa usiku. Ni kwa Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas: ((Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa anaulizwa [maswali] Yawm An-Nahr. Mtu mmoja akamuuliza akisema: Nimetupia baada ya kuingiliwa na jioni. Akamwambia: ((Hakuna ubaya)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1735) na wengineo]

 

Kwa Fuqahaa wa Kimaalik na Kihanafiy, wakati wa kutupia huanza tokea kuchomoza Alfajiri ya Yawm An-Nahr. Ama wa Kishaafi’iy na Kihanbali, huanzia usiku wa manane wa kuamkia Yawm An-Nahr kwa aliyesimama ‘Arafah kabla yake.

 

Na wakati wa mwisho wa kutupia Jamaratul ‘Aqabah kwa Mahanafiy, ni mpaka Alfajiri ya siku ya pili (tarehe 11), kwa Wamaalik mpaka Magharibi. Wote wawili wamewajibisha kuchinja mnyama kwa kuchelewesha utupiaji nje ya wakati wake.

 

Ama Mashaaf’iy na Mahanbali, wakati wa mwisho wa kutupia kwao ni Siku ya mwisho ya Tashriyq.  

 

 

Ni wakati gani madhaifu walioondoka Muzdalifah kabla ya Alfajiri wanatupia?

 

Hakuna makhitalifiano yoyote kuwa lililostahabiwa kwa wanawake madhaifu na wengineo, ni kutupia baada ya jua kuchomoza ili kumuiga Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam). Ama kutupia kabla jua kuchomoza, hili Ash-Shaafi’iy kalijuzisha walau kabla ya Alfajiri, na Jumhuri wamelijuzisha baada ya Alfajiri hadi kuchomoza jua.

 

Sheikh wetu amesema: [Jaami’u Ahkaamin Nisaa cha Sheikh wetu Mustwafaa bin ‘Adawiy (2/563) kwa mabadilisho kidogo)]:

 

“Ninaloona mimi kuhusiana hasa na wanawake ni kuwa wanaweza kutupia wanapowasili Minaa. Kwani Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliwaruhusu kuondoka usiku. [Hadiyth kuhusu hili zimetajwa nyuma katika kipengele cha kulala Muzdalifah, nazo ni Swahiyh]. Na Asmaa (Radhwiya Allaah ‘anhaa alitupia kabla ya Swalaat As-Subh (kama ilivyoelezwa nyuma).  Na nyuma Hadiyth ya Saalim imeeleza: ((Baadhi yao wapo wanaokuja Minaa kwa Swalaah ya Alfajiri, na wengine wanakuja baada ya hapo. Na wanapofika, hutupia Al-Jamarah. Na Ibn ‘Umar alikuwa anasema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amewaruhusu hao hilo”. [Angalia nyuma]

 

 

Na’am, na hata kama Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas ni Swahiyh, basi katazo litakuwa ni kwa vijana wadogo na si wanawake. Au amri inaweza kuchukulika kama ni jambo manduwb katika kuoanisha dalili kama alivyosema Ibn Hajar katika Al Fat-h. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

 

Sunan Za Kutupia Viguzo Yawm An-Nahr

 

1- Kuacha Talbiyah kabla ya kuanza kutupia.

 

Ni kwa Hadiyth ya Al-Fadhwl bin ‘Abbaas (Radhwiya Allaah ‘anhumaa): ((Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) hakuacha kuleta Talbiyah mpaka alipofika Al-Jamarah)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1670) na Muslim (1281)]

 

Jumhuri ya ‘Ulamaa wamelisema hili. [Fat-hul Baariy (3/623), Al-Majmuw’u (8/177), Nihaayatul Muhtaaj (3/303) na Al-Mubdi’u (3/340). Ama kwa upande wa Ibn Hazm katika Al-Muhallaa (7/180), Talbiyah hukatwa baada ya kumaliza kutupia]

 

2- Kuleta Takbiyr sambamba na kila kijiwe anachotupa.

 

Ni kwa yaliyomo kwenye Hadiyth ya Jaabir: ((..mpaka akafika kwenye Al-Jamarah [nguzo] iliyoko pembeni ya mti, akaitupia kwa vijiwe saba akileta Takbiyr kwa kila kijiwe kati yake..)).

 

3- Aitupie toka chini yake akiwa ndani ya bonde.

 

Hili limeelezwa nyuma kidogo.

 

4- Atupie baada ya jua kuchomoza.

 

Hili pia lishaelezwa.

 

5- Kuondoka baada ya kutupia bila kusimama. Ni kwa Hadiyth ya Jaabir: ((..alitupia toka ndani ya bonde kisha akaondoka kwenda mahala pa kuchinjia)). Asisimame mbele ya Jamaratul ‘Aqabah, si kwa kuomba du’aa wala kwa jingine lolote.

 

Al-Haafidh amesema kwenye Al Fat-h (3/679): “Jamaratul ‘Aqabah ina sifa nne mahususi kulinganisha na nguzo nyingine mbili: Ni peke yake inayotupiwa Yawm An-Nahr (tarehe 10), watu hawasimami mbele yake (baada ya kutupia), hutupiwa wakati wa Dhuhaa, na hutupiwa toka chini yake kama Sunnah”. 

 

 

Amali zinazofanywa Yawm An-Nahr na mpangilio wake

 

‘Amali za kisharia kwa Hujaji katika Yawm An-Nahr baada ya kufika Minaa ni nne: Kutupia Jamaratul ‘Aqabah, kisha kuchinja, halafu kunyoa na mwisho kufanya Twawaaful Ifaadhwah. Mpangilio huu ni Sunnah na si Waajib. Na kama atatufu kabla ya kutupia, au akachinja wakati wa kuchinja kabla hajatupia, au akanyoa kabla ya kutupia na kutufu, basi inajuzu na hana fidia, lakini atakosa ubora. [Al-Majmuw’u (8/168)]

 

Haya ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy, Jumhuri ya Salaf, ‘Ulamaa, na Fuqahaa Aswhaabil Hadiyth. [Fat-hul Baariy (3/668)]

 

Dalili ya hili ni Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas: ((Kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliulizwa kuhusu kuchinja, kunyoa na kutupia, na kutanguliza na kuchelewesha akasema: ((Hakuna ubaya)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1734) na wengineo]

 

Na hii bila shaka ni kwa ajili ya kuondosha dhambi na fidia kwa pamoja, na hii ndio maana ya “Hakuna ubaya”.

 

Baadhi ya ‘Ulamaa kama Imaam Ahmad na wengineo wamesema kuwa ruksa ya kutopangilia ‘amali hizi inamhusu aliyesahau au asiyejua tu, na si kwa anayekusudia (kuvuruga utaratibu). [Al-Mughniy (3/447) na Fat-hul Baariy (3/668)]

 

Ni kwa Hadiyth ya ‘Abdullaah bin ‘Amri: ((Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alisimama katika Hijjah ya Kuaga na watu wakawa wanamuuliza. Mtu mmoja akasema: Sikuhisi [sikujua], nikanyoa kabla sijachinja. Akamwambia: Chinja na hakuna ubaya. Akaja mwingine akasema: Sikuhisi, nikachinja kabla sijatupia vijiwe. Akamwambia: Tupa na hakuna ubaya. Na hakuulizwa siku hiyo kuhusu jambo lolote lililotangulizwa au lililocheleweshwa isipokuwa alisema:

((افعل ولا حرج))

((Fanya na hakuna ubaya)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1736, 1737) na Muslim (1306)]

 

Ibn Daqiyq amesema katika Sharhu ‘Umdatil Ahkaam (3/79): “Aliyoyasema Ahmad ni imara kwa upande kuwa dalili imehabarisha wajibu wa kumfuata Rasuli katika Hajj kwa neno lake:

خذوا عني مناسككم

 ((Jifunzeni kutoka kwangu Manaasik zenu)).

 

Na Hadiyth hizi zenye kuruhusu kutanguliza la kufanywa baadaye zimetanguliwa na kauli ya muulizaji “Sikuhisi” [Sikujua], hivyo hukmu hapa imehusishwa na hali ya kutokujua. Na kwa muktadha huo, hali ya kukusudia inabakia katika asili ya waajib wa kumfuata Rasuli kama alivyofanya katika Hajj. Kadhalika, hukmu ikifungamana na hali yenye uzito wa kuzingatiwa, haijuzu kuitupa hali hiyo kando. Na hakuna shaka kwamba kutokujua ni hali mwafaka ya kusameheka na kutoadhibiwa kwa kosa, nayo imefungamana na hukmu, hivyo haiwezekani kuiweka kando na kuifungamanisha na kukusudia”.

 

Ninasema: “Maneno haya yanakuwa katika kilele cha usahihi lau Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) angeishilia kusema “Hakuna ubaya” tu katika kumjibu muulizaji. Na aliposema: “Fanya na hakuna ubaya” na yakawa matamshi haya yanadulisha kuwa hakuna ubaya kwa siku zijazo, imejulikana kuwa hakuna tofauti kati ya aliyesahau, asiyejua, mwenye kukumbuka na mwenye kujua. Na hili likiwa kama hoja imara, linawafikiana na makusudio ya sharia na hususan katika zama zetu za leo. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”. [Al-‘Allaamah Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahul Laah) ameashiria hoja hii katika Al-Mumti’u (7/367)]

 

Tatizo linabakia katika kutanguliza kunyoa kabla ya kuchinja kutokana na Kauli Yake Ta’aalaa:

 وَلَا تَحْلِقُوا رُءُوسَكُمْ حَتَّىٰ يَبْلُغَ الْهَدْيُ مَحِلَّهُ

((Na wala msinyoe vichwa vyenu mpaka mnyama afikie machinjoni pake)). [Al-Baqarah 196]

 

Hili limejibiwa kuwa muradi wa mnyama kufika machinjoni mwake ni kufika mahala ambapo ni halali kumchinja hapo, na hili lishafanyika. Na tatizo lingebakia lau Allaah Angesema: “Na msinyoe mpaka mchinje”.

 

Hivyo ni sahihi kuwa si wajibu kufuatanisha ingawa ni bora zaidi. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

 

Share