29-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Hajj Na 'Umrah: Kunyoa Na Kupunguza

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Hajj Na ‘Umrah

 

29-Kunyoa Na Kupunguza

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

Hukmu Yake

 

Jumhuri ya ‘Ulamaa wamekubaliana kuwa kunyoa nywele za kichwa au kuzipunguza ni waajib kati ya waajibaat za Hajj. Ni madhehebu ya Hanafiy, Maalik na Hanbal. [Fat-hul Qadiyr (2/178, 252), Sharhu Ar-Risaalati Bihaashiyatil ‘Adawiy (1/478), Al-Mughniy (3/435) na Al-Furuw’u (3/513)]

 

Kwa Ash-Shaafi’iy, kwa ilivyo mashuhuri kwake ni kuwa kunyoa au kupunguza ni nguzo ya Hajj. [Al-Mjmuw’u (8/189)]

 

Sababu ya kukhitalifiana kwao ni kukosekana dalili ya hili au lile pamoja na kuthibiti la kunyoa na kupunguza katika Qur-aan, Sunnah na Ijma’a. Allaah Amesema:

 

((لَّقَدْ صَدَقَ اللَّـهُ رَسُولَهُ الرُّؤْيَا بِالْحَقِّ ۖلَتَدْخُلُنَّ الْمَسْجِدَ الْحَرَامَ إِن شَاءَ اللَّـهُ آمِنِينَ مُحَلِّقِينَ رُءُوسَكُمْ وَمُقَصِّرِينَ لَا تَخَافُونَ))

((Kwa yakini Allaah Amemsadikisha Rasuli Wake ndoto kwa haki. Bila shaka mtaingia Al-Masjidal-Haraam In Shaa Allaah mkiwa katika amani, wenye kunyoa vichwa vyenu na wenye kupunguza, hamtakuwa na khofu)). [Al Fat-h (48:27)].

 

Na toka kwa Ibn ‘Umar kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

 

اللهم ارحم المحلقين

((Ee Allaah! Warehemu wenye kunyoa)).

 

Wakasema: Na wenye kupunguza ee Rasuli wa Allaah. Akasema:

 اللهم ارحم المحلقين

((Ee Allaah! Warehemu wenye kunyoa)).

 

Wakasema: Na wenye kupunguza ee Rasuli wa Allaah. Akasema:

اللهم ارحم المحلقين

((Ee Allaah! Warehemu wenye kunyoa)).

Wakasema: Na wenye kupunguza ee Rasuli wa Allaah. Akasema:

 والمقصرين

((Na wenye kupunguza)).

 

[Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1727) na Muslim (1301)]

 

Na kunyoa ni bora zaidi kuliko kupunguza. Ni kwa Hadiyth ya Ibn ‘Umar iliyotangulia. Na kunyoa si waajib isipokuwa kama atanadhiria kufanya hivyo. Na akipunguza, atakusanya nywele zake kisha atazikata kwenye mkusanyikio kiasi cha pingili ya kidole au chini yake au zaidi.

 

 

Ama wanawake, wao hupunguza na hawanyoi. Toka kwa Ibn ‘Abbaas: ((Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alituambia)):

 

((ليس على النساء حلق، إنما على النساء التقصير))

((Si waajib kwa wanawake kunyoa, bali waajib kwa wanawake ni kupunguza)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (1985), Ad-Daaramiy (1905) na wengineo]

 

Zaidi ya mtu mmoja wamesimulia Ijma’a ya kuwa wanawake hawanyoi bali wanapunguza.

 

 

Ni kiasi gani cha nywele anapunguza mwanamke aliyehirimia?

 

Hili halikugusiwa na Qur-aan wala Sunnah. Baadhi ya ‘Ulamaa wamesema kuwa atakata kiasi cha pingili ya kidole katika kila quruni (fundo la msuko). Waliosema hili ni Ibn ‘Umar, Ash-Shaafi’iy, Ahmad na Abu Thawr. Wengine wamesema: Atajichonga pembeni pembeni kidogo, na wengine wamesema msichana hatopunguza sana, lakini mama mzee atapunguza kwa kiasi kisichozidi robo ya nywele zake. [Angalia aathaar za hili katika Muswannaf Ibni Abiy Shaybah (1/4/115-117) na Jaami’u Ahkaamin Nisaa cha Sheikh wetu (2/566)]

 

Ninasema: “Inavyoonekana ni kuwa anaweza kupunguza kiasi anachopenda mwenyewe muhimu tu asifanane na wanaume. Na kama atafanana na wanaume, haitofaa. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.  

 

 

Wakati wa kunyoa na kupunguza

 

Ni Sunnah kunyoa au kupunguza Yawm An-Nahr baada ya kutupia Jamaratul ‘Aqabah na kuchinja kwa kufuata kitendo cha Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam).

 

Jumhuri wanasema kunyoa au kupunguza hakuhusishwi na muda maalum au mahala maalum, lakini Sunnah ni kufanya hayo katika eneo la Al-Haram katika Siku za kuchinja.

 

Mahanafiy wanasema wakati wake ni katika siku za Kuchinja katika eneo la Al-Haram. Na lau Hujaji atakosea chochote katika mawili haya, basi ataipata tahallul (kuvua Ihraam) lakini ni lazima achinje. [Angalia vitabu rejea tulivyovitaja katika hukmu ya kunyoa]

 

Kati ya adabu za kunyoa

 

1- Asijinyoe mwenyewe bali anyolewe na mtu.

 

2- Kinyozi aanze kumnyoa upande wa kulia wa kichwa chake. Dalili ya mawili haya (1 na 2) ni Hadiyth ya Anas:

 

((أن رسول الله -صلى الله عليه وسلم- أتى مِنَى، فأتى الجَمْرَةَ فرماها، ثم أتى منزله بمِنَى ونحر، ثم قال للحلاق: «خُذْ» وأشار إلى جانبه الأيمن، ثم الأيسر، ثم جعل يعطيه الناسَ))

((Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alifika Mina, akaenda Jamarah akalitupia vijiwe, kisha akaenda sehemu yake aliyoshukia Mina akachinja. Kisha akamwambia mnyoaji: Kamata [kichwa ukinyoe], akamwashiria upande wake wa kulia, kisha wa kushoto, halafu akaanza kuwapa watu nywele zake [wazihifadhi ili watabaruku nazo])). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1305)]

 

[Riwaya nyingine inasema alimwita Abu Twalha Al-Answaariy (Radhwiya Allaah ‘anhu) akampa nywele zake hizo na akamwamuru azigawe kwa watu]

 

3- Akate kucha zake na sharubu zake baada ya kunyoa. Imesimuliwa kwa njia sahihi: ((Kuwa Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaah ‘anhumaa) alikuwa anaponyoa katika Hajj au ‘Umrah hukata kidogo ndevu zake na masharubu yake)).  

 

Na Ibn Al-Mundhir amesema: “Imethibiti kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliponyoa kichwa chake, alikata kucha zake [pia]”. [Angalia Al-Majmuw’u (8/186, 195)]

 

 

Nini atafanya mwenye kipara?

 

Mwenye kipara kichwa kizima, hana cha kunyoa na hana fidia. Lakini imestahabiwa apitishe wembe (au mashine ya kunyolea) juu ya kichwa chake. Ibn Al-Mundhir amenukuu Ijma’a ya ‘Ulamaa kuwa mwenye kipara anapitisha wembe juu ya kichwa chake, lakini Jumhuri wanasema hilo si lazima. [Al-Majmuw’u (8/192, 193)]

 

 

Share