Maana Ya Taqwa

 

Maana Ya Taqwa

 

Alhidaaya.com

 

 

Taqwa ni mojawapo ya maneno ya kipekee katika lugha ya Kiarabu ambayo hayawezi kutafsiriwa kwa neno moja au mawili. Kwa hiyo maana zake kilugha    ni kinga, kujilinda, himaya, hifadhi, kutahadhari, kukhofu.    

 

Na katika istilahi, Salaf wametaja mengi kuhusu taqwa, miongoni mwayo ni kumwabudu Allaah ipasavyo, kutekeleza yaliyoamrishwa na Allaah (سبحانه وتعالى) na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم), kujiepusha makatazo Yao  na kubakia katika mipaka ya Shariy’ah ya Dini, kumkhofu Allaah na kukhofu Adhabu na Ghadhabu Zake, kuwa na raghba (utashi) na kutaraji thawabu Zake, kumuadhimisha Allaah (سبحانه وتعالى) na kumpenda mapenzi ya kikweli  pamoja  na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

Na taqwa haihitajii kuhakikishwa mtu kuwa mahali fulani au wakati fulani, bali taqwa ya hakika  ni pale mtu anapokua yuko peke yake, akajiepusha na yaliyo haraam japokuwa hakuna mtu anayemuona. Na ndipo aliposema Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kuwa “Taqwa ipo hapa!” Akiashiria kwenye kifua chake palipo na moyo na kusema mara tatu.

  

Umar (رضي الله عنه) alimuuliza ‘Ubayy bin Ka’b (رضي الله عنه): “Taqwa ni nini?” Akajibu: “Ee Amirul-Muuminyn! Je, hukuwahi kupita njia yenye miiba?” Akasema: “Naam!” Akasema: “Ulifanya nini?”   Akasema: “Niliinua miguu yangu huku nikiitazama  na kuinua  mguu mmoja na mwingine, nikikhofia mwiba usije kunichoma.” ‘Ubay akamwambia: “Hiyo ndiyo taqwa!”

 

        

‘Aliy bin Abi Twaalib (رضي الله عنه) amesema: “Taqwa ni kumkhofu Al-Jaliyl (Allaah) na kufanyia kazi Tanziyl (Qur-aan) na kuridhika na kidogo, na kujiandaa Siku ya Rahiyl (kuondoka duniani, kufariki).”

 

 

Share