30-Swahiyh Fiqh As-Sun nah: Mlango Wa Hajj Na 'Umrah: Kupitwa Na Hajj Na Kuzuilika

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Hajj Na ‘Umrah

 

30-Kupitwa Na Hajj Na Kuzuilika

 

Alhidaaya.com

 

 

 

1- Kupitwa:

 

Ni kutenda jambo la kuikosa Hajj. Atakayepitwa na Kisimamo cha ‘Arafah mpaka ikachomoza Alfajiri ya Siku ya Kuchinja, basi huyo kaikosa Hajj. Dalili kuhusu hili imeelezwa nyuma wakati wa kuzungumzia nguzo ya Kusimama.

 

Aliyeikosa Hajj afanye nini?

 

Aliyepitwa na Kisimamo cha ‘Arafah basi ameikosa Hajj. Atavua Ihraam ya Hajj kwa ajili ya ‘Umrah ambapo atatufu, atasai, na atanyoa au kupunguza, na Manaasik nyingine zilizobakia kama kulala Muzdalifah, kutupia viguzo, kuwepo Minaa na mfano wake atakuwa hanazo tena, lakini itamlazimu ailipe Hajj yake mwaka unaofuatia, na achinje wakati wa kuilipa. Hii ni kauli ya Jumhuri kinyume na Mahanafiy ambao wanasema kuchinja si waaajib. [Al-Badaai’u (2/220), Al-Hidaayah (2/136), Al-Qawaaniynu Al-Fiqhiyyah (uk. 95), At-Taaju wal Ikliyl (3/200), Rawdhwat At-Twaalibiyna (3/182) na Al-Kaafiy (360)]  

 

Ikiwa aliyeikosa Hajj ataonelea aendelee kubakia na Ihraam yake aje ahiji tena mwakani, basi anaruhusiwa hilo, kwa kuwa kurefuka muda baina ya kuhirimia na kufanya tendo la Hajj hakuzuii kulikamilisha. Ni kama ‘Umrah, au mtu aliyehirimia Hajj katika miezi isiyo ya Hajj.

 

 

Watu Wakikosea Tarehe Ya  Kusimama ‘Arafah

 

Watu wakikosea wakasimama ‘Arafah tarehe nane au kumi, basi itawatosha, na si lazima walipe, kwa kuwa wamefanya waliloamuriwa. [Al-Majmuw’u (8/281)]

 

2- Kuzuilika:

 

Ni kushindikana aliyehirimia kukamilisha Hajj yake. Na asili ya hili ni Kauli Yake Ta’aalaa:

 

 ((فَإِنْ أُحْصِرْتُمْ فَمَا اسْتَيْسَرَ مِنَ الْهَدْيِ))

((Na kama mkizuilika basi chinjeni wanyama walio wepesi kupatikana)). [Al-Baqarah (2:196)]

 

 

Sababu za zuio ni zipi?

 

[Al-Majmuw’u (8/283), Bidaayatul Mujtahid (1/528), na Al-Inswaaf (4/71)]

 

Kutokana na ‘Ulamaa kutofautiana katika kuifahamu Aayah iliyotangulia, wamekhitalifiana pia kwa upande wa sababu ya kimsingi ya kuleta zuio. Baadhi yao wamesema aliyezuilika ni aliyezuiliwa na maadui tu. Ni madhehebu ya Mashaafi’iy na Mahanbali. Kwa kuwa Aayah hii ilishuka baada ya washirikina kumzuia Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) asifanye ‘Umrah ya Al-Hudaybiyah. Wametoa hoja pia kwa Kauli Yake (تعالى):

  فَإِذَا أَمِنتُمْ

((mkipata amani))

 

baada ya Kauli Yake:

 فَإِنْ أُحْصِرْتُمْ

((Kama mkizuilika))

 

na Kauli Yake baada ya hapo:

فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا

((na atakayekuwa mgonjwa miongoni mwenu)).

 

Wamesema:

 

Kama aliyezuilika ni kwa sababu ya ugonjwa, basi kutajwa ugonjwa kusingelikuwa na faida baada ya hapo. Na haya ni madhehebu ya Ibn ‘Umar na Ibn ‘Abbaas.

 

Wengine wamesema, mwenye kuzuilika ni aliyezuilika kwa ugonjwa, adui na kila lenye kumzuia asiweze kutimiza Hajj yake. Ni kauli ya Maalik, riwaya toka kwa Ahmad na chaguo la Sheikh wa Uislamu, nayo ndiyo yenye nguvu. [Bidaayatul Mujtahid (1/529), Al-Inswaaf (4/71) na Al-Ikhtibaaraat (uk. 120)]

 

Na hii ni kwa ujumuishi wa Kauli Yake Ta’aalaa:

 فَإِنْ أُحْصِرْتُمْ

((Kama mkizuilika)).

 

Ama kuwa sababu ya kuteremka Aayah ni Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kuzuiwa na adui, hii ni kuibania na kuifinyia dalili kwenye sababu yake tu [bila mtizamo mpana], na hili halifai. Ama kutolea dalili Kauli Yake Ta’aalaa:

 فَإِذَا أَمِنتُمْ

 ((mkipata amani))

 

hili ni katika mlango wa kutaja hukmu ya baadhi ya vipengele vya jambo zima, na hii haihukumii takhswiys (uainisho wa kitu fulani tu) kama inavyoeleza taaluma ya Uswuwl. Na hapo hapo, Kauli Yake Ta’aalaa

 فَإِذَا أَمِنتُم   

inaonekana kwa nguvu kuwa haimhusu aliyezingirwa bali inahusiana na Tamattu’u ya kihakika, kana kwamba maana ya Aayah ni: Kama hamna hofu lakini mmefanya Tamattu’u kwa kuanza ‘Umrah kisha Hajj, basi chinjeni mnyama anayepatikana kwa wepesi. Taawili hii inaashiriwa na Kauli Yake Ta’aalaa:

 

((َٰذلِكَ لِمَن لَّمْ يَكُنْ أَهْلُهُ حَاضِرِي الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ))

((Hayo ni kwa ajili ya yule ambaye watu wake hawaishi karibu na Al-Masjidil-Haraam))

 

Na mwenye kuzuilika anaweza kuwa yupo Al-Masjid Al-Haraam na mwengine kwa Ijma’a.

 

 

Ninasema (Abu Maalik): “Lililo wazi zaidi kuliko haya yote ni Hadiyth ya ‘Aaishah aliyesema: ((Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliingia kwa Dhwubaa’ah binti Az-Zubayr akamwambia: (([Huenda] ulitaka kuhiji)). Akasema: Wal-Laah, najihisi kuumwa sana. Akamwambia: ((Hiji, na ushurutishe, na sema:

اللهم محلي حيث حبستني

((Ee Allaah! Pangu pa kuvua Ihraam ni pale Utakaponizuia)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5089) na Muslim (1207)]

 

Iko wazi kabisa bila utata kuwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amezingatia ugonjwa na maumivu ni sababu ya kuzuilika na Hajj. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.”

 

 

Aliyezingirwa afanye nini?

 

Aliyezingirwa akashindwa kutimiza Hajj yake, ikiwa alishurutisha (wakati wa kuhirimia) kuwa pahala pa kuvua Ihraam ni pale alipozuilika, basi atavua Ihraam na hatowajibikiwa na jambo lolote. Ni kwa Hadiyth ya ‘Aaishah iliyotangulia.

Na kama hakuwa ameshurutisha, basi atavua Ihraam na kufanya ‘Umrah, na itamlazimu achinje kwa mujibu wa kauli ya Jumhuri. Ni kwa Kauli Yake Ta’aalaa:

 

 ((فَإِنْ أُحْصِرْتُمْ فَمَا اسْتَيْسَرَ مِنَ الْهَدْيِ))

((Na kama mkizuilika, basi chinjeni wanyama walio wepesi kupatikana)). [Al-Baqarah (2:196)]

 

 

Je ni lazima aliyezuilika alipe Hajj yake?

 

Jumhuri wanasema kuwa aliyezuilika si lazima alipe Hajj yake kama atavua Ihraam –kinyume na Mahanafiy- isipokuwa kama itakuwa tokea awali ni Hajj ya waajib kama Hijjah ya Uislamu. Atatakiwa uwajibu uliotangulia. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi. 

 

 

Share