12-Riyaadhw Asw-Swaalihiyn: Mlango Wa Kupendeza Kutoa Bishara na Kupongeza Kwa Kufikiwa na Kheri

 

Riyaadhw Asw-Swaalihiyn

 

باب استحباب التبشير والتهنئة بالخير

12-Mlango Wa Kupendeza Kutoa Bishara na Kupongeza Kwa Kufikiwa na Kheri

 

Alhidaaya.com

 

قَالَ الله تَعَالَى:

فَبَشِّرْ عِبَادِ ﴿١٧﴾ الَّذِينَ يَسْتَمِعُونَ الْقَوْلَ فَيَتَّبِعُونَ أَحْسَنَهُ ۚ  ﴿١٨﴾

Basi wabashirie waja Wangu.Wale wanaosikiliza kwa makini kauli, wakafuata yaliyo mazuri yake zaidi. [Az-Zumar: 17-18]

 

يُبَشِّرُهُمْ رَبُّهُم بِرَحْمَةٍ مِّنْهُ وَرِضْوَانٍ وَجَنَّاتٍ لَّهُمْ فِيهَا نَعِيمٌ مُّقِيمٌ﴿٢١﴾

Rabb wao Anawabashiria kwa rahmah kutoka Kwake na radhi na Jannaatwatapata humo neema zenye kudumu. [At-Tawbah: 21]

 

وَأَبْشِرُوا بِالْجَنَّةِ الَّتِي كُنتُمْ تُوعَدُونَ﴿٣٠﴾

Na pokeeni bishara njema ya Jannah ambayo mlikuwa mkiahidiwa. [Fusw-swilat: 30]

فَبَشَّرْنَاهُ بِغُلَامٍ حَلِيمٍ ﴿١٠١﴾

Basi Tukambashiria ghulamu mvumilivu. [Asw-Swaffaat: 101]

 

وَلَقَدْ جَاءَتْ رُسُلُنَا إِبْرَاهِيمَ بِالْبُشْرَىٰ ﴿٦٩﴾

Na kwa yakini walimjia Ibraahiym Wajumbe Wetu kwa bishara. [Huwd: 69]

 

 

وَامْرَأَتُهُ قَائِمَةٌ فَضَحِكَتْ فَبَشَّرْنَاهَا بِإِسْحَاقَ وَمِن وَرَاءِ إِسْحَاقَ يَعْقُوبَ﴿٧١﴾

Na mkewe amesimama wima, akacheka; Tukambashiria Is-haaq na baada ya Is-haaq ni Ya’quwb. [Huwd: 71]

 

فَنَادَتْهُ الْمَلَائِكَةُ وَهُوَ قَائِمٌ يُصَلِّي فِي الْمِحْرَابِ أَنَّ اللَّـهَ يُبَشِّرُكَ بِيَحْيَىٰ  ﴿٣٩﴾

Basi mara Malaika akamwita (Zakariyyaa) naye akiwa amesimama anaswali katika chumba kwamba: Hakika Allaah Anakubashiria Yahyaa. [Aal-'Imraan: 39]

 

إِذْ قَالَتِ الْمَلَائِكَةُ يَا مَرْيَمُ إِنَّ اللَّـهَ يُبَشِّرُكِ بِكَلِمَةٍ مِّنْهُ اسْمُهُ الْمَسِيحُ  ﴿٤٥﴾

Na pale Malaika waliposema: Ee Maryam! Hakika Allaah Anakubashiria Neno (la Kun!) kutoka Kwake (umzae mtoto), jina lake ni Al-Masiyhu. [Aal-'Imraan: 45]

 

 

Hadiyth – 1

عن أَبي إبراهيم ، ويقال : أَبُو محمد ، ويقال : أَبُو معاوية عبد اللهِ بن أَبي أوفى رضي الله عنهما : أنّ رسول الله صلى الله عليه وسلم بَشَّرَ خَدِيجَةَ رضي اللهُ عنها ببَيْتٍ في الجَنَّةِ مِنْ قَصَبٍ ، لاَ صَخَبَ فِيهِ ، وَلاَ نَصَبَ . متفقٌ عَلَيْهِ .

Imepokewa kutoka kwa Abu Ibraahiym na panasemwa Abu Muhammad, na panasemwa Abu Mu'awiyah 'Abdillaah bin Abu Awf (Radhwiyah Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimbashiria Khadiyjah (Radhwiyah Allaahu 'anhaa) kuwa atapat nyumba Peponi iliyotengenezwa na lulu, ambako hakutakuwa na makelele wala taabu." [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Hadiyth – 2

وعن أَبي موسى الأشعري رضي الله عنه : أَنَّهُ تَوَضَّأ في بَيْتِهِ ، ثُمَّ خَرَجَ ، فَقَالَ : لأَلْزَمَنَّ رسول الله صلى الله عليه وسلم ، وَلأَكُونَنَّ مَعَهُ يَوْمِي هَذَا ، فَجَاءَ الْمَسْجِدَ ، فَسَألَ عَنِ النَّبيِّ صلى الله عليه وسلم، فَقَالُوا وجَّهَ هاهُنَا، قَالَ : فَخَرَجْتُ عَلَى أثَرِهِ أسْألُ عَنْهُ ، حَتَّى دَخَلَ بِئْرَ أريسٍ، فَجَلَسْتُ عِندَ البَابِ حتَّى قضى رسول الله صلى الله عليه وسلم حاجتهُ وتوضأ ، فقمتُ إليهِ ، فإذا هو قد جلسَ على بئرِ أريسٍ وتوَسَّطَ قُفَّهَا ، وكشَفَ عنْ ساقيهِ ودلاّهُما في البئرِ ، فسلمتُ عَليهِ ثمَّ انصَرَفتُ ، فجلستُ عِندَ البابِ ، فَقُلْتُ : لأَكُونَنَّ بَوَّابَ رسولِ اللهِ صلى الله عليه وسلم الْيَوْمَ ، فَجَاءَ أَبُو بَكْرٍ رضي الله عنه فَدَفَعَ الْبَابَ ، فقلتُ : مَنْ هَذَا ؟ فَقَالَ : أَبُو بَكْرٍ ، فقُلتُ : عَلَى رِسْلِكَ ، ثُمَّ ذَهبْتُ ، فقلتُ : يَا رسول الله ، هَذَا أَبُو بَكْرٍ يَستَأْذِنُ ، فَقَالَ : (( ائْذَنْ لَهُ وَبَشِّرْهُ بِالْجَنَّةِ )) فَأقْبَلْتُ حَتَّى قُلْتُ لأَبي بَكْرٍ : ادْخُلْ وَرسول الله صلى الله عليه وسلم يُبَشِّرُكَ بِالجَنَّةِ ، فَدَخَلَ أَبُو بَكرٍ حَتَّى جَلَسَ عَنْ يَمينِ النَّبيِّ صلى الله عليه وسلم مَعَهُ في القُفِّ ، وَدَلَّى رِجْلَيْهِ في البِئْرِ كَمَا صَنَعَ رسول الله صلى الله عليه وسلم ، وَكَشَفَ عَنْ سَاقَيْهِ ، ثُمَّ رَجَعْتُ وَجَلَسْتُ ، وَقَدْ تَرَكْتُ أخِي يَتَوَضَّأ وَيَلْحَقُنِي ، فقلتُ : إنْ يُرِدِ الله بِفُلانٍ – يُريدُ أخَاهُ – خَيْراً يَأتِ بِهِ . فَإذَا إنْسَانٌ يُحَرِّكُ الْبَاب ، فقلتُ : مَنْ هَذَا ؟ فَقَالَ : عُمَرُ بن الخَطّابِ ، فقلتُ : عَلَى رِسْلِكَ ، ثُمَّ جِئْتُ إِلَى رسول الله صلى الله عليه وسلم ، فَسَلَّمْتُ عَلَيْهِ وَقُلْتُ : هَذَا عُمَرُ يَسْتَأذِنُ ؟ فَقَالَ : (( ائْذَنْ لَهُ وَبَشِّرْهُ بالجَنَّةِ )) فَجِئْتُ عُمَرَ ، فقلتُ : أَذِنَ وَيُبَشِّرُكَ رسول الله صلى الله عليه وسلم بِالجَنَّةِ ، فَدَخَلَ فَجَلَسَ مَعَ رسول الله صلى الله عليه وسلم في القُفِّ عَنْ يَسَارِهِ وَدَلَّى رِجْلَيْهِ في البِئرِ ، ثُمَّ رَجَعْتُ فَجَلَسْتُ ، فَقُلتُ : إنْ يُرِدِ اللهُ بِفُلاَنٍ خَيْراً – يَعْنِي أخَاهُ – يَأْتِ بِهِ ، فَجَاءَ إنْسَانٌ فَحَرَّكَ الْبَابَ . فَقُلتُ : مَنْ هَذَا ؟ فَقَالَ : عُثْمَانُ بن عَفَّانَ . فقلتُ : عَلَى رِسْلِكَ ، وجِئْتُ النَّبيَّ صلى الله عليه وسلم فأخْبَرْتُهُ ، فقالَ : (( ائْذَنْ لَهُ وَبَشِّرْهُ بِالجَنَّةِ مَعَ بَلْوَى تُصِيبُهُ )) فَجِئْتُ ، فقلتُ : ادْخُلْ وَيُبَشِّرُكَ رسولُ الله صلى الله عليه وسلم بِالجَنَّةِ مَعَ بَلْوَى تُصيبُكَ ، فَدَخَلَ فَوجَدَ الْقُفَّ قَدْ مُلِئَ ، فجلس وِجَاهَهُمْ مِنَ الشِّقِّ الآخرِ . قَالَ سَعيدُ بْنُ الْمُسَيَّبِ : فَأوَّلْتُهَا قُبُورَهُمْ . متفقٌ عَلَيْهِ .

وزاد في رواية : وأمرني رسولُ الله صلى الله عليه وسلم بحفظِ الباب . وَفيها : أنَّ عُثْمانَ حِيْنَ بَشَّرَهُ حَمِدَ اللهَ تَعَالَى ، ثُمَّ قَالَ : اللهُ المُسْتَعانُ .

Imepokewa kutoka kwa Abu Muwsaa Al-'Ash'ariy (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuwa yeye alitawadha nyumbani kwake kisha akatoka huku akisema: Leo nitajilazimisha kuwa pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Hivyo Alifika Msikitini na kumuulizia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) naye akaambiwa kuwa amepita njia fulani. Akasema: Nilifuata nyayo zake na huku naulizia kwa watu mpaka nikafika sehemu inayoitwa Bi'r Ariys. Nikasimama kwenye mlango mpaka Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamaliza haja yake (haja ndogo) na akatawadha, nilienda kwake na kumuona kuwa amekaa kwenye ukingo wa kisima cha Ariys. Alikuwa amekunja kikoi chake na miguu yake inaeleaelea kisimani. Nikamsalimia kisha nikaondoka na kusimama mlangoni. Nikasema: "Nitakuwa ni mlinzi wa mlango kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) leo." Akaja Abu Bakr (Radhwiya Allaahu 'anhu) na kusukuma mlango, nami nikamuuliza: "Ni nani huyo?" Alijibu: "Ni mimi Abu Bakr." Nikamwambia: "Ngoja kidogo." Kisha nilikwenda na kusema: "Ee Rasuli wa Allaah! Abu Bakr amekuja na anomba ruhusa kuingia." Akasema: "Mpe ruhusa na umbashirie Pepo." Nilirudi mlangoni na kumfungulia Abu Bakr na kumpa bishara ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa ataingia Peponi. Aliingia Abu Bakr (Radhwiya Allaahu 'anhu)na kukaa upande wa kulia wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya ukingo ule wa kisima na akanyoosha miguu yake kisimani kama alivyofanya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na akainyanyua nguo yake mpaka miundi ikawa inaonekana. Kisha nilirudi na kukaa mlangoni, kwani nilikuwa na ndugu yangu niliyemwacha nyumbani akitawadha na alikuwa aje kwangu. Nikasema: "Ikiwa allaah anamtakia kheri fulani - akikusudia ndugu yake, basi atamleta hivi sasa." Mara kukawa na mtu aliyekuwa akiusukuma mlango, nami nikauliza: "Ni nani huyo?" Naye akajibu: "Ni mimi 'Umar bin Al-Khattwaab." Nikamwambia: "Ngoja kidogo." Nilikwend na kumsalimia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kusema: "Ee Rasuli wa Allaah!  'Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu) amekuja na anaomba ruhusa kuingia." Akasema: "Mpe ruhusa na umbashirie Pepo." Nilirudi mlangoni na kumfungulia 'Uamar (Radhwiya Allaahu 'anhu) na kumpa bishara ya Rasuli wa Allaah (Swaalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa ataingia Peponi. Aliingia na kukaa upande wa kushoto wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya ukingo ule wa kisima. Kisha nilirudi na kukaa mlangoni, nikasema: "Ikiwa Allaah anamtakia kheri fulani - akikusudia ndugu yake, basi atamleta hivi sasa." Mara kukawa na mtu aliyekuwa akiusukuma mlango, nami nikauliza: "Ni nani huyo?" Naye akajibu: "Ni mimi 'Uthmaan bin 'Affaan." Nikamwambia: "Ngoja kidogo." Nilikwenda na kumpasha habari Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) naye akasema: "Mpe ruhusa na umbashirie Pepo pamoja na balaa itakayomfika." Nilirudi mlangoni na kumwambia: "Ingia na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anakupa bishara ya kuingia Peponi pamoja na balaa itakayokufika." Aliingia na kukuta kuwa ule ukingo umejaa, hivyo alikaa ule upande mwengine akielekeana nao. Amesema Sa'iyd bin Al-Musayyab: "Huu mpangilio waliokaa hawa watu wa mwanzo yatakuwa karibu." [Al-Bukhaariy na Muslim].

Na imezidishwa katika riwaayah: "Na akaniamuru Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kutunza mlango. Na hapo pia: Hakika pindi 'Uthmaan alipobashiriwa, alimuhimidi Allaah Ta'aalaa, kisha akasema: Allaah ndiye msaidizi." 

 

 

Hadiyth – 3

وعن أَبي هريرة رضي الله عنه ، قَالَ : كُنَّا قُعُوداً حَوْلَ رسولِ الله صلى الله عليه وسلم ، وَمَعَنَا أَبُو بَكرٍ وَعُمَرُ رضي الله عنهما في نَفَرٍ ، فَقَامَ رسولُ الله صلى الله عليه وسلم مِنْ بَيْنِ أظْهُرِنَا فَأبْطَأ عَلَيْنَا ، وَخَشِينَا أنْ يُقْتَطَعَ دُونَنَا وَفَزِعْنَا فَقُمْنَا ، فَكُنْتُ أَوَّلَ مَنْ فَزِعَ ، فَخَرَجْتُ أبْتَغِي رسولَ الله صلى الله عليه وسلم ، حَتَّى أتَيْتُ حَائِطاً للأنصَارِ لِبَني النَّجَارِ ، فَدُرْتُ بِهِ هَلْ أجِدُ لَهُ بَاباً ؟ فَلَمْ أجِدْ ! فَإذَا رَبيعٌ يَدْخُلُ في جَوْفِ حَائِطٍ مِنْ بِئْرٍ خَارِجَهُ – وَالرَّبِيعُ : الجَدْوَلُ الصَّغِيرُ – فَاحْتَفَرْتُ ، فَدَخَلْتُ عَلَى رسول الله صلى الله عليه وسلم، فَقَالَ: (( أَبُو هُرَيْرَةَ ؟ )) فقلتُ : نَعَمْ ، يَا رسول اللهِ ، قَالَ : (( مَا شأنُكَ ؟ )) قُلْتُ : كُنْتَ بَيْنَ أظْهُرِنَا فَقُمْتَ فَأبْطَأتَ عَلَيْنَا ، فَخَشِينَا أنْ تُقْتَطَعَ دُونَنَا ، ففزعنا ، فَكُنْتُ أوّلَ مَنْ فَزِعَ ، فَأتَيْتُ هَذَا الحَائِطَ ، فَاحْتَفَرْتُ كَمَا يَحْتَفِرُ الثَّعْلَبُ ، وهؤلاء النَّاسُ وَرَائِي . فَقَالَ : (( يَا أَبَا هُرَيرَةَ )) وَأعْطَانِي نَعْلَيْهِ ، فَقَالَ : (( اذْهَبْ بِنَعْلَيَّ هَاتَيْنِ ، فَمَنْ لَقِيتَ مِنْ وَرَاءِ هَذَا الحَائِطِ يَشْهَدُ أنْ لا إله إِلاَّ الله مُسْتَيْقِنَاً بِهَا قَلْبُهُ ، فَبَشِّرْهُ بِالجَنَّةِ ... )) وَذَكَرَ الحديثَ بطوله ، رواه مسلم .

Imepokewa kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: Tulikuwa tumekaa huku tumemzunguka Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na pamoja nasi yupo Abu Bakr na 'Umar (Radhwiya Allaahu 'anhumaa). Akasimama Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) baina yetu na kutoka nje. Akakawia sana bila ya kurudi, hivyo tukawa na wasiwasi mkubwa kuhusu usalam wake. Nilikuwa wa kwanza kuhisi hivyo, nami nikatoka kumfuata Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) mpaka nikafika katika ukuta wa Answaar kutoka kwa ukoo wa An-Najjar. Nilizunguka ukuta huo kutafuta mlango lakini bila mafanikio. mara nikaona kijimto kilichokuwa kikileta maji kutoka katika kisima nje ya bustani kikipitia katika ukuta. Nikajikunja mpaka nikaweza kupita kwenye kishimo na kumfikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), ambaye aliponiona alimaka kwa kusema: "Ee Abu Hurayrah!" Nikasema: "Naam (ndio)! Ee Rasuli wa Allaah." Akasema: "Una nini (ni kitu gani kilichokuleta hapa)?" Nikasema: "Ulikuwa pamoja nasi, na kwa ghafla ukaondoka na ukakawia kurudi, hivyo tukawa na wasiwasi kuwa huenda umefikwa na jambo bila ya sisi kuwepo. Mimi nilikuwa wa kwanza kubabaika, hivyo nikaja kwenye ukuta wa bustani hili na nikajikunja kama anavyojikunja mbwa mwitu ili niweze kupita katika shimo. Wengine wapo nyuma yangu." Akasema: "Ee Abu Hurayrah!" na akanipa viatu vyake na kuniambia: "Nenda na viatu vyangu hivi na yeyote utakayekutana naye nyuma ya ukuta huu anashuhudia ya kwamba hapana anayepaswa kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah akiwa na yakini katika moyo wake, mpe bishara njema kuwa ataingia Peponi." Baada ya hayo Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) aliieleza Hadiyth hii kwa urefu wake." [Muslim]

 

 

Hadiyth – 4

وعن ابن شِمَاسَة ، قَالَ : حَضَرْنَا عَمْرَو بنَ العَاصِ رضي الله عنه وَهُوَ في سِيَاقَةِ الْمَوْتِ ، فَبَكَى طَوِيلاً ، وَحَوَّلَ وَجْهَهُ إِلَى الجِدَارِ ، فَجَعَلَ ابْنُهُ ، يَقُولُ : يَا أبَتَاهُ ، أمَا بَشَّرَكَ رسولُ الله صلى الله عليه وسلم بكَذَا ؟ أمَا بَشَّرَكَ رسولُ الله صلى الله عليه وسلم بِكَذَا ؟ فَأقْبَلَ بِوَجْهِهِ ، فَقَالَ : إنَّ أفْضَلَ مَا نُعِدُّ شَهَادَةُ أنْ لا إلهَ إِلاَّ الله ، وَأنَّ مُحَمَّداً رسول اللهِ ، إنِّي قَدْ كُنْتُ عَلَى أطْبَاقٍ ثَلاَثٍ : لَقَدْ رَأيْتُنِي وَمَا أحَدٌ أشَدُّ بُغضاً لرسولِ الله صلى الله عليه وسلم مِنِّي ، وَلاَ أحَبَّ إليَّ مِنْ أنْ أكُونَ قدِ اسْتَمكنتُ مِنْهُ فَقَتَلْتُه ، فَلَوْ مُتُّ عَلَى تلكَ الحَالِ لَكُنْتُ مِنْ أهْلِ النَّارِ ، فَلَمَّا جَعَلَ اللهُ الإسلامَ في قَلْبِي أتَيْتُ النبيَّ صلى الله عليه وسلم ، فقُلْتُ : ابسُطْ يَمِينَكَ فَلأُبَايِعُك ، فَبَسَطَ يَمِينَهُ فَقَبَضْتُ يَدِي ، فَقَالَ : (( مَا لَكَ يَا عَمْرُو ؟ )) قلتُ: أردتُ أنْ أشْتَرِطَ ، قَالَ : (( تَشْتَرِط مَاذا ؟ )) قُلْتُ : أنْ يُغْفَرَ لِي ، قَالَ : (( أمَا عَلِمْتَ أن الإسلامَ يَهْدِمُ مَا كَانَ قَبْلَهُ ، وَأن الهِجْرَةَ تَهْدِمُ مَا كَانَ قَبلَهَا ، وَأنَّ الحَجَّ يَهْدِمُ مَا كَانَ قَبْلَهُ ؟ )) وَمَا كَانَ أحدٌ أحَبَّ إليَّ مِنْ رَسُولِ الله صلى الله عليه وسلم ، وَلاَ أجَلَّ في عَيني مِنْهُ وَمَا كُنْتُ أُطيقُ أن أملأ عَيني مِنْهُ ؛ إجلالاً لَهُ ، ولو سئلت أن أصفه مَا أطقت ، لأني لَمْ أكن أملأ عيني مِنْهُ ، ولو مُتُّ عَلَى تِلْكَ الحالِ لَرجَوْتُ أن أكُونَ مِنْ أهْلِ الجَنَّةِ ، ثُمَّ وَلِينَا أشْيَاءَ مَا أدْرِي مَا حَالِي فِيهَا ؟ فَإذَا أنَا مُتُّ فَلاَ تَصحَبَنِّي نَائِحَةٌ وَلاَ نَارٌ ، فَإذا دَفَنْتُمُونِي ، فَشُنُّوا عَليَّ التُّرابَ شَنّاً ، ثُمَّ أقِيمُوا حَوْلَ قَبْرِي قَدْرَ مَا تُنْحَرُ جَزورٌ ، وَيُقْسَمُ لَحْمُهَا ، حَتَّى أَسْتَأنِسَ بِكُمْ ، وَأنْظُرَ مَا أُرَاجعُ بِهِ رسُلَ رَبّي . رواه مسلم .

Imepokewa kutoka kwa Ibn Shumaasah kuwa amesema: Tulimzuru 'Amruw bin Al-'Aaas (Radhwiya Allaahu 'anhu) akiwa katika uchungu wa kifo. Alilia sana na kwa muda mrefu mpaka akageuza uso wake ukutani. Kuona hivyo, mtoto wake akawa anamliwaza kwa kumwambia: "Ee baba yangu! Si rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikubashiria kadhaa na kadhaa? Si Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) alikubashiria kadhaa na kadhaa?" 'Amru (Radhwiya 'anhu) alituangalia na kusema: "Hakika matayarisho bora (kujiandaa kwa Aakhera) ni kuikariri shahada ya kwamba hapana Mola apasae kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Rasuli wa Allaah. Hakika mimi nimepitiwa na wakati ambao hakuwa yeyote mwenye chuki zaidi kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuniliko na hakukuwa na kitu nilichokuwa nikipenda kama kumkamata na kumuua (yaani kumuua Nabiy). Lau ningekufa katika hali hiyo ningekuwa mtu wa motoni. Allaah Alipoujaalia Uislaamu katika moyo wangu nilikuja kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumwambia: 'Tafadhali nyoosha mkono wako wa kulia ili nikubai'. Alinyoosha mkono wake wa kulia lakini nilirudisha mkono wangu. Akasema: 'Una nini ee 'Amruw?' Nikasema: 'Napenda kuweka sharti.' Akasema: 'Unaweka sharti gani?' Nikasema: 'Nisamehewe madhambi yangu yote.' Akasema: 'Je, hujajua ya kwamba Uislaamu unafuta madhambi yote yaliyofanywa kabla yake (yaani ya kusilimu); na Hijrah (kuhama/kugura kwa ajili ya Allaah) inafuta yote yaliokuwa kabla yake; na pia Hijjah inafuta yaliyokuwa kabla yake.' Baada ya hapo hakukuwa na yeyote niliyekuwa nikimpenda kuliko Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na wala hakukuwa na aliyekuwa mtukufu machoni pangu kuliko yeye. Na kwa ajili ya utukufu wake kwangu, sikuweza kumtizama uso wake mzima kwa makini na lau nitaulizwa nimsifu (au nimueleze) sitoweza kufanya hivyokwa kuwa sikuwahi kumwangalia kwa kitambo. Lau ningekufakatika hali hiyo basi nilikuwa na matumaini makubwa kuwa nitakuwa miongoni mwa watu wa Peponi. Kisha baada ya hapo tumetawalishwa mambo mengi na sijui hali yangu ndani yake? Hivyo, ninapofariki asifuate jeneza langu muombolezi wala moto. Mnaponizika tupeni mchanga kidogo kidogo, kisha kaeni pembezoni mwa kaburi langu kwa muda unaotosha kuchinja ngamia na kugawa nyama yake, ili nipate kujituliza kwa sababu ya kuwepo kwenu na kuanza kutafakari majibu kwa wajumbe wa Rabb wangu (yaani Malaaika)." [Muslim].

 

 

 

 

Share